Zingatio: Mirungi Ni Jamii Moja Na Bangi

 

Zingatio: Mirungi Ni Jamii Moja Na Bangi

 

Naaswri Haamid

 

Alhidaaya.com

 

 

Iwapo atafufuka binaadamu aliyezikwa karne tatu bora na kuziangalia tabia za viumbe wa zama hizi, atakamata kichwa na kusema: "Hawa ni punguwani!"

 

Kwa hakika dunia ya leo imejaa mambo ya kutatanisha na kumtoa mwanaadamu nje ya dira lake la Uwanaadamu. Kwani binaadamu wa sasa hawana tofauti na wanyama, au ni bora tuseme wameshtadi kuliko hao wanyama. Juu ya ujinga wa mbwa, katu hajafikia kupitia wala kutafuna Mirungi hata siku moja. Ngo'mbe ni kiumbe kinachokula majani kwa wingi, lakini hasogelei hata siku moja majani hayo ya Mirungi.

 

Uislamu umeyaweka Mirungi kwenye jamii ya kilevi, na kila kilevi kimeharamishwa ndani ya Uislamu. Nayo inaangukia chini ya mambo mabaya yanayoitwa 'khabaaith', kama Alivyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

الَّذِينَ يَتَّبِعُونَ الرَّسُولَ النَّبِيَّ الأُمِّيَّ الَّذِي يَجِدُونَهُ مَكْتُوبًا عِندَهُمْ فِي التَّوْرَاةِ وَالإِنْجِيلِ يَأْمُرُهُم بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَاهُمْ عَنِ الْمُنكَرِ وَيُحِلُّ لَهُمُ الطَّيِّبَاتِ وَيُحَرِّمُ عَلَيْهِمُ الْخَبَآئِثَ

Wale wanomfuata Rasuli; Nabiy asiyejua kusoma wala kuandika ambaye wanamkuta ameandikwa kwao katika Tawraat na Injiyl, anawaamrisha mema na anawakataza munkari, na anawahalalishia vizuri na anawaharamishia maovu..[ Al-A’raaf: 157]

 

Pia kipenzi chetu Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

Kila chenye kulevya inatambuliwa kuwa ni khamr (ulevi) na kila khamr ni haraam (hairuhusiwi).” [Imesimuliwa na Sayyidna 'Umar (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) na kupokelewa na Imaam Al-Bukhariy]

 

Kinachobadilika baina ya bangi, kokeni, tumbaku na Mirungi ni ladha tu na kiwango cha kilevi (wenyewe wanaita 'stimu'). Lakini yote yabakia kuwa ni aina moja ya vilevi na hivyo kumtoa akili mwanaadamu akawa hajielewi wala hajifahamu.

 

Kawaida ya Mirungi huwa inatafunwa kwenye makundi ya watu, hapo kunajaa gumzo zisizo na maana, michezo michafu, kupoteza muda, matusi na maovu chungu nzima. Bila ya kusahau kwamba, wanawake waliomo kwenye ndoa wanawalalamikia mno waume zao wanaotumia mirungi kwa sababu ya kukoseshwa haki zao za jimai.

 

Halikadhalika, Mirungi ni majani ambayo yanapingwa vikali mno na wanaharakati wa afya duniani kote. Faida zake ni chache chache mno. Baadhi ya athari zake ni kupoteza wakati na fedha, kuvunja ndoa, kupunguza heshima mbele ya kadamnasi na pia utovu wa adabu.

 

Basi kwa hizi amri za Rabb wetu na Nabiy Wake, pamoja na Ma’ulamaa tofauti walioikataza, haujafika wakati Waislamu kujiepusha nayo?! Tumche Rabb wetu kutokana na ghadhabu Zake zisizomithilika na kitu chochote. Tuseme kwa pamoja:  

سَمِعْنَا وَأَطَعْنَا ۖ 

“Tumesikia na tunatii.” [Al-Baqarah: 285]

 

 

Share