Zingatio: Krismasi 3: ‘Sala’ Zake Zimezidiwa Na Matamanio Ya Nafsi

 

Zingatio: Krismasi 3: 'Sala' Zake Zimezidiwa Na  Matamanio Ya Nafsi

 

Naaswir Haamid

 

 

Alhidaaya.com

 

 

Amesema kweli Rabb wetu Mtukufu (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

زُيِّنَ لِلنَّاسِ حُبُّ الشَّهَوَاتِ مِنَ النِّسَاءِ وَالْبَنِينَ وَالْقَنَاطِيرِ الْمُقَنطَرَةِ مِنَ الذَّهَبِ وَالْفِضَّةِ وَالْخَيْلِ الْمُسَوَّمَةِ وَالْأَنْعَامِ وَالْحَرْثِ ۗ ذَٰلِكَ مَتَاعُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۖ وَاللَّـهُ عِندَهُ حُسْنُ الْمَآبِ ﴿١٤﴾

Watu wamepambiwa huba ya matamanio miongoni mwa wanawake, na watoto, na mirundi ya mali iliyorundikwa ya dhahabu na fedha na farasi wenye chapa ya aina bora na wanyama wa mifugo na mashamba. Hayo ni starehe za uhai wa dunia, na Allaah Kwake kuna marejeo mazuri. [Al-‘Imraan: 14]

 

Kutokana na utashi wa mwanaadamu kufakamia anasa kwa sana pamoja na kutotaka kumuabudia Rabb wake kama Alivyoamrisha, ndio amebuni mambo yenye kutia huzuni na mengine yakafanywa kuwa ati ndio ibada. Ibada inapokuwa sahihi bila ya shaka itaegemezwa kwa Muumba wa Mbingu na Ardhi. Kinyume na hivyo ni kufanya ibada ambazo hazipo na zitakuwa ni zenye kuitimizia nafsi matamanio yake.

 

Katika masuala ambayo ni ya msingi, basi Uislamu ni Diyn ya vitendo isiyotaka kuiga wala kujifunza kutoka kwenye dini nyengine. Miongoni mwa ibada zake Uislamu ambazo hazihitaji kutiwa mkono wala kupunguzwa chumvi ni sikukuu.

 

Naye Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuusia kuchagua marafiki wa kuwa nao. Pamoja na sababu nyenginezo, bila ya shaka wale wanaojitumbukiza kwenye sherehe hizi za Krismasi, wamewafanya Wakristo kuwa ni watu wao wa karibu hadi kufikia kutoona tofauti ya Uislamu na dini nyenginezo. Sikukuu zetu zinaanza kwa kutimiza nguzo za Kiislamu, zinafuatia kuadhimishwa na kusherehekewa kwa kuswali Swalaah ya ‘Iyd pamoja na kuleta takbiyr kwa wingi. Watwambie iwapo yapo haya kwa Krismasi, mwaka mpya au hata kuzaliwa kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Matendo ya unyenyekevu kwa Muumba hayapo kwa upande wa Krismasi. Ni wachache ambao wanahudhuria Kanisani siku hiyo na wengi wao wanakuwepo kwenye starehe zao. Pia ile ladha ya ibada kwa Krismasi haipo kwani haieleweki asili yake. Ndio maana hata wakienda kununua kadi za Krismasi hao wenyewe wananunua zile ambazo hazina mvuto wa kiimani ya Kikristo.[1]Pia walio wengi siku hii ni wenye kuiadhimisha kwa kuchana mifuko ya suruali (kuishiwa na pesa).[2] Halikadhalika, Krismasi ni siku za kufanya biashara kwa makampuni tofauti. Kwa mfano, kampuni kuu ya kusafirisha barua ya Royal Mail kwa mwaka wa 2008 ilitarajia kusafirisha kadi za Krismasi milioni 750 na bidhaa takribani milioni 123.[3]

 

Hayo ni madogo tu ndugu zangu wa Kiislamu, bali tathmini zinaonesha kwamba tarehe 8 ya Januari inakuwa ni kibarua kipevu kwa mawakili wanaosimamia masuala ya talaka. Ambapo takwimu zaonesha kuwa wanandoa wamoja kati ya watano wanaulizia kuhusu talaka kutokana na matatizo ya Krismasi pamoja na kuanza kwa mwaka mpya.[4]

 

Halikadhalika, yapo ambayo sisi wenyewe tunayashuhudia na wala hatuhitaji kupatiwa tochi kuyamurika. Hicho ndicho kipindi ambacho unywaji wa pombe unaongezeka, ajali kuzidi barabarani, uzinzi unaongezeka hadi kufikia kwamba ni lazima mkesha wa Krismasi kila mtu awe na mpenzi (wa jinsia moja au tofauti, iwapo wameoana ama laa kwao haijali). Je Waislamu, tupo tayari na sisi kuzifanya sikukuu zetu kama ilivyo Krismasi? Kama tupo tayari, tuelewe Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Hayupo tayari na tuieweke milango yetu wazi ili ghadhabu Zake ziweze kupita. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atukinge na ghadhabu Zake.

 

Tumalizie kwa kuwasisitiza Waislamu kuacha kushiriki masuala ambayo hayana ithbati. Sio nje ya Uislamu tu, bali hata yale mambo yaliyozushwa ndani ya Uislamu. Mfano kusherehekea kuzaliwa kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambayo imefanywa kuwa ni ibada. Ni ajabu, kwasababu Krismasi ilianza hivyo hivyo hadi kuonekana ni sikukuu kubwa kabisa ilhali sivyo hivyo. Tuikamate Diyn ya Uislamu kwa mikono yetu miwili, tutafanikiwa tu iwapo tutashikamana kisawa sawa na mafundisho ya Qur-aan na Sunnah ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atuwezeshe kuisimamisha Diyn Yake tukufu namna Alivyoamrisha Allaah.

 

 

 

[1] Uchunguzi uliofanywa na Daily Mail umeonesha kwamba kati ya kadi 5,500 zilizonunuliwa kwenye maduka makubwa maarufu, kama vile WH Smith, Clinton Cards na Hallmark, basi ni kadi 67 tu ndizo zilikuwa na picha za hadiyth za Biblia. Halikadhalika, ni kadi moja tu kati ya mia ndio yenye ujumbe wa kidini wa asili. Nyengine zote zinaondosha picha zenye mnasaba wa Krismasi. [Imeripotiwa kwenye Daily Mail 9/12/2006]. Pia kati ya watu 10,000 waliohojiwa ambao wamevuka miaka 50, asilimia 85% wamesema kwamba hawafurahii taa za Krismasi kubadilishwa jina na kuitwa “Winter lights.” Pia dodoso hiyo inaonesha kwamba asilimia 84% hawafurahii ubadilishwaji wa michezo ya kidini kufanywa kuwa sio ya kidini na asilimia 80% hawafurahii makampuni na maskuli kupiga marufuku utumaji wa kadi za Krismasi ama kuweka hadharani mapambo ya Krismasi. [Imeripotiwa kwenye Christian Today 8/12/2007].

[2] Uchunguzi kutoka moneysupermarket.com unaonesha kwamba asilimia 45% wana wasiwasi wa kuweza kuimudu Krismasi kifedha na asilimia 66% watashindwa kulipa madeni yao. Hivyo, kuengeza madeni [na ribaa] kupitia credit cards na overdrafts.

[3] Imeripotiwa kwenye Daily Telegraph 4/11/2008.

[4] Imeripotiwa kwenye Daily Telegraph 8/1/2007.

 

Share