Mashairi: Kokeni, Hiroini, Bangi, Mirungi - Haramu

Mashairi: Kokeni, Hiroini, Bangi, Mirungi - Haramu

                ‘Abdallah Bin Eifan

             (Rahimahu Allaah)

Nawatumia salaamu, kila pembe ardhini,

Sikuja kuwashutumu, nawaomba samahani,

Hapa nashika kalamu, niwape yangu maoni,

Kokeni na Hiroini, Bangi, Mirungi, haramu.

Bangi, Mirungi, haramu, Kokeni na Hiroini,

Vyote hivi ndio sumu, vinatuua jamani,

Wenyewe tujilaumu, alotuponza ni nani ?

Kokeni na Hiroini, Bangi, Mirungi, haramu.

Hawaeshi Maimamu, kusema misikitini,

Hata shuleni Walimu, hukanya madarasani,

Lakini vichwa vigumu, hatutubu abadani,

Kokeni na Hiroini, Bangi, Mirungi, haramu.

Mwisho wake jahanamu, milele pale motoni,

Tunamuudhi Rahimu, kwenda kinyume na dini,

Wenyewe twajidhulumu, katughilibu shetani,

Kokeni na Hiroini, Bangi, Mirungi, haramu.

Bangi huvutwa kwa hamu, akikosa taabani,

Huyo hapewi jukumu, kwa sababu ni mhuni,

Humdharau kaumu, kwa kweli hana thamani,

Kokeni na Hiroini, Bangi, Mirungi, haramu.

Huwa ni mwendawazimu, kunusa “unga” puani,

Humpoteza fahamu, huwa kama hayawani,

Akili sio timamu, kichaa tupu kichwani,

Kokeni na Hiroini, Bangi, Mirungi, haramu.

Hiroini kwenye damu, ni uraibu mwilini,

Hukufanya chakaramu, sindano kanunuweni,

Sana itakugharimu, uingie utumwani,

Kokeni na Hiroini, Bangi, Mirungi, haramu.

Mirungi tumefahamu, makala yamebaini,

Haihitaji elimu, kutafuta vitabuni,

Madhara yake adhimu, yapo wazi hadharani,

Kokeni na Hiroini, Bangi, Mirungi, haramu.

Watu hawakuheshimu, unadondoka machoni,

Hapo wameshahukumu, huajiriwi kazini,

kwa vile huna nidhamu, na wala huna imani,

Kokeni na Hiroini, Bangi, Mirungi, haramu.

Kuua Waislamu, ndio yao madhumuni,

Adui ni gurudumu, hutufuata mitaani,

Amri hawasalimu, mpaka tuwe kaburini,

Kokeni na Hiroini, Bangi, Mirungi, haramu.

Hutupa asali tamu, sumu wametia ndani,

Twadhani watukirimu, kumbe tupo hatarini,

Wanatupiga mabomu, kutumaliza nchini,

Kokeni na Hiroini, Bangi, Mirungi, haramu.

Njama zao zinatimu, zafanywa chini kwa chini,

Zafanywa kitaalamu, na sisi hatuyaoni,

Wamasoni maalumu, pamoja na Mazeyuni,

Kokeni na Hiroini, Bangi, Mirungi, haramu.

Duniani binadamu, tupo kwenye mitihani,

Shika kamba ya Karimu, na ngao ya Qur-aani,

Omba dua ni muhimu, Aitikie Manani,

Kokeni na Hiroini, Bangi, Mirungi, haramu.

Milele hatutadumu, tukumbuke ya mwishoni,

Tunamuomba Rahimu, Atuingize peponi,

Shairi nalikhitimu, kalamu naweka chini,

Kokeni na Hiroini, Bangi, Mirungi, haramu.

Share