Zingatio: Allaah Wao Ni Mpira

 

Zingatio: Allaah Wao Ni Mpira

 

Naaswir Haamid

 

 

Alhidaaya.com

 

 

Iwapo mwanaadamu anataka kuonekana mtu wa maajabu, basi aseme kwamba hana ushabiki wa mpira wala sie mfuasi wa timu yoyote. Hapo uwanja wa stihzai, lawama na matusi utafunguliwa dhidi yake.

 

Kwa hakika mpira ni mfumo mwengine wa maisha, kwani ina ratiba yake na ushabiki wake ni kinyume kabisa na mfumo mzima wa Kiislamu. Tunapozungumzia mpira hatumaanishi yale mazoezi ambayo wanaume wengi wanayafanya. Hapa tunazungumza kuhusiana na mechi ambazo vijana kwa wazee wanazifuatilia kuliko hata Qur-aan na Sunnah yake. Ingawa kwa upande fulani hayo mazoezi ya mpira nayo pia yana walakin, kwani kivazi chake ni cha utupu, mazoezi yanafanywa hadi wakati wa Swalaah na kituko chengine ni kuwepo timu za wanawake.

 

Muislamu atambue kuwa mwenye kuamini muongozo wa asiyekuwa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na akaitakidi kwamba huo ndio muongozo ulio kamili kuliko muongozo wa Nabiy, basi mtu huyo ni kafiri.

 

Halikadhalika, ratiba za mpira haswa klabu za Uingereza na timu za taifa za Ulaya ni zenye kuzishughulisha akili za Waislamu. Akili ambazo zinashindwa kuhifadhi ya maana zikadumazwa kwa majina ya wachezaji na historia zao. Basi tambua kwamba kuikataa na kuipa mgongo diyn ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na ukawa hujifunzi chochote katika diyn ni kutoka nje ya Uislamu. Naye Anasema Muumba wa Mbingu na Ardhi: 

 

وَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّن ذُكِّرَ بِآيَاتِ رَبِّهِ ثُمَّ أَعْرَضَ عَنْهَا ۚ إِنَّا مِنَ الْمُجْرِمِينَ مُنتَقِمُونَ ﴿٢٢﴾

Na nani dhalimu zaidi kuliko yule anayekumbushwa Aayaat za Rabb wake, kisha akazikengeukia? Hakika Sisi Tutawalipiza wahalifu. [As-Sajdah: 22]

 

Kwaweza kuwa na ukweli fulani katika burudani hiyo ya mpira kwamba Muislamu hana starehe nyengine zaidi ya hiyo. Na kwa wapenzi wa mpira wanasema ni bora kuliko ushabiki wa pombe ama uzinifu. Hayo yametolewa na mashabiki wa mpira. Tunawaambia kwamba hakuna kitu chochote katika dunia hii ambacho ni kibaya kwa asilimia mia moja. Kila kitu kina madhara na manufaa yanayohusiana nacho.

 

Hata hivyo, mtazamo wa Sharia’h ya Kiislamu, pamoja na mambo mengine, unajumuisha kupima uzito wa faida na hasara za vitu. Kwani tumeshuhudia kuwa ligi za mpira zina madhara mengi kuliko manufaa. Hii ni kwa dalili ya Tamko Lake Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

يَسْأَلُونَكَ عَنِ الْخَمْرِ وَالْمَيْسِرِ ۖ قُلْ فِيهِمَا إِثْمٌ كَبِيرٌ وَمَنَافِعُ لِلنَّاسِ وَإِثْمُهُمَا أَكْبَرُ مِن نَّفْعِهِمَا ۗ

Sema: Katika viwili hivyo mna dhambi kubwa na (baadhi ya) manufaa kwa watu. Na dhambi yake viwili hivyo ni kubwa kuliko manufaa yake. [Al-Baqarah: 219]

 

Miongoni mwa madhara makubwa ya mpira ni kuwafanya Waislamu kurukwa na akili ikawa hata kutoleana salamu ni kazi ngumu kabisa. Utawakuta kwenye vigenge na hata kazini wakizozana kuhusu mechi hizo.

 

Katika maajabu makubwa ni pale mshabiki wa mpira ambaye ni kijana wa miaka 29 alipoamua kujidhulumu nafsi yake kwa kujinyonga huko Embakasi, Nairobi – Kenya mnamo tarehe 06/05/09. Kisa na mkasa? Ati timu yake imeshindwa! Kiroja kikubwa ni kwamba hiyo mechi wenyewe ilichezwa Uingereza hali ya kuwa yeye yupo Kenya. Kama si wazimu ni nini?!

 

Ni vyema Waislamu wakatafuta ya maana kuliko kupotezewa muda wao katika mambo yasiyokuwa na manufaa yoyote. Sio kaburini wala siku ya Hisabu ambayo Muislamu ataulizwa: "Ni ipi timu yako" au "Nitajie wachezaji wawili wa timu fulani na historia zao." Hilo halipo, isipokuwa jitayarishe na masuala haya: "Nani Rabb wako" na "Nani Nabiy wako". Na iwapo hayo masuala ni mepesi basi endelea kufanya istihzai na diyn yako uyaone ya mtema kuni.

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atuongoze katika njia sahihi na Atughufurie madhambi yetu.

 

 

Share