Zingatio: Ihisabu Nafsi Yako

 

Naaswir Haamid

 

Ukweli ni kwamba kila sekunde yetu hapa duniani ni yenye kuhesabiwa kwa udhati wa uhakika wake. Ndio kusema kuwa tunachunguzwa dhidi ya matendo yetu na tunamurikwa kwa tochi ya Allaah Mtukufu.

 

Wala hapana shaka yoyote kwamba, wengi wetu hapa duniani ni wenye kuhesabu mali, tukisahau kabisa kwamba, mali yenye kheri na yenye kubakia ni ile itakayomvusha Muislamu kutoka katika dimbwi la moto wa Jahannam.

 

Kwa hapa tusihesabu saa, siku, wiki, mwezi, mwaka dahari wala karne; wanahesabu wanatwambia kwamba ‘hesabu huanza na sefuri’, hivyo kwa hapa tunaanza kuhesabu sekunde tunayoitumia. Hivyo, kwa kila sekunde inayopita basi na Muislamu aelewe kwamba imeshaondoka kwenye macho yake tu, lakini imebaki kwenye kumbukumbu za Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na hakuna shaka yoyote kwamba imeshahisabiwa.

 

Tunazinasihi nyoyo zetu na za Waislamu wenzetu kuzihesabu nafsi zao katika matendo mema. Halikadhalika, kuzihesabu katika matendo maovu, kwani pia itatusaidia kuelewa wingi na ukubwa wa deni tulilokuwa nalo mbele ya Muumba, na mwisho wake kufanya haraka ya kuomba maghfira.

 

Mola wetu Mtukufu na Mkarimu Anatuambia ndani ya Qur-aan:

وَنَضَعُ الْمَوَازِينَ الْقِسْطَ لِيَوْمِ الْقِيَامَةِ فَلَا تُظْلَمُ نَفْسٌ شَيْئًا ۖ وَإِن كَانَ مِثْقَالَ حَبَّةٍ مِّنْ خَرْدَلٍ أَتَيْنَا بِهَا ۗ وَكَفَىٰ بِنَا حَاسِبِينَ 

{{Nasi Tutaweka mizani za uadilifu Siku ya Qiyaamah, na nafsi yoyote haitadhulumiwa hata kidogo. Na hata kama ikiwa (jambo hilo lina) uzito mdogo wa chembe ya hardali nalo Tutalileta; Nasi Tunatosha kuwa wajuzi (wazuri kabisa) wa hisabu.}} [Suuratul-Anbiyaa: 47]

 

Basi na tujitahidi kujiuliza masuala yafuatayo kwa kila sekunde yetu inayoyoma hapa duniani:

1.     Je, umemdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na umemshukuru wakati wa kuamka kutoka usingizini?

2.     Je, umesali leo Swalah tano na haswa Swalah ya Alfajiri/’Ishaa Msikitini?

3.     Je, umesoma leo nyiradi za asubuhi na jioni?

4.     Je, umemuomba siku ya leo Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Akuruzuku riziki ya halali?

5.     Je, umemshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) juu ya neema ya kuwa wewe ni Muislamu?

6.     Je, umemshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) juu ya neema ya kuwa Amekupa masikio yenye kusikia na macho yenye kuona na moyo wenye kutwita?

7.     Je, umekifungua leo Kitabu Kitukufu cha Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) (yaani Qur-aan) ukasoma baadhi ya aayah Zake?

8.     Je, umemuomba Allaah akuingize katika Pepo Yake tukufu   kabisa ya Firdaws?

9.     Je, umejikinga kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) dhidi ya Moto mkali wa Jahannam?

10.             Je, leo umemsalia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)?

11.             Je, leo umeamrisha mema na kukataza maovu?

12.             Je, leo ulikuwa na khushuu katika Swalah zako?

13.             Je, umependa kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na
     kuchukia kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala)?

14.             Je, leo umemuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) msamaha Akusamehe madhambi yako yote makubwa na madogo?

15.             Je, umemuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Athibiti moyo wako juu ya Diyn Yake?

16.             Je, leo umetabasamu mbele ya uso wa ndugu yako Muislamu?

17.             Je, umeusafisha ulimi wako kutokana na uongo, kusengenya na kusema maneno ya upuuzi?

18.             Je, umeusafisha moyo wako kutokana na maradhi ya hasad, choyo na kibri?

19.             Je, umeuzoesha moyo wako tabia njema za subira, ucha Mungu, huruma, kumtegemea Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na Ikhlaas?

20.             Je, umekumbuka mauti, kaburi na Qiyaamah?

21. Ewe dada Muislamu, Je, ushaanza kuvaa Hijaab kikamilifu?

22. Ewe kaka Muislamu, Je, umeshaanza kumwiga Mtume kitabia na kimatendo? Ndevu umeanza kufuga na kuvaa mavazi ya heshima na ucha Mungu?

23. Ewe kama Muislamu, Je, umeshaacha kuvuta sigara, kula mirungi, na kupoteza wakati mabarazani?

24. Ewe ndugu Muislamu, Je, umeshaacha kusikiliza miziki na sauti za Shaytwaan?

 
Huu ni wakati wa kuwaza na kufikiri haya kila siku ili tuweze kupata na kufika katika daraja ya utukufu pamoja na kusamehewa makosa yetu yote na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Tusisahau kuwa kila jambo hata liwe mfano wa mdudu chungu basi Mwenyezi Mungu Mtukufu Atatulipa tu (21:47).

 

Tunamuelekea Mola Jalali Atujaalie kuwa ni wenye kufuata na kutii amri Zake na kufuata nyayo za Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) – Aamiyn.

 

 

Share