043-Sifa Ya Swalah Ya Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam): Tahiyyaatu (Tashahhud) Ya Kwanza

 

TAAHIYYAATU (TASHAHHUD) YA KWANZA

 

Kisha, alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) akikaa kwa tashahhud baada ya kumaliza rakaa ya pili. Swalah ikiwa ya rakaa mbili kama Alfajiri, hukaa "muftarishan"([1]) kama alivyokuwa akikaa baina ya Sajdah mbili. Na hivi hivi ndivyo anavyokaa katika tashahhud ya kwanza([2]) katika Swalah za rakaa tatu au nne.

 

 

Alimuamrisha hivyo aliyeswali vibaya kwa kumuambia: ((Utakapokaa katikati ya Swalah, jitulize, na utandaze paja lako la kushoto na lete tashahhud)).([3])

 

 

Abu Huraryah (رضي الله عنه) amesema: "Rafiki yangu  (صلى الله عليه وآله وسلم) amenikataza kuchutama (iq'aa) mchutamo wa mbwa."([4])  [katika riwaaya nyingine] Alikuwa   (صلى الله عليه وآله وسلم)akikataza kuchutama kama Shaytwaan.([5])

 

Na alikuwa  (صلى الله عليه وآله وسلم)anapokaa katika tashahhud huweka kiganja chake cha mkono wa kulia juu ya paja [katika usimulizi mwingine: goti] la kulia, na huweka kiganja chake cha kushoto katika paja [katika usimulizi mwengine: goti] la kushoto([6]). Na alikuwa  (صلى الله عليه وآله وسلم)akiweka  kisugudi cha mkono wake wa kulia katika paja lake la kulia.([7])

 

Pia  (صلى الله عليه وآله وسلم)alimkataza mtu aliyekaa katika Swalah hali ya kuwa anautegemea mkono wake wa kushoto akamwambia: ((Hakika hiyo ni Swalah ya Mayahudi))([8]). Na katika kauli nyingine: ((Usikae hivi, kwani hakika hiki ni kikao cha wale wanaoadhibiwa))([9]). Katika Hadiyth nyingine: ((Ni kitako cha wale walioghadhibikiwa [Na Allaah]))([10]).

 

 





[1] An-Nasaaiy(1/173) ikiwa na isnaad Swahiyh. "Muftarishan" ni kukalia tumbo la mguu wa kushoto na kuusimamisha unyayo wa mguu wa kulia kama ilivyotangulia.

[2] Al-Bukhaariy na Abu Daawuud.

[3] Abu Daawuud na Al-Bayhaqiy ikiwa na isnaad nzuri.

[4] Atw-Twayaalisiy, Ahmad na Ibn Abi Shaybah. Kuhusu "iq'aa", Abu 'Ubaydah na wengineo wamesema: "Ni mtu anapogandamiza kikalio chake ardhini, akiweka muundi wake wima, na kuegemeza mikono yake ardhini kama mbwa anavyofanya". Hii ni tofauti na "iq'aa" baina ya Sajdah ambayo imekubaliwa katika Sunnah kama ilivyotangulia kabla.

[5] Muslim, Abu 'Awaanah na wengineo. Imetolewa katika Al-Irwaa (316).

[6] Muslim na Abu 'Awaanah.

[7]Abu Daawuud na An-Nasaaiy ikiwa na isnaad Swahiyh. Inayokusudiwa ni kwamba hakutenganisha viwiko vyake na ubavu wake kama alivyofafanua Ibn Al-Qayyim katika Zaad Al-Ma'aad.

[8]Al-Bayhaqiy na Al-Haakim ambaye amekiri ni Swahiyh, na Adh-Dhahabiy amekubali. Imetolewa pamoja inayofuatia katika Al-Irwaa (380).

[9] Ahmad na Abu Daawuud ikiwa na isnaad nzuri.

[10] 'Abdur-Razaaq; 'Abdul-Haqq amekiri ni Swahiyh katika Ahkaam yake (Namba 1284 katika utafiti wangu).

Share