044-Sifa Ya Swalah Ya Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam): Kutikisa Kidole Kwenye Tashahhud

 

KUTIKISA KIDOLE KATIKA TASHAHHUD

 

Alikuwa  (صلى الله عليه وآله وسلم)akitandaza kiganja chake cha mkono wa kushoto juu ya goti la mkono wa kushoto, na akikunja vidole vyake vya mkono wa kulia vyote, huku akiashiria kinachofuatia kidole cha gumba -kidole cha Shahada- upande wa Qiblah huku akikitupia jicho lake.[1]

 

Na alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) anapoashiria kwa kidole chake, huweka kidole cha gumba juu ya kidole cha kati([2]),  na mara nyingine alikuwa akifanya duara kwa hivyo viwili.([3])

 

Alikuwa   (صلى الله عليه وآله وسلم) - anaponyanyua kidole chake - akikitikisa (huku) akiomba du'aa nacho([4]) akisema: ((Hakika kina nguvu zaidi kuliko chuma dhidi ya Shaytwaan)), akimaanisha kidole cha shahada.))([5]) 

 

 

Pia, Maswahaba wa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) walikuwa wakikumbushana baina yao, yaani, kuhusu kuashiria kwa kidole wakati wa kuomba du'aa.([6])

 

Na alikuwa   (صلى الله عليه وآله وسلم)akifanya hivyo katika tashahhud zote mbili.([7])

 

Wakati mmoja, alimuona mtu akiomba du'aa kwa vidole vyake viwili akasema: ((Pwekesha (Kimoja, [kimoja])) na akaashiria kidole chake cha shahada.([8])

 

 

 

 

[1] Muslim, Abu 'Awaanah na Ibn Khuzaymah. Al-Humaydiy (13/1) na Abu Ya'laa (275/2) wameongeza katika isnaad Swahiyh kutoka kwa Ibn 'Umar, ((Na hii ni kumdunga Shaytwaan, hakuna atakayesahau akifanya hivi)). Na Al-Humaydiy alinyosha kidole chake. Al-Humaydiy pia alisema kwamba Muslim bin Abi Maryam amesema: "Mtu alisimulia Hadiyth kwangu katika kanisa la Syria, aliona Surah za Mitume wakiwa katika taswira kama hiii", na Al-Humaydiy akanyosha kidole chake. Hii ni kauli ya ajabu lakini sanad yake hadi kwa 'huyo mtu' ni Swahiyh.

[2] Muslim na Abu 'Awaanah.

[3]Abu Daawuud, An-Nasaaiy, Ibn Al-Jaruud katika Al-Muntaqaa (208), Ibn Khuzaymah (1/86/1-2) na Ibn Hibbaan katika Swahiyh yake (485) ikiwa na isnaad Swahiyh. Ibn Al-Mulaqqin amekiri ni Swahiyh (28/2), na inayo usimulizi madhubuti kutoka kwa Ibn 'Addiy (287/1).

[4] Kifungu kile kile kilichotajwa hapo mbeleni. Kuhusu 'kuomba du'aa nacho', Imaam Atw-Twahaawiy amesema: "Hii ni dalili kwamba ilikuwa ni mwisho wa Swalah". Hivyo kuna dalili kwamba Sunnah ni kuendelea kukielekeza na kukitikisa hadi katika Tasliym, kwani du'aa huwa hadi hapo. Hii ni rai ya Maalik na wengineo. Imaam Ahmad aliulizwa: "Je mtu akitikise kidole chake katika Swalah"? Akajibu: "Ndio, kwa nguvu" (Imetajwa na Ibn Haaniy katika Masaail yake Imaam Ahmad 1/80). Kutokana na hii, ni dhahiri kwamba kutikisa kidole ni Sunnah iliyothibiti ya Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) na ni desturi ya Ahmad na Maimamu wengineo wa Sunnah. Kwa hiyo wale wanaodhani kwamba hakuna maana na haipasi wala haihusu  katika Swalah, wamche Allaah, kwani kwa sababu hii hawatikisi vidole vyao ingawa wanajua kuwa imethibiti katika Sunnah; na wanajitahidi kufasiri kwa njia isiyo mantiki na isiyolingana na ufasaha wa Kiarabu  na kinyume cha ufahamu wa Imaam kuhusu hii.

 

Jambo la ajabu ni kwamba wengine watamtetea Imaam katika mas-ala mengine, japo kama rai yake inapingana na Sunnah, kwa hoja kwamba kudhihirisha makosa ya Imaam ina maana ni kufanya dhihaka na kumdharau. Kisha wanasahau hii na kukanusha Sunnah hii iliyothibiti na huku wakifanya istihzai kwa wanaoitekeleza. Ikiwa wanatambua au hawatambui, istihzai zao pia zinajumuisha wale Maimaam ambao kwa kawaida yao wanawatetea kwa yaliyo batili, na ambao wako sahihi katika Sunnah mara hii! Bali wanambeza Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) mwenyewe, kwani yeye ndiye aliyetuletea Sunnah hii. Kwa hiyo kuifanyia mzaha ni sawa na kumfanyia yeye ((...فَمَا جَزَاء مَن يَفْعَلُ ذَلِكَ مِنكُمْ إِلاَّ)) ((Basi hana malipo mwenye kutenda hayo miongoni mwenu ila….)) [Al-Baqarah: 85]

 

Ama kukiweka kidole chini baada ya kukielekeza, au kupunguza kutikisa na kukithibitisha (katika kusema 'Laa ilaaha [Hakuna apasaye kuabudiwa kwa haki…) na kukanusha (kusema 'illa-Allaahu ...' [isipokuwa Allaah']) vyote hivi hakuna asili katika Sunnah; bali ni kinyume na Sunnah, kama Hadiyth hii inavyothibitisha.

 

Juu ya hivyo, Hadiyth ambayo inasema hakutikisa kidole chake haina isnaad Swahiyh, kama nilivyoelezea katika Dhwa'iyf Abu Daawuud (175). Hata kama ingelikuwa ni Swahiyh, inakanusha na Hadiyth ya juu inathibitisha. Uthibitisho unapewa kipaumbele juu ya ukanushaji kama inavyojulikana kwa Maulamaa.

 

[5] Ahmad, Al-Bazzaar, Abu Ja'far, Al-Bukhtiriy katika Al-Amaail (60/1), 'Abdul-Ghaniy Al-Maqdisiy katika Sunan yake (12/2) ikiwa na isnaad nzuri, Ar-Ruuyaaniy katika musnad yake (249/2) na Al-Bayhaqiy.

[6] Ibn Abi Shaybah (2/123/2) ikiwa na isnaad nzuri.

[7] An-Nasaaiy na Al-Bayhaqiy ikiwa na isnaad Swahiyh.

[8] Ibn Abi Shaybah (12/40/1, 2/123/2) na An-Nasaaiy. Al-Haakim amekiri ni Swahiyh, na Adh-Dhahabiy amekubali. Kuna usimulizi unaotilia nguvu kutoka kwa Ibn Abi Shaybah.

Share