Mashairi: Neema Za Allaah Hazihesabiki

Neema Za Allaah Hazihesabiki

 

‘Abdallah Bin Eifan(Rahimahu-Allaah)

Alhidaaya.com

 

 

Salaam kwa marafiki, kwa ndugu na majirani,
Ninaomba tawfiki, na radhi za Muhisani,
Azidi kutubariki, viumbe bara na pwani,

Neema za Rahmani, katu hazihesabiki.

 

 

 

Katu hazihesabiki, neema za Rahmani,*

Yote tunayomiliki, tumepewa na Manani,

Hutugawia riziki, kutoka Kwake mbinguni,**

Neema za Rahmani, katu hazihesabiki.

 

 

 

Wanyama, ndege, samaki, pakavu na baharini,

Vidudu kwenye handaki, nyoka na mamba mitoni,

Huruzukiwa kwa haki, ni viumbe ardhini,

Neema za Rahmani, katu hazihesabiki.

 

 

 

Protestanti, Katoliki, hata yule Baniyani,

Riziki haikatiki, hata kwa Makadiyani,

Kiumbe hadhulumiki, Mungu (Allaah) sio Athumani,

Neema za Rahmani, katu hazihesabiki.

 

 

 

Ndugu usione dhiki, neema uzithamini,

Mkizitaka zibaki, kamba ya Mungu (Allaah) shikeni,

Maasi ndio halaki, hukuporomosha chini,

Neema za Rahmani, katu hazihesabiki.

 

 

 

Mola wetu Haridhiki, na ufisadi nchini,

Binadamu hukumbuki, Alokuumba ni nani?

Sasa kwa nini hutaki, kukumbuka ihsani?

Neema za Rahmani, katu hazihesabiki.

 

 

 

Kwake Yeye kashtaki, kama upo matatani,

Kama Kujibu Hataki, subiri ni mtihani,

Usifanye kuhamaki, akughilibu shetani,

Neema za Rahmani, katu hazihesabiki.

 

 

 

Wazazi walikulaki, ulipotoka tumboni,

Walisambaza makeki, na vitamu mitaani,

Hayuko aliebaki, watu wote furahani,

Neema za Rahmani, katu hazihesabiki.

 

 

 

Umeumbika vizuri, kwa umbo zuri yakini,***

Kila kilicho kizuri, Amekiumba mwilini,

Hautakuta dosari, jichunguze kwa makini,

Neema za Rahmani, katu hazihesabiki.

 

 

 

Amekufanya tayari, kuingia maishani,

Kaa ukitafakari, mwanzo ulikua nini?

Alikuumba Qahari, ulitoka udongoni,

Neema za Rahmani, katu hazihesabiki.

 

 

 

Inapokufika shari, tazama sababu gani,

Ukae ujishauri, ulifanya dhambi gani?

Ikiwa wewe hodari, utajua jibu gani,

Neema za Rahmani, katu hazihesabiki.

 

 

 

Hakika utasubiri, ikiwa ni Muumini,

Shari hugeuka kheri, dua nyingi ziombeni,

Utamkuta Jabbari, Anawaitikieni,

Neema za Rahmani, katu hazihesabiki.

 

 

 

Na tupo kwenye safari, mwisho wake kaburini,

Sana tujitahadhari, mwisho kutakua nini,

Tuwekwe kwenye tanuri, au kwenye bustani !

Neema za Rahmani, katu hazihesabiki.

 

 

 

Hapa nafunga shairi, nimefika kikomoni,

Tutoke kwenye hatari, ibada zingatieni,

Tufe na sisi bukheri, Radhi Zake tafuteni,

Neema za Rahmani, katu hazihesabiki.

 

 

 

*An-Nahl: 18

 

 

وَإِن تَعُدُّوا نِعْمَةَ اللَّـهِ لَا تُحْصُوهَا ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَغَفُورٌ رَّحِيمٌ﴿١٨﴾

18. Na mkihesabu neema za Allaah hamtoweza kuziorodhesha hesabuni. Hakika Allaah bila shaka ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu.

 

 

 

** Adh-Dhaariyaat: 22  

 

 

وَفِي السَّمَاءِ رِزْقُكُمْ وَمَا تُوعَدُونَ﴿٢٢﴾

22. Na katika mbingu kuna riziki yenu na yale mnayoahidiwa.

 

 

 

***At-Tiyn: 4   

 

لَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ فِي أَحْسَنِ تَقْوِيمٍ ﴿٤﴾

4. Kwa yakini Tumemuumba mwana Aadam katika umbile bora kabisa.

 

 

 

Share