Zingatio: Subira Katika Qudra za Allaah

 

Zingatio: Subira Katika Qudra Za Allaah

 

Naaswir Haamid

 

 

Alhidaaya.com

 

 

Wema kwa Muislamu sio tu kuswali, bali ni kuziamini nguzo zote sita za iymaan kwa ukamilifu wake. Iymaan hii yaenda sambamba kwa kuzifanyia kazi nguzo hizo. Miongoni mwa nguzo za iymaan ni kuamini kwamba Allaah Amekwishakadiria khayr na shari zote.

 

Ni katika mipango ya Muumba kuhakikisha kwamba Yeye Ndiye Mwenye elimu na ujuzi usioweza kulinganishwa na kiumbe chochote. Amesema: 

إِنَّا كُلَّ شَيْءٍ خَلَقْنَاهُ بِقَدَرٍ ﴿٤٩﴾

Hakika sisi Tumekiumba kila kitu kwa Qadar (majaaliwa). [Al-Qamar: 49]

 

Iymaan ya qadar ni lazima ieleweke kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anatambua kila kitu kwa ujumla na umoja wake, yaliyopita na yaliyopo sasa hivi. Ni sawa kwamba hayo matendo yanatokana na mipango Yake Muumba ama mwanadamu. Kwa mfano Yeye Muumba Anaelewa kuwa mwanadamu kadhaa atafanya bidii ya kuvumbua formula fulani ya hesabu, pia Anatambua kwamba siku kadhaa mzazi wa fulani ataaga dunia.

 

Hakuna haja ya kuwa na huzuni yenye kuchupa mpaka kwa yale yanayomkuta Muislamu. Kwani kila kitu kimekwishapangwa katika Lawhul-Mahfuudh. Hii ni sehemu ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ameweka kumbukumbu ya yote yatakayotokezea ulimwenguni. Hata hichi unachokisoma kimekwishakadiriwa! Kama msiba ndugu yangu umekwisha, subiri upate malipo makubwa kwa Allaah. Iwapo umekosa nafasi ya kazi, ndoa, masomo na mfano wa hayo; hiyo ni kudra ya Mola wala hakuna wa kuyatengeneza yaliyopita. Hayo yamekwishapita wala hatuna mkono wa kuyarekebisha. Allaah Anasema ndani ya Kitabu Chake: 

أَلَمْ تَعْلَمْ أَنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ ۗ إِنَّ ذَٰلِكَ فِي كِتَابٍ ۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ ﴿٧٠﴾ 

Je, hujui kwamba Allaah Anajua yale yote yaliyomo katika mbingu na ardhi? Hakika hayo yamo katika Kitabu. Hakika hayo kwa Allaah ni mepesi. [Al-Hajj: 70]

 

Hakuna haja ya kujitia dhiki ya moyo kwa matatizo yaliyokukumba. Huo ni mtihani na kuipata kwetu Jannah kunaambatana na kushikamana na subira katika qadari za Allaah zenye kuumiza. Kama dhiki basi hakuna wanaoipata dhiki hivi sasa kuliko ndugu zetu waliopo Palestina. Allaah Awatunukie hadhi ya kuwa ni mashaahid siku ya Qiyaamah. Aamiyn!

 

Katika Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Ameandika Allaah makadirio ya viumbe kabla ya kuumba mbingu na ardhi kwa miaka hamsini alfu.” [Imepokewa na Muslim, ameisimulia 'Amru bin 'Aasw]

 

Sasa ni kipi cha kujiumiza iwapo unatambua kwamba ni kale wa kale Allaah Amekwishakukadiria raha na shida zako ulimwenguni? Miaka hamsini alfu kabla ya kuumbwa mbingu na ardhi, sio kabla ya kuumbwa wewe na mimi!

 

Tutambue pia kwamba hakuna kinachokuwa isipokuwa kile Alichokikadiria Muumba. Hivyo, haifai kwa Muislamu kusema kwamba "laiti ningefanya hivi au kadhaa wa kadhaa… ingelikuwa hivi", kwani kalimah ya 'lau/inge' inamfungulia mlango Shaytwaan. Naye Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametufunza kuachana na fikra potofu kama hizo na ametufundisha mwenendo maalumu wa kushikamana nao Muislamu pale anapokutana na misukoko:

 

Amesema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

Muumini mwenye nguvu ni bora na anapendeza zaidi kwa Allaah kuliko Muumini dhaifu, na wote wana khayr. Fanya pupa kwa kile kitakachokunufaisha na taka msaada kwa Allaah wala usichoke, na kikikupata kitu chochote kibaya basi usiseme “lau” kama ningefanya kadhaa na kadhaa  yasingenitokea haya, lakini sema: 

 

Amepanga Allaah na Analolitaka Anafanya”

 

...hakika neno la “lau” linafungua matendo ya Shaytwaan’

Hakika Allaah Analaumu mwenye kukata tamaa, lakini usivunjike moyo na ukishindwa na jambo kabisa sema:

 

“Allaah Ananitosheleza, naye ni Mbora wa kutegemewa.”

 

Ee Allaah hakika sisi tunajilinda kwako kutokana na hamu na huzuni na uvivu na ubakhili na uoga na uzito wa deni na kushindwa na watu.

 

 

Share