Mashairi: Umuhimu Wa Swalah

Umuhimu Wa Swalah

‘Abdallaah Bin Eifan,

(Jeddah, Saudi Arabia)

(1)   Bismillahi  naanza, salaam kwa ikhwani,
           nalifungua  baraza, nitowe yangu maoni,
           tupate kulisambaza, liende kila makani,
           Swalah Ni Nguzo Muhimu, Msingi Wa Dini Yetu.

(2)   Sote sasa tunajuwa, Mtume kwenda mbinguni,
          usiku kachukuliwa, Makkah msikitini,
          safari hakuchelewa, alirudi ardhini,
          Swalah Ni Nguzo Muhimu, Msingi Wa Dini Yetu.

(3)    Mitume wakaswalishwa, Al-Aqsa tunaamini,
           halafu kaondolewa, akapazishwa angani,
           mbinguni kapokelewa, kwa heshima ya mgeni,
           Swalah Ni Nguzo Muhimu, Msingi Wa Dini Yetu

(4)     Mengi alieyaona, kwa ushahidi machoni,
           kwa marefu na mapana, kayaona kwa yakini,
           kaitwa na Subhana, kuzungumza kileleni,
           Swalah Ni Nguzo Muhimu, Msingi Wa Dini Yetu.

(5)    Kaitwa kupewa amri, Swalah ziwe khamsini,
          Musa akamshauri, arudi kwa Rahmani,
          zikapunguzwa nambari, Swalah tano sio duni,
          Swalah Ni Nguzo Muhimu, Msingi Wa Dini Yetu.

(6)   Swalah tano ndio nguzo, muhimu katika dini,
          hizo hazina mchezo, wala hazina utani,
          ukipunguza kigezo, hakuna cha samahani,
          Swalah Ni Nguzo Muhimu, Msingi Wa Dini Yetu

(7)    Swalah tano kila siku, tuziswali kwa makini,
          kusujudu, kurukuu, tuzifanye kwa imani,
          bila kufanya makuu, kila kitu wastani,
          Swalah Ni Nguzo Muhimu, Msingi Wa Dini Yetu.

(8)    Akhera kitu cha kwanza, huulizwa muumini,
          kama amezitimiza, Swalah tano kwa mizani,
          na kama amepunguza, sunnah ziwe hisabuni,
          Swalah Ni Nguzo Muhimu, Msingi Wa Dini Yetu.

(9)   Swalah jama'ah ni bora, bora kuliko nyumbani,
          Watu wakupe hongera, ukiswali hadharani,
          au waimbe ngonjera, ukifeli mtihani,
          Swalah Ni Nguzo Muhimu, Msingi Wa Dini Yetu.

(10)  Binadamu kurupuka, pale anapoadhini,
          fanya uende haraka, uwe mbele ya foleni,
          kuwa mbele ni baraka, ni safu yenye thamani,
          Swalah Ni Nguzo Muhimu, Msingi Wa Dini Yetu.

(11)   Lazima kunyenyekea, swali kwa matumaini,
          makinika na tulia, utulivu wa mwilini,
          Swalah kuiizingatia, kwa utulivu moyoni,
          Swalah Ni Nguzo Muhimu, Msingi Wa Dini Yetu

(12)   Swali bila wasiwasi, tahadhari na shetani,
           usimwachie nafasi, apenyeze akilini,
           usiihusishe nafsi, na mambo ya duniani,
           Swalah Ni Nguzo Muhimu, Msingi Wa Dini Yetu.

(13)   Kwenye sijda ukifika, kwa Mungu sana ombeni,
          Yupo karibu Rabuka, hapo dua zisomeni,
          dua zenu zitafika, kwa haraka kwa Manani,
          Swalah Ni Nguzo Muhimu, Msingi Wa Dini Yetu.

(14)   Ukishatoa salaamu, utulie hapo chini,
          uzitimize timamu, dhikri zote mwishoni,
          Fuata nyayo za Imamu, ni Mtume Muhisani,
          Swalah Ni Nguzo Muhimu, Msingi Wa Dini Yetu.

(15)   Bila Swalah ndugu zangu, mtakuwa mashakani,
          Bila Swalah walimwengu, vyote havina thamani,
          Vitendo vyote kwa Mungu, Swalah Kaweka mbeleni,
          Swalah Ni Nguzo Muhimu, Msingi Wa Dini Yetu.

(16)   Ujuwe unakufuru, Swalah kutupa pembeni,
          mwenyewe utajidhuru, utakufa masikini,
          nani atakunusuru, ukiingia motoni?
          Swalah Ni Nguzo Muhimu, Msingi Wa Dini Yetu.

(17)  Mziswali kwa wakati, msichelewe jamani,
          nawaombea umati, salaama-u-salimini,
          na hapa ndio tamati, nawaaga kwaherini,
          SWALAH NI NGUZO MUHIMU, MSINGI WA DINI YETU.

Share