Mashairi: Unapopata Mitihani Subiri

          Unapopata Mitihani Subiri

             ‘Abdallaah Bin Eifan (Rahimahu-Allaah)

          

 

Salaam waheshimiwa, nawaombea baraka,
Tunaomba kujaliwa, kila kheri na fanaka,
Tupate kuondolewa, mitihani na mashaka,
Mtihani Ukifika,
Subira Inatakiwa.

 

Subira inatakiwa, mtihani ukifika,

Utajiri ukinyimwa, halafu ukasumbuka,
Usidhani umetupwa, Kakusahau Rabuka,
Mtihani Ukifika,
Subira Inatakiwa.

 

Na mitihani mikubwa, kama inamiminika,
Tumshukuru MKUBWA, subira hulazimika,
Tuzidi kuomba duwa, hapana kulalamika,

Mtihani Ukifika, Subira Inatakiwa.

 

Msiba unapokuwa, dhaifu hutetemeka,
Kama mwehu anakuwa, imani inamtoka,
Anasahau ya kuwa, Mungu hivyo Ametaka,

Mtihani Ukifika, Subira Inatakiwa.

 

Na makelele kupigwa, maafa yakimfika,
Na yote yamekatazwa, Mungu Anaghadhibika,
Apenda  Kushukuriwa, Mola wetu Mtukuka,

Mtihani Ukifika, Subira Inatakiwa.

 

Kuvumilia ni sawa, na imani kuiweka,
Hadhulumiwi muumbwa, kwa haki kinatendeka,
Hakuna cha kuonewa, imani ya nguvu shika,

Mtihani Ukifika, Subira Inatakiwa.

 

Yote yamesajiliwa, Mungu Ameshaandika,
Kalamu kuinuliwa, wino umeshakauka,
Mitihani ukikumbwa, hakuna kubadilika,

Mtihani Ukifika, Subira Inatakiwa.

 

 

Tangu bado kuzaliwa, vyote vimeandikika,

Riziki imegawiwa, na ajali kadhalika,

Yote hayo majaliwa, hapana kunung’unika,

Mtihani Ukifika, Subira Inatakiwa.

 

Usikubali kushindwa, shetani akakuteka,
Utageuka mfungwa, wa shetani ni mateka,
Hapo umeshaangushwa, na imani kutoweka,

Mtihani Ukifika, Subira Inatakiwa.

 

Hapa nafunga baruwa, pengine mmeshachoka,
Tunaomba maridhawa, Mola Apate Ridhika,
Tunaomba kuepushwa, na madhambi kufutika,

Mtihani Ukifika, Subira Inatakiwa.

 

 

 

Share