Mashairi 6: Ramadhani Inakwisha, Mola Tusamehe Dhambi.

Mashairi 6:  Ramadhani Inakwisha, Mola Tusamehe Dhambi.

      ‘Abdallah Bin Eifan (Rahimahu-Allaah)

 Alhidaaya.com

Salaam napiga hodi, hebu nipe karatasi,

Usichelewe uledi, unitowe wasiwasi,

Nimeshaweka ahadi, sitoweza kuiasi,

Ramadhani Inakwisha, Mola Tusamehe Dhambi.

Tumefunga kwa salama, Tumshukuru Mkwasi,

Zikubali zetu mema, tuingize Ferdausi,

Dumisha Yako neema, tuwe mbali na maasi,

Ramadhani Inakwisha, Mola Tusamehe Dhambi.

Toa Zakaat-ul-Fitri, chakula kwa mafakiri,

Ngano, mchele, ni nzuri, kutoa uwe tayari,

Iwe tohara dhahiri, na saumu kunawiri,

Ramadhani Inakwisha, Mola Tusamehe Dhambi.

Tupite lango”Rayani,” kuelekea peponi,

Afungae Ramadhani, atapita mlangoni,

Malaika Radhwani, atukaribishe ndani,

Ramadhani Inakwisha, Mola Tusamehe Dhambi.

Unatuondoka mwezi, utatutia majonzi,

Tutapatwa na simanzi, anaondoka mpenzi,

Tumeacha usingizi, mwezi huu kuuenzi,

Ramadhani Inakwisha, Mola Tusamehe Dhambi.

Inshallaah tuswali Idi, tukusanyike kikundi,

Nguo mpya maridadi, tujifukize na udi,

Tumshukuru Wadudi, sana bila ya idadi,

Ramadhani Inakwisha, Mola Tusamehe Dhambi.

Tusibaki majumbani, sote tuwe uwanjani,

Waume na wanandani, pamoja tukutaneni,

Tunapokwenda njiani, takbira mdomoni,

Ramadhani Inakwisha, Mola Tusamehe Dhambi.

Ni sunna kidogo kula, kabla kwenda kuswali,

Waamshe waliolala, waswali hata vigoli,

Tukamshukuru Mola, Azikubali amali,

Ramadhani Inakwisha, Mola Tusamehe Dhambi.

Nawapa wote hongera, wa pwani hata wa bara,

Waumini wa Tabora, hadi kufika Mtwara,

Hongera na Ifakara, na ndugu wote Kagera,

Ramadhani Inakwisha, Mola Tusamehe Dhambi.

Hongera wa Morogoro, na kule Kilimanjaro,

Hongera wa Mvomero, Kidodi na Kilombero,

Pasiwepo na kasoro, hongera na wa Comoro,

Ramadhani Inakwisha, Mola Tusamehe Dhambi.

Hongera ndugu Dodoma, pamoja na Mzizima,

Sikusahau Musoma, na Waumini Kigoma,

Waume na kina mama, nawatakia uzima,

Ramadhani Inakwisha, Mola Tusamehe Dhambi.

Hongera ndugu Iringa, na Waumini wa Tanga,

Sikusahau Shinyanga, msiseme ninaringa,

Na Mola Atawakinga, muepuke kila janga,

Ramadhani Inakwisha, Mola Tusamehe Dhambi.

Hongera ndugu wa Pemba, twajuana kwa vilemba,

Mimi kwetu ni Kimamba, nitakwenda kuupamba,

Tulimiliki mashamba, na biashara sembamba,

Ramadhani Inakwisha, Mola Tusamehe Dhambi

Hongera ninazirusha, ziwafikie Arusha,

Mola Atawaepusha, kila baya kukomesha,

Yawe mazuri maisha, hakuna cha kuwatisha,

Ramadhani Inakwisha, Mola Tusamehe Dhambi.

Moshi, Mwanza na Rufiji, Bukoba hadi Ujiji,

Yawafikie faraji, Mola Ndiye Mlipaji,

Atimize mahitaji, asibaki muhitaji,

Ramadhani Inakwisha, Mola Tusamehe Dhambi

Bagamoyo na Kilosa, na ndugu zetu Mombasa,

Mola Atawatakasa, na madhambi Kupangusa,

Tupigwe sote msasa, tufutwe dhambi kabisa, 

Ramadhani Inakwisha, Mola Tusamehe Dhambi.

Waumini wa Unguja, na wa Lamu kwa pamoja,

Mola Awavike koja, Awapandishe daraja,

Inshaallah siku moja, kutembea nitakuja,

Ramadhani Inakwisha, Mola Tusamehe Dhambi.

Ndugu Kenya, Tanzania, na Uganda kadhalika,

Hongera nawatumia, mkono Iddi Mbaraka,

Popote kwenye dunia, Mola Atawamulika,

Ramadhani Inakwisha, Mola Tusamehe Dhambi.

Tovuti ya Alhidaaya, izidi kutunawiri,

Nawaombea hidaya, baraka na kila kheri,

Muepushwe na mabaya, yawafikie mazuri,

Ramadhani Inakwisha, Mola Tusamehe Dhambi.

Nakimbilia futari, uji sasa unapoa,

Mama watoto tayari, yupo ananingojea,

Tutaonana kwa kheri, Mola Akitujalia,

Ramadhani Inakwisha, Mola Tusamehe Dhambi.

Share