Mashairi: Gaza - Viumbe Vyako Jalali

 

                     Abdallah Bin Eifan

                  (Jeddah, Saudi Arabia)

 

 

Salaamu nawatumia, wa karibu na wa mbali,

Gaza wanaangamia, Allaah Atawakafili,

Waarabu wangetumia, silaha ya petroli,

Viumbe Vyako Jalali, wanazidi kuumia.

 

Wanazidi kuumia, viumbe Vyako Jalali,

Adui kawakamia, hasikii na hajali,

Gaza inadidimia, wanakufa kikatili,

Viumbe Vyako Jalali, wanazidi kuumia.

 

Tazama wanavyolia, ni chini ya matofali,

Watoto wameumia, kilema cha wakabili,

Maisha watabakia, na adhabu kwenye mwili,

Viumbe Vyako Jalali, wanazidi kuumia.

 

Adui hana sheria, Wazeyuni Israeli,

Yupo hapo Kibandia, eti ndio serekali,

Na ardhi anaibia, huyu adui tapeli,

Viumbe Vyako Jalali, wanazidi kuumia.

 

Silaha anatumia, silaha zilizo kali,

Anapingwa na dunia, kelele kila mahali,

Hataki kuyasikia, na kutumia akili,

Viumbe Vyako Jalali, wanazidi kuumia.

 

Haachi yake tabia, na chuki zake jahili,

Waliua Manabia, zile zama za awali,

Jihadi ndio ni njia, ya kupambana na nduli,

Viumbe Vyako Jalali, wanazidi kuumia.

 

Kitu kilichobakia, tuombe tunaposwali,

Na Allaah kumlilia, Anajua yetu hali,

Apate Kutujalia, na dua Kuzikubali,

Viumbe Vyako Jalali, wanazidi kuumia.

 

Sasa tunashuhudia, tunaziona dalili,

Madhambi yamezidia, tazama kila pahali,

Wakati wa kutubia, sasa umeshawasili,

Viumbe Vyako Jalali, wanazidi kuumia.

 

Tusafishe yetu nia, tufanye mambo halali,

Na dini kuzingatia, na tabia kubadili,

Haramu kuikimbia, kuwa nae mbalimbali,

Viumbe Vyako Jalali, wanazidi kuumia.

 

Beti Kumi naishia, hata usiku silali,

Uchungu umezidia, uzito kama jabali,

Watu wanasubiria, jihadi wakasajili,

Viumbe Vyako Jalali, wanazidi kuumia.

 

 

Share