Mashairi: Omba Toba Kwa Haraka, Madhambi Unapotenda

Omba Toba Kwa Haraka, Madhambi Unapotenda

         ‘Abdallaah Bin Eifan (Rahimahu Allaah)
     
Alhidaaya.com

Salaam zangu natuma, ziwafike Afrika,

Mola Awape hekima, mzidi kuneemeka,

Naomba Zake rehema, zivuke zote mipaka,

Omba Toba kwa haraka, madhambi unapotenda.

Madhambi unapotenda, omba toba kwa haraka,

Mola sana Anapenda, Aombwe kila dakika,

Hujuwi unapokwenda, lini roho itatoka,

Omba Toba kwa haraka, madhambi unapotenda.

Yupo macho Maulana, Halali na Kuzeeka,

Kila kitu Anaona, yote yanayotendeka,

Si usiku si mchana, Yupo macho Mtukuka,

Omba Toba kwa haraka, madhambi unapotenda.

Yupo karibu na sisi, dua Kwake zinafika,

Ili zifike upesi, tuzidi Kumkumbuka,

Tuache yote maasi, ili Apate ridhika,

Omba Toba kwa haraka, madhambi unapotenda.

Wakati unatoroka, tupo kwenye hekaheka,

Mauti yatatufika, ghafla tutaanguka,

Hapo tunapodondoka, toba imeshafungika,

Omba Toba kwa haraka, madhambi unapotenda.

Shetani yupo mbioni, humuoni akichoka,

Hutupambia machoni, baya sawa huliweka,

Atutie mtegoni, halafu anatucheka,

Omba Toba kwa haraka, madhambi unapotenda.

Alipokua peponi, Adamu kahadaika,

Kadanganywa na shetani, balaa ikamfika,

Akatubu Kwa Manani, mwishowe akaokoka,

Omba Toba kwa haraka, madhambi unapotenda.

Kuomba toba ni nzuri, kosa linapofanyika,

Unajiweka tayari, ajali inapofika,

Kumbuka mbele kaburi, na moto usozimika,

Omba Toba kwa haraka, madhambi unapotenda.

Omba toba kila mara, huku ukisikitika,

Omba sana maghfira, toa kidogo sadaka,

Kumbuka sana akhera, na siku ya kufufuka,

Omba Toba kwa haraka, madhambi unapotenda.

Mola Atupe uzima, hapa mwisho kuandika,

Atupe nguvu na hima, radhi Zake tunataka,

Atupe nzuri hatima, na madhambi kufutika,

Omba Toba kwa haraka, madhambi unapotenda.

Share