Wanawake Wanayopasa Kufanya Wakati Wa Jeneza Linapotoka

 

Wanawake Wanayopasa Kufanya Wakati Wa Jeneza Linapotoka

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI: 

 

Assalamu Aleikum natoa shukurani nyingi kwa ALLAAH pia nawatakia kilala kheri namafanikio mema ndugu zangu kwa iman ALHIDAAYA ALLAAH atawalipa In shaa Allaah.

BISMILLAH: suali yangu jee mtu akienda kilioni kuzika kwa upande wa kina mama sasa jeneza ikitoka jee wasimame ama wakae pia hao wakina mama wanakua wakizungumza mara nyingi jee wanyamaze? Naomba jibu mapema ili waelimike waislam

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Ni Sunnah kwa watu kulipa jeneza linalopita heshima zao za mwisho kwa kunyanyuka hata kama si la Muislamu. Hii ni kwa mujibu alivyofanya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). "Wakati mmoja alikuwa ameketi mara likapita jeneza naye akasimama. Wakamwambia kuwa hilo lilikuwa ni jeneza la Myahudi. Hapo aliwajibu: “Je, yeye si mwanaadamu?" [al-Bukhaariy].

 

 

Swahaba zake (Radhwiya Allaahu ‘anhum) walifuata Sunnah hiyo. Wakiwa al-Qaadisiyah, Sahl bin Hanif na Qays bin Sa‘ad (Radhwiya Allaahu ‘Anhumaa) wakiwa wameketi, lilipita jeneza mbele yao. "Nao wakasimama papo hapo, watu waliokuwepo walikataa kwa kusema: “Hawa ni watu wa kawaida tu”, wakimaanisha dhimmi (wasiokuwa Waislamu katika dola ya Kiislamu). Swahaba hawa wawili walijibu: “Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisimama jeneza lilipopita mbele yake, na watu waliposema kuwa ni jeneza la Myahudi, alisema: "Je, yeye si mwanaadamu?" [al-Bukhaariy].

 

 

Ama wakina mama wakiwa wapo katika nyumba ya wafiwa haifai kwao kuanza kuzungumza mambo mengine kama ilivyokuwa ada. Huo ni wakati wa kuzingatia kuwa leo unakwenda kumzika mwenzio na kesho inaweza kuwa ni wewe. Kifo ni mazingatio makubwa kwa walio hai, hivyo inatakiwa watumie fursa hiyo ya kuzingatia hilo na sio kupiga soga. Ili kuondosha shughuli hiyo isiyo njema ya wao kuzungumza ovyo ni muhimu kuwe na ukumbusho wa kuwakumbusha watu kuhusu mauti na matayarisho yao kwa safari ambayo anayekwenda harudi tena.

 

 

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Atuepushe na kwenda kinyume na Sunnah za Nabiy(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Atufanye ni wenye kujikita katika Sunnah zake.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share