Kusamehewa Madhambi Baada Ya Tawbah

Kusamehewa Madhambi Baada Ya Tawbah

 

Alhidaaya.com

 

 

Swali:

 

 

Asalaam alaykum

 

Swali langu ni kwamba, eti Allaah anasamehe dhambi zote kama mtu akitubu, (na dhambi kama kuua) Allaah azidi kutuongoza

 

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho. 

 

 

Muislamu anaweza kusamehewa madhambi yote yanayohusiana na kumuasi Rabb wake pindi akiamua kuacha hizo dhambi na kuendelea kufanya mema. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):    

 

 

قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِن رَّحْمَةِ اللَّـهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا ۚ إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ﴿٥٣﴾

Sema: Enyi waja Wangu ambao wamepindukia mipaka juu ya nafsi zao: “Msikate tamaa na rahmah ya Allaah; hakika Allaah Anaghufuria dhambi zote; hakika Yeye Ndiye Mwenye kughufuria, Mwenye kurehemu.” [Az-Zumar: 53]

 

 

Aayah hiyo tukufu ni mwito kutoka kwa Muumba wa mbingu na ardhi kwa wote wenye kumuasi Rabb wao, na wale waliozama na kufurutu mpaka katika maasi hata wakakata tamaa kuwa hawatoweza tena kusamehewa kwamba wasikate tamaa bali warudi haraka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Naye yuko tayari kuwapokea kuwaghufuria na kuwasamehe madhambi yao hata yawe makubwa vipi.

 

Lakini kuna mashari ya kutubia kama yafuatayo:

 

1-Ayaache maasi hayo.

 

2-Ajute kwa kuyafanya maasi hayo.

 

3-Atie nia ya kutoyarudia tena.

 

Na endapo kosa hilo litahusiana na haki ya mtu hapo litaongezeka sharti la nne nalo:

 

4-Ni kumuomba msamaha uliyemkosea kwa ulichomkosea ikiwa ni kuhusu haki za binaadamu.

 

 

Dhambi za kuua pia zinasamehewa, na kifutacho ni kisa chenye mafunzo yanayohusu mas-ala haya na dalili yake kuwa hata mtu akiua nafsi mia anaweza kusamehewa:

 

 

عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ أَنَّ نَبِيَّ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ: (( كَانَ فِيمَنْ كَانَ قَبْلَكُمْ رَجُلٌ قَتَلَ تِسْعَةً وَتِسْعِينَ نَفْسًا، فَسَأَلَ عَنْ أَعْلَمِ أَهْلِ الأَرْضِ فَدُلَّ عَلَى رَاهِبٍ فَأَتَاهُ فَقَالَ: إِنَّهُ قَتَلَ تِسْعَةً وَتِسْعِينَ نَفْسًا فَهَلْ لَهُ مِنَ تَوْبَةٍ؟ فَقَالَ: لاَ‏.‏ فَقَتَلَهُ فَكَمَّلَ بِهِ مِائَةً، ثُمَّ سَأَلَ عَنْ أَعْلَمِ أَهْلِ الأَرْضِ فَدُلَّ عَلَى رَجُلٍ عَالِمٍ فَقَالَ: إِنَّهُ قَتَلَ مِائَةَ نَفْسٍ فَهَلْ لَهُ مِنْ تَوْبَةٍ؟ فَقَالَ: نَعَمْ ، وَمَنْ يَحُولُ بَيْنَهُ وَبَيْنَ التَّوْبَةِ، انْطَلِقْ إِلَى أَرْضِ كَذَا وَكَذَا فَإِنَّ بِهَا أُنَاسًا يَعْبُدُونَ اللَّهَ فَاعْبُدِ اللَّهَ مَعَهُمْ وَلاَ تَرْجِعْ إِلَى أَرْضِكَ فَإِنَّهَا أَرْضُ سَوْءٍ.‏ فَانْطَلَقَ حَتَّى إِذَا نَصَفَ الطَّرِيقَ أَتَاهُ الْمَوْتُ، فَاخْتَصَمَتْ فِيهِ مَلاَئِكَةُ الرَّحْمَةِ وَمَلاَئِكَةُ الْعَذَابِ، فَقَالَتْ مَلاَئِكَةُ الرَّحْمَةِ: "جَاءَ تَائِبًا مُقْبِلاً بِقَلْبِهِ إِلَى اللَّهِ"‏.‏ وَقَالَتْ مَلاَئِكَةُ الْعَذَابِ: "إِنَّهُ لَمْ يَعْمَلْ خَيْرًا قَطُّ" ‏.‏ فَأَتَاهُمْ مَلَكٌ فِي صُورَةِ آدَمِيٍّ فَجَعَلُوهُ بَيْنَهُمْ فَقَالَ: قِيسُوا مَا بَيْنَ الأَرْضَيْنِ فَإِلَى أَيَّتِهِمَا كَانَ أَدْنَى فَهُوَ لَهُ .‏ فَقَاسُوهُ فَوَجَدُوهُ أَدْنَى إِلَى الأَرْضِ الَّتِي أَرَادَ فَقَبَضَتْهُ مَلاَئِكَةُ الرَّحْمَةِ))  قَالَ قَتَادَةُ فَقَالَ الْحَسَنُ ذُكِرَ لَنَا أَنَّهُ لَمَّا أَتَاهُ الْمَوْتُ نَأَى بِصَدْرِهِ ‏.‏

Imetoka kwa Abuu Sa'iydil-Khudriyyi (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: ((Alikuweko mtu kabla yenu aliua nafsi tisiini na tisa. Akauliza kutaka kumjua aliyekuwa na elimu kuliko wote duniani, akapelekwa kwa mtawa. Akawambia kuwa ameua watu tisini na tisa kisha akamuuliza kama atasamehewa. Mtawa akamwambia "husamehewi". Akamuua na yeye pia ikawa ni watu mia aliowaua.

 

Akauliza tena kutaka kujua mtu mwenye elimu kabisa duniani akapelekwa kwa mtaalamu. Akamwambia kuwa ameua watu mia na akamuuliza kama atasamehewa. Mtaalamu akamwambia. "Ndio, kwani nani atakayejiweka  baina yako na baina ya Tawbah? Nenda mji fulani kwani huko kuna watu wanaomuabudu Allaah. Nenda ukaabudu pamoja nao na usirudi mji wako kwani ni mji mbaya huo."

 

Akaelekea huko lakini alipofika nusu njia Malaika wa kutoa roho akachukua roho yake. Malaika wa Rahma na Malaika wa adhabu   wakaanza kumgombania. Malaika wa Rahma akasema: "Ametubu na amekuja kumtafuta Allaah." Malaika wa adhabu akasema: "Hakufanya lolote jema." Akatokea Malaika katika umbo la binaadamu akawajia na wakamuomba awahukumie jambo hilo. Akasema: "Pimeni umbali baina ya miji miwili (yaani mji wake aliotoka na mji aliokuwa anaelekea) na wowote utakaokuwa ni karibu zaidi basi ndio huo utakaokuwa ni wake." Wakapima na kuona kwamba mji ambao alikuwa anaelekea kwenda ulikuwa karibu zaidi. Hivyo Malaika wa Rahma akamchukua [Muslim]

 

 

Kwenye As-Swahiyh imesema: ((Mji mwema ulikuwa karibu kwa dhiraa moja. Hivyo akahesabiwa kuwa ni mtu wa mji huo))

 

Riwaaya nyingine katika As-Swahiyh inasema: ((Allaah Aliamrisha (mji muovu) usogee mbali hivyo (mji mwema) ukasogea karibu na akasema: Pimeni umbali baina yao. Walipopima waliona kwamba yuko karibu na mji mwema kwa umbali wa dhiraa moja, kwa hiyo akasamehewa))

 

 

Ili upate maelezo zaidi ya mas-ala haya ambayo yametajwa kwa kirefu mno ingia katika viungo vifuatavyo.

 

 

 

Tawba Ya Shirk Inakubaliwa? Na Vipi Kuomba?

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share