Kuchelewa Kugawa Mirathi

SWALI

Assalam alaykum,

Hapa tafadhali nna suali jengine muhimu kuhusu Mirathi

Mtu amefariki na kuacha mke na watoto, na pia amewacha watoto kwa tumbo jengine ambalo mama yao aliachika zamani. Huu sasa unaelekea mwaka wa tatu, wahusika hawa hawajarithishwa mali zao. Na mali zote za aliyefariki alimuwachilia kaka yake. Kaka yake huyu ni mtu ambaye naweza kusema anaswali na msikitini hatoki na wala hana ila mbaya kama kupenda wanawake, kulewa na kama hayo. Yeye na mkewe na watoto wake tuu.

Jee tunaambiwa nini katika Dini yetu tukufu kucheleweshwa huku kwa kurithisha? Naomba maelezo ya uhakika tafadhalini

 

 
 

JIBU:

 

AlhamduliLlaah - Himdi Na Sifa Zote Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Uislamu ni njia kamili ya maisha ya mwanadamu, hivyo imemuelekeza mwanadamu huyo katika yatakayomfaidisha hapa duniani na kumpatia ufanisi kesho Akhera. Uislamu umetoa muongozo kabambe kuhusu urithi. Ikiwa mtu amefariki anafaa afanyiwe mambo yafuatayo kabla ya kugawanywa kwa hela au rasilmali aliyoacha. Mambo yenyewe ni:

  1. Kuanza kumtayarisha kwa kutoa thamani ya sanda, kumuosha, kumkafini na kufukua kaburi.

 

  1. Kumlipia deni sawa likiwa ni la Allah kama Zakah, kafara, nadhiri, Hijjah iliyo wajibu kwake au deni la wanadamu wengine wanaomdai.

 

 

  1. Kutoa alichousiya lakini kisiwe zaidi ya thuluthi.

 

  1. Kuswaliwa na kuzikwa.

 

 

  1. Baada ya yote hayo, kilichobakia watagaiwa warithi  wake kwa mujibu  wa sheria

Kutegemea watu waliobaki katika jamaa zake, Aliyefariki atakuwa ni mwenye kurithiwa na warithi kila mmoja na sehemu yake kama ilivyoelezwa katika Qur’an na Hadithi Sahihi za Bwana Mtume (s.a.w.w.) kama mke au wake, watoto, wazazi, ndugu halisa na wengineo. Ni madhambi makubwa kwa mtu kuwarithisha wasiokuwa warithi au kutowarithisha warithi wenyewe wa haki au kuwapatia sehemu ndogo au kurithisha sawa baina ya wavulana na wasichana, kwani hivyo itakuwa ni kwenda kinyume na hukmu ya Allah kwa kufuata baadhi ya taasisi au vyama vya kikafiri ili kuonyesha kuwa Uislamu unakwenda sambamba na matakwa ya hawa maadui. Anayefanya hivyo anafaa atubie kabla hajafariki na arudi katika mwendo wa sawa na afanye mema na arudishe haki za watu.

Mirathi inatakiwa igawanywe haraka iwezekenavyo ili kila mmoja aangalie shughuli zake na aweze kujimudu kimaisha isipokuwa kuwe na udhuru wa kisheria. Mfano ni ikiwa watoto wa aliyefariki ni wadogo inafaa mlezi au wasii wao awatunzie mpaka wabaleghe na wawe na akili ya kuweza kutunza mali hiyo. Allah Anasema:

“Na wajaribuni mayatima mpaka wafike umri wa kuoa. Mkiwaona ni wekevu, basi wapeni mali yao. Wala msiyale kwa fujo na pupa kwa kuwa watakuja kuwa watu wazima. Na aliyekuwa tajiri na ajizuilie, na aliye fakiri basi na ale kwa kadri ya ada. Na mtakapowapa mali yao washuhudizieni. Na Allaah Anatosha kuwa Mhasibu” (4: 6).

 Na wale ambao ni wajinga pia wanafaa watunziwe urithi wao ili wasipate kuchezea mali hiyo. Allah Anasema:

“Wala msiwape wasio na akili mali yenu ambayo Allaah  Ameyajaalia yawe ni kiamu yenu. Walisheni katika hayo na muwavike, na mseme nao maneno mazuri” (4: 5). 

Haifai kubadilisha vizuri vya mayatima warithi kwa vibaya na wala haifai kula mali yao. Allah Anasema:

“Na wapeni mayatima mali yao. Wala msibadilishe kibaya kwa kizuri. Wala msile mali zao pamoja na mali zenu. Hakika yote hayo ni jukumu kubwa”

(4: 2).

Na mwenye kula mali ya mayatima kwa dhulma basi anatia moto matumboni mwake. Allah Anasema:

“Hakika wanaokula mali ya mayatima kwa dhulma, hapana shaka yoyote wanakula matumboni mwao moto, na wataingia Motoni” (4: 10).

Allah Ametuekea mipaka katika mas-ala ya kugawa urathi na yeyote atakayeaswi basi atatiwa katika moto na huko atakaa milele. Allah Anasema:

“Hiyo ni mipaka ya Allaah. Na anayemtii Allaah na Mtume wake, Yeye Atamtia katika Pepo zipitazo mito kati yake, wadumu humo. Na huko ndiko kufuzu kukubwa. Na anayemuasi Allaah  na Mtume wake, na akaipindukia mipaka yake, (Allaah) Atamtia Motoni adumu humo, na atapata adhabu ya kudhalilisha” (4: 13 – 14).

Hivyo ni vyema kaka huyo wa aliyefariki ikiwa hakuna dharura tulizozitaja za kukaa na hela hiyo au rasilmali agawe na kila mmoja apate haki yake. Hii ni kuwa mara nyingi shetani anaingia katikati ya mas-ala na kumfanya hata mcha Mungu asitende haki na hivyo kuwa katika hali mbaya hapa duniani na kesho Akhera. Waislamu walio karibu na kaka huyo inafaa wampe nasaha ili aweze kuwapatia warithi haki yao na yeye aondoke katika dhima hiyo ya kuwa na amana ya watu.

Wenye kuuliza maswali ya MIRATHI wanaombwa watimize yafuatayo: 

Ili maswali yenu yajibike haraka inatakiwa kuwa wale watu wote ambao wana ukaribu wa kidamu na aliyefariki wawe ni wenye kuandikwa ili pasiwe na utata wowote. Na katika hayo tungependa watu wafuatao watiliwe maanani sana kutajwa katika swali ikiwa atahusika:

1.       Kijana mwanamume.

2.       Kijana mwanaume wa kijana mwanaume (mjukuu).

3.       Baba.

4.       Babu wa kwa baba.

5.       Ndugu mume wa kwa baba na mama (khalisa).

6.       Ndugu wa kwa baba.

7.       Ndugu mume wa kwa mama.

8.       Kijana mwanaume wa ndugu mume khalisa.

9.       Kijana mwanaume wa ndugu mume wa kwa baba.

10.    Ami wa kwa baba na mama.

11.    Ami wa kwa baba.

12.    Kijana mwanaume wa ami wa kwa baba na mama.

13.    Kijana mwanaume wa ami wa kwa baba.

14.    Mume.

15.    Binti.

16.    Binti wa kijana mwanaume.

17.    Mama.

18.    Dada khalisa.

19.    Dada wa kwa baba.

20.    Dada wa kwa mama.

21.    Bibi mzaa baba.

22.    Bibi mzaa mama.

23.    Mke.

Hii itatusaidia sana katika kujibu maswali yenu ya mirathi. Shukran.

 

Na Allah Anajua Zaidi.

 

Share