Masiyhud-Dajjaal Alikosa Nini? Zipi Alama Zake? Ni Kweli Zimo Katika Noti Ya Dola?

 

Masiyhud-Dajjaal Alikosa Nini? Zipi Alama Zake? Ni Kweli Zimo Katika Noti Ya Dola?

 

Alhidaaya.com

 

SWALI:

 

Asalam aleikum, inshaallah nyote wazima, ndugu zangu ningependa kuuliza maswali kuhusu massih dajal; je alikosa nini kwa mwenyezi mungu mpaka ALLAH SWT akampa adhabu hiyo? ni kweli kuwa amefungwa kwenye island ambayo watu wengi wasema kuwa ni bermuda triangle ambayo haipiti kitu chochote karibu yake bila kuungamia? Maana ukifuata historia za Bermuda triangle mambo yote yanaotokea niyakimuijiza hayaeleweki. Je kuhusu hela za marekani ukiangalia kwenye noti ya dola moja nyuma yake kuna triangle na ina jicho moja katikati yake watu wengi wasema kuwa ni jicho lake masih dajal na kuwa hizo ni signs kutoka kwa mwenyezi mungu na kuwa yuko kweli huko Bermuda triangle maana pia ardhi hiyo iko shape ya triangle ni kweli hayo yote? Ndugu zangu niuweni radhi ikiwa nimekosea naomba majibu yenu na pia nielimisheni zaidi kuhusu swala hili wasalam aleikum shukran.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Allaah Aliyetukuka ni Mwelewa wa kila kitu hapa duniani na mbinguni – Hufanya Atakalo wala hakuna wa kumuuliza bali sisi ndio wakuulizwa na Yeye. Anayofanya Allaah Aliyetukuka si majaribio bali ni hakika. Allaah Aliyetukuka Mwenyewe huleta mitihani kwa waja wake kwa njia na aina mbali mbali. Mtihani mmoja ambao wanaadamu watapata ni kuletwa kwa Masiyhud Dajjaal na pia Juuj na Maajuuj.

 

Kuletewa kitu kuwa ni mtihani ili tujulikanwe msimamo wetu sio kuwa kitu kile kimekosea. Saa nyingine yapo mambo ambayo hatuna majibu nayo. Mfano kwa nini punda wa mjini akawa haramu na punda milia akawa halali kwa Muislamu kula. Haya ni mtihani kwetu nasi kama Waumini tunatakiwa tuamini kwani yatoka kwa Allaah Aliyetukuka wala tusiwe kama Mayahudi. Allaah Aliyetukuka Anasema:

 

....وَقَالُوا سَمِعْنَا وَأَطَعْنَا ۖ غُفْرَانَكَ رَبَّنَا وَإِلَيْكَ الْمَصِيرُ ﴿٢٨٥﴾

Na wakasema: Tumesikia na tumetii, tunakuomba maghfirah Rabb wetu na Kwako ni mahali pa kuishia. [Al-Baqarah: 285]

 

Ilhali Mayahudi, msimamo wao ni:

وَإِذْ أَخَذْنَا مِيثَاقَكُمْ وَرَفَعْنَا فَوْقَكُمُ الطُّورَ خُذُوا مَا آتَيْنَاكُم بِقُوَّةٍ وَاسْمَعُوا ۖ قَالُوا سَمِعْنَا وَعَصَيْنَا.. 

Na Tulipochukua fungamano lenu na Tukaunyanyua juu yenu mlima; (Tukasema): Shikilieni Tuliyokupeni kwa nguvu na sikilizeni. Wakasema: Tumesikia na tumeasi. [Al-Baqarah: 93].

 

Na Allaah Aliyetukuka Anatuambia:

 

هُوَ الَّذِي أَنزَلَ عَلَيْكَ الْكِتَابَ مِنْهُ آيَاتٌ مُّحْكَمَاتٌ هُنَّ أُمُّ الْكِتَابِ وَأُخَرُ مُتَشَابِهَاتٌ ۖ فَأَمَّا الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِمْ زَيْغٌ فَيَتَّبِعُونَ مَا تَشَابَهَ مِنْهُ ابْتِغَاءَ الْفِتْنَةِ وَابْتِغَاءَ تَأْوِيلِهِ ۗ وَمَا يَعْلَمُ تَأْوِيلَهُ إِلَّا اللَّـهُ ۗ وَالرَّاسِخُونَ فِي الْعِلْمِ يَقُولُونَ آمَنَّا بِهِ كُلٌّ مِّنْ عِندِ رَبِّنَا ۗ وَمَا يَذَّكَّرُ إِلَّا أُولُو الْأَلْبَابِ ﴿٧﴾

Yeye Ndiye Aliyeteremsha kwako Kitabu humo mna Aayaat zenye maana wazi, hizo ndio msingi wa Kitabu, na nyinginezo zisizokuwa wazi maana zake. Basi wale ambao katika nyoyo zao mna upotovu hufuata zile zisizokuwa wazi maana zake kutafuta fitnah (upotofu) na kutafuta maana zake zilofichika, na hakuna ajuae maana zake isipokuwa Allaah. Na wenye msingi madhubuti katika elimu husema: Tumeziamini, zote ni kutoka kwa Rabb wetu. Na hawakumbuki ila wenye akili. [Aal-‘Imraan: 7]

 

Kwa hivyo, mas-ala mengi ya ndani hatujui isipokuwa ni mtihani kwetu, na sisi kama Waumini tunatakiwa tuamini kuwa kama Alivyotueleza Nabiy(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa huyo Masiyhud Dajjaal yupo amefungwa na atafunguliwa mwisho wa dunia.

 

Ama yupo katika Bahari gani hilo linajulikana na Allaah Aliyetukuka peke yake sio sisi wanaadamu. Na haiwezekani kuwa Bermuda kwa kuwa iko mbali na Peninsula ya Arabuni na Abu Ruqayyah Tamiym ad-Daariy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipokuja kumueleza Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumuona kwake Dajjaal akiwa amefungwa na silsila katika kisiwa cha bahari.

 

Ama yanayosemwa na yatakayoendelea kusemwa kutoka kwa watu kuwa Dajjaal ni Marekani na dalili ya noti na Dola moja, si ya sawa kwani katika maelezo ya Dajjaal si nchi bali ni kiumbe. Inawezakana labda kuwa Marekani kuwa mshirika wa kiumbe huyo lakini katika hilo pia hakuna ushahidi bali ushahidi uliopo ni kuwa wafuasi wake wengi watakuwa ni Mayahudi kama alivyoashiria Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na tunachojua kutoka kwa dalili za wazi ni kuwa Dajjaal huyo atauliwa Palestina katika mlango wa kuingilia mji unaoitwa al-Lud na Nabii ‘Iysa (‘Alayhis salaam).

 

Bonyeza kiungo kifuatacho upate maelezo zaidi

 

Hadiyth Ya Al-Jassaasah

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share