Kuhusu Mashaytwaan Na Vipi Kujikinga Nao

 

Kuhusu Mashaytwaan Na Vipi Kujikinga Nao

 

Alhidaaya.com

 

SWALI:

 

Asalam alaykum.ALLAH awajaze kheri kwa kujibu maswali yetu mana mnatuweka wazi kwa vitu vilokua vigumu kwetu.Swali langu ni QUR-AAN inatufundisha nini kuhusu mashetani au majini? Pia naomba dua za kujikinga na kujitibu sie na watoto wetu dhidi ya viumbe hivi(mashetani au majini)

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Hakika swali hili jibu lake linahitaji maelezo marefu kwani kuna aya na Hadiyth nyingi kabisa zilizotaja kuhusu mashaytwaan au majini kwa hiyo tujaribu kuelezea kwa kadiri tuwezavyo In shaa Allaah:

 

Qur'aan inatufahamisha kuwa majini wapo na kuwa iko sababu ya kuweko kwao katika maisha haya, sababu ni kuwa wamuabudu Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa Pekee bila ya kumshirikisha. Anasema Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa :

 وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ ﴿٥٦﴾

  Na Sikuumba majini na wana Aadam isipokuwa waniabudu. [Adh-Dhaariyaat: 56]

 

Majini kama binaadamu wana baadhi ya vitu ambavyo vinafanana kama katika ufahamu wa kujua lipi jema na jipi baya kwani waliposikia Qur'aan inasomwa walishangazwa na kisha wakasema kuwa:   

وَأَنَّا مِنَّا الصَّالِحُونَ وَمِنَّا دُونَ ذَٰلِكَ ۖ كُنَّا طَرَائِقَ قِدَدًا﴿١١﴾وَأَنَّا ظَنَنَّا أَن لَّن نُّعْجِزَ اللَّـهَ فِي الْأَرْضِ وَلَن نُّعْجِزَهُ هَرَبًا﴿١٢﴾وَأَنَّا لَمَّا سَمِعْنَا الْهُدَىٰ آمَنَّا بِهِ ۖ فَمَن يُؤْمِن بِرَبِّهِ فَلَا يَخَافُ بَخْسًا وَلَا رَهَقًا﴿١٣﴾وَأَنَّا مِنَّا الْمُسْلِمُونَ وَمِنَّا الْقَاسِطُونَ ۖ فَمَنْ أَسْلَمَ فَأُولَـٰئِكَ تَحَرَّوْا رَشَدًا﴿١٤﴾

Na kwamba miongoni mwetu ni wema, na miongoni mwetu kinyume chake; tumekuwa makundi ya njia mbali mbali. Na kwamba tulikuwa na yakini kwamba hatutoweza kumshinda Allaah ardhini, na wala hatutoweza kumkwepa kutoroka. Na kwamba sisi tuliposikia mwongozo (huu Qur-aan) tukaiamini; basi atakayemuamini Rabb wake hatoogopa kupunjwa mazuri yake na wala kuzidishiwa adhabu ya madhambi. Na kwamba miongoni mwetu ni Waislamu, na miongoni mwetu wakengeukaji haki; hivyo atakayesilimu, hao ndio waliofuata uongofu. [Al-Jinn:11-14]

 

Kwa hiyo siku ya Qiyaamah nao pia watasimamishwa kuwa na hesabu yao mbele ya Rabb wao kama Anavyosema Allaah Subhaanahu wa Ta'alaa:

 وَجَعَلُوا بَيْنَهُ وَبَيْنَ الْجِنَّةِ نَسَبًا ۚ وَلَقَدْ عَلِمَتِ الْجِنَّةُ إِنَّهُمْ لَمُحْضَرُونَ ﴿١٥٨﴾

Na wakafanya baina Yake (Allaah) na baina ya majini unasaba. Na hali majini wamekwishajua kwamba wao bila shaka watahudhurishwa (kuadhibiwa). [As-Swaafaat :158]

 

Wanaishi kama sisi binaadamu, wanakula, na kunywa na wanaoana na kuzailiana. Nao ni viumbe vinavyoishi na kutembea, na sisi binaadamu hatuwaoni bali wao wanatuona kama Anavyosema Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa:  

إِنَّهُ يَرَاكُمْ هُوَ وَقَبِيلُهُ مِنْ حَيْثُ لَا تَرَوْنَهُمْ ۗ 

 Hakika yeye (Ibliys) anakuoneni, yeye na kabila lake (la mashaytwaan) na hali ya kuwa nyinyi hamuwaoni. [Al-A'raaf: 27] Kuumbwa kwao ni kutokana na moto; 

وَالْجَانَّ خَلَقْنَاهُ مِن قَبْلُ مِن نَّارِ السَّمُومِ﴿٢٧﴾

Na majini Tuliwaumba kabla kutokana na moto ulio mkali mno. [Al-Hijr 27]

 وَخَلَقَ الْجَانَّ مِن مَّارِجٍ مِّن نَّارٍ ﴿١٥﴾

Na Akaumba majini kutokana na mwako wa moto. [Ar-Rahmaan: 15]

 

Na wao wanaweza kujibadilisha maumbile yao waonekane kama ni vitu vingine kama vile wanyama kama mbwa au nyoka, na kadhalika. Wana uwezo wa kusafiri masafa makubwa kwa haraka kabisa.  

 

Wanapenda sana kuishi katika sehemu chafu kama vyooni, katika mashimo, jaani, makaburini, katika magofu na kadhalika na ndio maana Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha tunapoingia chooni kuomba du'aa hii: 

(بِسْمِ الله ) اللّهُـمَّ إِنِّـي أَعـوذُ بِـكَ مِـنَ الْخُـبْثِ وَالْخَبائِث    

 .Bismillah, Allaahumma Inni A'udhu Bika Minal-Khubthi Wal-Khabaaith

(Kwa jina la Allaah ) Ee Allaah  najilinda Kwako kutokana na mashetani ya kiume na ya kike.

 

Wana uhusiano na sisi binaadamu na kila mmoja wetu anaye jini ambaye anakuwa ni mwenye kumuandama kama rafiki yake. 

عن ابن مسعود أنه قال : قال رسول الله: (( ما منكم من أحد إلا وقد وكل به قرينه من الجن)) . قالوا : وإياك يا رسول الله؟ قال :  ((وإياي إلا أن الله أعانني عليه فأسلم فلا يأمرني إلا بخير))   رواه مسلم

Ibn Mas'uud amesema: Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Hakuna mmoja wenu ila anaye jini anayemuwakilisha qariyn (rafiki) katika majini)) Wakasema: Hata wewe ee Rasuli wa Allaah? Akasema: "Hata mimi isipokuwa mimi Allaah Amenisaidia kwa kumsilimisha kwa hiyo haniamrishi ila mema tu". [Muslim]

 

Na shatwaan anaweza kuwa ni binaadamu au jini, na ndio Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa Anasema:

 مِن شَرِّ الْوَسْوَاسِ الْخَنَّاسِ ﴿٤﴾الَّذِي يُوَسْوِسُ فِي صُدُورِ النَّاسِ ﴿٥﴾مِنَ الْجِنَّةِ وَالنَّاسِ ﴿٦﴾

Kutokana na shari za anayetia wasiwasi, mwenye kurejea nyuma akinyemelea. Ambaye anayenong’ona kutia wasiwasi vifuani mwa watu. Miongoni mwa majini na watu.  [An-Naas 114: 46]

 

Na kuhusu mashetani wa kibinadamu: 

وَإِذَا لَقُوا الَّذِينَ آمَنُوا قَالُوا آمَنَّا وَإِذَا خَلَوْا إِلَىٰ شَيَاطِينِهِمْ قَالُوا إِنَّا مَعَكُمْ إِنَّمَا نَحْنُ مُسْتَهْزِئُونَ ﴿١٤﴾

Na wanapokutana na wale walioamini husema: Tumeamini. Na wanapokuwa peke yao pamoja na mashaytwaan wao, husema: Hakika sisi tuko pamoja nanyi, hakika sisi ni wenye kuwadhihaki tu.  [Al-Baqarah: 14]

  

Kujikinga Na Mashaytwaan

 

Kuna njia nyingi za kujikinga na mashaytwaan kutokana na madhara yao kama ilivyo katika Qur'aan na Sunnah:

 

1-Kujikinga nao kama Alivyotufundisha Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa kuwa tuseme:

..رَّبِّ أَعُوذُ بِكَ مِنْ هَمَزَاتِ الشَّيَاطِينِ ﴿٩٧﴾وَأَعُوذُ بِكَ رَبِّ أَن يَحْضُرُونِ ﴿٩٨﴾            

.Rabb wangu! Najikinga Kwako kutokana na udokezi wa mashaytwaan. Na najikinga Kwako Rabb wasinihudhurie. [Al-Muuminuwn: 97-98]

  

2-Kusoma Suwrah mbili za mwisho (Al-Falaq na An-Naas)

 

3-Kusema 'Bismillah' kabla ya kula, kunywa, kuingia katika nyumba, kujamiiana, unapoingia chooni pamoja na du'aa yake.

 

4-Kusoma Ayatul-Kursiy unapolala pamoja na Aya mbili za mwisho katika Suwrah Al-Baqarah.

 

5-Kusoma Qur'aan sana na khaswa Suwrah Al-Baqarah ambayo Nabiy  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema atakayesoma  suwrah hiyo haingii shaytwaan nyumbani kwake. 

عن أبي هريرة رضي الله عنه أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال)) : لا تجعلوا بيوتكم قبورًا فإن البيت الذي تقرأ فيه سورة البقرة لا يدخله الشيطان))   صحيح الجامع

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Msifanye nyumba zenu makaburi kwani nyumba inayosomwa Suwrah Al-Baqarah haingii shaytwaan". [Sahiyh Al-Jaami'i]

 

6-Kusoma nyiradi za asubuhi na jioni kila siku ambazo ni za Sunnah nazo zinapatikana katika kitabu cha Hisnul-Muslim kinachopatikana hata kwa lugha yetu ya Kiswahili. Na pia utaweza kukipata kitabu hicho katika kiungo kifuatacho katika ALHIDAAYA:

 

Bonyeza hapa:

 

Kitabu Cha Hiswnul-Muslim- Du'aa Katika Qur-aan na Sunnah

  

 Na humo utapata pia Du'aa za kuwakinga watoto kama alivyokuwa akifanya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)

 

7-Kutia wudhuu kila mara.

 

Kwa ujumla ni kuimarisha iymaan yako kwa kumkumbuka Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa  kila wakati katika harakaat zako, kwani hivyo utajikinga na mashaytwaan na hawatoweza kukudhuru. 

 

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

 

 

Share