Wapi Katika Biblia Kumetajwa Kuhusu Kuharamishwa Kula Nguruwe?

SWALI:

 

Assalaamu Alaykum Warahmatullah.

 

Nashukuru kwa majibu yenu mazuri. Mungu awabariki kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kutuelimisha, Ahsanteni sana. Leo nina maswali mengine mawili kama yafuatavyo: Ni aya ipi katika Biblia ambayo Wakristo wanaitumia kuhalalisha kula Nguruwe?


 

JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kutajwa  kula nguruwe katika Biblia.

 

Hakika ni kuwa Agano la Kale katika Biblia imekataza ulaji wa nguruwe na akafanywa kuwa ni haramu: “Nguruwe msimle; ana kwato zilizogawanyika lakini hacheui; kwenu ni najisi. Kwa sababu wanyama hao ni najisi msile nyama yao wala msiguse mizoga yao (Walawi 11: 7 – 8).

 

Agizo hilo limerudiwa katika Kumbukumbu la Shari’ah 14: 7 – 8 na pia Isaya 66: 17. Na katika Agano Jipya, Yesu naye amesema kuwa hakuja kutangua shari’ah na mafundisho ya manabii bali kukamilisha (Mathayo 5: 17). Kwa ibara hiyo ni kuwa Yesu pia aliharamisha ulaji wa nguruwe.

 

Hata hivyo, Nabii Paulo ndiye aliyekuja akaenda kinyume na shari’ah hiyo kwa kutoa agizo kwa barua aliyowaandikia Warumi:

 

Basi, usiiharibu kazi ya Mungu kwa sababu ya ubishi juu ya chakula. Vyakula vyote ni halali, lakini haifai kula chakula ambacho kitamfanya aanguke katika dhambi” (Waroma 14: 20).

 

Pia, “Katika kuungana na Bwana Yesu, nina hakika kwamba hakuna kitu chochote kilicho najisi kwa asili yake” (Waroma 14: 14).

Paulo amesema tena kuwa kila kitu alichoumba Mungu ni chema wala hakuna kinachohitaji kukataliwa (1 Timetheo 4: 3 – 5).

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share