Anampenda Mke Mdogo Zaidi, Anamsifia Sana Mbele Ya Mke Mkubwa, Je Ni Haki Hivi

 

SWALI:

 

Assalam aleykum warahma tullwahi wabarakat...

Suala langu ni kuhusu ndoa. Ikiwa mume kaowa mke mwengine japo atakua anampenda sana huyo mke mdogo kuliko mkubwa je pia anatakiwa huyo mume kuwaridhisha wake zake inatakiwa iwe tofauti au? Anaruhusiwa kumsifia mke mdogo mbele ya mke mkubwa na huyo mdogo akiwa yupo hapo hapo kama mke mdogo ni queen na mke mkubwa ni princess na kumsifia kwa sifa nyingi tu na kufanya mambo mengine tofauti..kama kwamba kumfurahisha yule mke mdogo..

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mume kumpenda mke mdogo zaidi kuliko yule mkubwa.

Uislamu umetoa ruhusa kwa mwanamme kuoa mke zaidi ya mmoja ikiwa ataweza kutekeleza uadilifu baina yao (an-Nisaa’ [4]: 3). Uadilifu ni katika malazi, makazi, chakula, matibabu, na mengineyo. Haifai kwa hali yoyote ile kwa mume kumpendelea mke mdogo kwa sababu ya udogo wake kiumri, uzuri wake na mengineyo.

 

Anafaa mume afanye juhudi kuwapenda wake zake wote sawa sawa wala hafai kuwatofautisha baina yao. Pia haifai kwa mume kumsifia mke wake wa pili au wa kwanza kwa mke mwenza kwa hali ambayo itaonekana kuwa amemfadhilisha mmoja juu ya mwengine.

 

 

Haifai Kiislamu kumtweza mwanaadamu yeyote awaye kwa mwenziwe. Kwa hivyo, hayo ni makosa na inafaa kwa mume aache hayo na badala yake ajenge mahusiano mema kwa wake zake wote wawili.

 

Pia haifai kuwafanyia mambo tofauti baina ya wakeze bali anatakiwa atekeleze uadilifu na usawa.

 

Bonyeza viungo vifuatavyo upate manufaa zaidi:

 

Mume Hatoi Haki Kwa Mke Wa Pili Kama Atoavyo Kwa Mke Wa Kwanza

 

Haki Za Mke Mkubwa Na Mke Mdogo

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share