Kampenda Msichana Na Kakataliwa Kumuoa Kwa Sababu Anasemekana Kadanganya Kabila Lake, Nao Wanaangalia Kabila

 

 

SWALI:

 

Assalam Aleykum

 

Je vp naweza kurekekebisha Makosa yangu kumpata Msichana nilompenda katika Maisha yangu ikiwa niliposa Msichana kwa kutumia Kabila Jingine nikakubaliwa Posa yangu na Baadaye Wazazi wake waliikata mimi Kumuoa Mtoto wao ingawa sijawahi kukutana na Wazazi wake kwani mi siko East-Africa kwa sasa.

 

Wazee wangu walinitolea Posa na Msichana nampenda sana na namuhitaji katika Maisha yangu yote, ingawa si kweli kama anavyoeleza Ndugu yetu **** wale si wazee Wangu wale ni wazee wangu wa Damu Kabisa, na hawakudanganya isipokuwa tumechangia Tumbo la Bibi yetu Mzazi yaani Bibi yangu aliolewa na Babu yangu baadaye waliachana na kuolewa na mtu Mwingine mwenye Asili ya Kihindi ndiyo Maana familia yetu iko Vile ndiyo Maana wao wakadhani wamedanganya.

 

Sasa nisaidieni Ndugu yangu kwani mimi Msichana nampenda Kupita Kiasi, au watu Huoa kutoka Katika Milango waliyozaliwa tuu?

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kumpenda msichana kwa dhati yako.

Inatakiwa tufahamu kuwa Muislamu hafai kumpenda yeyote zaidi ya Allaah Aliyetukuka na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Mwanzo kabla ya kumpata au kutaka kumpata huyo msichana ujaribu kuingia katika msitari wa Dini na kumpenda Allaah Aliyetukuka na Mtumewe (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ukifanya hilo mwanzo hayo mengine yatakuwa sahali kwani Allaah Aliyetukuka na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) watakuongoza katika ya kheri, baraka na fanaka hapa duniani na Kesho Akhera.

 

Kisha inatakiwa tufahamu kuwa ukweli ni kitu muhimu sana kwa Muislamu.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametwambia kuwa Muislamu hawezi kuwa muongo kabisa (Ahmad). Na pia katika Hadiyth ya Muslim: “Mwenye kutughushi (kutudaganya) si katika sisi (Waislamu)”.

Ilikuwa ufahamu kuwa kabila lako ni fulani na haliwezi kubadilika kwani pia sisi hatuna uchaguzi wa kutaka kuzaliwa katika ukoo, familia au kabila lolote lile. Kwa hiyo, wale waliokwenda kuposa walikuwa wataje lile kabila lako mbali na kuwa kabila si muhimu katika ndoa wala haitamfalia lolote mtu Siku ya Qiyaamah. Kinachohitajika ni uchaji Mungu na kushikamana na Uislamu inavyotakiwa na Dini. Lakini kwa leo tumekengeuka na Dini mpaka tumeona kuwa kabila ndio kila kitu hapa duniani.

 

 

Kwa hiyo, la kurekebisha mwanzo ni watu wako kurudi kwa wazee wa msichana unayemtaka kumposa na wao kuwaeleza nasaba yako ilivyo na vipi labda hamukueleweka vyema mara ya kwanza. Ukisha rekebisha hilo nadhani kutakuwa hakuna shida isipokuwa wazazi wa msichana watake kuleta matatizo. Zipo ibara nyingine hazikueleweka kama: “Na hawakudanganya isipokuwa tumechangia Tumbo la Bibi yetu Mzazi yaani Bibi yangu aliolewa na Babu yangu baadaye waliachana na kuolewa na mtu Mwingine mwenye Asili ya Kihindi ndiyo Maana familia yetu iko Vile ndiyo Maana wao wakadhani wamedanganya”.

 

 

Sasa mlipokwenda kuposa walisema kuwa wewe ni Mhindi, ikiwa itakuwa ni hivyo itakuwa ni uongo kwani kinasaba wewe si Mhindi ila tu bibi yako aliolewa na Mhindi. Na kusema ndiyo maana familia yetu iko vile ndio maana wao wakadhani wamedanganya. Masuala hayataki dhana bali uhakika, na ndio maneno hayo hayaeleweka kwetu. Hata hivyo, inataka msawazishe hilo kwa kuweka kila kitu wazi kabisa na kuondoa utata wote.

 

Tunahisi kuwa kama hilo litafanyika basi mambo mengine yote yatakwenda vyema. Hata hivyo, huyo msichana ambaye unampenda kabisa anatakiwa awe ameshika Dini ikiwa hajashika Dini huenda mkasumbuana bure bila ya kutarajia. Ndio kwa ajili hiyo, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akausia sana mume atafute mke mwenye Dini barabara, na kutofanya hivyo ni kujitakia balaa ya bure. Wewe mwenyewe pia uwe umeshika Dini ili Nikaah ikikubalika mambo yaende sawa kabisa baina yenu.

 

 

Ikiwa bado wazazi wake watakuwa wamekataa usikate tamaa kwani hata ukimkosa huyo wapo wengine wengi walioshika Dini barabara ambao unaweza kuoa na ukaishi nao vizuri. Ikiwa utamkosa huyo huenda akawa hana kheri nawe hapa duniani na kwa Akhera yako.

 

Nasaha yetu kwako ni kuwa swali Swalah ya Istikhaarah umtake ushauri Allaah Aliyetukuka kuhusiana na msichana huyo. Ikiwa ishara ni kuachana naye basi achana naye na ikiwa ishara ni kuwa uendelee kufuatilia basi fanya hivyo.

 

Bonyeza kiungo kifuatacho upate maelezo zaidi:

 

Kadanganya Kabila Lake Apate Kukubaliwa Posa

 

Nasi twakutakiwa kila la kheri.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share