Misikiti Miwili Imejengwa Sehemu Moja Je Msikiti Upi Unaopasa Kuswaliwa?

  

SWALI:

 

Namshukuru sana Allah Subhana Wa Taala kwa kumpa maarifa na elmu ambayo inanufaisha wengi. Hivi majuzi waasilamu walitofautiana na ikabidi msikiti ujengwe hatua chache kama mita 150 hivi kutoka kwa mwingine. La ajabu ni kwamba misikitii hii yote huandaa salaa za ijumaa. Sasa Je ni sawa hivyo, khutba mbili kingiana kila siku ya ijumaa? Ni msikiti upi ambao hupata fadhila za ijumaa? Ni nini shuruti za Ijumaa? Shukran.


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kujenga Msikiti mwingine kwa sababu ya kutofautiana. Hata hivyo, inaonyesha kuwa swali lako halikukamilika ili kuweza kukusaidia kwa njia nzuri. Umesema tu Waislamu wametofautiana, kivipi, kwa misingi gani, na mengineyo. Kwa hiyo, tujaribu kukujibu kwa ujumla ili upate nadharia ya sawa na hapo huenda swali lako likajibiwa.

 

Tofauti baina ya Waislamu zitaendelea kuwepo mbali na kuwa Allaah Aliyetukuka ni Muweza wa kuwafanya kitu kimoja. Allaah Aliyetukuka Anatulezea kuwa maadamu Waislamu ni wanadamu basi wataendelea kutofautiana: “Na Mola wako Mlezi Angelipenda Angewafanya watu wote wakawa ummah mmoja. Lakini hawaachi kukhitalifiana” (Huud [11]: 118). Na kwa ajili hiyo, Waislamu kama wanadamu huenda wakagombana, lakini wanapofikia hadi hiyo ni lazima kupatikane ufumbuzi wa tatizo lenyewe. Allaah Aliyetukuka Anasema: “Hakika Waumini ni ndugu, basi patanisheni baina ya ndugu zenu, na mcheni Allaah ili mrehemewe” (al-Hujuraat [49]: 10). Waislamu wakitofautiana hawafai kuacha tatizo hilo lilipuke bali wanahitajika warudi katika mchimbuko ya kisheria ambayo yanaweza kuwarudisha wao kuwa kitu kimoja. Hakika ni kuwa umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Allaah Aliyetukuka Anasema: “Enyi mlioamini! Mtiini Allaah, na mtiini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi. Na mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume, ikiwa mnamuamini Allaah na Siku ya Mwisho. Hayo ndiyo bora zaidi na ndiyo yenye mwisho mwema” (an-Nisaa’ [4]: 59). Na Anasema tena: “Na mtiini Allaah na Mtume Wake, wala msizozane mkaingiwa woga, na zikapotea nguvu zenu. Na subirini. Hakika Allaah yu pamoja na wanao subiri” (al-Anfaal [8]: 46).

 

Kujengwa Msikiti mpya inahitajika katika Dini ili iwe sahali kwa kila Muislamu kupata jamaa lakini kuanzishwa huko Msikiti mpya kusiwe kwa malengo ya maslahi, kuwatumikia maadui, ukabila na urangi au tofauti ndogo ambazo si za msingi. Hata hivyo, ikiwa tofauti ni katika ‘Aqiydah kumaanisha kuwa walioanzisha Msikiti mpya ni kutoroka ‘Aqiydah mbaya zenye kumtoa mtu katika Uislamu katika msikiti wa zamani au mabid’ah mengi basi kuanzishwa Msikiti huo kutakuwa hakuna tatizo kisheria bali litakuwa ni jambo linalohitajika. Ama ikiwa walionzisha msikiti mpya ni kuhuisha ‘Aqiydah mbaya na bid’ah ambazo ni upotevu katika Dini Msikiti huo utakuwa ni wa kuleta madhara na unahitajiwa ususiwe na Waumini.

 

Katika mji mmoja kunaweza kuwa na majumaa hata zaidi ya mawili au kumi kutegemea wakaazi wenyewe na idadi yao iliyo kubwa. Ni vyema ikiwa Msikiti katika kijiji unawatosha Waumini basi wasianzishe Msikiti mpya wa Ijumaa. Lakini kukiwa na matatizo kama tulivyoyaeleza hapo juu basi itakuwa ni wajibu kuanzisha Msikiti huo.

 

Ama kuhusu masharti ya Ijumaa ni kama yafuatayo:

 

1.       Kuwe na jamaa, na jamaa ni kuanzia watu wawili, yaani Imaam na mtu mmoja kama maamuma.

2.       Jamaa iwe ni ya watu walio huru, wanaume, wakaazi na wenye akili timamu.

 

Yakipatakana masharti hayo tayari Msikiti huo unaweza kuswali Swalaah ya Ijumaa. Mbali na kuwa tumetangulia kusema ikiwa Msikiti mmoja unawatosha wakaazi wa mji basi hakuna haja ya kuwa na juma la pili.

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

Share