Baba Yetu Alitutupa Sasa Amefariki Nataka Kumsamehe, Mnashaurije?

Baba Yetu Alitutupa Sasa Amefariki Nataka Kumsamehe, Mnashaurije?

 

www.alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

assalam alaykum warahmatuh-llah wabarakatuh.

swala langu ni kuhusu babayangu, Aliyefariki kwanzia afariki sijawahi kumuombea mungu kwa sababu nilikuwa na uchungu sana wa kuwa hakuweza kutuangalia kwa lolote kwanzia kuzaliwa kwangu, na hata ndugu zangu.  Yaani ametutupa kwa kila kitu,kwahivyo hatukuwa na uhusiano hata kidogo twajua tu yule ndio baba yetu, kila nikikaa najiuliza kwa nini ametufanya hivi na alikuwa akijiweza hata kututazama alikuwa hakutaka tu!  Mpaka sasa ndio naona nimeanza kurudi nyuma manake nisingelipenda kumchukia mpaka ikafika hali ya zaidi ningelipenda kumuombea dua anisamehe na vile ashafariki mungu amsamehe. tafadha kwa kila shukrani munisaidie manake yananisumbua sana.ahsante.

 


 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Hapana shaka kutokana na hisia zako ulizokuwa nazo kuhusu aliyefariki mzazi wako kuwa zimetokana na hali ilivyokuwa baina yenu na aliyefariki mzazi wenu ambaye hakuwa akikutazameni. Lakini tunapenda kukumbusha kwamba vyovyote itakavyokuwa yeye ni mzazi wako, na pia hamuwezi kujua sababu gani alifanya hivyo. Kwa hiyo mpeni udhuru kwa kumdhania vizuri badala ya kumwekea dhana mbaya kama inavyopasa baina wa Waislamu. Juu ya hivyo kwa vile ni mzazi wako hakuna budi kumuombea kwani ni maamrisho kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala).

 

Kumsamehe makosa yake na kumuombe du’aa mzazi wenu kutapatikana faida kubwa kuliko kuzidi kuweka chuki. Kwani kwa vyovyote imeshatokea la kutokea na ima uchague kumuombea du’aa na kumfanyia wema ambao utaendelea kumfikia na kumnufaisha, au umwache aendelee kuteseka mzazi wako huko katika maisha yake ya Barzakh nawe huku ubakie na dukuduku, huzuni na dhiki? Ipi mojawapo itakayokupa wewe furaha? Bila ya shaka kumsamehe na kumfanyia wema!  Faida zenyewe ni zifuatazo:

 

1. Utakuwa umetekeleza amri za Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) za kuwaombea du’aa mzazi au wazazi wako.

 

2. Kila utakapomuombea Maghfirah atakuwa anapandishwa daraja moja juu, na hali itakuwa kama ilivyo katika usimulizi ufuatao:

 

 

عن أبي هريرة رضي الله عنه ، قال : قال رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّه عَلَيْه ِ وَ سَلَّمَ : إِنَّ الرَّجُلَ لَتُرْفَعُ دَرَجَتُهُ فِي الْجَنَّةِ   فَيَقُولُ : أَنَّى هَذَا ؟ فَيُقَالُ :باسْتِغْفَارِ  وَلَدِكَ لَكَ)) لإمام أحمد  و في سنن ابن ماجة أيضاً بإسنادٍ صحيح  

 

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakika mtu hupandishwa daraja yake Peponi. Kisha huuliza: Kwa ajili ya nini? [huku kupandishwa kwangu daraja?] Huambiwa: Kwa ajili ya kuombewa Maghfirah na mtoto wako)) [Ahmad, na katika Sunan Ibn Maajah ikiwa na isnaad Swahiyh]

 

3. Kumsamehe mtu ni sawa na kusamehewa wewe madhambi yako. Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipotaka kumgomea kuendelea kumsadiia jamaa yake ambaye alikuwa mmojawapo aliyechangia katika uzushi wa kumzulia mwanawe  Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anhaa), Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Akateremsha Aayah ifautayo:

 

((وَلاَ يَأْتَلِ أُوْلُوا الْفَضْلِ مِنْكُمْ وَالسَّعَةِ أَنْ يُؤْتُوا أُوْلِي الْقُرْبَى وَالْمَسَاكِينَ  وَالْمُهَاجِرِينَ فِي سَبِيلِ اللَّهِ وَلْيَعْفُوا  وَلْيَصْفَحُوا أَلاَ تُحِبُّونَ أَنْ يَغْفِرَ اللَّهُ لَكُمْ  وَاللَّهُ غَفُور ٌ رَحِيم))

((Na wala wasiape wale wenye fadhila miongoni mwenu na wenye wasaa wa mali kuwa hawatowapa (swadaqah) jamaa wa karibu, na masikini, na Muhaajiriyn katika njia ya Allaah. Na wasamehe na waachilie mbali. Je, hampendi Allaah Akughufurieni? Na Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu)) [An-Nuwr: 22]

 

Hisia zako tayari zinaonyesha kuwa unakaribia kumsamehe na hii ni alama ya iymaan na mapenzi ya kimaumbile baina ya mtoto na mzazi. Kwa hiyo usiache Shaytwaan akakughilibu na kukubakisha katika hali isiyomridhisha Mola wako Mtukufu wala kukuridhisha wewe nafsi yako. Muombee mzazi wako Maghfirah, muombee du’aa na mfanyie wema kama kwamba yuhai duniani.

 

Na la muhimu zaidi ni kuwa uwape nasaha ndugu zako wote nao wapate ujumbe huu na nyote mtapata malipo mema kutoka kwa Mola wenu.

 

Bonyeza kiungo kifuatacho kwa faida zaidi:  

 

‘Amali Za Kuwatendea Wazazi Waliofariki Waendelee Kupokea Thawabu

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share