Afanyeje Ili Aweze Kumrudia Mke Aliyemuacha Kwa Kukataa Kwake Kusilimu Sasa Anataka Kusilimu??

SWALI:

Assalam Alleykum. Natoa pongezi kwenu kwa kutupa elimu ya dini ya kiislam katika masuala mbalimbali.

Mimi ni muislamu ambaye nilifunga ndoa ya kiserikali na kuishi na mwanamke ambaye si muislam kwa muda wa miaka 6. Tulifanikiwa kupata watoto wawili. Nilimuacha mke wangu baada ya kujaribu kumshawishi abadili dini na yeye kuwa mzito katika hilo. Niliamua kuoa mwanamke mwingine ambaye ni muislam. Katika kipindi cha takribani miezi 4 iliyopita mwanamke niliyemuacha amekuwa akiniomba msamaha na kusema yupo tayari kusilimu na kuwa mke mwenza. Nipo katika mkakati wa kumrudia. Je ni mambo gani ambayo kwa taratibu za kislam ninapaswa kuyafuata na ambayo sistahili kuyafuata kuweza kumrudia na kuishi katika ndoa ya kiislam? Wabilah Tawfiq


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani  kwa swali lako kuhusu kumuoa mwanamke uliyeishi naye kwa miaka sita akiwa si Muislamu.  

Awali ya yote inatakiwa kwako kurudi kwa Allaah Aliyetukuka na kuomba msamaha kwa kuishi na mwanamke asiyekuwa Muislamu bila ya ndoa. Uazimie kabisa kuwa hutorudia tena kufanya kosa hilo maishani mwako kabla ya kumrudia huyo mwanamke uliyekuwa naye. 

Kisha baada ya wewe kuomba msamaha huo kwa Allaah Aliyetukuka, jaribu kumshawishi mwanamke huyo kuingia katika Uislamu mwanzo. Usiichukue kauli yake kuwa yeye anataka kusilimu tu, jambo hilo linatakiwa litiwe katika matendo ambayo ndio muhimu zaidi kwa maslahi yake. Baada ya kusilimu, muingize katika madrasah au markaz inayofundisha Dini inavyotakiwa na Uislamu. Kufanya hivyo utaweza kujilinda wewe na kumlinda na kizazi chenu kutokana na mitihani yanayowakumba wengi miongoni mwa wenye kuoa waliosilimu bila ya kuwapatia msingi wa Dini yenyewe. 

Kisha pia, hakikisha kuwa mwanamke huyo hana mimba na utaweza kujua kuwa hana mimba kwa kuwa utakuwa umechukua miezi kama 6 hadi mwaka katika kipindi cha yeye kusoma. Ukiona kuwa ameshika Dini endelea na mipango ya kumuoa na Allaah Aliyetukuka Atawatilia tawfiki na baraka. 

Kwa kuwa lengo la kumuoa ni Da’wah jaribu kushirikisha wazazi wake ambao si Waislamu katika ndoa japokuwa idhini haitotoka kwao ikiwa si Waislamu. Kuwashirikisha huko kutaweza kukupatia wewe fursa ya kuweza kuwaonyesha uzuri wa Uislamu na kuwavutia katika Uislamu. Na ujira wako kwa kufanya hivyo utaupata kwa Allaah Aliyetukuka. 

Yatakapotekelezeka yote hayo na akasilimu kikwelikweli mwanamke huyo baada ya kuujua Uislamu na ukaweza kumuoa, fanya uadilifu baina ya wake zako na dhihirisha Uislamu kwa mke wako aliyesilimu ili aweze kuipenda Dini hii ya Uislamu.

Tafadhali bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo na manufaa zaidi:

 

Amemuoa Mkristo Bila Kufuata Sheria Za Kiislamu Hataki Kuingia Katika Uislamu Nini Hukmu Yake Na Watoto Watakaozaa?

 

 

Kumsilimisha Kafiri Na Hukmu Ya Kuoana

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share