Nimedai Talaka Sababu Mume Ana Ukimwi Kisha Anataka Kuoa Mke Mwengine Nami Sikuwafiki

SWALI:

 

ASSALAM ALAYKUM.

KUNA TATIZO KUBWA LIMETOKEA NA NDOA IMEVUNJIKA NAOMBA UFAFANUZI WA KISHERIA

 

NINA NDUGU YANGU MWANAMKE JINA NALIHIFADHI ALIOLEWA NA BAADA YA MUDA MUMEWE ALIMWAMBIA KUWA YEYE MUME ANAVIRUSI VYA UKIMWI. WALIENDELEA KUISHI MUDA WA MIAKA ZAIDI YA MITATU BILA UNYUMBA NA BAADAE WALITUMIA MIPIRA KWA KUJAMII. NA BAADA YA HAPO MUME ALITAKA KUOA MKE MWINGINE NA HUYU NDUGU YANGU HAKUAFIKI HILO NA AKADAI TALAKA JE ALIFANYA MAKOSA IWAPO MUMEWE HAJAWAHI KUMWAMBIA KAMA AMEPONA VIRUSI? MWANZONI HATUKUJUA TATIZO MKE ALIAMUA KUMHURUMIA NA KUISHI NA MUME HUYO KWA TABU BILA JAMII KUJUA LAKINI SASA TUNAJUA BAADA YA MKE KUVUNJA NDOA. SHERIA INASEMAJE KUHUSU HAKI YA UNYUMBA AMBAPO KAMA KWELI MUME ALIKUWA NA VIRUSI NA MKE AKAVUMILIA KISHA MUME KUOA MKE MWINGINE NA HUYU WA KWANZA ALIPATA UNYUMBA KWA KONDOM BAADA YA MUDA MREFU WA KUKOSA UNYUMBA KABISA?


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani kwa swali lako kuhusu kudai talaka kwa mume mwenye virusi vya ukimwi.

Hakika iliyo wazi ni kuwa shari’ah imekataa kabisa watu kudhulumiana kwa namna moja au nyingine. Haifai mume kumdhulumu mkewe wala mke kumdhulumu mumewe.

 

Msingi mkubwa wa Uislamu ni ile Hadiyth ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

Haifai kudhuru wala kudhuriana” (Ibn Maajah).

Ni makosa kwa mwanamme au mwanamke anayetaka kuoa au kuolewa kuficha hali yake ya maradhi ambaye yanaweza kumdhuru mwenziwe. Na kujulikana kwa hali hiyo ikiwa imefichwa ni sababu moja ya mtu kuomba talaka akiwa ni mwanamke. Mwanamke huyo alikuwa ana haki ya kudai talaka pale mumewe alipomuambia kuwa yeye ana ukimwi kwani kufanya tendo la ndoa hata kwa kutumia kondom si hakika au usalama wa kuhifadhika kwani kondomu haizui mia kwa mia mtu kupatwa na ugonjwa huo.

 

Kosa linakuja kwa dada huyo kukasirika pale mumewe anapotaka kuoa mke wa pili ambalo ni jambo la kishari’ah akiweza kutimiza masharti yake. Inaonyesha wakati wa kutafuta haki zake amepaacha na wakati alipokuwa hana haki ndio anakurupuka kwa mkurupuko wa kishaytwaan kudai talaka. Ikiwa dada huyo amepitia mengi kwa kusubiri ana thawabu kwa Mola wake haifalii kwake kubomoa yote hayo kwa dakika chache. Huenda alikuwa hajui hayo na hivyo anafaa aombe msamaha na maghfira kwa Mola wake, kwani Yeye ni Mwingi wa kusamehe.

 

Kisha nasaha yetu kuu kwake ni dada yetu kwenda kupima hospitali kuhakikisha kama yu salama au naye ameambukizwa. Ikiwa naye atakuwa amepata virusi hivyo itabidi akija kuposwa amwambie wazi mwanamme kuwa yeye ana virusi hivyo. Na pia atume watu wamshauri mtalaka wake kuwa anapokwenda kuposa aieleze hali yake hiyo ya ugonjwa huo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share