Inafaa Kukubali Mwaliko Wa Anayedanganya Serikali Kuwa Wametengana (Seperation)

 SWALI:

KATIKA MAISHA YA HAPA UENGEREZA WENGI WETU TUMEDANGANYA KWA KUSEMA TUMETOKA KATIKA NCHI YENYE VITA AMBAYO SIO HALISI NCHI ULIOKUA UNAISHI AU RAIA WA NCHI HIO, VILEVILE TUMETUMIA MANENO YA UONGO KWA AJILI YA KUTAKA TUPATE KUKUBALIWA KUISHI, JEE HII NI HALALI?

(b) KATIKA NCHI HIO KUNA SHERIA ZAKE, KAMA HUWEZI KUFANYA KAZI MPAKA UWE NA RUHUSA YA KUFANYA KAZI, NA KAMA HUNA HIO RUHUSA HUWA UNASAIDIWA KWA PESA ZA KUWEZA KUPATA KULA NA UNA PEWA PA KUKAA, JEE UNAPOVUNJA SHERIA HIO NA UKAFANYA KAZI KWA KUTAKA KUTUMIA JASHO LAKO HIO PESA UTAKAYO IPATA ITAKUA NI HALALI?

(C) WATU WENGINE WANAISHI PAMOJA KINDOA LAKINI MKE ANASEMA HANA MUME NA ANAPO PATA RIZKI YA MTOTO ANASEMA AMEPATA MWANAMUME KWA USIKU MMOJA NA AKAPATA UJA UZITO YOTE HAYA YANAKUJA KWA KUFICHA UKWELI KWANI AKISEMA ANA MUME ATATAKIWA MUME KUMHUDUMIKIA MKE NA MTOTO KWA KUWALIPIA PA KUKAA NA KULA NAO WANAYAKIMBIA HAYO MAJUKUMU, JEE HII NI HALALI. NA MTU KAMA HUYU AKIKUALIKA CHAKULA NYUMBANI KWAKE JEE INAFAA KUITIKIA MWITO WAKE?


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani kwa swali lako kuhusu mas-ala ya kudanganya ili kupata maslahi mbalimbali kutoka katika nchi za Ulaya.

Ifahamike kuwa uongo wa aina zote haukubaliki katika Uislamu kabisa. Muislamu ni yule mwenye sifa ya ukweli na kuwa na marafiki walio wakweli. Hivyo kwa kila hali Muislamu anafaa awe mkweli.

Kwa hiyo, haifai kwa Muislamu kudanganya ili kupata maslahi ya aina yoyote yale.

Ikiwa ni kanuni ya nchi kuwa ikiwa hufanyi kazi utakuwa ni mwenye kupatiwa pesa basi hufai kufanya kazi au ukifanya kazi basi urudishe pesa unazopewa kama posho yako.

Hivyo, ukifanya kazi pesa unayopewa haitakuwa halali kwako.

Ni makosa kama tulivyosema kudanganya, kwa hiyo ikiwa umeolewa inafaa useme umeolewa hata kama utakosa pesa za kutoka serikalini.

Kwa kudanganya kuwa mtu amezini au alipata mwanamme kwa usiku mmoja na akazaa naye, hiyo hakika ni udhalili na ushaytwaan usio na mfano kabisa! Ni utumwa wa mali uliosababishwa na kukosa hayaa na Iymaan ya Dini kabisa!

Na isitoshe huko ni kuutukanisha Uislamu na kujidhalilisha kuwa wewe ni Malaya na kiumbe mchafu usiye na thamani mbele ya Allaah na mbele ya wanaadamu.

Tuwe na tahadhari sana tusije tukajiingiza kwa mikono yetu Motoni.

Kuitikia mwito wa aliyekualika ni miongoni mwa haki za Muislamu kwa Muislamu mwenziwe. Hivyo, ni muhimu sana kuweza kuitikia mwito huo bila ya kuingia katika madhambi yoyote yale.

Ikiwa Muislamu amekualika nenda ila tu ukiwa na yakini asilimia 100 kuwa mapato yake ni ya haramu ndio unapaswa usiende. Hata hivyo, unatakiwa uwe ni mwenye kumnasihi sana kila mara na kila wakati ili aweze kujimudu kujitoa katika madhambi hayo.

Hili ni kwa mujibu alivyotuambia Jariyr bin ‘Abdillaah (Radhiya Allaahu ‘anhu) pale aliposema:

Nilimbai (nilimpa mkono wa utii) Mtume wa Allaah (Swala Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika kusimamisha Swalaah, kutoa Zakaah na kumnasihi kila Muislamu” (Muslim).

Kadhalika umjulishe uharamu na ubaya wa kula chumo cha haramu na kwamba mlaji haramu hazikubaliwi du’aa zake na matendo yake mengine kama Hadiyth ifuatayo inavyotujulisha.

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye alisema:  Mtume wa Allaah (Swala Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema:

Allaah ni Mwema na Anakubali kilicho chema tu. 

Allaah Ameamrisha kasema "Enyi Mitume Kuleni katika vitu vyema na mfanye yaliyo sawa." Allaah  Akasema: "Enyi mlioamini kuleni katika vitu vyema ambavyo tumekuruzukuni”

Kisha akataja (kisa cha yule) mtu aliyesafiri safari ndefu, kachafuka na kajaa mavumbi na huku anayanyua mikono yake mbinguni akisema "Ee Mola! Ee Mola! Nipe kadhaa, nikinge na kadhaa… wakati chakula chake cha haramu, na kinywaji chake ni cha haramu, na kivazi chake ni cha haramu, na anakuzwa na haramu, je, vipi atajibiwa (du’aa zake?)

Imesimuliwa na Al-Bukhaariy na Muslim

Tafadhali bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo na manufaa zaidi:

Nasaha Kwa Wakimbizi Wanaoishi Kusema Hawajaoana Ili Wapate Ruzuku Ya Serikali

Mkimbizi Anapokea Pato La Serikali Kwa Kudanganya, Je, Anaweza Kutoa Zakaah Dhahabu Zake Au Sadaqah Na Hizo Pesa?

Pesa Anazopewa Za Ukimbizi Zinafaa Ajenge Msikiti Au Atoe Sadaka Kwa Waislamu?

Kutoa Sadaka Na Pesa Za Kusaidiwa Na Serikali Na Zile Za Chumo La Haraam

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Atuepushe na madhambi madogo kwa makubwa.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share