Siku Kumi Za Mwisho Za Ramadhwaan

Siku Kumi Za Mwisho Za Ramadhwaan

Shaykh Swaalih Ibn Fawzaan Al-Fawzaan

Imetarjumiwa na: Ummu Iyyaad

www.alhidaaya.com

 

 

 

عَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا قَالَتْ : "كَانَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ إِذَا دَخَلَ الْعَشْرُ أَحْيَا اللَّيْلَ وَأَيْقَظَ أَهْلَهُ وَجَدَّ وَشَدَّ الْمِئْزَرَ" رواه البخاري (2024) ومسلم (1174)

Imepokelewa kutoka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) kwamba: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa pindi zilipoinga kumi za mwisho, akikesha usiku na akiamsha ahli zake na akijitahidi na kukaza shuka yake." [Al-Bukhaariy, Muslim]

     

Hadiyth hii ni uthibitisho kuwa siku kumi za mwisho za Ramadhwaan zina fadhila mahsusi na adhimu kuliko siku nyenginezo ambazo Muislamu inampasa aongeze utiifu na kutekeleza ‘ibaadah kama kuswali, kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kusoma Qur-aan.

 

‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) amtuelezea hali ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) inavyokuwa kama ni mfano bora kabisa kwa sifa nne zifuatazo:

 

1-Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akikesha katika ‘ibaadah.

 

Alikuwa halali usiku. Kwa hiyo yeye Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akikesha usiku mzima kufanya ‘ibaadah na akihuisha nafsi yake kwa kutumia usiku wake kukaa macho na kuacha kulala. Hii ni kwa vile kulala usingizi ni mauti madogo. Maana ya "akihuisha (akikesha usiku)" ni kwamba yeye Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akitumia wakati huo katika hali ya Qiyaam (kusimama kuswali usiku) na kufanya ‘ibaadah ambazo zinatendwa kwa ajili ya Allaah, Rabb wa walimwengu. Inatupasa tukumbuke kuwa siku kumi za mwisho za Ramadhwaan ni chache zilizokadariwa kwa idadi.

 

Ama kuhusu ilivyonukuliwa katika Hadiyth ya 'Abdullaah Ibn ‘Amr, imekatazwa kukesha usiku mzima katika Swalaah, hii inahusu mtu anayefanya hivyo kwa mfululizo wa siku zote za mwaka.

 

  

2-Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiamsha ahli zake.

 

Ni wake zake waliotakasika ambao ni Mama wa Waumini, ili nao wanufaike katika ‘ibaadah hizo za kumdhukuru Allaah na ‘ibaadah nyenginezo katika siku hizo zenye baraka nyingi.

 

 

3-Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akifanya bidii.

 

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akijizuia na akijitahidi sana katika ‘ibaadah, akiongeza ‘amali njema zaidi kuliko alivyokuwa akifanya siku ishirini za mwanzo (wa Ramadhwaan). Akifanya hivi kwa sababu Laylatul-Qadr inatokea katika usiku mmoja wa siku hizo kumi.  

 

 

4-Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikaza shuka yake.

 

Alikuwa akijihimiza na kufanya bidii kubwa katika ‘ibaadah nzito. Inasemekeana vile vile Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akijitenga na wake zake. Hii ni kauli iliyo sahihi zaidi kwa vile inakubaliana na ilivyotajwa kabla katika Hadiyth ya Anas (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akikunja kitanda chake na akijitenga na wake zake" [Latwaaif-ul-Ma'aarif, Uk. 219]

 

Vile vile Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akifanya I'tikaaf katika siku za mwisho za Ramadhwaan na watu wenye kuwa katika hali ya I'itikaaf hujizuia kujamii na wake zao.

 

Kwa hiyo enyi ndugu Waislamu, jitahidini kujizoesha na kuwa katika sifa na khulka hizi. Na tekelezeni Swalaah za usiku pamoja na Imaam hata baada ya kuswali Taraawiyh ili jitihada zenu katika siku hizi kumi za mwisho zipindukie siku ishirini za mwanzo na ili mpate kufaulu kupata sifa ya "kuuhuisha usiku kwa ’ibaadah" kwa kuswali. 

 

Na ni lazima muwe na subira katika utiifu wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na ‘ibaadah za usiku kwani hakika Tahajjud ni ngumu lakini thawabu zake ni kubwa sana. Naapa kwa Allaah, ni fursa kubwa katika maisha ya Muislamu na vile vile ni faida kubwa kuitumia fursa hii kwa yule aliyejaaliwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Kwani mwana Aadam hawezi kujua kama ataweza kuchuma tena thawabu nyingi kama hizi, ambazo zitamfaa katika maisha yake ya dunia na ya Aakhirah. 

 

Salafus-Swaalih (Wema waliotangulia) wa Ummah huu walikuwa wakijitahidi katika ‘ibaadah za masiku haya kwa kuzirefusha Swalaah za usiku. As-Swaa'ib bin Yaziyd amesema, "'Umar bin Al-Khattwaab alimuamrisha Ubay bin Ka'ab na Tamiym Ad-Daariy kuimamisha watu katika Swalaah kwa Raka'ah kumi na moja. Imaam alikuwa akisoma Aayah mia moja hadi ilibidi tuegemee mkongojo kwa sababu ya kisimamo kirefu, na tulikuwa hatupumziki hadi inapoanza kuingia Alfajiri".  [Al-Muwattwa, Mjalada 1, Uk. 154]

 

'Abdulllaah Bin Abiy Bakr amesema "Nimemsikia baba yangu akisema, wakati wa Ramadhwaan, tulikuwa tukichelewa  kumaliza Swalaah za usiku hata tukiwahimiza watumishi kutuwekea suhuwur (daku) kwa kuogopa Alfajiri isitufikie"  [Muwattwa ya Imaam Maalik, Mjalada 1, Ukurasa 156]

 

Nafsi ya Muumini inapambana na jitihada mbili katika Ramadhwaan; Jitihada ya mchana kwa swiyaam na jitihada ya usiku kwa Qiyaam. Kwa hiyo yeyote atakayejumuisha jitihada mbili hizi na akatimiza haki zake, basi yeye atakuwa miongoni mwa wenye subira kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 إِنَّمَا يُوَفَّى الصَّابِرُونَ أَجْرَهُم بِغَيْرِ حِسَابٍ ﴿١٠﴾

  Hakika wanaosubiri watalipwa kikamilifu ujira wao bila ya hesabu. [Az-Zumar: 10]

 

Siku kumi hizi ni za mwisho katika mwezi mtukufu huu, na ‘amali za Muislamu zinazohesabika zaidi ni zile za mwisho, kwa sababu huenda akafaulu kukutana na usiku wa Laylatul-Qadr wakati akiwa amesimama katika Swalaah ikawa ni fursa nzuri ya kufutiwa madhambi yake yote na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).

 

Ni wajibu wa kila mtu kuamsha na kuhimiza na kushurutisha familia yake kutekeleza ‘ibaadah khasa nyakati hizi tukufu, kwani hakuna atakayedharau kufanya hivi ila yule aliyenyimwa fadhila hizi.  Jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba wakati wengine wako katika ‘ibaadah khasa za masiku haya kumi, wengine wanatumia wakati wao katika vikao vya maasi. Hakika hii ni khasara kubwa.

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atuhifadhi na Atuhidi. 

 

Kwa hiyo Muislamu atakayejishughulisha na ‘ibaadah katika siku kumi hizi za mwisho atakuwa amejiingiza katika milango ya kuchuma mema yaliyobakia katika mwezi huu mtukufu. Ni khasara kwa mtu aliyeanza mwezi wa Ramadhwaan kusimama kwa nguvu kuswali, kusoma Qur-aan na dhikru-Allaah kisha siku za mwisho akawa na mzito na mvivu katika kufanya ‘ibaadah na hali hizi siku za mwisho ndio siku muhimu na zenye uzito wa thawabu za kusimama kuswali na kadhaalika kuliko zote. Hivyo kila mmoja inampasa aongeze bidii zaidi na kujitahidi kwa kadiri awezavyo kuongeza ‘ibaadah katika kumalizia mwezi mtukufu huu. Na kukumbuka kuwa ‘amali za mtu zinahesabika zile za mwisho.

 

Du’aa ya Laylatul-Qadr:

 

Katika siku hizi kumi za mwisho ni vizuri sana kuisoma du'aa hii kila mara khasa katika usiku wa Laylatul-Qadr kama ilivyothibiti katika Hadiyth ifuatayo:

 

عَنْ عَائِشَةَ , أَنَّهَا قَالَتْ : يَا رَسُولَ اللَّهِ  أَرَأَيْتَ إِنْ وَافَقْتُ لَيْلَةَ الْقَدْرِ مَا أَدْعُو؟ , قَالَ : ((تَقُولِينَ : اللَّهُمَّ إِنَّكَ عَفُوٌّ تُحِبُّ الْعَفْوَ فَاعْفُ عَنِّي))  ابن ماجه و صححه الألباني

Imepekelewa kutoka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) amesema: “Ee Rasuli wa Allaah! Je nitakapojaaliwa kufikia Laylatul-Qadr niombe nini?" Akasema, ((Sema: Allaahumma Innaka 'Afuwwun Tuhibbul-'Afwa fa'fu 'anniy - Ee Allaah Hakika Wewe Ndiye Mwenye Kusamehe Unapenda Kusamehe basi Nisamehe)) [Ibn Maajah na kaisahihisha Al-Albaaniy]     

 

 

 

Share