Soko La Ramadhwaan Hiloo Linafunguliwa Na Karibu Kufungwa!

 

Soko La Ramadhwaan Hiloo Linafunguliwa

Na Karibu Kufungwa!

 

Muhammad Faraj Saalim As-Sa’ay (Rahimahu-Allaah)

 

Alhidaaya.com

 

 

Ndugu Zangu Waislamu

 

Soko la Ramadhwaan ndiyo kwanza linafunguliwa na hiloo linakaribia kufungwa.

 

Ndugu Zangu Waislamu

 

Ramadhwaan ni Soko linalofunguliwa kila mwaka kisha likafungwa, hupata faida ndani yake mwenye kutaka kupata faida na hula hasara mwenye kutaka kula hasara.

 

Ramadhwaan ni soko tulilowekewa na Rabb wetu Mtukufu (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa ajili ya kuchuma ndani yake thawabu nyingi kiasi cha uwezo wa mtu. Soko liko wazi na milango yake iko wazi na idadi yake ni ishirini na tisa au thelathini tu haizidi, na kila siku mlango mmoja unafungwa. Kwa hivyo anayetaka kuwahi na awahi.

 

Ndugu Zangu Waislamu

 

Inatupasa kuukaribisha mwezi huu kwa furaha na tabasamu na kwa moyo mkunjufu, kwani ndani yake mna kheri nyingi sana, na baina yake na baina ya Ramadhwaan nyingine Allaah husamehe madhambi mengi sana yakiepukwa yale makubwa.

 

Ndugu Zangu Waislam

 

Kutokana na manufaa mengi yaliyomo ndani ya mwezi huu, Rasuli wetu mtukufu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiusubiri kwa hamu kubwa sana.

 

Huyu ni Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyekwisha samehewa madhambi yake yaliyotangulia na yale yanayofuatilia, Nabiy aliyekabidhiwa funguo zote za hazina za ardhini. Alikuwa mara unapoingia mwezi huu akiikaza barabara nguo yake ya chini (saruni) na nyakati za usiku akiwaamsha watu wake ili wajishughulishe na ibada ndani yake, na hii ni kwa sababu alikuwa akiujua vizuri utukufu wa Mola wake na alikuwa akiitambua vizuri zawadi aliyowatayarishia waja Wake wanaoshindana katika kufanya mema ndani ya mwezi huu.

 

Imepokelewa pia katika athar kuwa Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) walikuwa wakimuomba Rabb wao kabla ya Ramadhwaan kwa miezi sita ili awafikishe mwezi huu, na baada ya kumalizika mwezi wa Ramadhwaan walikuwa wakiendelea kumuomba Allaah kwa muda wa miezi sita mingine ili azikubali ‘amali zao njema walizofanya ndani yake na ili awaghufirie madhambi yao.

 

Starehe Ya Dunia:

 

Walikuwa wakifanya yote hayo kwa sababu walikuwa wakitambua vizuri kuwa starehe za dunia ni haba sana.

 

Allaah Anasema:

 ۗ قُلْ مَتَاعُ الدُّنْيَا قَلِيلٌ

Sema Starehe ya dunia ni chache [An-Nisaa: 77]

 

Starehe za dunia hakika ni ndogo sana, kwani tukichukulia mfano wa mwezi huu wa Ramadhwaan ambao ndani ya mchana wake utamuona mtu aliyefunga, akijishughulisha kukusanya kila aina ya vyakula. Sambusa, mikate ya chila maandazi n.k. Lakini magharibi inapoingia akishakula tende na kunywa gilasi ya maji, na baada ya kuswali Magharibi akarudi nyumbani na kunywa bakuli lake la uji, ile hamu ya kula vile alivyojikusanyia wakati wa mchana ishaondoka. Hana hamu tena ya kula hata kama chakula hicho ni kizuri namna gani, na iwapo atajilazimisha kula basi atakuwa anajitafutia mwenyewe matatizo katika tumbo lake.

Kwa ajili hii Allaah Akatujulisha kuwa starehe za dunia ni haba sana. Ama starehe za huko Jannah ni kubwa, nyingi na hazichoshi.

 

Allaah Anasema: 

 

خَالِدِينَ فِيهَا لَا يَبْغُونَ عَنْهَا حِوَلًا ﴿١٠٨﴾

 Ni wenye kudumu humo hawatotaka kuihama. [Al-Kahf: 108]

 

 

Kwani huko hakuna kushiba wala kukinai, isipokuwa ni kufaidika na kutaladhadh kusikokuwa na mwisho. Ladha ya chakula, ladha ya mandhari nzuri nzuri, ladha zote za huko hazikatiki wala hazichoshi.

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

“Al-Firdaws ni sehemu ya juu huko Jannah, ipo kati kati, na hiyo ndiyo sehemu iliyo bora kupita zote”.

 

Na katika [Al-Bukhaariy na Muslim], Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Mnapomuomba Allaah, basi muombeni Al-Firdaws, kwani hiyo ipo sehemu ya juu kabisa na kati kati ya Jannah, na hapo ndipo chemchem za mito ya Jannah inapoanzia”.

 

“Kwa ajili hiyo” anasema Ibn Kathiyr:

 

“Allaah Anaposema: “Hawatataka kuondoka humo”, maana yake ni kuwa hawatachoka kutizama mandhari zake na hawatopenda kuchagua mahali pengine badala yake, na hawatopenda kuhamishwa kutoka hapo”.

 

Vyakula Vya Jannah:

 

Ama starehe ya vyakula vya huko inakhitalifiana na starehe ya vyakula vya hapa duniani, kwani huko hakuna kushiba wala kukinai, bali ni kustarehe na kutaladhadh tu.

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema;

“Watu wa Jannah wanakula na kunywa, hakuna kwenda haja ndogo huko wala haja kubwa wala kutema mate.”

Wakamuuliza;

“Vipi chakula (kitatokaje tumboni)?”

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

“Kinatoka kwa njia ya jasho lenye harufu ya Miski. Aliye katika daraja la chini kabisa Jannah, anahudumiwa na watumishi elfu kumi, kila mmoja kati yao anabeba sinia mbili (za vyakula), moja ya dhahabu na moja ya fedha zenye rangi tofauti, ladha anayoipata katika chakula alichokula ndani ya sinia ya mwanzo ni ile ile anayoipata katika sinia ya mwisho.” [Ibn Abi Duniya, At-Twabaraaniy na ameisahihisha Al-Mundhiry katika kitabu chake cha At-Targhiyb wat-Tarhiyb].

 

Na Allaah Anasema: 

وَإِذَا رَأَيْتَ ثَمَّ رَأَيْتَ نَعِيمًا وَمُلْكًا كَبِيرًا﴿٢٠﴾

Na utakapoona huko, utaona neema na milki adhimu” [Al-Insaan: 20]

  

Qiyaamul Layl Ya Ramadhwaan (Tarawiyh)

  

Umuhimu wa Swalaah:

 

Tukiwa bado tumo ndani ya soko la Ramadhwaan leo tutalitembelea angalau kwa ziara fupi soko la Swalaah, soko ambalo ndani yake mna faida nyingi zaidi kupita biashara zote nyingine.

 

Swalaah ni nguzo ya pili ya Kiislamu baada ya Shahada mbili, na Swalaah ni ibada anayoipenda sana Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), na daraja yake ni kubwa kupita ibada zote zilizobaki, nayo ni nguzo ambayo kwayo Dini inasimama juu yake.

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Kichwa cha jambo ni Uislaam na nguzo yake ni Swalaah na kilele chake ni Jihaad”.

 

Na Swalaah ni ‘amali ya mwanzo atakayoulizwa mja siku ya Qiyaamah. Ikikubaliwa, basi ‘amali zote zilizobaki zitakubaliwa, ama ikikataliwa basi zilizobaki nazo pia zitakataliwa, kwani tofauti iliyopo baina yetu na baina ya makafiri ni Swalaah.

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliendelea kuusia juu ya Swalaah katika maisha yake yote na hata pale alipokuwa akivuta pumzi zake za mwisho alikuwa akiusia huku akisema:

 

“Swalaah Swalaah na kilichomilikiwa na kuume kwenu”.

 

Swalaah za Sunnah:

 

Allaah Ametuwekea shari’ah ya kuswali Swalaah za Sunnah ili zipate kutusaidia katika kuinyanyua Swalaah ya Fardhi kutokana na makosa au upungufu wowote unaopatikana ndani yake kutoka kwetu.

 

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“La mwanzo atakaloulizwa mja siku ya Qiyaamah katika ‘amali zake ni Swalaah. Allaah Atawaambia Malaika wake akiwa Yeye ni mwenye kujua zaidi:

“Tizameni katika Swalaah ya mja Wangu. Ameitimiza au hakuitimiza”.

Ikiwa ameitimiza, basi ataandikiwa thawabu za Swalaah iliyotimia, ama ikiwa imepungua chochote ndani yake, basi Allaah Atasema;

“Tizameni ikiwa mja Wangu ameswali Swalaah za Sunnah”.

Ikiwa anazo Swalaah za Sunnah, atasema:

“Mtimizieni mja Wangu fardhi yake kutoka katika Sunnah zake.” Kisha ‘amali zilizobaki zitakubaliwa kwa njia hiyo.” [Abu Daawuud]

 

Kutokana na Hadiyth zilizotangulia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatuwekea shari’ah ya kuswali Swalaah za Sunnah, na akaitilia nguvu sana katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhwaan kwa kutuwekea shari’ah ya kuswali Swalaah ya Qiyaam Ramadhwaan (Taraawiyh).

 

Qiyaam Ramadhwaan pia inajulikana kwa jina la ‘Taraawiyh’ (mapumziko), kwa sababu Swahaba wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) walikuwa wanaposwali Swalaah hii wakipumzika baada kila rakaa nne, na Swalaah hii ni Sunnah kwa wanawake na wanaume.

 

Anasema Irfijah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa:

 

‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akiamrisha watu kuiswali Jamaa’ah Swalaah ya Qiyaam Ramadhwaan (Taraawiyh), na alikuwa akimweka Imaam mwanamume upande wa wanaume na Imaam mwanamke upande wa wanawake na mimi nilikuwa Imaam wa wanawake”. [Al-Bayhaqiy na Fiqhus Sunnah, Sayyid Saabiq]

 

Swalaah hii huswaliwa baada ya Swalaah ya ‘Ishaa na kabla ya Swalaah ya witri na huswaliwa rakaa mbili mbili, na inaweza pia kucheleweshwa mpaka wakati wowote katika nyakati za usiku.

 

Imepokelewa na imaam wa Hadiyth wa Ahlus Sunnah kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa amesema: “Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akipendekeza watu waiswali Swalaah hii lakini bila kulazimisha. Alikuwa akisema:

 

“Atakayeswali Qiyaam Ramadhwaan kwa imani na kwa kutaraji thawabu, atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia”.

 

Hii ni neema kubwa sana ambayo hatoiacha isipokuwa yule ambaye hana madhambi aliyotanguliza.

 

Na imepokelewa na Imaam wote wa Ahlus Sunah isipokuwa At-Tirmidhiy kutoka kwa Bibi ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu anhaa) kuwa amesema:

 

“Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali Msikitini, na watu wengi wakaswali pamoja naye, kisha akaswali tena siku ya pili yake na watu wakaongezeka, kisha wakakusanyika usiku wa tatu, lakini Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwatokea. Ulipoingia wakati wa asubuhi akasema;

“Nilikuoneni mlichofanya (kuningoja kwenu), na hakuna kilichonizuwia nisitoke nikasali pamoja nanyi isipokuwa nilihofia isije ikafaridhishwa juu yenu”. Na hii ilikuwa katika mwezi wa Ramadhwaan.

 

Idadi Ya Rakaa Zake:

 

Imepokelewa kutoka kwa Bibi ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu anhaa) kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hajapata kuswali zaidi ya rakaa kumi na moja, iwe katika mwezi wa Ramadhwaan au mwezi mwingine wowote ule, ingawaje zipo baadhi ya riwaya ambazo Shaykh Al-Albaaniy anasema kuwa zina udhaifu ndani yake zinazosema kuwa Swahaba wengine (Radhwiya Allaahu ‘anhum) walikuwa wakisali rakaa ishirini.

 

Kuiswali Jamaa’ah:

 

Taraawiyh inaweza kuswaliwa Jamaa’ah na pia anaweza mtu kuiswali peke yake, isipokuwa ’Ulamaa wengi wanaona kuwa kuiswali Jama’ah Msikitini ni bora zaidi, ingawaje wapo wanaoona kuwa kuiswali nyumbani ni bora zaidi na kila mmoja anazo hoja zake.

 

Tulitangulia kueleza kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliiswali Jama’ah Swalaah hii na akasema kuwa hakuna kilichomzuia kuendelea kufanya hivyo isipokuwa kwa ajili ya kuwahofia ummati wake isije ikateremshwa amri ya kufaridhishwa, kisha ‘Umar bin Al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) wakati wa ukhalifa wake akawakusanya watu wawe wanaiswali Jamaa’ah nyuma ya Imaam mmoja.

 

Anasema ‘Abdur-Rahmaan bin ‘Abdil-Qaariy:

 

“Nilitoka usiku mmoja katika mwezi wa Ramadhwaan mimi na ‘Umar bin Al-Khatwaab kuelekea Msikitini, tukawaona watu wamegawanyika na kufarikiana, kila mmoja anaswali peke yake. Mtu anakuwa anaswali peke yake kisha kundi lingine (linakuja na) linaswali nyuma yake. ‘Umar akasema:

 

Mimi naona ikiwa tutawakusanya wote wasali nyuma ya imamu mmoja itakuwa bora. Kisha akafanya hivyo na akamweka Ubay bin Ka’ab awasalishe watu. Kisha nikatoka naye usiku uliofuata na tukawaona watu wote wanasali nyuma ya imamu mmoja akasema;

 

‘Ni’mal bid’at haadhihi’ “Jitihada jema sana hii na ile wanayolala ikawapita ni bora zaidi kuliko wanayoiswali”, akikusudia kuwa kuiswali nyakati za mwisho za usiku ni bora zaidi.

 

Neno Bid’ah alotumia ‘Umar bin Al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) katika riwaya hii halina maana ya ‘Uzushi’, kwani ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) hawezi kuwa mzushi, bali Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha kuwa atakalotufundisha ‘Umar au yeyote kati ya Makhalifa walioongoka (Radhwiya Allaahu ‘anhum) Khulafaa Raashidiyn ni katika Sunnah.

 

Kutoka kwa Al-Irbaadh bin Saariyah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema:

 

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitutolea mawaidha yaliyoingiza hofu nyoyoni na kututoa machozi machoni. Tukamuuliza; ‘Ee Rasuli wa Allaah kama kwamba mawaidha (haya ni) ya kutuaga?’

Akatuusia, akasema:

“Nakuusieni kumcha Allaah na kusikia na kutii hata akiwa amri wenu mtumwa, kwani atakayeishi kati yenu ataona khitilafu nyingi, kwa hivyo ni juu yenu kufuata Sunnah yangu na Sunnah za Makhalifa waadilifu walioongoka (katika riwaya nyingine amesema; “watakaokuja baada yangu) muzibane Sunnah zao kwa magego…” [Imepokelewa na At-Tirmidhiy na Abu Daawuud na Ibn Maajah na wengineo].

 

Hii ni sawa na muadhini wa pili aloongeza ‘Uthmaan bin ‘Affaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) wakati wa ukhalifa wake, muadhini ambao wakati wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) haukuwepo, lakini ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliyetawala ukhalifa baada yake aliuendeleza na wala hakuusimamisha, na hii ni kutokana na fahamu yao Makhalifa hawa juu ya Hadiyth iliyotangulia iliyosimuliwa na Al-Irbaadh bin Saariyah (Radhwiya Allaahu ‘anhu).

 

Kwa ajili hiyo neno Bid’ah, alokusudia ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) hakukusudia Bid’ah ya upotofu (kullu bid’atin dhwalaalah), bali alikusudia Bid’ah ya kilugha na si ya kidini na maana yake ni ‘jitihada jema’ (Mubdi’u), kwani ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ni mcha Allaah kuliko hao wanaojaribu kumkosoa na ni mtu wa mwisho kabisa kutegemewa kuleta uzushi katika Dini.

 

Na ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) asingeruhusu watu waiswali Jamaa’ah Swalaah hiyo angekuwa hakumuona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiiswali Swalaah hii Jamaa’ah pamoja na Swahaba wake (Radhwiya Allaahu ‘anhum), yeye mwenyewe (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa Imaam wao, na akaacha kuendelea kufanya hivyo kwa kuhofia wasije wakafaridhishiwa. Ama baada ya kufa kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ile hofu ya kufaridhishiwa ikaondoka kwa kukatika kwa Wahyi, na Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) walikuwa wakiiswali Jamaa’ah Swalaah hiyo, isipokwa walikuwa wakisali kila kundi nyuma ya Imaam yeyote yule, na Jamaa’ah zikawa nyingi Msikitini wakati mmoja, na kwa ajili hiyo ‘Umar akawakusanya ili waiswali nyuma ya Imaam mmoja.

 

Udhuru aloutoa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pale alipoacha kutoka na kuswali nao ulikuwa:

 

“Hakuna kilichonizuwia nisitoke kuswali pamoja nanyi isipokuwa……” hii ikimaanisha kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akitamani kutoka na kuswali pamoja nao, isipokuwa hofu yake ilikuwa ni moja tu, nayo ni kuwa Isije Ikafaridhishwa juu yao.

 

Anasema Imaam Maalik katika Muwattwaa kuwa:

 

“Swalaatut-Taraawiyh ni Sunnah iliyotiliwa nguvu, na kwa ajili hiyo Makhalifa wote waongofu (Radhwiya Allaahu ‘anhum) waliitilia mkazo Swalaah hii wakiwemo ‘Uthmaan na ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhum) na wakawa wanaipendekeza kuswaliwa Jamaa’ah wanaume na wanawake pia.

 

“Ama kauli yake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema:

 

“Nilihofia isije ikafaridhishwa juu yenu”, anaendela kusema Imaam Maalik:

 

“Anasema Al-Qaadhiy Abu Bakr kuwa huenda ikawa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alifunuliwa kuwa akiendelea kuiswali pamoja nao itakuja faridhishwa, au labda alidhania tu kuwa huenda ikafaridhishwa, au huenda akawa anahofia asije mmoja katika umati wake atakaposikia kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiiswali siku zote Swalaah hiyo katika Jamaa’ah akadhania kuwa ni fardhi kisha akawajulisha watu hiyvo kisha watu wakaionea uvivu” [Mwisho wa maneno ya Imaam Maalik].

 

Imepokelewa pia kutoka kwa [Abu Daawuud na An-Nasaaiy na Ibn Maajah na Al-Haakim na At-Tirmidhy], na lafdhi ya Hadiyth hii ni ya Imaam At-Tirmidhiy kama ilivyoandikwa katika sharh ya Tuhfatul-Ahwadhiy anasema:

 

“Kutoka kwa Abu Dharr amesema: ‘Tulifunga pamoja na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na hakuswali pamoja na sisi (Swalaah ya Taraawiyh) mpaka zilipobaki siku saba kabla kumalizika mwezi (wa Ramadhwaan), akatuswalisha Taraawiyh mpaka ilipomalizika thuluthi ya mwisho. Kisha usiku wa sita (kabla ya kumalizika kwa Ramadhwaan) hakutuswalisha, akatuswalisha usiku wa tano (kabla ya kumalizika Ramadhwaan) mpaka ulipomalizika nusu ya usiku.

Tukamwambia; ‘Ee Rasuli wa Allaah, si bora ungeendelea kutuswalisha sehemu ya usiku iliyobaki?’ Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

“Atakayeswali na Imaam mpaka atakapomaliza (Imaam) Swalaah, ataandikiwa thawabu ya aliyeswali usiku wote”.

 

Kisha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakutuswalisha mpaka zilipobaki siku tatu kabla ya kumalizika mwezi, akatuswalisha na akawaita Jamaa’ah zake na wake zake na akatuswalisha mpaka wakati wa kula daku ulipoingia.

 

Hadiyth hii ina faida nyingi sana ndani yake, lakini ili nisiwachoshe wasomaji nitaelezea faida mbili tu nazo ni kuwa:

 

1- Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaswalisha Swahaba zake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Swalaah ya Taraawiyh yeye akiwa Imaam wao na akawaita watu wa nyumba yake pia.

 

2- Katika Soko hili la Taraawiyh, atakayeswali nyuma ya Imaam mpaka mwisho ataandikiwa thawabu ya aliyeswali usiku kucha.

 

Khitilafu Ya Ubora:

 

Hata hivyo ipo khitilafu baina ya ’Ulamaa kuhusu namna bora wa kuiswali Swalaah ya Taraawiyh.

 

Anasema Imaam Ash-Shaafi’iy na wengi katika wanafunzi wake, na pia Imam Abu Haniyfah na Ahmad na baadhi ya Wanavyuoni wa madhehebu ya Imaam Maalik na wengineo kuwa ni bora kuiswali Jamaa’ah kama alivyofanya ‘Umar na kama walivyofanya Makhalifa waongofu waliokuja baada yake na pia Swahaba na waliokuja baada yao, na ikaendelea katika hali hiyo mpaka wakati wetu huu sasa.

 

Ama Imaam Maalik na Abu Yuusuf na baadhi ya wafuasi wa Imaam Ash-Shaafi’iy wao ingawaje wanaona kuwa ni vizuri kuiswali Jamaa’ah, lakini wanasema kuwa ni bora zaidi kuiswali nyumbani mtu peke yake.

 

Qur-aan Tukufu:

 

Ndugu zangu Waislam

 

Assalaam alaykum wa Rahmatullahi wa Barakatuh

 

Ramadhwaan inaendelea kututoka na milango inaendelea kufungika, na biashara inaendelea kuchangamka. Kwani kila siku zinapokaribia kumalizika Nabiy wetu Mtukufu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akizidi kuikaza shuka yake na kukesha usiku wake na kuamsha watu wake.

 

Ndugu zangu Waislam

 

Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema;

“Hakika bidhaa ya Allaah (mnayoinunua) ni yenye thamani sana, hakika bidhaa ya Allaah ni Jannah”. [At-Tirmidhiy, Al-Haakim, Al-Bayhaqiy na wengineo].

 

Anasema Ibnul Qayyim:

 

“Ajabu mtu baada ya kutambua kuwa Allaah ndiye Mwenye bidhaa bora, kisha anakwenda kufanya biashara na mwengine mwenye bidhaa duni, na ajabu kubwa zaidi ni pale mtu anapotambua kuwa hana budi Naye Rabb wake na kwamba hapana awezae kuondoa shida zake isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), kisha anajiweka mbali naye”.

 

Kwa ajili hiyo ndugu zangu Waislam, tuzidishe kufanya biashara na Rabb wetu mtukufu katika mwezi huu wa Ramadhwaan huku tukitarajia bidhaa yake tukufu, bidhaa ghali kupita zote, Jannatul Firdaws.

 

Biashara Ya Kusoma Qur-aan:

  

Allaah Anasema;

 

 إِنَّ الَّذِينَ يَتْلُونَ كِتَابَ اللَّـهِ وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَأَنفَقُوا مِمَّا رَزَقْنَاهُمْ سِرًّا وَعَلَانِيَةً يَرْجُونَ تِجَارَةً لَّن تَبُورَ ﴿٢٩﴾

Hakika wale wanaosoma Kitabu cha Allaah na wakasimamisha Swalaah, na wakatoa kutokana na yale Tuliyowaruzuku kwa siri na dhahiri wanataraji tijara isiyoteketea. [Fwaatwir: 29]

 

Na Akasema: 

شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ ۚ 

Mwezi wa Ramadhwaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan ili iwe mwongozo kwa watu na hoja bayana za mwongozo na pambanuo (la haki na batili). [Al-Baqarah: 185]

 

Katika Aayah hii Allaah Anausifia Mwezi huu mtukufu wa Ramadhwaan kuwa ni bora kuliko miezi yote kutokana na kuuchagua kwa kuiteremsha Qur-aan tukufu ndani yake, kitabu chenye uongofu, kilichopambanua baina ya haki na batili, ili kiwe hoja zilio wazi kwa kila mwenye kukisoma.

 

’Ulamaa wanasema kuwa ili kufaidika na mafundisho yake, lazima kusoma huko kuwe kwa kutafakari na kuzingatia. Kwani yeyote anayetaka kufaidika na Kitabu hiki kitukufu lazima awe anakisoma kwa moyo mkunjufu ulio hadhir na kwa kuzingatia aya zake huku akitambua kuwa yaliyomo ndani yake ni maneno anayohutubiwa yeye.

 

Allaah Anasema:

إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَذِكْرَىٰ لِمَن كَانَ لَهُ قَلْبٌ أَوْ أَلْقَى السَّمْعَ وَهُوَ شَهِيدٌ﴿٣٧﴾

Hakika katika hayo, bila shaka ni ukumbusho kwa aliyekuwa na moyo au akatega sikio naye mwenyewe awe hadhiri kwa moyo wake. [Qaaf: 37]

 

Anasema Ibn Qutaybah katika kitabu chake kiitwacho ‘Tafsiyr Ghariyb Al-Qur-aan’:

 

“Aayah hii inatufundisha kuwa ili mtu afaidike na mafundisho yaliyomo ndani ya Qur-aan tukufu lazima moyo wake uwe hadhiri pale anapiosoma au anapoisikiliza”.

 

Imetolewa na Ad-Daylamiy kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhiwya Allaahu ‘anhu) katika Hadiyth aloinyanyua moja kwa moja kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa:

 

“Mnapoisoma Qur-aan muisome vilivyo na muibainishe kwa ubainifu, muwe mnasimama (na kutafakiri) penye maajabu yake, na muusitue na kuuamsha moyo (muuharikishe) kwa hiyo Qur-aan, na isiwe hamu ya mtu ni kuimaliza sura tu.”

 

Ndugu zangu Waislam

 

Allaah hutukuza na kuadhimisha anachotaka. Kama alivyowachagua baadhi ya Malaika wake akawafanya kuwa wajumbe, na kuwachagua miongoni mwa wanaadamu na kuwafanya kuwa , akauchagua mwezi wa Ramadhwaan na miezi mitukufu kwa kuiadhimisha kuliko miezi mingine, Allaah Ameichagua pia Qur-aan tukufu ambayo ni maneno yake akayaadhimisha juu ya maneno yote mengine, kwa hivyo kuweni wenye kufahamu na wenye kutukuza yale Aloyatukuza Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), kwa sababu hatukuzi yale Aloyatukuza Allaah isipokuwa mwenye kufahamu na mwenye akili.

 

 

Ndugu zangu Waislam

 

Mwezi wa Ramadhwaan ni mwezi wa Qur-aan, na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiisoma na kuiadhimisha Qur-aan tukufu zaidi katika mwezi huu kupita miezi mingine yote. Kwa hivyo na sisi tujitahidi kuuhitimisha msahafu ndani ya mwezi huu angalau mara moja, hii ni kwa uhaba kabisa, kwani mwezi huu ni mwezi wake, na ndani yake mna thawabu nyingi sana na manufaa mengi sana kwa ajili yetu.

 

Kutoka kwa ‘AbduAllaah bin Mas’uud (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Atakayesoma herufi moja (tu) katika Kitabu cha Allaah atalipwa thawabu. Na kwa kila thawabu moja atalipwa kumi (nyingine). Si semi kuwa alif laam miym ni herufi moja, bali ‘alif’ ni herufi (moja), ‘laam’ ni herufi (moja) na ‘miym’ ni herufi (moja)”.

 

Yaani mtu anapotamka; ‘Alif laam miym’, anakuwa keshajipatia thawabu thelathini, na Allaah humzidishia amtakae.

 

Huyu ndiye Rabb wetu mkarimu, na bila shaka katika mwezi Wake huu wenye baraka malipo yake huongezeka maradufu.

 

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema:

 

“Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa mkarimu kupita wote katika mambo ya kheri, na alikuwa mkarimu zaidi katika mwezi wa Ramadhwaan wakati anapokutana na Jibriyl (‘Alayhis-salaam), na alikuwa akikutana naye kila Ramadhwaan mpaka mwezi unapomalizika, na alikuwa akimsikiliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Qur-aan yote, na kila anapokutana na Jibriyl, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa mwingi wa kheri mfano wa upepo uliopelekwa (kwa ajili ya kueneza kheri)” [Al-Bukhaariy na wengine]

 

Ndugu zangu Waislam

 

Kila kitu kwa hesabu yake. Imepokelewa kutoka kwa ‘AbduAllaah bin ‘Amru bin Al-‘Aas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Ataambiwa msomaji wa Qur-aan; ‘Soma upande daraja (za juu Peponi). Isome vilivyo kama ulivyokuwa ukiisoma duniani na daraja yako inaishia mwisho wa aya utakayoisoma” [Abu Daawuud na At-Tirmidhiy na wengineo]

 

Kwa hivyo ukisoma juzuu moja tu, basi daraja yako itaishia hapo, na hivi ndivyo ilivyo kila unapoisoma zaidi utapandishwa zaidi katika daraja za juu kabisa za huko Jannah.

 

Baadhi Ya Hadiyth Juu Ya Fadhila Za Qur-aan: 

 

Kutoka kwa Abu Umaamah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema:

“Nilimsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

“Someni Qur-aan, kwa sababu itakuja siku ya Qiyaamah kuwaombea shafa’ah wasomaji wake” [Muslim]

 

Kutoka kwa An-Nawwaas bin Sam’aan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema:

“Nilimsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

 

“Italetwa Qur-aan siku ya Qiyaamah pamoja na wasomaji wake waliokuwa wakiifanyia kazi duniani ikitanguliwa na Suratul Baqarah na Aali ‘Imraan zikiwatetea wasomaji wake” [Muslim]

 

Kutoka kwa ‘Uthmaan bin ‘Affaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema:

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

“Mbora wenu ni yule atakayejifunza Qur-aan kisha akafundisha [Al-Bukhaariy]

 

Kutoka kwa Bibi ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu anhaa) amesema:

“Amesema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

“Mwenye kuisoma Qur-aan akiwa mahiri katika kuisoma, atakuwa pamoja na Malaika watiifu. Na mwenye kuisoma Qur-aan huku akihangaika katika kuyatamka maneno yake atalipwa ujira mara mbili” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Kutoka kwa ‘Umar bin Al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Allaah kwa Kitabu hiki Atayanyanua makundi ya watu na Atayaacha (makundi) mengine” [Muslim]

 

Kumi La Mwisho:

 

Hii ni tafsiri ya makala yaliyoandikwa na Al-Haafidh Ibn Rajab Al-Hanbaliy niliyobahatika kuyasoma na kufaidika nayo sana, nikaona bora kuyatafsiri katika lugha ya Kiswahili ili na wenzangu wafaidike pia:

 

BismiAllaahir Rahmaanir Rahiym,

 

Shukrani zote ni za Allaah peke Yake na Swalaah na salaam zimfikie yule ambaye hapana Nabiy baada yake, Amma ba’ad:

 

Kutoka kwa Bibi ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu anhaa) amesema:

“Alikuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) linapoingia kumi la mwisho akiikaza vizuri shuka yake, akikesha usiku wake na akiamsha watu wa nyumba yake” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

‘Amali Za Kutenda Katika Kumi La Mwisho La Ramadhwaan:

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akilihusisha kumi la mwisho la mwezi wa Ramadhwaan kwa ‘amali zifuatazo ambazo hakuwa akizifanya katika siku nyingine zisizokuwa hizo:

 

Akikesha:

 

Na maana ya kukesha inaweza kuwa alikuwa akifanya ibada usiku kucha, na hii inatokana na Hadiyth ya Bibi ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu anhaa) aliposema:

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa katika siku ishirini za mwanzo za Ramadhwaan akichanganya baina ya Swalaah na kulala, lakini zinapobaki siku kumi (yaani za mwisho), alikuwa akipania na kuikaza barabara shuka yake” [Ahmad bin Hanbal]

 

Huenda pia ikawa na maana kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akikesha sehemu kubwa ya usiku na si usiku wote, na hii inatokana na Hadiyth nyingine ya Bibi ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu anhaa) katika Swahiyh Muslim isemayo:

 

“Sikumbuki kama aliwahi kuswali usiku woote mpaka asubuhi”

 

Akiamsha Watu Wake:

 

Alikuwa akiamsha watu wake kwa ajili ya kuswali katika usiku wa kumi la mwisho tofauti na usiku wa siku nyingine.

 

Anasema Sufyaan At-Thawriy:

 

“Napenda linapoingia kumi la mwisho mtu awe anaswali nyakati za usiku na ajitahidi sana ndani yake, na awaamshe watu wa nyumba yake pamoja na wanawe ikiwa wataweza kustahamili, kwani imesihi kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akimgongea mlango Bibi Faatwimah na ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhum) huku akiwaambia;

 

“Hamuamki mkaswali?”

 

Na imesihi pia kuwa akishamaliza kuswali Tahajjud katika nyakati za usiku na kabla ya kusali Witri alikuwa akimuamsha Bibi ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa), na imepokelewa pia kupendeza kwa mtu na mkewe kuamshana kwa ajili ya kusali tahajjud hata ikibidi kummichia maji mwenzake usoni.

 

Imetolewa na Imaam Maalik katika Muwattwaa kuwa ‘Umar bin Al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akishaswali kiasi cha kuswali katika nyakati za usiku, na inapoingia nusu ya pili ya usiku akiwaamsha watu wa nyumba yake kwa ajili ya kuswali huku akiwasomea Aayah ifuatayo:

وَأْمُرْ أَهْلَكَ بِالصَّلَاةِ وَاصْطَبِرْ عَلَيْهَا ۖ .. ﴿١٣٢﴾

Na amrisha ahli zako Swalaah, na dumisha kusubiri kwayo..[Twaahaa: 132]

 

Akiikaza Vizuri Shuka Yake:

 

Ama kuhusu ‘kuikaza vizuri shuka yake’, ’Ulamaa wamekhitalifiana juu ya tafsiri yake. Wapo wanaosema kuwa hii ni kutujulisha juu ya jitahada kubwa anayofanya katika ibada ndani ya kumi la mwisho. Na wengine wakasema kuwa maana yake ni kuwa alikuwa akijiepusha kulala na wake zake, na zipo riwaya zinazotilia nguvu maana hii zinazoeleza kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa hapandi kitandani mpaka imalizike Ramadhwaan. Na katika Hadiyth iliyosimuliwa na Anas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) anasema;

 

“Alikuwa akilikunja tandiko lake na kuwaepuka wake zake”.

 

Kuakhirisha Futari Mpaka Wakati Wa Daku.

 

Kutoka kwa Bibi ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu anhaa) na pia kutoka kwa Anas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiichelewesha futari yake na kuila wakati wa daku. Na Hadiyth yenyewe kama ilivyoelezwa na Bibi ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu anhaa) inasema:

 

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa inapoingia Ramadhwaan akiswali nyakati za usiku na akilala (pia), na linapoingia kumi la mwisho akiikaza shuka yake vizuri, na akijiepusha na wake zake (kulala nao), na alikuwa akikoga baina ya adhana mbili na alikuwa akiila futari yake wakati wa daku” [Ibni Abi ‘Aaswim]

 

Na kutoka kwa Abu Sa’iyd Al-Khudriy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:

 

“Msiiendeleze (Swawm yenu), (lazima mule futari) na kama yeyote kati yenu anataka kuendelea na Swawm (bila kula futari yake), basi aendelee mpaka wakati wa daku (tu)”.

Wakasema;

“Lakini wewe unaendeleza ee Rasuli wa Allaah”.

Akasema;

“Mimi nakhitilafiana na nyinyi, mimi nina mlishaji anayenilisha na mnywishaji anayeninywisha” [Al-Bukhaariy]

 

Kutokana na haya, inaonesha kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anaendela na Swawm yake usiku wote, na huenda ikawa alikuwa akifanya hivyo kwa sababu alikuwa akiona kuwa anakuwa mwepesi zaidi katika jitihada zake za kufanya ibada nyakati za usiku ndani ya kumi la mwisho la Ramadhwaan, na hakuwa akipata udhaifu wowote kwa sababu Allaah alikuwa akimlisha na kumnywesha.

 

Kuoga Baina Ya Adhana Mbili:

 

Tulitangulia kueleza katika Hadiyth ya Bibi ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu anhaa) kuwa (Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ‘alikuwa akikoga baina ya adhana mbili’, na kusudi lake ni kuwa alikuwa akioga baina ya adhana ya Magharibi na adhana ya ‘Ishaa.

 

Anasema Ibn Jariyr:

 

“Walikuwa wakipendelea kuoga kila usiku katika kumi la mwisho. Na Al-Nakha’iy alikuwa akikoga katika kumi la mwisho kila usiku, na walikuwepo miongoni mwao waliokuwa wakipenda kuoga na kujipaka mafuta mazuri kila usiku wanaoutegemea kuwa Laylatul Qadr itakuwa ndani yake.

 

Kutokana na haya inatubainikia kuwa kila usiku unaotegemewa kuwa Laylatul Qadr utakuwa ndani yake inapendeza mtu kuoga na kuvaa nguo nzuri na kujipaka mafuta mazuri, na pia inapendeza kufanya hivyo kila Ijumaa na katika Sikukuu na inapendeza mtu kuvaa vizuri katika kila Swalaah.

 

Na kujipamba sehemu za nje ya mwili hakukamiliki pambo lake mpaka mtu ajipambe ndani ya nafsi yake pia kwa kujitakasa kutokana na madhambi yake kwa njia ya kutubu na kurudi kwa Rabb wake. Kwani kujipamba mtu mwili wake wakati ndani yake kumeharibika hakutomsaidia kitu. Na haijuzu kumkabili Mfalme wa wafalme Mwenye kujuwa yaliyo dhahir na yaliyo siri na yaliyofichikana zaidi kuliko siri, ambaye hatizami nyuso zenu, bali anazitizama nyoyo zenu na matendo yenu bila ya mtu kujitakasa nje na ndani yake.

 

Kwa hivyo atakayesimama mbele Yake inampasa ajipambe nje yake kwa nguo safi na ndani yake kwa moyo msafi wenye kumcha Allaah.

 

I’tikaaf:

 

Katika Al-Bukhaariy na Muslim kutoka kwa Bibi ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu anhaa) amesema:

 

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akifanya itikafu katika kila kumi la mwisho la mwezi wa Ramadhwaan mpaka alipofariki dunia.”

 

Na katika [Swahiyh Al-Bukhaariy], kutoka kwa Bibi ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu anhaa) amesema:

 

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akifanya itikafu katika kila Ramadhwaan siku kumi, ama katika mwaka alofariki ndani yake alifanya itikafu siku ishirini”.

 

Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akifanya itikafu katika siku kumi zile ambazo ndani yake unatarajiwa usiku wa Laylatul Qadr ili asijishughulishe na jingine ghayri ya kumuomba na kumdhukuru Rabb wake.

 

Hujitenga na kuacha shughuli zake zote kwa ajili ya kufanya itikafu kwa moyo wake wote ili apate kumtii Mola wake na kujikurubisha Kwake.

 

Kwa hivyo mwenye kufanya itikafu anakuwa amejitenga na kuacha shughuli zake zote kwa ajili ya kumtii Rabb wake kwa moyo wake wote, na kwa ajili hiyo hapana kinachomshughulisha isipokuwa twa’aa ya Rabb wake na kufanya yale yanayomridhisha tu.

 

Na kila mja anapomjua zaidi Rabb wake akampenda, basi huwa hastarehe isipokuwa pale anapoacha shughuli zake zote kwa ajili ya kumuabudu.

 

Laylatul-Qadr

 

Allaah Anasema:

 

 إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةِ الْقَدْرِ ﴿١﴾ وَمَا أَدْرَاكَ مَا لَيْلَةُ الْقَدْرِ ﴿٢﴾ لَيْلَةُ الْقَدْرِ خَيْرٌ مِّنْ أَلْفِ شَهْرٍ ﴿٣﴾ تَنَزَّلُ الْمَلَائِكَةُ وَالرُّوحُ فِيهَا بِإِذْنِ رَبِّهِم مِّن كُلِّ أَمْرٍ ﴿٤﴾ سَلَامٌ هِيَ حَتَّىٰ مَطْلَعِ الْفَجْرِ ﴿٥﴾

Hakika Sisi Tumeiteremsha Qur-aan katika Laylatil-Qadr (usiku wa Qadar). Na nini kitakachokujulisha ni nini huo Laylatul-Qadr? Laylatul-Qadr ni mbora kuliko miezi elfu. Wanateremka humo Malaika na Ar-Ruwh (Jibriyl) kwa idhini ya Rabb wao kwa kila jambo. Amani mpaka kuchomoza Alfajiri. [Al-Qadr: 1-5]

  

Na kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema juu ya mwezi wa Ramadhwaan;

 

“Ndani yake mna usiku ulio bora kuliko miezi elfu, na alonyimwa kheri zake, basi amenyimwa (amekula khasara)” [Ahmad na An-Nasaaiy]

 

Ama kuhusu ‘amali za mtu kufanya katika usiku wa Laylatul Qadr, imepokelewa Hadiyth sahihi ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa amesema;

 

“Atakayesimama usiku wa Laylatul Qadr kwa imani na kwa kutaraji thawabu, atasamehewa alotanguliza katika madhambi yake”.

 

Na maana ya neno ‘kusimama usiku wake’, ni kuuhuisha usiku huo kwa kuswali Tahajjud, na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimtaka Bibi ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) awe anaomba du’aa ndani yake.

 

Sufyaan Ath-Thawriy amesema;

 

“Du’aa ndani yake usiku huo kwangu mimi ni bora kuliko Swalaah”.

 

Na kusudi lake ni kuwa kuomba du’aa kwa wingi ndani ya Swalaah katika usiku huo ni bora kuliko Swalaah isiyokuwa na du’aa ndani yake, na kama mtu atasoma Qur-aan na kuomba du’aa, hii itakuwa bora zaidi.

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali ndani ya usiku wa Laylatul Qadr huku akisoma Qur-aan kwa utulivu, na kila anapoifikia Aayah inayozungumzia Rehma, alikuwa akimuomba Allaah Amrehemu, na anapoifikia Aayah inayozungumzia adhabu alikuwa akimuomba Amuepushe nayo. Kwa hivyo katika Swalaah yake yalikuwa yakijumuika mambo manne; Swalaah, kusoma Qur-aan, kuomba du’aa na kutafakari, na hii ndiyo ‘amali bora iliyokamilika kupita zote katika usiku wa kumi la mwisho na katika usiku mwengine pia.

 

Bibi ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) alisema kumuuliza Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

“Unaonaje ninapofanya ibada katika usiku wa Laylatul Qadr niwe nikisema nini?”

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia;

“Sema; “Allaahumma innaka ‘afuwun tuhibbul ‘afwa, faafu ‘anniy.”

 

Na maana yake ni:

 

“Rabb wangu wewe ni Mwingi wa kusamehe, unapenda kusamehe, kwa hivyo nisamehe”.

 

Na ‘Al-‘Afuwwu’, ni katika majina ya Allaah, na Yeye ni Mwingi wa kusamehe madhambi ya waja Wake, Mwenye kuyafuta na kuyaondoa na Mwenye kuacha kumtia adabu anayestahiki.

 

Na kwa vile Yeye Anapenda kusamehe, kwa hivyo bila shaka Anapenda pia waja Wake wawe wanasameheana wao kwa wao, na wakishasameheana wao kwa wao, na Yeye Anawapitishia ‘afwa Yake. Na Allaah Anapenda kusamehe kuliko kuadhibu. Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisema;

 

“Najikinga kwa radhi Zako kutokana na ghadhabu Zako, na najikinga kwa kusamehe Kwako kutokana na adhabu Yako” [Muslim]

 

Na tumeamrishwa kuomba maghfira katika usiku wa Laylatul Qadr baada ya kujitahidi katika kufanya ‘amali njema nyakati za usiku katika kumi la mwisho, na hii ni kwa sababu ‘wanaojua’, wanajitahidi katika kufanya ‘amali njema huku wakiona kama kwamba hawakufanya lolote, kisha wanamuomba Rabb wao awasamehe kama kwamba wamefanya madhambi au wamepunguza katika haki za Rabb wao.

 

Sababu Za Maghfirah Katika Mwezi Wa Ramadhwaan:

  

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Atakayefunga Ramadhwaan kwa imani na kutaraji thawabu, atasamehewa yaliyotangulia katika madhambi yake, na atakayesimama (akaswali) usiku wa Laylatul Qadr kwa imani na kwa kutaraji thawabu, atasamehewa yaliyotangulia katika madhambi yake”.

 

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Atakayeswali usiku wa Ramadhwaan kwa imani na kwa kutaraji thawabu, atasamehewa madhambi aliyotanguliza” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

·        Hadiyth hizi zilizosimuliwa na Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) zinatufundisha kuwa kila moja katika sababu tatu hizi zinasababisha kusamehewa mtu madhambi yake aliyotanguliza.

 

Na mambo yenyewe ni Swawm ya mwezi wa Ramadhwaan, kuswali katika usiku wake (Taaraawiyh), na kuswali katika usiku wa Laylatul Qadr (Tahajjud).

 

Kuswali katika usiku wa Laylatul Qadr peke yake kunatosheleza mtu kufutiwa madhambi yake, yote sawa ikiwa katika siku ya mwanzo ya kumi la mwisho au kati yake au mwisho wake, na yote sawa pia ikiwa ameihisi Laylatul Qadr au hakuihisi, na kufutiwa madhambi kunaendelea mpaka mwezi unapomalizika.

 

Ama katika kufunga mwezi wa Ramadhwaan na kuswali usiku wake (Taraawiyh), ili mtu asamehewe madhambi yake, sharti awe amefunga na kusali mwezi mzima.

 

Akishaukamilisha mwezi, Muislam anakuwa keshatimiza kufunga Ramadhwaan na kuswali ndani ya usiku wake, na kwa ajili hiyo anastahiki kughufiriwa madhambi yake baada ya kutimiza masharti mawili hayo ya kufunga na kuswali.

 

·       Kwa hivyo atakayeukamilisha mwezi wa Ramadhwaan kwa kufunga na kuswali atakuwa keshakamilisha sharti alopewa, na kitakachobaki ni kupokea ujira wake kutoka kwa Mola wake na ujira huo ni kughufiriwa madhambi yake. Na Waislamu wanapotoka kwenda kuswali siku ya ‘Iyd wanagawiwa ujira wao huo na kwa ajili hiyo wanarudi majumbani mwao wakiwa washalipwa ujira wao kwa ukamilifu. Na atakayepunguza katika ‘amali zake, na ujira wake pia utapunguzwa. Kila kitu kwa hesabu yake, na kwa ajili hiyo mtu asiilaumu isipokuwa nafsi yake.

 

Amesema Sulaymaan:

 

“Swalaah ni mezani, atakayekamilisha na Allaah Atamkamilishia, ama atakayepunguza, basi wenyewe mnajuwa nini Allaah Amesema juu ya wapunjao”

وَيْلٌ لِّلْمُطَفِّفِينَ 

Ole kwa wanaopunja [Al-Mutwaffifiyn: 1]

 

Swalaah na ibada zote hukmu zake ni kama hivyo, atakayekamilisha, huyo anakuwa kipenzi cha Allaah, ama atakayepunja basi Waylun lilmutwaffifiyn.

 

Basi haoni hayaa mtu, katika matamanio ya nafsi yake anafanya kwa ukamilifu, kisha anakwenda kupunja katika Swawm na Swalaah yake?

 

·        Watu wema waliotangulia walikuwa wakijitahidi kufanya amali zao kwa ukamilifu kisha wanajishughulisha kumuomba Allaah Azikubali ‘amali zao hizo huku wakiogopa Allaah Asije akazikataa.

 

Hawa ndio wale ambao Allaah Amesema juu yao; 

وَالَّذِينَ يُؤْتُونَ مَا آتَوا وَّقُلُوبُهُمْ وَجِلَةٌ ..﴿٦٠﴾

Na ambao wanatoa vile walivyopewa na huku nyoyo zao zinakhofu [Al-Muuminuwn: 60]

 

Imepokelewa kuwa ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akisema;

“Kuweni watu mnaojishughulisha sana na kukubaliwa kwa ‘amali zenu kuliko mnavyojishughulisha na amali zenyewe, hamkumsuikia Allaah aliposema;

إِنَّمَا يَتَقَبَّلُ اللَّـهُ مِنَ الْمُتَّقِينَ ﴿٢٧﴾

Hakika Allaah Anatakabalia wenye taqwa. [Al-Maaidah: 27]

 

Na kutoka kwa Al-Hasan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema:

 

“Hakika Allaah Ameujaalia Mwezi wa Ramadhwaan kuwa ni uwanja wa waja Wake, wanashindana ndani yake katika kumtii na katika kutaka radhi Zake. Wengine wanashinda na kufuzu, na wengine wanabaki nyuma kisha wanajuta. Inastaajabisha kuona watu wanacheka na kucheza katika siku ambazo wafanyao mema wanafuzu na wafanyao maovu wanakula hasara”.

 

Na miongoni mwa sababu za mtu kusamehewa madhambi yake ni kumfuturisha aliyefunga, kumdhukuru Allaah na kuomba maghfirah. Du’aa ya aliyefunga inakubaliwa wakati anapokuwa amefunga na baada ya kufuturu, na pia Malaika wanawaombea maghfirah waliofunga mpaka pale wanapofuturu.

 

Kwa vile sababu za mtu kusamehewa madhambi ndani ya mwezi huu ni nyingi sana, basi mtu anayenyimwa maghfirah ndani yake huwa amekula hasara kikweli.

 

·       Basi lini anaweza kughufiriwa yule aliyekosa maghfirah katika mwezi huu? Lini anaweza kusamehewa yule aliyekataliwa ombi lake katika usiku wa Laylatul Qadr? Atatengenea lini yule asotengenea ndani ya mwezi huu? Lini ataamka yule asiyeujua utukufu kisha akaghafilika katika mwezi wa Ramadhwaan? Kisichochumwa na kuvunwa kinapokuwa juu ya mti wakati wa mavuno, basi matokeo yake kitakatwa na kuchomwa moto, na atakayefanya mchezo asipande siku za kupanda, basi siku ya kuvuna hatovuna isipokuwa majuto na hasara.

 

Ramadhwaan Ni Mwezi Wa Kuepushwa Na Moto:

 

Kwa vile katika kumi la mwisho la Ramadhwaan watu wengi wanaepushwa na Moto, na kwa vile kusamehewa kwa madhambi kunapatikana pia kwa njia ya kufunga na kusali, ndiyo maana Allaah akatutaka pale mwezi unapomalizika tumtukuze na kumshukuru.

 

Allaah Anasema: 

وَلِتُكْمِلُوا الْعِدَّةَ وَلِتُكَبِّرُوا اللَّـهَ عَلَىٰ مَا هَدَاكُمْ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ ﴿١٨٥﴾

Na ili mkamilishe idadi na ili mumkabbir Allaah kwa kuwa Amekuongozeni na ili mpate kushukuru. [Al Baqarah: 185]

 

Kwa hivyo shukrani zote ni Zake yule aliyewaneemesha waja Wake kwa kuwawezesha kufunga na kwa kuwaghufuria madhambi yao na kuwaepusha na Moto.

 

Ee ambaye Rabb wake amemuacha huru na Moto, usije ukarudia tena baada ya kuepushwa nao. Mola wako anakuepusha nao na wewe bado tu unendelea kuusogelea? Mola wako anakuepusha nao na wewe hutaki kuukimbia?

 

·     Kwa hivyo anayetaka kunusurika na Moto katika mwezi wa Ramadhwaan azitafute sababu zitakazomwezesha aachwe huru nao, na Allaah Amezieneza sababu hizo ndani ya mwezi huu.

 

Katika Swahiyh ya Ibn Khuzaymah imeandikwa:

 

“Zidisheni ndani yake mambo manne. Mambo mawili kwa ajili ya kumridhisha Rabb wenu na mambo mawili hamwezi kuepukana nayo;

Ama mambo mawili mtakayomridhisha kwayo Rabb wenu ni kutamka Laa ilaaha illa Allaah, na kusema ‘AstaghfiruAllaah’.

Ama mawili msiyoweza kuepukana nayo; Mumuombe Rabb wenu akuingizeni Jannah na akuepusheni na Moto.”

 

Sababu zote nne zilizotajwa katika Hadiyth hii zinamwezesha mtu aachwe huru na Moto na kupata maghfirah, na hii ni kwa sababu tamko la Tawhiyd’; ‘Laa ilaaha illa Allaah, linaondoa madhambi na kuyafutilia mbali, na neno hili ni sawa na mtu kumuacha huru Mtumwa.

 

Ama neno ‘Astaghfiru-Allaah’, litasababisha kusamehewa mtu madhambi yake, na du’aa ya aliyefunga inakubaliwa pale anapokuwa amefunga na hata anapofuturu. Na Ishtighfaar bora ni ile inayoambatanishwa na tawbah. Kwani anayeomba maghfirah kwa ulimi wake wakati moyo wake umeazimia baada ya kumalizika mwezi kurudi tena katika maasi, huyo Swawm yake inakataliwa na mlango wa tawbah anafungiwa.

 

Katika du’aa muhimu pia ni kumuomba Allaah Akuingize Jannah na akuepusha na Moto, kwani Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwahi kusema juu yake:

 

“Hayo ndiyo lengo letu” [Abu Daawuud na Ibn Maajah]

 

Share