Wasiya Wa Kishariy'ah Wa Muislamu Kabla Hajafariki

 

Wasiya Wa Kishariy'ah Wa Muislamu Kabla Hajafariki 

 

Alhidaaya.com 

 

BismiLlaahi Rahmani Rahiim

 

 Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:  

وَاتَّقُواْ يَوْمًا تُرْجَعُونَ فِيهِ إِلَى اللّهِ ثُمَّ تُوَفَّى كُلُّ نَفْسٍ مَّا كَسَبَتْ وَهُمْ لاَ يُظْلَمُونَ

 Na iogopeni Siku mtakayorejeshwa ndani yake kwa Allaah, kisha kila nafsi italipwa kamilifu iliyoyachuma nao hawatodhulumiwa. [Al-Baqarah: 281]

 

Utangulizi

 

Shukrani zote Anastahiki Allaah, Rabb wa walimwengu wote. Swalah na amani ziwe juu ya aliyetumwa awe ni Rahmah kwa ulimwengu wote Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Ahli zake, Swahaba na wale ambao wamefuata Sunnah zake mpaka siku ya mwisho.

 

Nimefikiri kuhusu mauti mara kadhaa na nimejaribu sana kule kukutana kwangu na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kuwe ni kwenye kumridhisha na kuwe mbali na uzushi wa zama hizi. Nami nina yakini kabisa kuwa kila bid’ah (uzushi) ni upotevu na kila upotevu malipo yake ni moto. Na pia kila uzushi ni upotevu, japokuwa watu watayaona ni mazuri na mema.

 

Nimesoma mengi kuhusu janaza na wasiya wa kishariy’ah lakini sijapata kilichokamilika wala bora kuliko kitabu “Hukumu ya Janaza na Uzushi wake” cha Shaykh Muhammad Naaswirud Diyn Al-Albaaniy Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amrehemu.

 

Ee ndugu yangu… Tukumbuke mauti daima… Mpaka tufanye 'amali ya baada ya mauti. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: 

  أكثروا من ذكر هادم اللذات..

“Zidisheni katika kukumbuka mauti” [At-Tirmidhiy, Ahmad na Ibn Maajah]

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesisitiza kuhusu kuacha wasiya ulioandikwa, akasema: 

 ما حق إمرئ مسلم يبيت ليلتين وله شئ يوصى فيه إلا ووصيته مكتوبة عند رأسه, البخارى ومسلم

“Ni haki gani ya Muislamu anayekaa masiku mawili na ana kitu cha kukitolea wasiya ila na wasiya wake umeandikwa chini ya kichwa chake”.  [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Wasiya Wangu Wa Kijumla

 

Watu wa nyumbani kwangu watukufu, nawausia:

 

1). Mpwekesheni Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Pekee (At-Tawhiyd) na mujihadhari na kuingia katika kumshirikisha. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa): 

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ۚ 

Hakika Allaah Haghufurii kushirikishwa; lakini Anaghufuria yasiyokuwa hayo kwa Amtakae. [An-Nisaa: 48]

 

2). Muogopeni na kumpenda Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na mufuate shariy’ah zake kwa siri na dhahiri. Hifadhini nguzo za Uislaam, amrisheni mema na mkatazane mabaya, ungeni ujamaa na kizazi na mushikamane na kila kitukufu na twa’a ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Aliyetukuka na fuateni Sunnah za Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)

 

3). Nawausia mfanye tawbah ya kweli kweli na sawa kutokana na kila maovu na maasi na ombeni maghfirah (msamaha), mkumbukeni na mumtaje Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa wingi na muisome Qur-aan kila mchana na usiku.

 

4). Nawausia muwe na subira na kuridhika wakati wa msiba mara ya kwanza na museme:

إنا لله وإنا إ ليه راجعون اللهم أجرنا فى مصيبتنا واخلف لنا خيرا منها

“Bila shaka tunatoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Kwake ndio marudio. Ee Allaah Tupe ujira katika msiba wetu huu na Utubadilishiye lililo bora zaidi kuliko huo msiba.”

 

5).  Msinitangaze katika magazeti wala vipaza sauti bali wasilianeni na jamaa zangu na marafiki ili wanioshe na kuniswalia….Na kunivisha sanda na kuniombea Du‘aa pamoja na kuniombea maghfirah (msamaha).

 

6). Msikae sehemu ya msiba…wala katika hema au nyumba za sherehe au kumbi za kukodisha au nyumba za kawaida. Haikuonekana kwa Nabiy(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wala Swahaba wala Tabi’iyn kuwa wamekusanyika katika msiba baada ya kuzikwa.

 

7).  Na msiba katika shariy’ah ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Na Sunnah ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni kumsomea mtu wakati wa kukata roho “La ilaaha illa Allaah”. “Hapana muabudiwa wa haki ila Allaah”. Na kisha kumwosha, kumvisha sanda, kufuata jeneza lake, kumzika na kungojea saa baada ya kuzika kwa kumuombea du‘aa na maghfirah maiti. Amesema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na yeye akiwa kwenye mazishi kaburini: 

استغفروا لأخيكم وسلوا له التثبيت فإنه الآن يسأل

“Muombeeni maghfirah ndugu yenu na mumtakiye uimara (kutoyumba) kwani sasa anaulizwa”. [Abu Daawuud]

 

Na hivyo hivyo muwatayarishie chakula watu walio na msiba (waliofiliwa). Huu ndio utaratibu wa msiba wa kishariy’ah na kinyume na hayo ni uzushi (bid’ah).

 

8). Msinililie kwa sauti….Wala msiyahesabu mazuri yangu. Wala msilie kwa sauti kubwa…wala msikwaruze nyuso zenu. Wala msizichane nguo... wala msijipige.

 

9). Kunakatazwa kabisa ada zote za uzushi kama kukusanyika Alkhamiys, arobaini, au baada ya maiti kutimiza mwaka, au siku za ‘Iyd na kujiliza na sherehe za wakati mbali mbali. Msisome Qur-aan kwenye makaburi wala msigawanye Swadaqah na wala msichinje chochote chini ya Jeneza.

 

10). Kwa jamaa zangu na marafiki wapendwa wanilipie madeni kabla ya kuoshwa na kukafiniwa (kuvishwa sanda) na watekeleze nadhiri zangu.

 

11). Nawausia watoto wangu, msiba na huzuni usizidi siku tatu. Na kwa mke wangu msiba ni miezi minne na siku kumi. Na asivae kwa wakati huo hariri wala nguo za rangi au asitie wanja, mafuta na asijipambe.

 

12). Pia nawausia watoto na jamaa zangu wazuru kaburi langu, waniombee du’aa pamoja na kuniombea maghfirah. Hii itawasaidia kupata mazingatio na mawaidha katika mauti.

 

13). Vivyo hivyo nawausia watoto, jamaa, marafiki na watu wa Msikiti wanikumbuke kwa wema, na kuniombea du’aa na kunitakia maghfirah katika wakati wa Swalah zao kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Wanaposujudu, baada ya Swalah na kusoma Qur-aan tukufu… Wakati wanapohiji kwenye nyumba tukufu ya Allaah ili Allaah Aniondolee adhabu ya kaburi na adhabu ya moto wa Jahannam na Aniingize kwa Rehma Yake Jannah.

 

14). Inaruhusiwa kwa mke wangu (na kinyume chake) kuniosha na kunikafini.

 

15). Inaruhusiwa kungojewa kwa mzazi au mtoto mpaka afike kwa muda usiochelewa (kwa haraka na si kwa kupita siku au masiku).

 

16). Inawezekana kuniswalia kwenye makaburi kwa yule aliyekosa Swalah ya Jeneza kabla ya kupita mwezi baada ya kuzika.

 

17).  Gawanyeni kopi za wasiya kwa waliohudhuria mazishi na Swalah punde tu wanapoingia ili wapate kusoma na kutekeleza yaliyo ndani ya wasiya.

 

18).  Ninawapatia khabari kama nimemsamehe kila mwanaadamu aliye na haki yangu na ninawaomba nilio na haki zao wanisamehe.

 

19). Jueni kuwa Nabiy(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:                     

ينقطع عمل ابن آدم من الدنيا إلا من ثلاث : صدقة جارية أو علم ينتفع به أو ولد صالح يدعو له

“Amali ya binadamu hukatika baada ya kufa ila kwa mambo matatu: Swadaqah yenye kuendelea, elimu yenye manufaa au mtoto mwema anayemuombea”. [Muslim na Ibn Maajah].

 

20). Ninawaageni kwa jina la Allaah Ambaye mwagano wake haupotei.

 

 

Wakati Wa Kutoka Roho

 

Enyi Wapenzi Wangu!

 

Wakati unapokaribia wa kukata roho waiteni watu wema. Wahesabuni hivyo, wala simtakasi yeyote mbele ya Allaah.

 

Jina

Simu

Jina

Simu

 

 

 

 

  

 

Wakati Wa Kukata Roho

 

Enyi Vipenzi Vyangu:

 

i. Msiwe na wasiwasi na msubiri kwani napenda kukutana na Allaah na kuweni na dhana nzuri. Na nisomeeni kalimah ya Tawhiyd, “La ilaaha illa Allaah” kwa ulaini na upole mpaka hayo yawe maneno ya mwisho ya kukutana na Mola wangu. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: 

من كان آخر كلامه لا إله إلا الله دخل الجنة

“Yeyote yatakayokua maneno yake ya mwisho La illaah illa Allaah ataingia peponi.”

 

ii. Nifungeni macho... Na museme Khayr (wema) kwani Malaika wanaamini munayosema:

 

 اللهم اغفر له .. وارحمه.. وارفع درجته فى المهديين المقربين.. واخلفه فى عقبه فى الغابرين.. واغفر لنا وله يا رب العالمين.. وافسح له قبره.. ونور له فيه

Ee Rabb Msamehe… na Umrehemu…Muinue daraja yake awe wa karibu walioongoka… Wabadilishie kizazi chake kwa yaliyopita…Na Utusamehe sisi na yeye. Ee Rabb wa Ulimwengu…Mpanulie kaburi lake…na Umtilie mwangaza.

 

iii. Nifunikeni kikamilifu na mnisitiri mwili wangu mzima.

 

iv. Na ikiwa nimehirimia kwa Hijjah au Umrah, basi msinifunike kichwa, uso wala msinitie manukato.

 

v. Na nikiwa niko katika vita vya Jihaad, basi asinioshe yeyote, bali niacheni na nguo zangu hizo na nizikeni na damu yangu.

 

vi. Msinielekeze Qiblah na niacheni katika hali yangu hiyo wala msinisomee Qur-aan.

 

vii. Nizikeni katika sehemu ambayo itakua rahisi kwenu.

 

viii. Nilipieni madeni kabla ya kunikafini kutoka kwa mali yangu mwenyewe. Ikiwa sina mali basi waulizeni watu wa kheri katika jamaa na marafiki zangu… Allaah Atawajaza (Atawapa) kila la kheri. Ikiwa hawatapatikana basi Allaah Aliyetukuka Atanilipia deni langu.

 

 

Wakati Wa Kuoshwa

 

a) Asihudhurie kuoshwa kwangu ila mwaminifu na aliye mwema.

 

b) Nisitirini wakati wa kuoshwa tupu yangu kutoka kitovu mpaka magoti.

 

c) Mwanzo nitoeni najasa. Kisha ziosheni viungo vya Wudhuu na mwili wangu wote kwa maji na sabuni.

 

d) Kisha nitieni Wudhuu wa Swalah kwa maji twahara lakini msiingize maji kwenye mdomo wala pua yangu. Kisha utieni mwili wangu kwa maji twahara mara tatu au tano… au saba.

 

e) Kisha nitieni maji ya waridi (marashi) kwenye nywele na vitanga vya mikono na sehemu zinazosujudu baada ya kumaliza kuniosha na kukauka.

 

f) Nivisheni bafta (kitambara) tatu nyeupe na mtie manukato baina yake na munistiri uso na miguu yangu.

 

g) Na ikiwa nimekufa shahidi katika vita basi asinioshe yeyote, niacheni na nguo hizo na munizike (nilivyokufa) na damu (kama imetoka).

 

 

Swalah Ya Jeneza

 

Imaam wa Swalah hiyo ni…………………………… au awe ni mtu yeyote mwema. Swalah ya maiti (au Jeneza) ina Takbira nne:

 

Utasoma Suratul Faatihah baada ya Takbira ya kwanza.

 

Kisha du’aa ya Ibraahiym(‘Alayhis-sallam) baada ya Takbira ya pili yaani,

 (اللهم صلى على محمد ...)

“Allaahumma swali ‘alaa Muhammad wa ‘alaa aali Muhammad kama Swallayta ‘alaa Ibraahyima wa ‘alaa aali Ibraahiym…”  mpaka mwisho baada Takbira ya pili.

 

Na mniombee baada ya Takbira ya tatu.

اللهم إنا جئناك شفعاء له .. فشفعنا فيه اللهم اغفر له وا رحمه .. وعافه واعف عنه وأكرم نزله .. ووسع مدخله وأغسله بالماء والثلج والبرد .. ونقه من الخطايا كما ينقى الثوب الأبيض من والدنس وأبدله دارا خيرا من داره .. وأهلا خيرا من أهله وزوجا خيرا من زوجه وأعذه من عذاب القبر وعذاب النار اللهم أبدل سيئاته حسنات اللهم إن كان مسيئا فتجاوز عن سيئا

Allaahumma inna ji-inaaka shufa’a-an lahu fashfi‘na fiyhi

 

“Ee Rabb sisi tumekuja kwako kumuombea Shafa’a basi mpatie Shafa’a”

 

Allaahumma ghfir lahu warhamhu wa ‘afihi waa‘fu ‘anhu

 

“Ee Rabb Mghufirie na Umrehemu”.

 

Wa akrim nuzulahu wa wasi‘i mudkhalahu.

 

“Na Ukirimu kushuka kwake na Yapanue maingilio yake”.

 

Waaghsilhu bilmai wath-thalji walbard. Wanaqih minal Khatwaaya kama yunaqqath-thawabul abyadhw minad-danas. Wa-abdilhu daaran Khayran min daarihi wa ahlan khayran min ahlihi. Wazawjan khayran min zawjih Wa a ‘idhhu min adhabil Qabr wa adhaabin-naar Allaahumma abdili sayyiatahu hasanaat. Allaahumma in Kaana musiy-an fatajawaz ‘an sayyiatihi.

‘Na muoshe kwa maji, theluji na ubaridi (barafu)’ Na yasafishe makosa yake kama inavyosafishwa nguo nyeupe kutokana na uchafu. Na mbadilishie nyumba bora kuliko nyumba yake na jamaa bora kuliko jamaa zake. Ikiwa anayeswaliwa ni mwanamke basi maneno haya hayatajwi (Na mke bora kuliko wake). Na mwepushe na adhabu ya kaburi na adhabu ya moto. Ee Rabb mbadilishie makosa yawe ni thawabu. Na akiwa ni muovu basi yasamehe maovu yake.

 

Baada ya Takbira ya nne soma du‘aa ifuatayo:

 االلهم لا تحرمنا أجره ولا تفتنا بعده واغفر لنا وله وللمسلمين 

Allaahumma laa tahrimnaa ajrahu walaa taftinnaa ba‘adahu waghfirlanaa walahu walilmuslimiyn.

 

‘Ee Rabb Usituharamishie ujira wake wala Usitufitini baada yake na Utusamehe sisi na yeye na Waislamu wote’.

 

 

Katika Kulichukua Jeneza

 

·       Liharakisheni Jeneza langu enyi wapenzi wa Rasuli wa Allaah.

 

·       Na nyamazeni kabisa katika Jeneza kama kwamba katika vichwa vyenu kuna ndege.

 

·       Wala wasifuate Jeneza langu wanawake.

 

·       Wala asilie yeyote kwa sauti…

 

·   Subira wakati wa msiba mkubwa. Na kubwa zaidi ya hiyo kuna ujira wa ridhaa katika Qadhwaa (hukumu) ya Allaah yote… kheri na shari… Tamu na chungu.

 قل كل من عند الله فمال هؤلاء القوم لا يكادون يفقهون حديثا

Sema: Yote ni kutoka kwa Allaah. Basi wana nini hawa watu hawakaribii kufahamu kauli? [An-Nisaa: 78]

 

·    Kueni wanyenyekevu wakati wa Jeneza mkitafakari jambo hili kubwa la mauti. Wala musizungumze kwa hadiyth za dunia na musifanye dhihaka. Musiseme pia, “wahhiduhu” ‘mpwekesheni’ au “Astaghfiru Allaah”. Na amkumbuke Allaah yule mwenye kuchukua Jeneza.

 

·     Msiguse Jeneza kwa mikono, vitambara au vitu vingine kwa Niyyah ya kujipata baraka; Hii ni haraam.

 

 

Wakati Wa Kuzika Na Baada Yake

 

Mnapoingia kwenye makaburi semeni:

 

Assalaamu ‘alaykum daara qawmin muuminiyna antum saabiquuna wa ghadan in shaa Allaah nahnu bikum laahiquun. Nas-alu Allaah lana walakumu l’aafiya.

 

“Amani iwe juu yenu nyumbani mwa watu waumini Nyinyi mumetutangulia na sisi kesho Anapopenda Allaah tutakua ni wenye kuwafuatia. Tunamuomba Allaah Atupatie sisi na nyie.

 

§  Enyi watu, wanizike marafiki zangu walio wema. Mnaponiingiza kaburini semeni:

بسم الله وعلى سنة رسول الله 

“BismiLlaahi wa ‘alaa Sunnati Rasuuli Allaah.”

 

Kwa jina la Allaah na kwa Sunnah ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)

 

§  Enyi wapenzi wangu, marafiki na ndugu zangu katika imani ambao niliwapenda duniani kutafuta radhi za Allaah. Msiniache peke yangu wakati huu ambao nina haja kubwa nanyi. Kaeni pamoja nami kwenye kaburi kiasi cha kutosha huku mkiniombea du‘aa Allaah Atawaruzuku mwenye kuwaombea du’aa mnapokufa.

 

Allaah Awalipe wote… Msiba wa kishariy’ah umemalizika kwa kulifuata Jeneza na wala hakuna msiba kabisa kwa wanawake….Allaah Awarehemu.

 

§  Mimi niko mbali na maneno au vitendo vinavyokwenda kinyume na shariy’ah ya Allaah na Sunnah ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).  

 

§  Muogopeni Allaah mwisho wa kumuogopa na sikilizeni na kutii na muwe na hadhari na maneno ya Allaah Aliyetukuka: 

 إِنَّ الَّذِينَ يَكْتُمُونَ مَا أَنزَلْنَا مِنَ الْبَيِّنَاتِ وَالْهُدَى مِن بَعْدِ مَا بَيَّنَّاهُ لِلنَّاسِ فِي الْكِتَابِ أُولَئِكَ يَلعَنُهُمُ اللّهُ وَيَلْعَنُهُمُ اللَّاعِنُونَ. إِلاَّ الَّذِينَ تَابُواْ وَأَصْلَحُواْ وَبَيَّنُواْ فَأُوْلَئِكَ أَتُوبُ عَلَيْهِمْ وَأَنَا التَّوَّابُ الرَّحِيمُ.

Hakika wale wanaoficha yale Tuliyoyateremsha katika hoja bayana na mwongozo baada ya kuwa Tumeyabainisha kwa watu katika Kitabu, hao Anawalaani Allaah na wanalaaniwa na kila mwenye kulaani. Isipokuwa wale waliotubu na wakatengenea na wakabainisha (haki); basi hao Napokea tawbah zao, Na Mimi ni Mwingi wa kupokea tawbah, Mwenye kurehemu. [Al- Baqarah: 159-160].

 

§  Zingatieni maneno ya Allaah: 

أَلاَّ تَزِرُ وَازِرَةٌ وِزْرَ أُخْرَى﴿٣٨﴾. وَأَن لَّيْسَ لِلْإِنسَانِ إِلاَّ مَا سَعَى﴿٣٩﴾ وَأَنَّ سَعْيَهُ سَوْفَ يُرَى﴿٤٠﴾ ثُمَّ يُجْزَاهُ الْجَزَاء الْأَوْفَى﴿٤١﴾ وَأَنَّ إِلَى رَبِّكَ الْمُنتَهَى﴿٤٢﴾  

Na kwamba mbebaji dhambi hatobeba mzigo wa mwenginewe. Na kwamba insani hatopata (jazaa) isipokuwa yale aliyoyafanyia juhudi. Na kwamba juhudi yake itakuja kuonekana. Kisha atalipwa jazaa kamilifu. Na kwamba kwa Rabb wako ndio kikomo [An-Najm: 38-42]

 

 

Wasiya Wangu Wa Mwisho

 

I.  Nawausia mugawe mirathi kulingana na shariy’ah ya Allaah na yenye kumridhisha Yeye na kuweni enyi vipenzi vyangu ni wenye kupendana nyinyi kwa nyinyi. Na pendaneni na wapatieni wenzenu nafasi ya mwanzo ingawa hali zenu ni ndogo. Kila mmoja atapitia njia hii ya mauti kama mimi. Fanyeni ‘amali kwa siku hii, mutapata furaha kukutana na Allaah mukiwa katika hali ya amani na utulivu. Siku ya Qiyaamah Ataita Allaah Aliyetukuka:

أين المتحابون بجلالى ؟ اليوم أظلهم فى ظلى يوم لا ظل إلا ظلى, رواه مسلم

“Wawapi waliopendana kwa ajili ya Utukufu wa Allaah leo nitawaweka kwenye kivuli Changu siku ambayo hakutakuwa na kivuli ila kivuli Changu”. [Muslim]

 

II. Kuweni karibu na mama yenu

[1]katika kheri na mpatieni badali kwa safari yake pamoja nami na nyinyi. Na kuweni wenye kumshughulikia kihakika, mtapata furaha hapa duniani na kesho Aakhirah. Nami najikosha na kila kitendo au maneno yanayokwenda kinyume na shariy’ah ya Allaah na Sunnah ya Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Ninawaageni kwa jina la Allaah ambaye muagano Wake haupotei.

 

Imeandikwa tarehe…………………………..…

Mwenye kuusia…………………………………

Mashahidi…………………………………..……

 

Wasiya Wangu Haswa

  

“Inafaa kwa Mwenye kuusia, kuusia thuluthi ya alivyoacha kwa mwenye kupenda.” 

 

[1]Akiwa mama yuko hai. Wasiya huu unaweza kutumika kwa mtu yeyote yule  ingawa umekusudiwa kwa wanaume.

Share