Kuosha Maiti

 

Kuosha Maiti

 

Imetayarishwa Na: Abu ‘Abdillaah

 

Alhidaaya.com

 

 

 

·  Kumuosha, kumkafini, kumswalia na kumzika maiti ni ‘Fardhu Kifaayah’, yaani ni jambo ambalo baadhi ya Waislam wakifanya basi hukumu hiyo hutenguka kwa waliobaki (si lazima walifanye). Lakini ikiwa hakuna atakayelifanya basi jamii nzima itabeba madhambi kwa kuacha Fardh hiyo.

  

 

 

·   Ni bora zaidi wamuoshe maiti wale wenye elimu ya kuosha na hususan wale mawasii wake, yaani wale watu waliousiwa na maiti kumuosha. Na jamaa wa familia. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alioshwa na binamu yake ‘Aliy bin Abi Twaalib, Al-Fadhl bin ‘Abbaas na Usaamah bin Zayd ambaye ni mtoto wa mwana wa kupanga wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) [Abu Daawuud].

 

 

 

·   Mwanamke vilevile ataoshwa na wenye elimu katika wanawake wenzake hususan wasii wake wa kike, kisha mama yake na halafu binti yake kisha waliokaribu zaidi nae katika jamaa zake. Bint wa Nabiy (Swalla Allaahu’alayhi wa aalihi wa sallam) Zaynab (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) alioshwa na Ummu ‘Atwiyyah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) mama mwenye elimu akiwa na wanawake wengine ambaye waliamriwa na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumuosha. [Al-Bukhaariy, Muslim na wengine].

  

 

 

·  Mume atamuosha mkewe, Amesema mama ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa): “Aliporejea kwangu Nabiy akitoka mazikoni, na mimi nikiwa na maumivu kichwani, na huku nikisema Ee! Maumivu ya kichwa changu (kichwa chaniuma). Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) naye akasema, “Bali hata mimi Ee ‘Aaishah najisikia maumivu ya kichwa changu, maumivu hayo hayatakudhuru, na lau ukifa kabla yangu basi, nitakusimamia, kukuosha na kukuvika sanda, kukusalia na kukuzika.” [Ahmad, Ibn Maajah na wengine].

 

 

 

·     Mke vile vile atamuosha mumewe, kwani Amesema mama ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa): “Lau ningekuwa nimelielekeza jambo la kumuosha Nabiy Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam alipofariki kuwa jambo hilo katika amri yangu mimi, nisingelipa mgongo jambo hilo na wasingemuosha Nabiy Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam isipokuwa wakeze.” [Ibn Maajah, Ibn Hibbaan na Al-Haakim]. Kadhaalika Abu Bakr aliusia akifa aoshwe na mkewe. [‘Abdur-Razzaaq].

 

 

 

·     Akifa mwanaume katika kundi la wanawake watupu au akifa mwanamke katika kundi la wanaume, basi haoshwi bali hufanyiwa ‘Tayammum’ (yaani hutwaharishwa kwa udongo/mchanga), ataipiga mikono yake kwenye ardhi ambapo kuna mchanga au udongo kisha ataupangusa uso na viganja vya maiti.

  

 

 

·   Inapendeza maiti kuoshwa majosho matatu au matano kulingana na hali halisi ya maiti huyo. Hii ni kutokana na Hadiyth iliyosimuliwa na Ummu ‘Atwiyah kuwa: “Aliingia Nabiy Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam wakati tukiwa tunamuosha binti yake, Zaynab, akasema: “Muosheni mara tatu au mara tano au mara saba au zaidi ya hapo ikiwa mtaona haja ya kufanya hivyo...” [Al-Bukhaariy, Muslim na wengineo]

 

 

 

·    Hutumika maji ya kawaida kumuoshea maiti, lakini ikibidi hata ya vuguvugu yatatumika, kwa mfano ikiwa mwili wa maiti una uchafu ambao inabidi yatumike maji yenye umoto kiasi ndio yatoe uchafu huo. Pia atumie sabuni kuondosha uchafu lakini asitumie nguvu kumsugua asije akamchubua, vilevile atumie kitambaa kilichorowa kusafisha meno ya maiti.

 

 

 

·    Inatakiwa wakati wa kumuosha maiti wa kiume, kumsitiri utupu wake kwa kumfunika kwa nguo itakayomsitirina macho ya watu kuanzia juu ya kitovu hadi chini ya magoti. Na maiti ya kike kuanzia shingoni kwake hadi miguuni.

 

 

 

·   Muoshaji inapendeza avae glavu ‘gloves’ (vifuniko vya mikono) kabla ya kuanza kumuosha maiti kisha muoshaji anatakiwa akinyanyue kichwa cha maiti hadi kikaribie usawa wa kukaa kwake na kisha alichue kwa upole tumbo lake ili litoe uchafu ulioko tumboni na wakati huo huo azidishe kumwagia maji sehemu ya uchafu ili uondoke.

 

 

 

·     Kisha ausafishe utupu wa maiti bila ya kuutazama.

 

 

 

·    Kisha aseme BismiLlaah na kumtawadhisha Wudhuu kama wa Swalah kama alivyoelekeza Nabiy Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam  kwa wanawake waliokuwa wakimuosha binti yake aitwaye Zaynab, “Anzeni kuliani mwake wakati mnamuosha na pia sehemu za Wudhuu mwilini mwake” [Al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud na wengine]. Atumie kitambaa kilichokuwa kidogo chenye majimaji na kusafisha meno yake, puani mwake na masikioni mwake.

 

 

 

·    Inapendeza vilevile asafishe nywele na ndevu za maiti kwa kutumia sabuni, na kisha mwili mzima.

 

 

 

·     Kisha amsafishe (amuoshe) upande wa kuliani kwake, sehemu za mbele na za nyuma tena hivyo hivyo upande wa kushotoni kwake kwa Hadiyth ya Nabiy isemayo, “anzeni kuliani mwake…” [Al-Bukhaariy na Muslim], kisha aendelee kumsafisha hivyo hivyo mara ya pili na ya tatu kwa maneno yake Nabiy Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam, “muosheni mara tatu” [Al-Bukhaariy na Muslim], na wakati akimuosha aupitishe mkono wake katika mwili wake (maiti) kuusugua ili kutoa uchafu kama upo.

 

 

 

·     Inapendeza tuwawekee maiti manukato, Nabiy Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam alisema kuwaambia wanawake waliokuwa wakimuosha bint yake: “Na muwekeeni mwisho wa kumuosha chochote katika manukato” na riwaya nyingine Nabiy Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam amesema: “Tumieni Kaafuur katika muosho wa mwisho.” [Al-Bukhaariy, Muslim, At-Tirmidhiy na wengine].

 

 

 

·     Mwanamke nywele zake hugawanywa au husukwa minyoosho mitatu na kuunganishwa nyuma kama alivyofanyiwa Zaynab bint wa Nabiy Swalla Allaahu ‘alayhi wa aaliji wa sallam. Ummu ‘Atwiyyah anasema: “Tulipomuosha binti ya Nabiy Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam tulizifumua nywele zake, kisha tukaziosha na kuzichana, na kuzisuka kwa mistari mitatu tukazitupa nyuma yake.” [Al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud na Ibn Maajah].

 

 

 

·     Inapendeza kumpangusa maji na kumkausha baada ya kumuosha.

 

 

 

·     Ikiwa maiti atatokwa na uchafu wowote (mkojo, kinyesi au damu) baada ya kuoshwa mara saba, basi atawekewa pamba kwenye utupu wake na kisha kuoshwa pale pahala palipoingia najisi na kisha kutawadhishwa.

 

 

 

·    Endapo kitatoka kitu kichafu baada ya kwisha kukafiniwa basi hakuna haja tena kumuosha kwa kuepusha taklifa na usumbufu.

 

 

 

·   Kutopatikana udhuru wa kutoweza kuoshwa maiti ima kwa kukosekana maji au mwili wake unakatikakatika hauwezi kuosheka au umeungua kwa moto basi kwa hali hiyo anatakiwa atayamamishwe (afanyiwe tayammum): yaani mtu atapiga matumbo ya viganja vyake katika udongo au mchanga kisha ataupangusa uso na viganja vya maiti.

 

 

 

·    Anayemuosha maiti ni bora baada ya kuosha aoge. Na hakuna neno ikiwa hatooga. Kwani kuna Hadiyth mbili na zote sahihi zenye kuthibitisha kuoga na kutooga. Moja Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) anasema“Mwenye kumuosha maiti afanye ghusl (aoge) na anayembeba (kilili, machela, jeneza lake) achukue Wudhuu” [Abu Daawuud na Ibn Maajah]. Nyingine inasema: “Haiwapasi kufanya ghusl (kuoga) kwa kuosha maiti wenu, kwani hakika maiti wenu si najisi, yawatosha nyinyi kuosha mikono yenu” [Al-Bayhaqiy na Al-Haakim]

 

 

 

·   Inampasa muoshaji amsitiri maiti ikiwa ataona kuna kitu hakipendezi kwa maiti huyo, kama vile uso wake umeharibika au kuna jeraha katika kiwiliwili chake au kovu la kutisha, au kasoro yoyote mwilini mwake n.k. Kadhaalika muoshaji asitoe siri za maiti nje, kwani Nabiy Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam amesema, “Mwenye kumuosha maiti akaficha siri zake, basi Allaah Atamsamehe yeye mara arobaini”. [Al-Haakim na ikathibitishwa usahihi wake na Imaam Al-Albaaniy]

 

 

 

·    Atakapofariki   (mwenye kufanya Hajj au ‘Umrah) basi ataoshwa kwa maji na Sidr (majani ya mkunazi) kama ilivyotangulia lakini tofauti ni kwamba yeye hatotiwa manukato wala kufunikwa kichwa chake ikiwa ni mwanaume kama alivyosema Nabiy Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam kuhusu mtu aliyefariki akifanya Hajj: ”Msimpake manukato au msimuoshe kwa manukato” na akasema pia, “wala msimfunike kichwa chake kwani yeye anafufuliwa siku ya Qiyaamah akilabii (yaani akipiga talbiyah kwa kusema Labbayka Allahumma Labbayka)”. [Al-Bukhaariy, Muslim, na wengine].

 

 

 

·  Shahidi aliyefariki vitani haoshwi, kwani Nabiy Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam “aliamrisha mashahidi wa Uhud wazikwe na nguo zao bila kuoshwa”. [Al-Bukhaariy na Muslim]. Huzikwa shahidi anayekufa vitani na nguo zake baada ya kuondolewa silaha alizokuwa nazo mwilini mwake. Wala haswaliwi kwani Nabiy Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam hakuwaswalia mashahidi wa vita vya Uhud.

 

 

 

·  Kiumbe kilichofika miezi minne tumboni mwa mama yake kikitoka kinaoshwa na kinaswaliwa na kinapewa jina kwa kauli ya Nabiy Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam: “…Hakika mmoja wenu anakuwa katika tumbo la mama yake siku arobaini ni tone la manii, kisha anakuwa kipande cha damu mfano wa hivyo (yaani siku arobaini nyingine), kisha kinakuwa kipande cha nyama mfano wa hivyo (yaani siku arobaini nyingine), kisha anatumwa Malaika kukipulizia roho”. [Muslim]. Ama kikiwa kabla ya miezi minne kinakuwa kipande cha nyama kinazikwa pahala popote bila kuoshwa wala kuswaliwa.

  

 

 

·     Ni haramu kwa Muislamu kumuosha au kumzika kafiri kwa mujibu wa maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa),  

وَلَا تُصَلِّ عَلَىٰ أَحَدٍ مِّنْهُم مَّاتَ أَبَدًا

Na wala usimswalie yeyote abadani miongoni mwao akifa..” [At-Tawbah: 84]. 

 

Ikiwa imekatazwa kuwaswalia hao makafiri ambalo ndio jambo kubwa zaidi, basi kuwaosha na kuwazika nayo pia yamekatazwa. Hata hivyo, baadhi ya ’Ulamaa wamejuzisha mtu kuosha jamaa yake asie Muislamu na kusindikiza Jeneza lake.

 

 

 

·  Wanachuoni kama Imaam An-Nawawiy, Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahuma Allaah) na wengineo wanaona akiwa amefariki mama mja mzito na ikaonekana mtoto aliye tumboni yu hai na kuna uhakika wa mtoto huyo kuishi, basi anaweza mtoto kutolewa na ikibidi kupasuliwa mama kwa ajili hiyo inawezwa kufanywa hivyo kwa kauli iliyo na nguvu zaidi. La kama hakuna uhakika wa hilo, basi mama ataoshwa yeye mwenyewe -na kiumbe kikiwa tumboni kwake- na kukafiniwa na kuswaliwa mwenyewe na kuzikwa. [Rawdhatut Twaalibiyn 2/143  na Majmu’u Fataawa 11/333 ]

  

 

 

·     Ikiwa mtu kafariki na baadhi ya viungo vyake, kama mikono au mguu, vimekosekana. Na maiti huyu ameoshwa, kaswaliwa, na hatimaye kuzikwa akiwa hana viungo vyote. Mara tu baada ya kuzikwa kikaonekana kiungo au baadhi ya viungo vilivyokosekana, anasema Shaykh Muhammad bin Swaalih Al-‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah), akajibu: 

 

“Viungo vidogo vidogo kama mikono na miguu vitakapopatikana na maiti ameshaswaliwa, viungo hivi havitaoshwa wala kuswaliwa kwa kuwa ameshaswaliwa.”

 

“Ama itakapokuwa maiti haikupatikana bali kimepatikana kiungo katika mwili wake kama vile kichwa au mguu au mkono, basi kitaswaliwa na kuzikwa kilichopatikana baada ya kuoshwa vizuri na kuvishwa sanda.” [Fataawa Arkaanil Islaam uk. 406]

 

·     Amesema Mwanachuoni Shaykh Ibn Baaz (Rahimahu Allaah): “Utaratibu wa kuosha maiti ni kumsitiri sehemu zake za siri, kukamua tumbo lake kwa taratibu na kwa upole na kumsafisha kwa kitambaa sehemu za siri kisha kumtawadhisha Wudhuu wa Swalah na kisha kumuosha kichwa chake, ndevu zake, kisha upande wa kulia kisha kushoto mara tatu au tano, jinsi utakavyoona.” [Majmu’u Fataawa Ibn Baaz, Duruus Muhimah, uk. 12]

   

 

Yasiofaa

 

 

·    Kukanda au kuliminya tumbo la maiti kwa nguvu ili kutoa uchafu uliomo tumboni.

 

 

·    Kukata kucha za maiti na kunyoa nywele za kwapani au za sehemu za siri.

 

 

·    Kuweka pamba kuziba tundu za sehemu zake za siri za nyuma, pua, koo, masikio n.k. hali ya kuwa hakuna kinachotoka au kuvuja katika sehemu hizo. Kukiwa na dharura ya kuvuja au kutoka chochote sehemu hizo baada ya kuoshwa, basi hakuna ubaya kwa hali hiyo kuzibwa kwa pamba.

 

 

·  Kusoma Adhkaar maalum wakati vinaoshwa viungo vya maiti, au waoshaji kusoma Adhkaar kwa pamoja tena kwa sauti ya juu.

 

 

·    Kusoma Surat Yaasiyn au Aayah zingine za Qur-aan wakati wa kumuosha maiti.

 

 

·    Kusuka nywele za mwanamke na kuzilaza kifuani mwake.

 

 

 

Share