Kukafini Maiti

 

Kukafini Maiti

 

Imetayarishwa Na: Abu ‘Abdillaah

 

 

Alhidaaya.com

 

 

·     Yampasa kumkafini maiti na vile vile yapasa gharama za sanda zitokane na mali ya maiti mwenyewe kama alivyosema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wakati alipofariki mtu akiwa katika hali ya kuhirimia, “Mkafinini kwa nguo yake” [Al-Bukhaariy na Muslim] yaani vazi lake la ihraam na huko kumkafini (kumpamba) maiti kunatangulizwa kabla ya deni lake kulipwa kama analo na hata kabla ya kuutekeleza wasiya wake wa Mirathi.

 

·     Sanda huwa ni shuka tatu (3) tu, na si zaidi, kutokana na Hadiyth iliyosimuliwa na Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) “Alikafiniwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika nguo tatu nyeupe, hakuna kanzu wala kilemba katika sanda hizo.” [Imaam Ahmad na Abu Daawuud]. Hili la sanda vipande vitatu ni kwa wanaume na kwa wanawake kwani Hadiyth hapo juu inaweka kanuni ya jumla na hakuna kauli iliyokuja kutofautisha baina yao. Ama Hadiyth inayoeleza kuwa mwanamke anakafiniwa kwa vipande tano, hiyo ni Dhaifu.

 

·    Ni wajibu kumvika sanda nzuri maiti, au thamani ya sanda itokane na mali ya maiti, ndugu zake, jamaa zake, na isiwe sanda ya thamani kubwa, na avikwe maiti sanda hiyo kwa utaratibu alofundisha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) bila kuzidisha chochote, na amesema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) “Mmoja wenu anapomvika sanda ndugu yake, basi amvike sanda iliyo nzuri akiweza.” [Muslim, Abu Daawuud, na Ahmad]. Na makusudio ya sanda nzuri ni ile sanda ilio safi na yenye kutosha kumsitiri maiti mwili wake wote, na sio kufanya israfu katika sanda kwa kununua sanda ya thamani kubwa kama alivyofafanua Imaam ‘Abdullaah bin Mubaarak.

 

·    Endapo maiti huyo hakuwa na uwezo wa kuwa na sanda basi jamaa zake wenye kuhusiana naye watakuwa na wajibu wa kuandaa sanda kwa ajili yake. Nao ni watu wake kama baba yake, babu, mwanae wa kiume au mtoto wa mwanae (mjukuu). Na endapo wote hao watashindwa au atakuwa hana jamaa, basi litakuwa jukumu la Baytul Maal’, yaani litatolewa fungu kutoka katika hazina ya Waislam kama ipo, na kama haipo basi litakuwa jukumu la Muislam yeyote aifahamuye hali ya huyo maiti.

 

·     Kinachopasa kumkafini maiti ni nguo itakayomsitiri mwili mzima.

 

·    Sanda inapendeza iwe nyeupe kwa Hadiyth isemayo: “Vaeni nguo nyeupe kwani ni vazi bora katika mavazi yenu, na mkafiniane kwazo” [Abu Daawuud, At-Tirmidhiy, na Ibn Maajah kaisahihisha].

 

·    Vipande hivyo vya sanda hutiwa harufu nzuri ya aina ya ubani uliosagwa, kisha hukunjwa moja juu ya nyingine na pia hutiwa kwenye sanda hiyo ‘Hanuut’ aina ya unga wenye harufu nzuri ambayo ni maalum kwa maiti na kisha baada ya hapo maiti hulazwa juu ya hiyo sanda iliyotiwa vitu hivyo, na hulazwa chale.  

 

·    Ukubwa wa shuka hizo za sanda unatakiwa uzidi kimo cha maiti kutegemea na urefu na upana wa maiti. Kuongezwe futi mbili kuzidi kile kimo cha maiti, kwa mfano kama maiti ana urefu wa futi sita, basi urefu wa shuka uwe futi nane na upana uwe futi sita ili stara iwe nzuri zaidi.

 

·    Baada ya kutandikwa sanda, maiti atalazwa juu yake akiwa amefunikwa sehemu zake za siri; juu ya kitovu hadi chini ya magoti yake. Itachukuliwa ncha ya upande wa kulia na iletwe hadi kifuani mwake, na ncha ya kushoto itafanywa hivyo hivyo, akishafunikwa na sanda hizo wakati huo huo itachomolewa ile shuka au taulo aliyokuwa amesitiriwa nayo sehemu zake za siri. Utaratibu huo utafuatwa kwa shuka ya pili na ya tatu. Kisha sanda hiyo husokotwa mwisho wake na kuanza kufungwa ili isije ikaachia sehemu yeyote na kulegea; husokotwa ncha ya hivyo vipande vya sanda upande wa kichwani na miguuni na kufungwa kwa kamba zilizotayarishwa. Na hufungwa nchani na katikati ya mwili hizo kamba kuweka himaya tu sanda zisiachie na kufunuka maiti, bila kukazwa kamba hizo. Na anawezwa maiti kufungwa mafundo matatu hadi saba kulingana na uimara na mahitajio.

 

·  Mpaka hapa, maiti itakuwa tayari kwa ajili ya kutekelezewa jambo la tatu ambalo ni kuswaliwa. 

 

·   Maiti ikishafikishwa kaburini na kuingizwa kwenye mwanandani, zinaweza kamba hizo kufunguliwa au kuachwa hakuna neno.

 

·   Kukikosekana vitambaa kama ilivyotajwa juu, huruhusiwa kumkafini maiti kwa vazi la kawaida kama shuka ya chini (kikoi) na nguo ya juu kama kanzu au shati ila ni bora zaidi kutumia mfumo uliotajwa mbeleni.

 

·    Na kukikosekana kabisa sanda atakafiniwa kwa vazi lake alilonalo au vazi lolote la kuweza kumsitiri, na ikiwa kakosa cha kumsitiri mfano yuko jangwani au porini, basi atasitiriwa na kitakachopatikana kama majani, matawi au chochote cha stara.

 

·   Mwanamke anakafiniwa kwa nguo au vitambaa vitatu kama tulivyotangulia kutaja huko nyuma, na hakuna dalili inayothibitisha kuwa anakafiniwa kwa vipande vitano kama baadhi ya mapokezi dhaifu yanavyoonyesha. Kuna wanaosema kuwa mwanamke anakafiniwa kwa vipande vitano. Nao wanategemea Hadiyth ya Layla bint Qaaif Ath-Thaqafiy inayoeleza kuwa sanda ya kike ni nguo tano zikiwa shuka ‘Izaar’ mbili, kikoi, kanzu ‘Qamiys’, na kilemba, ‘Khimaar’. Hadiyth hii upokezi (isnadi) yake ni dhaifu. Ndani ya msururu wa wapokezi (isnadi) kuna mtu mmoja, anaitwa Nuuh bin Haakim Ath-Thaqafiy, ambaye hajulikani zaidi ya jina lake tu, kama alivyoelezea al-Haafidh bin Hajar na wengineo. Hivyo itabaki kuwa mwanamke hukafiniwa kama mwanaume kwa vipande vitatu maadam hakuna dalili sahihi ya kutofautisha mwanaume na mwanamke katika kafan.

  

Yasiofaa

 

·     Kutumia zaidi ya sanda tatu.

 

·     Kutumia sanda za ghali.

 

·   Kuandika jina la maiti kwenye kikaratasi au maneno mbalimbali kisha kukitia ndani ya sanda azikwe nayo.

 

·     Kutumia kipande cha sanda cha ziada kuzungushia sehemu za siri za maiti.

 

·     Kuandika baadhi ya du’aa au Aayah za Qur-aan juu ya sanda.

 

Share