Ramadhwaan Huishia Na 'Iyd?

 

Ramadhwaan Huishia Na 'Iyd?

 

Alhidaaya.com

 

 

Ukimuuliza Muislam yeyote suala hili bila shaka utapata jawabu la “ndio”, Ramadhwaan huisha ile siku tunayojumuika pamoja kwa furaha kusheherekea ‘Iyd-ul-Fitwr. Maamrisho ya kujizuwia kula, kunywa na mashirikiano ya kimwili kati ya mke na mume wakati wa mchana wa Mwezi wa Ramadhwaan tunayapata moja kwa moja kutoka kwenye Qur-aani Tukufu na Hadiyth za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam). Lakini kwa kweli kama tutachunguza kwa undani baraka zilizo katika Mwezi huu Mtukufu wa Ramadhwaan, tutaona kwamba mafunzo yake yanakusudiwa kubakia na kutekelezwa na kila mmoja wetu baada ya kumalizika kwa chuo hichi adhimu kwa muda wote utakaofuatia baada ya Ramadhwaan.

 

Kwanza kabisa, suala zima la kujizuwia na kula, kunywa na matamanio ya kiwiliwili kutoka alfajiri hadi magharibi tunapata mafundisho maalumu. Katika mafunzo hayo ni pamoja na:

 
1)     Utulivu na Upole

2)     Kuwa na tafakur

3)     Kuishi ndani ya Qur-aan

4)     Kuwafikiri waja wenzetu na hali ya Ummah wa Kiislam kwa ujumla

5)    Kujiweka mbali na mapambo na matamanio ya vitu vya kidunia
 

Mafunzo haya na neema nyingi nyingi yatatuwezesha, kwa uwezo wa Allaah, kutupa faida ya hali ya juu ya uvumilivu na ustahamilivu katika nafsi zetu. Allaah Anasema katika Qur-aan:

 

 يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اسْتَعِينُوا بِالصَّبْرِ وَالصَّلَاةِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ مَعَ الصَّابِرِينَ ﴿١٥٣﴾

Enyi walioamini! Tafuteni msaada kwa subira na Swalaah; hakika Allaah Yu pamoja na wanaosubiri. [Al-Baqarah: 153]

 

Kumpenda Allaah (Subhaanahu Wa Ta'aalaa) na kumtii kwa maamrisho Yake ndio msingi wa 'ibaadah na ndio lengo hasa la sisi wanaadamu kuwepo hapa ulimwenguni. Kwa ajili hiyo basi tunapojiuliza na kutafakari mafunzo tunayopata ndani ya Ramadhwaan na umuhimu wake kwa maisha yetu ya kila siku, inatubainikia kuwa lengo hasa la kuingia kwenye chuo hichi adhimu ni kuziweka nyoyo zetu ndani ya taqwa ya kumtii Allaah (Subhaanahu Wa Ta'aalaa) kwa muda wote unaofuatia baada ya Ramadhaan.

 

Allaah Anasema ndani ya Qur-aan:

 

يَا أَيُّهَا النَّاسُ قَدْ جَاءَتْكُم مَّوْعِظَةٌ مِّن رَّبِّكُمْ وَشِفَاءٌ لِّمَا فِي الصُّدُورِ وَهُدًى وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ﴿٥٧﴾قُلْ بِفَضْلِ اللَّـهِ وَبِرَحْمَتِهِ فَبِذَٰلِكَ فَلْيَفْرَحُوا هُوَ خَيْرٌ مِّمَّا يَجْمَعُونَ﴿٥٨﴾

Enyi watu! Kwa yakini yamekujieni mawaidha kutoka kwa Rabb wenu, na shifaa ya yale yaliyomo vifuani, na mwongozo na rahmah kwa Waumini. Sema: Kwa fadhila za Allaah na kwa rahmah Yake basi kwa hayo wafurahi. Hayo ni khayr kuliko wanayoyakusanya. [Yuwnus: 57–58]

 

Hivyo basi ni wazi kabisa kuwa 'ibaadah ya funga ya Ramadhwaan ni katika nguzo kubwa iliyo muhimu ya Dini ya Kiislam iliyokusudiwa kutusaidia kama wanaadamu katika kufanikisha  lengo la kuwepo kwetu duniani kama Makhalifa wa Allaah (Subhaanahu Wa Ta'aalaa).

 

 Kwa kuwa Ramadhwaan ni chuo adhimu cha kutuleta ndani yake taqwa pale tunapokuwa wastahamilivu na wanyenyekevu katika kufuata maamrisho ya Allaah ndani ya nafsi zetu tunapata faida ya kuwa waadilifu na kuipigania njia ya Allaah ndani ya nafsi zetu kwanza. Vita hivi vya kuzilea nafsi kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu Wa Ta'aalaa), huitwa Jihaad.

 

Jihaad inakusanya yale yote, kuanzia vita dhidi ya makafiri na ushirikina na yale yote yaliyokatazwa na Allaah (Subhaanahu Wa Ta'aalaa) ili kupata daraja ya juu kabisa ya mafanikio katika maisha ya Muislam mbele ya Allaah (Subhaanahu Wa Ta'aalaa) Allaah Anasema katika Qur-aan:

 

الَّذِينَ آمَنُوا وَهَاجَرُوا وَجَاهَدُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ بِأَمْوَالِهِمْ وَأَنفُسِهِمْ أَعْظَمُ دَرَجَةً عِندَ اللَّـهِ ۚ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْفَائِزُونَ﴿٢٠﴾

Wale walioamini na wakahajiri na wakafanya jihaad katika njia ya Allaah kwa mali zao na nafsi zao; wana daraja kuu kwa Allaah. Na hao ndio waliofuzu. [At-Tawbah: 20]

 

Wengi wetu huelewa neno Jihaad ni kuchukua silaha na kwenda vitani. Jihaad kubwa haswa ni kupigana na nafsi zetu kwa kuacha yale yote tuliyokatazwa na Allaah (Subhaanahu Wa Ta'aalaa) na Rasuli wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) na kufanya yale tuliyoamrishwa ndani ya Uislaam.

 

Kwa kufanya hivyo tu ndio tutafuzu mbele ya Allaah (Subhaanahu Wa Ta'aalaa) kwa kuishi maisha bora hapa duniani na kutarajia mema kesho Aakhirah.

 

Hivyo basi kwisha kwa Ramadhwaan isiwe ndiyo mwisho wa sisi kufanya mema na kuishi nje ya mipaka ya Allaah (Subhaanahu Wa Ta'aalaa), bali tubebe tabia zote njema tulizojifunza ndani ya mwezi huu mtukufu na kwa kufanya hivyo tu , ndio tutakuwa Waislamu wa kweli.

 

Share