Mashaytwaan Kufungwa Minyororo Mwezi Wa Ramadhwaan

 

Mashaytwaan Kufungwa Minyororo Mwezi Wa Ramadhwaan

 

Alhidaaya.com

 

 

Mashaytwaan kufungwa minyororo ukiingia mwezi wa Ramadhwaan. 

 

Imepokewa kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: 

 

إِذَا جَاءَ رَمَضَانُ فُتِّحَتْ أَبْوَابُ الْجَنَّةِ وَغُلِّقَتْ أَبْوَابُ النَّارِ وَصُفِّدَتْ الشَّيَاطِينُ 

Ukiingia mwezi wa Ramadhwaan, milango ya Jannah hufunguliwa, milango ya Moto hufungwa na Mashaytwaan hufungwa minyororo. [Al-Bukhaariy na Muslim] 

 

 

Ufafanuzi wa Hadiyth hii kwa mujibu wa Wanachuoni 

 

Al-Haafidhw Ibn Hajr (Rahimahu Allaah): 

 

“Inaweza kutafsiriwa kuwa Mashaytwaan hawana uwezo wa kuwatia katika mtihani Waumini kulinganisha na nyakati nyingine (miezi mingine) kwa kuwa Waumini wanakuwa hodari na funga zao na kukata matamanio yao kwa kusoma sana Qur-aan na kumdhukuru Allaah”.  

 

Wanachuoni wengine wamesema: 

 

“Mashaytwaan wanaokusudiwa ni Mashaytwaan wakubwa peke yao" 

 

 

Ibn Iyaadhw (Rahimahu Allaah) alisema: 

 

"Inaweza kufasiriwa kimaana kuwa; Mwezi wa Ramadhwaan unapoanza, Malaika huwashika na kuwazuia Mashaytwaan wasiwabugudhi Waumini. Au tafsiri nyingine kwa kuwa mwezi wa Ramadhwaan ndani yake kuna thawabu nyingi na kusamehewa madhambi ya mja, Mashaytwaan wanashindwa kuwa na ushawishi kwa wanaadamu kama vile wamefungwa minyororo.” 

 

Na hili la kufungwa minyororo ni makhsusi zaidi kwa Hadiyth iliyopokelewa na Yuwnus kutoka kwa Ibn Shihaab katika Swahiyh Muslim: 

 

Milango ya Rahma huwa wazi hivyo Mashaytwaan wanakuwa na uwezo mdogo katika ushawishi wao kwa Waumini katika matamanio." [Fat-hul Baariy, mj. 4, uk. 114]

 

 

Shaykh Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) aliulizwa:  

  

Swali: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: ((…Na Mashaytwaan hufungwa minyororo)) lakini tunaona watu wanakamatwa na Mashaytwaan yanawaangusha vifafa mwezi wa Ramadhwaan, je, inakuwaje Mashaytwaan kufungwa minyororo hali bado watu wanasibiwa na Mashaytwaan?” 

 

Akajibu: "Katika baadhi ya riwaayah ya simulizi hii kuna inayosema: ((Mashaytwaan wakubwa hufungwa)). [Simulizi kutoka kwa Imaam An-Nasaaiy]. Lakini Hadiyth hii inaongelea mambo ya ghayb (yaliyo katika elimu ya Allaah) lazima tukubali na kutokwenda mbali kujadili mas-alah haya kwani 'Abdullaah mwanawe Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) alimuuliza baba yake kuwa: “Kwanini watu wanashikwa na Mashaytwaan mchana wa Ramadhwaan?” Imaam Ahmad akamjibu: "Hadiyth ndio inavyosema haina haja ya kuijadili". 

 

Vile vile inavyoonekana katika tafsiri sahihi ya Hadiyth hii - kufungwa minyororo ni kuzuiwa kuwatia katika mitihani watu kwa ushahidi ulio wazi kwa kutazama watu wanavyobadilika mwezi wa Ramadhwaan na kurejea kwa Allaah". [Majmuw’ Al-Fataawa Ibn ‘Uthaymiyn] 

  

Imaam Qurtwubiy (Rahimahu Allaah) alisema: 

 

"Ikiwa imesemwa kuwa bado kuna uovu mwingi na madhambi kufanyika mwezi wa Ramadhwaan na Mashaytwaan huwa wamefungwa minyororo". Basi jibu ni kuwa: Matendo maovu hupungua sana kwa kufuata hukmu za Swawm na baadhi ya Mashaytwaan hufungwa hasa yale makubwa (yenye nguvu) na si wote kama baadhi ya riwaayah zinavyoonyesha. Na kuhusu kupungua kwa maovu ni jambo liko wazi mwezi wa Ramadhwaan kulinganisha na miezi mingineyo". [Fat-hul-Baariy katika Kitabu: Fataawa Asw-Swiyaam, uk. 466]

 

 

Shaykh Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) alisema: "Kutokea maovu mwezi wa Ramadhwaan haichanganyi Hadiyth inayosema Mashaytwaan hufungwa minyororo. Imesemwa katika riwaayah ya Hadiyth kuwa ((Mashaytwaan wakubwa hufungwa)) [Musnad Ahmad 7857] 

 

Japokuwa Shaykh Al-Albaaniy (Rahimahu Allaah) ameitaja kama dhwa’iyfu jiddan [Dhwa’iyf At-Targhiyb). 

 

Mashaytwaan mwezi huu yana athari ndogo katika upotovu wao kwa watu kulinganisha na miezi mingine" [Fataawa Asw-Swiyaam].

 

 

 

 

Share