Ndoa Baada Ya Kutubu Zinaa

 

SWALI:

 

Jee kama kuna boyfriend na girlfriend wamekuwa wakipendana na wao ni waislam, ikafika

wakati wakajikuta na kuelewa kuwa wanavyofanya ni dhambi kubwa na wakaamua kutubia

kwa Mola wao, lakini kwa kuwa hawana uhasama na wamekuwa wakipendana wameamua

kuoana kwa ajili ya Allah, tokea kutubia kwao sasa inakaribia ni miaka miwili hawajakutana

kimwili na wamekuwa wakifahamishana sana mawaidha mema na kumuomba Mola wao

awasamehe madhambi yao na awaweke pamoja katika ndoa. Kama wanaamua kuoana

jee ndoa yao itasihi?

 

 


JIBU:

Sifa zote njema anastahiki Allah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wasallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum)  na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Bila shaka kitendo cha Zinaa ni katika dhambi mojawapo kubwa kabisa, lakini kwa Rahma  ya Allaah سبحانه وتعالى  ambayo inaenea kwa kila kitu, Humghufuria yule anayerejea Kwake, na kama unavyosema kuwa mlifanya uasi huo kisha mkaamua kutubu na kurudi kwa  Mola wenu basi  Allaah سبحانه وتعالى   Ametubashiria kuwa Yeye hupokea Tawbah ya waja wake  kama Anavyosema;

}}إِنَّمَا التَّوْبَةُ عَلَى اللّهِ لِلَّذِينَ يَعْمَلُونَ السُّوَءَ بِجَهَالَةٍ ثُمَّ يَتُوبُونَ مِن قَرِيبٍ فَأُوْلَئِكَ يَتُوبُ اللّهُ عَلَيْهِمْ وَكَانَ اللّهُ عَلِيماً حَكِيماً{{

{{Hakika toba inayo kubaliwa na Mwenyezi Mungu ni ya wale wafanyao uovu kwa ujinga, kisha wakatubia kwa haraka. Hao ndio Mwenyezi Mungu huwakubalia toba yao, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na ni Mwenye hikima}}

An-Nisaa: 17

Kwa hivyo Tawbah  yenu iwe  Tawbatan-Nasuuha (Tawbah ya kweli) ambayo  ina shuruti zake nazo ni:

1.     Kuomba Tawbah  

2.     Kuacha hicho kitendo kiovu

3.     Kujuta

4.     Kuazimia (Kuweka nia) kutorudia tena

 

Na Allaah سبحانه وتعالى   Ametukataza tusikate tamaa na Rahma Yake kwani  Humghufuria  mja wake madhambi yote kama alivyosema katika Surat Az-Zumar:

}}قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَى أَنفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِن رَّحْمَةِ اللَّهِ إِنَّ اللَّهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ{{

{{Sema: Enyi waja wangu walio jidhulumu nafsi zao! Msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote. Hakika Yeye ni  Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu}} Az-Zumar: 53

 

Vile vile Ametuambia katika aya nyingi kabisa katika Qur-aan, na pia tunaona katika  Hadithi mbalimbali kuwa Yeye yuko tayari kupokea Tawbah zetu kwani Yeye ni  Mwingi wa Kusamehe na Mwingi wa Rahma.   

}}أَلَمْ يَعْلَمُواْ أَنَّ اللّهَ هُوَ يَقْبَلُ التَّوْبَةَ عَنْ عِبَادِهِ وَيَأْخُذُ الصَّدَقَاتِ وَأَنَّ اللّهَ هُوَ التَّوَّابُ الرَّحِيمُ{{

{{Je! Hawajui ya kwamba Mwenyezi Mungu anapokea toba ya waja wake, na anazikubali sadaka, na kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kupokea toba na Mwenye   kurehemu }} 

At-Tawbah: 104

 

Tafadhali pitia 'Nasiha Za Ijumaa' zilizomo katika tovuti hii zinazozungumzia kuhusu Tawbah upate faida mbalimbali katika maudhui hii na pia ujue Rahma tuliyojaaliwa sisi Waislamu.

Ama maendeleo ya mahusiano yenu hayatokuwa ni sawa baada kuwa mlishazini kabla, kwani kuzidi kuwasiliana huenda kukakupelekeeni karibu kabisa na maovu. Allaah سبحانه وتعالى   Anasema:

}}وَلاَ تَقْرَبُواْ الزِّنَى إِنَّهُ كَانَ فَاحِشَةً وَسَاء سَبِيلاً{{

{{Wala msikaribie uzinzi. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya}} Israa: 32.

 

Na Uislamu umefanya ndoa kuwa ni nyepesi na ikafunga milango yote ya kuiendea zina.  Kwa hiyo inakupaseni mfanye haraka kufunga ndoa kwa kufuata shuruti zake, ili mjiepushe na hatari ya kuanguka tena katika hicho kitendo kiovu.

 

Wa Allaahu A'alam

 

Share