Kuswali Kwenye Makaburi Na Masharti Ya Kuomba Shafaa’ah

 

Kuswali Kwenye Makaburi Na Masharti Ya Kuomba Shafaa’ah

 

Imetafsiriwa Na: Naaswir Haamid

 

Afisi Ya Kutoa Da’wah Ya Kiislamu Mjini Rabwah, Riyaadh

 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Shukrani zote ni za Allaah.

 

 

 

1 - Suala La Kuswali Katika Makaburi

 

Kuswali katika makaburi ipo katika namna mbili:

 

Aina ya kwanza ni kuswali kwa kumkusudia aliyezikwa ndani ya kaburi. Hii ni shirki kubwa ambayo inamsababishia mtu kwenda nje ya msingi wa Uislamu, kwa sababu kuomba ni tendo la ibada, na hairuhusiwi kufanya tendo la ibada yoyote kwa yeyote isipokuwa tu kwa Allaah. Allaah Anasema (tafsiri ya maneno):

 

 

وَاعْبُدُوا اللَّـهَ وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا ۖ

Na mwabuduni Allaah na wala msimshirikishe na chochote. [An-Nisaa: 36]

 

 

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ۚ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا بَعِيدًا ﴿١١٦﴾

Hakika Allaah Haghufurii kushirikishwa; lakini Anaghufuria yasiyokuwa hayo kwa Amtakae. Na yeyote atakayemshirikisha Allaah basi kwa yakini amepotoka upotofu wa mbali. [An-Nisaa: 116]

 

 

Aina ya pili ni kuswali kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika kaburi. Hii inajumuisha idadi ya mambo kadhaa:

 

 

 

i - Kuswali Swalah (Janaazah) Katika Sehemu Ya Kaburi, Ambayo Inaruhusiwa

 

Mfano: iwapo mtu anafariki na wewe hujapata nafasi ya kumswalia ndani ya Msikiti, basi inaruhusika kwako wewe kumswalia baada ya kuzikwa.

 

Ushahidi wa hili ni kwamba hili ndilo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alilolifanya. Imesimuliwa kutoka kwa Abu Hurayrah kwamba mwanaume mweusi au mwanamke mweusi alikuwa akisafisha Msikiti, na yeye akafariki. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliuliza kuhusiana naye na kuambiwa: “Amefariki.” Akasema: “Kwa nini hamkuniambia? Nionesheni kaburi lake.” Hivyo akaenda kaburini na kumswalia Swalah ya Janaazah. [Imesimuliwa na Al-Bukhaariy]

 

 

 

ii - Kuswali Swalah Ya Janaazah Katika Kaburi, Ambayo Inaruhusiwa

 

Mfano: mtu anafariki na wewe hujapata nafasi ya kumswalia ndani ya Msikiti, basi inaruhusika kwako wewe kumswalia kaburini baada ya kuzikwa.

 

 

Shaykh ‘Abdul-‘Aziyz bin Baaz (Allaah Amrehemu) amesema: “Inaruhusika kuswali Swalah ya Janaazah kwa maiti ndani ya kaburi kama ilivyokuwa ni ruhusa kuswali Swalah ya Janaazah baada ya kufariki, kwa sababu imethibitika kwamba mwanamke mmoja alikuwa akisafisha Msikiti na akafariki. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akauliza kuhusiana naye na wakasema: “Amefariki.” Akasema: “Kwanini hamkuniambia? Nionesheni kaburi lake.”  Hivyo wakamuonesha na akamswalia, kisha akasema: “Makaburi haya yamefunikwa na giza kwa waliozikwa, lakini Allaah Amewahasahilishia kutokana na maombi yangu juu yao.” [Imesimuliwa na Muslim]

 

 

 

iii - Kuswali Katika Sehemu Za Kaburi – Mbali Ya Swalah Ya Janaazah – Hii Hairuhusiki Na Wala Haina Nguvu, Iwapo Ni Swalah Ya Faradhi Au Naafilah

 

Ushahidi wa hayo ni kama ifuatavyo:

 

 

(a)- Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Ardhi yote ni Msikiti isipokuwa sehemu za makaburi na vyooni.”  [Imesimulimwa na At-Tirmidhiy, Ibn Maajah na kusahihishwa na Al-Albaaniy ndani ya Swahiyh Ibn Maajah].

 

 

(b) - Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Allaah Awalaani Mayahudi na Manasara, kwani wamefanya makaburi ya Manabii wao kuwa ni sehemu za ibada.” [Imesimuliwa na Al-Bukhaariy na Muslim].

 

 

(c) - Kuswali katika makaburi inaweza kuwa na maana ya kuabudia makaburi, au kuiga wale wenye kuabudia makaburi. Hivyo, kwa sababu makafiri walikuwa wakisujudia jua pindipo linapopanda na kuzama, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuzuia kuswali pale jua linapopanda au kuzama, kwa uchache yawezekana kumaanisha kwamba kunapelekea kuabudia jua badala ya Allaah, au kujinasibisha na makafiri.

 

 

iv - Kuswalia Mbele Ya Kaburi, Ambayo Ni Haramu, Kwa Mujibu Wa Kauli Sahihi

 

 

Mfano: unaswali, na eneo la kaburi au kaburi katika muelekeo wa Qiblah chako, lakini huswali katika eneo la kaburi, isipokuwa unaswali katika eneo jengine ambalo lipo karibu na eneo la kaburi, bila ya ukuta au kizuizi baina yako na kaburi.

 

Ushahidi wa hili kuwa ni haramu:

 

- Imesimuliwa kwamba Abu Marthad Al-Ghanawi amesema: Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Usikae katika makaburi, au kuswali kuyaelekea makaburi.” [Imesimuliwa na Muslim]. Hii inamaanisha kwamba ni haramu kuswali kuyaelekea maeneo ya makaburi au mbele ya makaburi au mbele ya kaburi moja.

 

- Sababu ya kuwa kwa nini hairuhusiwi kuswali kuyaelekea maeneo ya makaburi ni sababu ile ile [inayojibu] ni kwa nini hairuhusiwi kuswali kuyaelekea makaburi. Itakavyokuwa kwamba mtu anaelekea mbele ya kaburi au eneo la kaburi katika namna ambayo inaweza kusemwa kwamba anaswali kuyaelekea makaburi, basi hili linakuja chini ya kizuizi, na iwapo inaangukia chini ya makatazo basi hairuhusiki, kwa sababu Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Msiswali…”Kizuizi kwa hapa ni katika kuswali, hivyo iwapo mtu ataswali kuelekea kaburi, basi anaunganisha utiifu na uasi, na wala hairuhusiwi kujiweka karibu na Allaah katika namna hiyo.

 

 

 

- Angalizo: Iwapo kuna ukuta baina yako na eneo la kaburi, basi kanuni kuu [inaeleza] ni kwamba inaruhusika kuswali katika namna hii na wala haikatazwi. Vivyo hivyo, iwapo kuna mtaa au mwendo mkubwa ambao unamaanisha kwamba huwezi kunasibishwa kuswali kuyaelekea makaburi, basi hili linaruhusiwa. Na Allaah Anajua zaidi.

 

Angalia Al-Mughniy 1/403; Ash-Sharh Al-Mumti’ cha Ibn ‘Uthaymiyn, 2/232.

 

 

 

2 – Kuomba Shafaa’ah[1]

 

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ataomba Shafaa’ah siku ya Hukumu na wengine pia miongoni mwa Waumini.

 

 

Lakini hapa tutaongeza jambo ambalo halikutajwa hapo nyuma, ambalo ni kwamba kuna masharti yaliyounganishwa katika kuomba Shafaa’ah:

 

 

- Ruhusa ni lazima itolewe kutoka kwa Allaah kwa mwenye kuomba, kuweza kuomba Shafaa’ah.

 

 

 

- Allaah ni lazima Akubali kwa yule ambaye anaombewa hiyo Shafaa’ah.

 

 

Ushahidi kwa masharti haya mawili ni aayah ambazo Allaah Anasema (tafsiri ya maneno):

 

وَكَم مِّن مَّلَكٍ فِي السَّمَاوَاتِ لَا تُغْنِي شَفَاعَتُهُمْ شَيْئًا إِلَّا مِن بَعْدِ أَن يَأْذَنَ اللَّـهُ لِمَن يَشَاءُ وَيَرْضَىٰ ﴿٢٦﴾

Na Malaika wangapi mbinguni haitowafaa kitu chochote uombezi wao isipokuwa baada ya kuwa Allaah Ametolea idhini kwa Amtakaye na Akaridhia. [An-Najm: 26]

 

 

وَلَا يَشْفَعُونَ إِلَّا لِمَنِ ارْتَضَىٰ وَهُم مِّنْ خَشْيَتِهِ مُشْفِقُونَ ﴿٢٨﴾

na wala hawataomba shafaa’ah (yeyote) isipokuwa kwa yule ambaye (Allaah) Amemridhia, nao kutokana na kumkhofu, ni wenye khofu na kutahadhari. [Al-Anbiyaa: 28]

 

Ama kwa fikra na mawazo potofu ya Shafaa’ah ambayo wanaoabudu masanamu wanafikiria kuwa miungu yao watawafanyia, hii ni Shafaa’ah isiyokubalika. kwani Allaah Haruhusu Shafaa’ah isipokuwa pale Atakaporidhia kwa wote: mwenye kuomba Shafaa’ah na yule mwenye kuombewa Shafaa’ah.

 

Angalia Al-Qawl Al-Mufiyd Sharh Kitaab At-Tawhiyd cha Shaykh Muhammad bin ‘Uthaymiyn (Allaah Amrehemu), uk. 336-337.

 

Ukweli kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Waumini wataombea Shafaa’ah haithibitishi kuwaomba wao kuomba Shafaa’ah, kama baadhi ya watu wanavyofanya pale wanapomuomba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwaombea Shafaa’ah hata baada ya kifo chake.

 

 

 

[1] Shafaa’ah kwa mnasaba wa makala hii ina maana ya Muumini kuweza kumuombea Muumini mwenziwe mbele ya Allaah kwa ajili ya kumsamehe na badala yake kumshushia Rahma Zake Allaah. [Mfasiri]

 

Share