Swawm Ya ‘Ashuraa Baina Ya Wenye Kupinga Na Wenye Kuunga Mkono

 

Swawm Ya ‘Ashuraa Baina Ya Wenye Kupinga Na Wenye Kuunga Mkono

 

Muhammad Faraj Saalim As-Sa'ay (Rahimahu Allaah)

 

Alhidaaya.com

 

Tukio la ‘Ashuraa ni tukio muhimu sana kwa walimwengu wote kutoka wakati wa Nabiy wa Allaah Muwsaa (‘Alayhis-salaam) hadi wakati wa Nabiy wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Ndani ya siku hii aliuliwa kwa dhulma Al-Hussayn (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) kipenzi cha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na bwana wa vijana wa peponi. Aliyekuwa mfano mwema wa kuigwa na Ummah wote kutokana na hikmah yake na wema wake aliourithi kutoka kwa babu yake Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na sisi tunajitenga mbali kabisa na kila aliyeshiriki katika mauaji hayo mpaka siku ya Qiyaamah.

 

Masuala sasa yanakuja:

  • Ni kweli funga ya ‘Ashuraa imeanzishwa na Bani Umayyah kwa kufurahikia kifo cha Al-Hussayn (Radhwiya Allaahu ‘Anhu)?
  • Au ilikuwa sheria katika diyn tokea kabla hata ya kufaridhishwa funga ya mwezi wa Ramadhwaan?
  • Au ilianzishwa tokea wakati wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na inaruhusiwa kuifunga mpaka siku ya Qiyaamah?
  • Na Je! Anyepata hasara ni mwenye kuifunga siku hii au mwenye kuiacha?

 

Yafuatayo ni majibu ya masuala yaliyotangulia:

1 - Kutoka kwa Abul-Hassan (‘Alayhi swalaatu was-salaam) kuwa amesema: ‘Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameifunga siku ya ‘Ashuraa.’

 

[Tahdhiybul-Ahkaam 29/4, Al-Istibsaar 134/2, Al-Wafi 13/7, Wasailush-Shiy’ah 337/7, Jami’ah Ahaadiythush-Shiy’ah 475/9, Al-Hadaaiqun-Naadhirah 370-371/13, Funga ya ‘Ashuraa ukurasa 112].

 

2 - Kutoka kwa Abu Ja’afar (‘Alayhi swalaatu was-salaam) kuwa amesema: ‘Funga ya Ashura inafuta madhambi ya mwaka mzima.’

 

[Tahdhiybul-Ahkaam 300/4, Al-Istibsaar 134/2, Jami’ah Ahaadiythush-Shiy’ah 475/9, Al-Hadaaiqun-Naadhirah 371/13, Swiyaamul-‘Ashuraa ukurasa 112, Al-Wafi 13/7, Wasailush-Shiy’ah 337/7].

 

3 - Kutoka kwa As-Swaadiq (Rahimahu Allaahu) kuwa amesema: ‘Mwenye kufunga Muharram anajikinga na kila ovu.’

 

[Wasailush-Shiy’ah 347/7, Al-Hadaaiqun-Naadhirah 377/13, Jami’ah Ahaadiythush-Shiy’ah 474/9].

 

4 - Na Kutoka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa amesema: “Swalah bora baada ya zilizofaridhishwa ni ya usiku wa manane, na funga bora baada ya mwezi wa Ramadhwaan ni Funga ya mwezi wanaouita Muharram.” [Masdari zilizotangulia kutajwa]

 

Baada ya kuzisoma kauli hizi za maulamaa mbali mbali wenye kusifika wa Madhehebu ya Kishia walizoziandika ndani ya vitabu mbali mbali vinavyoheshimika, inatuwia wazi kuwa haijuzu kuikanusha swaumu hii ya ‘Ashuraa na kudai kuwa eti imeanzishwa na watawala wa kabila la Bani Umayyah.

 

Funga hii ni Sunnah yenye uhakika iliyothibiti ndani ya vitabu vya madhehebu mbali mbali ya Kiislamu, na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye ni mfano mwema wetu sisi wa kumfuata, ameifunga siku hii na akatutaka na sisi pia tuifunge.

 

Anaweza mtu kwa kuuendekeza moyo wake na kwa kufuata matamanio ya nafsi yake akasema kuwa: ‘Hizi ni hadithi za uongo zilizozushwa tu.’ n.k, lakini mwenye kuutafuta ukweli mara baada ya kuiona haki hatoweza kusema maneno haya, bali atasalimu amri na kuifuata Sunnah hii tukufu. Kwani moyo wa aliyeamini kikweli haukubali kufuata matamanio ya nafsi. Haukubali kufuata isipokuwa haki tu itokayo kwa Mola wake kupitia kwa Nabiy wake mtukufu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Ee ndugu yangu Muislamu! kumbuka kuwa hapana baada ya haki isipokuwa upotovu, na uikumbuke kauli ya Imaam ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) aliposema:

 

‘Ifungeni ‘Ashuraa siku ya tisa na ya kumi akiba ya maneno kwani inafuta madhambi ya mwaka uliotangulia.’ [Mustadrakul-Wasaail 1/594 na Jami’ah Ahaadiythush-Shia 475/9].

 

Na kutoka kwa Ibni ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) kuwa amesema: ‘Utakapouona mwezi wa Muharram anza kuhesabu, na itakapotimia ya tisa basi funga kuanzia asubuhi ya siku hiyo.’ Anasema mwenye kuisimulia Hadiyth hii kuwa aliuliza: ‘Mtume wa Allaah alifunga hivi pia?’

 

Akasema Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘Anhu): ‘Ndiyo.’ [Iqbaalul-A’amaal ukurasa 554, Wasailush-Shiy’ah 347/7, Mustadrakul-Wasaail 594/1].

 

Kumbuka pia ndugu yangu kuwa riwaya zote zilizokuja zenye kuitilia nguvu swaumu hii zimekuja kwa njia sahihi na zile zote zenye kuipinga swaumu hii zimekuja kwa njia dhaifu kama alivyokiri Ash-Shaykh Al-Hajj As-Sayyid Muhammad Ridha Al-Hussayn Al-Hairi katika kitabu chake kiitwacho Najatlul-Ummah Fiy Iqaamatil-‘Azaa Li Aal Husayn Wal-Aimmah ukurasa wa 145, 146 mpaka 148.

 

Je ndugu yangu baada ya ushahidi huu utatanguliza maneno ya watu wa kawaida au utatanguliza maneno ya mbora wa viumbe vyote (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)?

 

Tanbiyh:

 

Mauaji ya Al-Hussayn (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) ni mojawapo ya masaibu makubwa waliyokumbwa nayo Waislamu, na kubwa zaidi ni kuuliwa kwa baba yake Imaam ‘Aliy bin Abu Twaalib (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) na kubwa kupita yote ni kufariki kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Muislamu anapokumbwa na masaibu anatakiwa akumbuke masaibu haya matatu ili aweze kuona na kuhisi kuwa masaibu aliyokuwa ndani yake ni madogo sana akiyalinganisha na hayo.

 

Hata hivyo Allaah Ametufundisha katika Kitabu Chake kitukufu kuwa Muislamu anapokumbwa na masaibu aseme: ‘Innaa liLlaahi wa innaa ilayhi raaji’uun.’

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema: 

 

 الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ قَالُوا إِنَّا لِلَّـهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ﴿١٥٦﴾أُولَـٰئِكَ عَلَيْهِمْ صَلَوَاتٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَرَحْمَةٌ ۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُهْتَدُونَ ﴿١٥٧﴾

156. Wale ambao unapowafika msiba husema: Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea. 157. Hao zitakuwa juu yao Barakah kutoka kwa Rabb wao na rahmah, na hao ndio wenye kuongoka. [Al-Baqarah: 156-157]

 

Na kumbuka kuwa Al-Hussayn (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) ni shahiyd aliyeko peponi akineemeshwa na Rabb wake, na kwamba ishapita miaka elfu nyingi tokea alipouliwa kwa dhulma, na wajibu wa Muislamu ni kusubiri na kuomba na sio kutukana na kukufurisha.

 

Anasema At-Tijani ambaye ni mwandishi maarufu wa kitabu 'Then I was guided' (Thumma Ihtadaytu) kuwa: ‘Mengi kati ya wanayofanya watu hivi sasa katika kuomboleza kifo cha Al-Hussayn (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) hayakupata kufanywa na yeyote tokea alipokufa Rasuli wa Allaah hadi siku hii ya leo na wala hayakuwahi kufanywa na Al-Hassan wala Al-Hussayn (Radhwiya Allaahu ‘Anhu).’

 

Anasema kuwa mmoja katika aliyeshuhudia mauaji hayo yaliyofanyika Karbala amesema: ‘Nimehudhuria mkusanyiko usiopata kuhudhuriwa na mtu yeyote, na nikashuhudia kwa jicho langu yale ambayo hakupata kuyashuhudia mtu yeyote hapo Karbala alipouliwa baba yangu na ami zangu na ndugu zangu wote, na nikaona masaibu yanayoweza kuyaondoa majabali.’

 

Anasema At-Tijani: ‘Juu ya yote hayo aliyoyaona lakini hajapata kufanya haya yanayofanywa siku hizi wala kuamrisha watu wake kufanya hivyo.’ (Kitabu cha 'Kullu-l-huluul' ukurasa wa 151).

 

Anaongeza At-Tijani: ‘Hata ajitahidi vipi mwenye kujitahidi, lakini lazima aelewe kuwa hayo wanayotenda katika kupiga vifua na kuomboleza na kulaani na kutukana sio katika maamrisho ya diyn hata kama watatoa fatwa wenye kutowa, lazima waelewe kuwa hayo ni katika hisia zinazopindukia mipaka.’ (Kitabu cha 'Kullu-l-huluul' ukurasa wa 148).

 

Share