Kuoa Wanawake wa Kitabu (Wakrito Na Mayahudi)

 

SWALI:

 

Nini hukmu ya kumuoa mwanamke Myahudi au Mkristo? Je, Mayahudi na Wakristo wanatambulikana kuwa ni Ahlul-Kitaab (Watu waliopewa Kitabu) au ni Mushrikiyn (Washirikina)?

 


 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Kufunga ndoa na mwanamke Myahudi au Mkristo inaruhusiwa kutokana na rai ya 'Ulamaa wengi. 

 

Ibn Qudaamah (Allaah Amrehemu) alisema katika [Al-Mughniy 7/99]:  "Hakuna tofauti ya rai za 'Ulamaa kuhusu kuruhusiwa kuwaoa wanawake wa Kitabu. Na miongoni mwa walio na rai  hii ambayo ilisimuliwa kutoka  kwao ni 'Umar, 'Uthmaan, Twalhah, Hudhayfah, Salmaan, Jaabir na wengineo". 

 

 

Ibn Al-Mundhir kasema: "Hakuna usimulizi ulio sahihi kutoka kizazi cha mwanzo kusema kwamba hivyo ni haraam. Al-Khallaal amesimulia katika Isnaad yake kwamba Hudhayfah, Twalhah, Al-Jaaruud ibn Al-Mu'alla na Udhaynah Al-'Abdi wote walioa wanawake wa Ahlul-Kitaab. Hii pia ilikuwa ni rai ya 'Ulamaa wengine wote."

 

 

Ushahidi mkuu kuhusu mas-alah haya ni aya ambayo Allaah سبحانه وتعالى Anasema:

 

((الْيَوْمَ أُحِلَّ لَكُمُ الطَّيِّبَاتُ وَطَعَامُ الَّذِينَ أُوتُواْ الْكِتَابَ حِلٌّ لَّكُمْ وَطَعَامُكُمْ حِلُّ لَّهُمْ وَالْمُحْصَنَاتُ مِنَ الْمُؤْمِنَاتِ وَالْمُحْصَنَاتُ مِنَ الَّذِينَ أُوتُواْ الْكِتَابَ مِن قَبْلِكُمْ إِذَا آتَيْتُمُوهُنَّ أُجُورَهُنَّ مُحْصِنِينَ غَيْرَ مُسَافِحِينَ وَلاَ مُتَّخِذِي أَخْدَانٍ وَمَن يَكْفُرْ بِالإِيمَانِ فَقَدْ حَبِطَ عَمَلُهُ وَهُوَ فِي الآخِرَةِ مِنَ الْخَاسِرِينَ))

 

"Leo mmehalalishiwa vizuri. Na chakula cha wale waliopewa Kitabu ni halali kwenu, na chakula chenu ni halali kwao. Na wanawake walioimarisha sitara (wasiozini) miongoni mwa Waumini wanawake na wanawake walioimarisha sitara miongoni mwa wale waliopewa Kitabu kabla yenu; mtakapowapa mahari yao mkijistahi bila ya kuwa maasherati wala kuchukua hawara. Na yeyote atakayekanusha iymaan; basi kwa yakini imeporomoka ‘amali yake naye Aakhirah atakuwa miongoni mwa waliokhasirika."  [Al-Maaidah: 5]

 

 

Maana ya Muhswanaat (wanawake wema) ni wale ambao walio huru na walio katika stara. (Yaani katika heshima na aliye bikra, asiye mhuni) Ibn Kathiyr (Allaah Amrehemu) amesema katika Tafsiyr yake:

 

"Hii ni rai ya 'Ulamaa wengi wao na hii ndivyo inavyoelekea kuwa hali yenyewe.  Asije kuwa Dhimiyyah (mwanamke asiye Muislam aliye katika hifadhi ya Kiislam) lakini pia asiyekuwa katika stara (heshima, bikra). Ikiwa atakuwa katika hali hii atakuwa amepotoka na mwenye ufisadi, na mumewe atamalizikia kuwa kama inavyoeleza katika methali: "Amenunua tende mbaya na amekhiniwa katika uzito na mizani pia." 

 

 

Maana iliyo dhahiri katika Aayah ni vile ilivyomaanisha "Al-Muhswanah" (mwanamke mwenye stara, (aliyekuwa bikra, asiyekuwa mhuni) naye ni mwanamke aliyejiepusha na zinaa kama Allaah سبحانه وتعالى  anavyosema katika Aya nyingine:

 

((مُحْصَنَاتٍ غَيْرَ مُسَافِحَاتٍ وَلاَ مُتَّخِذَاتِ أَخْدَانٍ))

 

"Na mtachukuaje na hali nyinyi kwa nyinyi mmeingiliana, na wao wanawake wakapokea kwenu fungamano thabiti?" [An-Nisaa: 21]

 

 

Wakristo na Mayahudi ni Makafiri na washirikina, kutokana na Qur-aan, lakini wametolewa katika kuharamishwa kuolewa wanawake wao kwa sababu Allaah سبحانه وتعالى Anasema katika aya yenye maana:

 

((وَلاَ تَنكِحُواْ الْمُشْرِكَاتِ حَتَّى يُؤْمِنَّ وَلأَمَةٌ مُّؤْمِنَةٌ خَيْرٌ مِّن مُّشْرِكَةٍ وَلَوْ أَعْجَبَتْكُمْ وَلاَ تُنكِحُواْ الْمُشِرِكِينَ حَتَّى يُؤْمِنُواْ وَلَعَبْدٌ مُّؤْمِنٌ خَيْرٌ مِّن مُّشْرِكٍ وَلَوْ أَعْجَبَكُمْ أُوْلَئِكَ يَدْعُونَ إِلَى النَّارِ وَاللّهُ يَدْعُوَ إِلَى الْجَنَّةِ وَالْمَغْفِرَةِ بِإِذْنِهِ وَيُبَيِّنُ آيَاتِهِ لِلنَّاسِ لَعَلَّهُمْ يَتَذَكَّرُونَ))

 

"Na wala msiwaoe wanawake washirikina mpaka waamini. Na mjakazi Muumini ni bora kuliko mshirikina japo akikupendezeni. Na wala msiwaozeshe (wanawake wa Kiislamu) wanaume washirikina mpaka waamini. Na mtumwa Muumini ni bora kuliko mshirikina japo akikupendezeni. Hao wanaitia katika moto na Allaah Anaitia katika Al-Jannah na maghfirah kwa idhini Yake. Na Anabainisha Aayaat (na shariy’ah) Zake ili wapate kukumbuka." [Al-Baqarah: 221]

 

 

Hii ni njia ya dhahiri kabisa ya kuwafikiana baina ya Aayah mbili.

 

 

Allaah سبحانه وتعالى  Amewaelezea kuwa ni washirikina kama Anavyosema:

 

 

((اتَّخَذُواْ أَحْبَارَهُمْ وَرُهْبَانَهُمْ أَرْبَابًا مِّن دُونِ اللّهِ وَالْمَسِيحَ ابْنَ مَرْيَمَ وَمَا أُمِرُواْ إِلاَّ لِيَعْبُدُواْ إِلَهًا وَاحِدًا لاَّ إِلَهَ إِلاَّ هُوَ سُبْحَانَهُ عَمَّا يُشْرِكُونَ))

 

"Wamewafanya Wanavyuoni wao mafuqahaa wa dini na Wamonaki wao kuwa ni miola badala ya Allaah, na (pia) Al-Masiyh mwana wa Maryam na hali hawakuamrishwa isipokuwa kumwabudu Ilaah Mmoja Pekee. Hapana muabudiwa wa haki ila Yeye. Subhaanah! (Utakasifu ni Wake) kutokana na yale yote wanayomshirkisha nayo."   [At-Tawbah: 31] 

 

 

Kwa hiyo 'Watu wa Vitabu' ni makafiri na washirikina, lakini Allaah سبحانه وتعالى Ameturuhusu kula nyama zao na kuwaoa wanawake wao ikiwa watakuwa wenye stara (wenye heshima sio wahuni). Hii imeruhusiwa kutokana na maana ya aya iliyo katika Suwratul-Baqarah: 221 (tulioitaja hapo juu).

 

 

 

Lakini ifahamike kwamba ni bora na usalama kabisa kutokuoa wanawake wa Kitabu khaswa kwa siku hizi. 

 

 

Ibn Qudaamah (Allaah سبحانه وتعالى Amerehemu) alisema:  Kwa vile hali ni hii, ni bora kutokuoa mwanamke wa Kitabu kwa sababu 'Umar aliwaambia wale waliowaoa wanawake wa Kitabu "Waacheni (Wapeni talaka)" kwa hiyo wakawapa talaka isipokuwa Hudhayfah. 'Umar akamuambia: "Mpe talaka".  (Hudhayfah) akasema:  "Je, Unashuhudia kuwa yeye ni haraam?"  Akasema:  "Yeye ni mkaa wa moto wenye kuwaka mpe talaka".  Akasema:  "Je, Unashuhudia kuwa yeye ni haraam?"  Akasema:  "Yeye ni mkaa wa moto wenye kuwaka". Akasema: "Najua kuwa yeye ni mkaa wa moto wenye kuwaka lakini yeye ni halali kwangu". Baada ya muda akampa talaka na akaulizwa "Kwa nini hukumpa talaka alipokuamrisha 'Umar?" Akasema:  "Sikutaka watu wafikiri kuwa nimefanya kosa (kwa kumuoa)". 

 

Labda alikuwa akimpenda au labda kwa sababu walipata mtoto pamoja kwa hiyo alimpenda". [Al-Mughniy 7/99]

 

 

Vile vile Hadiyth hii ifuatayo  Sahiyh inasema:

 

Ibn 'Umar alipokuwa akiulizwa kuhusu kumuoa mwanamke Mkristo au Myahudi, alikuwa akisema: "Allaah Ameifanya kuwa ni Haraam kwa Muumini kuoa wanawake wanaomshrikisha Allaah katika 'ibaadah, na sijui lililo kubwa zaidi kuliko kumshirikisha Allaah katika ibada na kadhalika kama mwanamke kusema 'Iysaa ('Alayhis Salaam) ni muabudiwa ilhali yeye ('Iysaa  'Alayhis Salaam) ni mja tu wa Allaah."  [Al-Bukhaariy]

 

 

 

Imaam Ibn Baaz (Allaah Amrehemu) alisema:  "Ikiwa mwanamke wa Kitabu anajulikana kuwa ni mwenye stara (si muhuni) na kujiepusha na njia ambazo zinampeleka mtu katika uasharati, inaruhusiwa kwa sababu Allaah سبحانه وتعالى Ameruhusu hivyo na Ameturuhusu kuwaoa wanawake wao na kula nyama zao.

 

 

Lakini siku hizi kuna khofu kwamba wale wanaooa huenda wakakutana na uovu zaidi. Wanaweza (hao wanawake) kuwaita (kuwashawishi wakaingia) katika dini yao na wanaweza kuwalea watoto wao katika Ukristo. Kwa hiyo khatari  ipo hakika na ni kubwa. Ili (Muuin) kuwa katika amani, Muumini ni bora asiwaoe. Na katika hali nyingi hakuna uhakika kama mwanamke hatofanya vitendo vya uasharati au hatowaleta watoto waliotoka katika uhusiano wa mwanzo. Lakini mwanamme akitaka kufanya hivyo basi hana dhambi kwake ili ajiweke katika stara na ainamishe macho yake kwa kumuoa. Ajitahidi kumuita (kumlingania aingie) katika Uislamu na (kwa wakati huo huo) awe na hadhari na uovu wake na hadhari ya kumruhusu asimvute yeye au watoto wake katika ukafiri". [Fataawa Islaamiyyah, 3/172]

 

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share