Maulidi: Ufafanuzi Wa Maneno Katika Kitabu Cha Ibn Taymiyyah Kuhusu Bid'ah Ya Maulidi

 

Ufafanuzi Wa Maneno Katika Kitabu Cha Ibn Taymiyyah Kuhusu Bid'ah Ya Maulidi

 

Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI LA 1:

 

Bismillaahi rahmaani rahiim Asslaamu alaikum warahmatu llahi wabarakatu. Shukurani na sifa njema zote ni za Allah subhaanahu wataala na namtakia bwana wetu Mjumbe wa Allah Muhammad rehma na amani za Allah ziwe juu yake.

 

Ndugu zangu waislamu wa alhidaaya kwa hisani yenu nifafanulieni nami maneno ya fuatao ya sheikhu-l-islam Allah amrehemu ibnu taimiya. Kwa hakika maneno haya natutatanisha kulingana na yanavyo tafsiriwa na ahlusuna na ahlubidaa. Maneno haya yako katika kitabu kiitwacho iqtidhwaau swiratulmistaqiima, mjalada wapili, kilicho chapishwa na daarul-aaswima mwaka wa 1998m/1419h - Ahlusunnah Wanasema ibnu Taymia radhi za Allah ziwe juu yake amesema katika ukurasa wa 123 wa kitabu hicho kuwa kusoma maulidi na kuyafanya kila mwaka wakati fulani hayafai kwa sababu wanazuoni walopita awakuyafanya.

 

Ahlul-bidaa Wanasema ibnu Taymia radhi za Allah ziwe juu yake amesema katika ukurasa wa 126 wakitabu hich kuwa kusoma mawlid na kuyafanya wakati fulani kila mwaka basi mwenyekufanya hivyo atapata thawabu nyingi sana Ninaomba munifafanulie hizi tafsiri mbili. ipi iko sawa na ipi iko makosa.

 

Munielezee usawa wake na makosa yake. Na pia ikiwa kuna masuala ya nahwu muniwekee wazi kwamfano ikiwa kuna maneno yalio tangulia au yalio akhirishwa Kwa hisani yenu ikiwa mutaweza kuni jibu kwahara itakuwa uzuri zaidi. Kwa sababu tuna hitajia maneno haya kwenye mjadala utarajiwao kufanyika mwezi ujao. Asanteni sana. Allah atawajazi kheri

 

SWALI LA 2

 

Assalaam alaikum warahamatu llahi wa barakatu. ndu zangu niliwatumia suali kuhusu sheikhu-l-islam ibnu Taimiya kuwa kwenye kitabu chake cha iqtwidhwaau swiratu-l- mustaqiim, mjalada wapili, kilicho chapishwa na daarul-aaswima mwaka wa 1998m/1419h. Katika ukurasa wa 123 amesema mawlid hayafai kusherehekewa na kwenye ukurasa wa 126 hufaa kusherehekewa. Ni vipi masaala haya.

shukran

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Katika kitabu hicho ulichokitaja ‘Iqtidhwaa’ asw-Swiraatw al-Mustaqiym’ kilichochapishwa na al-Maktabuth Thaqaafiy as-Su‘udiyy, Morocco cha 1419 H, uk. 294–296 ambacho kimehakikiwa na mwanachuoni mkubwa Shaykh Muhammad Haamid al-Fiqqiy.

 

Ibn Taymiyyah amepatia kichwa cha habari, “Bid’ah za Sherehe za Mazazi ya Nabiy”. Amesema ndani: “Na hivyo hivyo yaliyozuliwa na baadhi ya watu ima kwa kuwafuata Manaswara kusherehekea mazazi ya ‘Iysaa (‘Alayhis Salaam) au kwa ajili ya kumpenda Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumuadhimisha. Huenda Allaah (‘Azza wa Jalla)  Akawapatia thawabu kwa mahaba haya na ijtihadi hii (1) sio kwa bid’ah. Pamoja na kuchukua mazazi ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa ni sherehe, pamoja na kutofautiana watu na mazazi yake. Kwa kuwa hili halikufanywa na watangu wema pamoja na kusimamia haja hiyo na kutokataza. Na lau kufanya hivyo ingekuwa ni kheri au yenye nguvu zaidi Watangu wema (Radhwiya Allaahu ‘anhum) wangetutangulia kwayo kwani wao walikuwa na mahaba makubwa na kumtukuza zaidi Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuliko sisi. Na wao katika kufanya kheri walikuwa msitari wa mbele. Na hakika ni kuwa mahaba kwake na kumtukuza ni kumfuata, kumtii, kufuata amri zake na kuhuisha Sunnah zake za wazi na za siri. Pia kueneza kwa aliyotumwa nayo na kutia juhudi katika hayo kwa moyo, mkono na ulimi. Hakika hii ndiyo iliyokuwa njia ya wale wa mwanzo miongoni mwa Muhaajiriyna na Answaariy na wale waliowafuata kwa wema na ihsani. Na utawakuta wengi wa hawa wenye kutilia mkazo bid’ah kama hizi pamoja na yale waliyo nayo, kama malengo mazuri na ile ijtihadi inayotazamiwa kuwapatia wao thawabu, utawakuta ni wavivu sana katika kutekeleza amri ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa nashati inayotakiwa. Hakika huyu yuko katika daraja sawa na mwenye Mswahafu asiyeusoma au akasoma pasi na kufuata. Na yuko daraja sawa na mwenye kupamba Msikiti pasi na yeye kuswali ndani yake au kuswali kwa uchache. Na katika daraja ya yule anayechukua tasbihi na miswala iliyopambwa. Na mifano ya hayo mapambo ya dhahiri ambayo hayapo katika Shariy’ah, yanayompeleka kwenye riyaa na kiburi na yenye kumshughulisha na sheria yenye kuharibu hali ya mwenye kuyafanya (2). Hii imekuja katika Hadiyth: “Haitoharibika ‘amali ya Ummah kabisa isipokuwa wanapamba Misikiti”.

 

Haya ndio maneno ya Ibn Taymiyyah katika kitabu chake hicho.

Shaykh Muhammad Haamid ameandika yafuatayo chini yake:  

 

(1) Vipi watapata thawabu kwa hilo? Na wao wamekwenda kinyume na uongofu wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na uongofu wa Maswahaba zake? Panaposemwa: Kwa kuwa wao wamefanya juhudi, wakakosea; sisi twasema: Ni ijtihaad gani katika hili. Je, nuswuus (maandiko) zimeacha nafasi kwa ijtihaad katika mas-ala ya Ibaadah? Na jambo hilo lipo wazi kabisa. Na hilo ni kushindwa na ujahili na kuhukumu kwa matamanio, yaliyowachukua watu kukengeuka na uongofu wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kufuata Uyahudi, Unaswara na Upagani. Wanastahiki juu yao laana ya Allaah na ghadhabu Yake. Na je, mahaba na kumuadhimisha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yanapatikana kwa kukengeuka na uongofu wake na kumchukia na kuchukia aliyokuja nayo ya kweli katika kuwatengeneza watu kutoka kwa Rabb wake na kuwaendea na kushidana na Upagani, Uyahudi na Unaswara? Na ni wapi hao waliohuisha sherehe hizo za Kipagani? Je, hao ni Maalik au Ash-Shaafi‘iy au Ahmad au Abuy Haniyfah au Sufyaan wawili au wengineo miongoni mwa Imaam waongofu (Radhwiya Allaahu ‘anhum)? Mpaka awaombe msamaha na makosa yao.

 

Sivyo hivyo! Bali yaliyozuliwa katika sherehe hizi za shirki ni kutoka kwa ‘Ubayd (‘Ubaydullaah) ambao Ummah umejumuika juu ya uzindiki wao na kuwa wao ni makafiri zaidi hata kuliko Mayahudi na Manaswara na kwamba wao walikuwa maafa kwa Waislamu. Na kwa mikono yao pamoja na vitimbi vyao na waliyopiliza kwa Ummah katika sumu za Kisufi ziliwapoteza Waislamu na njia nyoofu. Mpaka wakawa pamoja na walioghadhibikiwa na waliopotea.

 

Na maneno ya Ibn Taymiyyah mwenyewe ni dalili juu ya kinyume kwa alichosema kupata thawabu kwao. Kwa kuwa kumpenda na kumtukuza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni wajibu wa kila Muislamu: Hakika hiyo ni kufuata kwa aliyokuja nayo kutoka kwa Allaah (Ta’alaa). Hii ni kama Alivyosema Allaah (Subhaanahau wa Ta’aalaa):

 

 قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللّهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللّهُ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ وَاللّهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ

Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Mkiwa mnampenda Allaah, basi nifuateni mimi, Atakupendeni Allaah na Atakughufurieni dhambi zenu. Na Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. [Al-'Imraan: 31] 

  

Na Anasema tena Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ يَزْعُمُونَ أَنَّهُمْ آمَنُوا بِمَا أُنزِلَ إِلَيْكَ وَمَا أُنزِلَ مِن قَبْلِكَ يُرِيدُونَ أَن يَتَحَاكَمُوا إِلَى الطَّاغُوتِ وَقَدْ أُمِرُوا أَن يَكْفُرُوا بِهِ وَيُرِيدُ الشَّيْطَانُ أَن يُضِلَّهُمْ ضَلَالًا بَعِيدًا ﴿٦٠﴾

Je, huoni wale wanaodai kwamba wao wameamini yaliyoteremshwa kwako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) na yale yaliyoteremshwa kabla yako; wanataka wahukumiane kwa twaghuti (ubatilifu) na hali wameamrishwa wakanushe hiyo. Na shaytwaan anataka awapoteze upotofu wa mbali.

 

وَإِذَا قِيلَ لَهُمْ تَعَالَوْا إِلَىٰ مَا أَنزَلَ اللَّـهُ وَإِلَى الرَّسُولِ رَأَيْتَ الْمُنَافِقِينَ يَصُدُّونَ عَنكَ صُدُودًا ﴿٦١﴾

Na wanapoambiwa: Njooni kwenye yale Aliyoyateremsha Allaah na kwa Rasuli; utawaona wanafiki wanakugeukilia mbali kwa mkengeuko.

 

 

فَكَيْفَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ بِمَا قَدَّمَتْ أَيْدِيهِمْ ثُمَّ جَاءُوكَ يَحْلِفُونَ بِاللَّـهِ إِنْ أَرَدْنَا إِلَّا إِحْسَانًا وَتَوْفِيقًا ﴿٦٢﴾

Basi itakuwaje utakapowafika msiba kwa sababu ya yale iliyotanguliza mikono yao? Kisha wakakujia wakiapa Wa-Allaahi hatukutaka ila mazuri na mapatano. 

 

 

أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ يَعْلَمُ اللَّـهُ مَا فِي قُلُوبِهِمْ فَأَعْرِضْ عَنْهُمْ وَعِظْهُمْ وَقُل لَّهُمْ فِي أَنفُسِهِمْ قَوْلًا بَلِيغًا ﴿٦٣﴾ 

Hao ndio ambao Allaah Anayajua yaliyomo ndani ya nyoyo zao. Basi waachilie mbali na wape mawaidha na uwaambie maneno yatakayofikia kuathiri (nafsi zao). 

 

 

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن رَّسُولٍ إِلَّا لِيُطَاعَ بِإِذْنِ اللَّـهِ ۚ وَلَوْ أَنَّهُمْ إِذ ظَّلَمُوا أَنفُسَهُمْ جَاءُوكَ فَاسْتَغْفَرُوا اللَّـهَ وَاسْتَغْفَرَ لَهُمُ الرَّسُولُ لَوَجَدُوا اللَّـهَ تَوَّابًا رَّحِيمًا﴿٦٤﴾

Na Hatukutuma Rasuli yeyote ila atiiwe kwa idhini ya Allaah. Na lau wao pale walipojidhulumu nafsi zao wangelikujia (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) wakamwomba Allaah maghfirah na Rasuli akawaombea maghfirah, basi wangelimkuta Allaah ni Mwingi wa kupokea tawbah, Mwenye kurehemu. 

 

 

فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ حَتَّىٰ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لَا يَجِدُوا فِي أَنفُسِهِمْ حَرَجًا مِّمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُوا تَسْلِيمًا ﴿٦٥﴾

Basi Naapa kwa Rabb wako, hawatoamini mpaka wakufanye wewe ni mwamuzi katika yale wanayozozana baina yao, kisha wasipate katika nyoyo zao karaha katika yale uliyohukumu na wajisalimishe, kwa kujisalimisha kikamilifu. [An-Nisaa 4: 60-65]

 

 

Na pia Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

وَيَقُولُونَ آمَنَّا بِاللَّـهِ وَبِالرَّسُولِ وَأَطَعْنَا ثُمَّ يَتَوَلَّىٰ فَرِيقٌ مِّنْهُم مِّن بَعْدِ ذَٰلِكَ ۚ وَمَا أُولَـٰئِكَ بِالْمُؤْمِنِينَ ﴿٤٧﴾

Na (wanafiki) wanasema: Tumemwamini Allaah na Rasuli, na Tumetii. Kisha hugeuka kundi miongoni mwao baada ya hayo. Na wala hao si wenye kuamini.

 

 

وَإِذَا دُعُوا إِلَى اللَّـهِ وَرَسُولِهِ لِيَحْكُمَ بَيْنَهُمْ إِذَا فَرِيقٌ مِّنْهُم مُّعْرِضُونَ ﴿٤٨﴾

Na wanapoitwa kwa Allaah na Rasuli Wake ili Awahukumu baina yao, mara hapo kundi miongoni mwao wanakengeuka.

 

 

وَإِن يَكُن لَّهُمُ الْحَقُّ يَأْتُوا إِلَيْهِ مُذْعِنِينَ ﴿٤٩﴾

Na inapokuwa haki ni yao, wanamjia (Rasuli) wakitii.

 

 

أَفِي قُلُوبِهِم مَّرَضٌ أَمِ ارْتَابُوا أَمْ يَخَافُونَ أَن يَحِيفَ اللَّـهُ عَلَيْهِمْ وَرَسُولُهُ ۚ بَلْ أُولَـٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ ﴿٥٠﴾

Je, mna maradhi katika nyoyo zao, au wametia shaka, au wanakhofu kwamba Allaah na Rasuli Wake watawadhulumu katika kuwahukumu? Bali hao ndio madhalimu.

 

 

إِنَّمَا كَانَ قَوْلَ الْمُؤْمِنِينَ إِذَا دُعُوا إِلَى اللَّـهِ وَرَسُولِهِ لِيَحْكُمَ بَيْنَهُمْ أَن يَقُولُوا سَمِعْنَا وَأَطَعْنَا ۚ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ ﴿٥١﴾

Hakika kauli ya Waumini wa kweli wanapoitwa kwa Allaah na Rasuli Wake ili Awahakumu baina yao; husema: Tumesikia na Tumetii. Na hao ndio wenye kufaulu.

 

 

وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَيَخْشَ اللَّـهَ وَيَتَّقْهِ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْفَائِزُونَ ﴿٥٢﴾

Na yeyote yule atakayemtii Allaah na Rasuli Wake, na akamkhofu Allaah na akamcha; basi hao ndio wenye kufuzu.   [An-Nuwr 24: 47-52].

 

(2) Na vipi baada ya yote haya anatarajiwa kuwa atapata thawabu au kukubaliwa kwa mwito wa lengo jema? Na je, ‘amali za dhahiri ndio anuwani ya malengo na Niyyah? Na ikiwa hawa watapata thawabu kwa bid’ah zao, basi itakuwa kwa Mayahudi na Manaswara na kila kafiri thawabu kwa wanaokuja nayo katika ukafiri na upagani kwa kuwa wao pia wanafanya juhudi kwa Imani yao na hawakusudii kwayo ila wema na tawfiyq.

 

Yaliyotangulia juu ndio maneno ya Ibn Taymiyyah na maelezo na maelekezo yaliyofuatia ni uchambuzi wa Shaykh Muhammad Haamid.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share