020 - Twaahaa
طه
020-Twaaha
020-Twaahaa: Utangulizi Wa Suwrah
بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيم
طه ﴿١﴾
1. Twaaha.[1]
مَا أَنزَلْنَا عَلَيْكَ الْقُرْآنَ لِتَشْقَىٰ ﴿٢﴾
2. Hatujakuteremshia Qur-aan ili upate mashaka.
إِلَّا تَذْكِرَةً لِّمَن يَخْشَىٰ ﴿٣﴾
3. Isipokuwa ni ukumbusho kwa anayekhofu.
تَنزِيلًا مِّمَّنْ خَلَقَ الْأَرْضَ وَالسَّمَاوَاتِ الْعُلَى ﴿٤﴾
4. Ni uteremsho kutoka kwa Yule Aliyeumba ardhi na mbingu zilizo juu kabisa.
الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ ﴿٥﴾
5. Ar-Rahmaan (Mwingi wa Rehma) Yuko juu[2] ya ‘Arsh[3].
لَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ وَمَا بَيْنَهُمَا وَمَا تَحْتَ الثَّرَىٰ ﴿٦﴾
6. Ni Vyake Pekee vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini, na vilivyomo baina yake, na vilivyomo chini ya udongo.
وَإِن تَجْهَرْ بِالْقَوْلِ فَإِنَّهُ يَعْلَمُ السِّرَّ وَأَخْفَى ﴿٧﴾
7. Na ukinena kwa jahara, basi hakika Yeye Anajua siri na yanayofichika zaidi ya siri.
اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ لَهُ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ ﴿٨﴾
8. Allaah, hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye. Anayo Majina Mazuri kabisa.[4]
وَهَلْ أَتَاكَ حَدِيثُ مُوسَىٰ ﴿٩﴾
9. Na je, imekufikia hadithi ya Muwsaa?
إِذْ رَأَىٰ نَارًا فَقَالَ لِأَهْلِهِ امْكُثُوا إِنِّي آنَسْتُ نَارًا لَّعَلِّي آتِيكُم مِّنْهَا بِقَبَسٍ أَوْ أَجِدُ عَلَى النَّارِ هُدًى ﴿١٠﴾
10. Alipouona moto, akawaambia ahli zake: Bakieni (hapa), kwa yakini nimeona moto, huenda nikakuleteeni kutoka humo kijinga cha moto, au nipate mwongozo kwenye huo moto.
فَلَمَّا أَتَاهَا نُودِيَ يَا مُوسَىٰ ﴿١١﴾
11. Basi alipoufikia, aliitwa: Ee Muwsaa!
إِنِّي أَنَا رَبُّكَ فَاخْلَعْ نَعْلَيْكَ ۖ إِنَّكَ بِالْوَادِ الْمُقَدَّسِ طُوًى ﴿١٢﴾
12. Hakika Mimi ni Rabb wako. Basi vua viatu vyako, kwani wewe hakika uko katika bonde takatifu la Twuwaa.
وَأَنَا اخْتَرْتُكَ فَاسْتَمِعْ لِمَا يُوحَىٰ ﴿١٣﴾
13. Nami Nimekuchagua. Basi sikiliza kwa makini yanayofunuliwa Wahy (kwako).
إِنَّنِي أَنَا اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنَا فَاعْبُدْنِي وَأَقِمِ الصَّلَاةَ لِذِكْرِي ﴿١٤﴾
14. Hakika Mimi Ni Allaah, hapana mwabudiwa wa haki ila Mimi. Basi niabudu, na simamisha Swalaah kwa ajili ya kunidhukuru.
إِنَّ السَّاعَةَ آتِيَةٌ أَكَادُ أُخْفِيهَا لِتُجْزَىٰ كُلُّ نَفْسٍ بِمَا تَسْعَىٰ ﴿١٥﴾
15. Hakika Saa itafika tu. Nimekurubia kuificha ili kila nafsi ilipwe kwa yale iliyoyafanyia juhudi.
فَلَا يَصُدَّنَّكَ عَنْهَا مَن لَّا يُؤْمِنُ بِهَا وَاتَّبَعَ هَوَاهُ فَتَرْدَىٰ ﴿١٦﴾
16. Basi angalia asikukengeushe nayo yule asiyeiamini na akafuata hawaa, ukaja kuangamia.
وَمَا تِلْكَ بِيَمِينِكَ يَا مُوسَىٰ ﴿١٧﴾
17. Na nini hicho kilichoko katika mkono wako wa kulia ee Muwsaa?
قَالَ هِيَ عَصَايَ أَتَوَكَّأُ عَلَيْهَا وَأَهُشُّ بِهَا عَلَىٰ غَنَمِي وَلِيَ فِيهَا مَآرِبُ أُخْرَىٰ ﴿١٨﴾
18. (Muwsaa) akasema: Hii ni fimbo yangu, naiegemelea, na naangushia majani kwa ajili ya kondoo wangu, na pia nina maarubu mengineyo.
قَالَ أَلْقِهَا يَا مُوسَىٰ ﴿١٩﴾
19. (Allaah) Akasema: Basi iangushe ee Muwsaa.
فَأَلْقَاهَا فَإِذَا هِيَ حَيَّةٌ تَسْعَىٰ ﴿٢٠﴾
20. (Muwsaa) akaiangusha. Tahamaki hiyo ikawa ni nyoka anayetambaa mbio.
قَالَ خُذْهَا وَلَا تَخَفْ ۖ سَنُعِيدُهَا سِيرَتَهَا الْأُولَىٰ ﴿٢١﴾
21. (Allaah) Akasema: Ichukue na wala usikhofu. Tutairudisha katika hali yake ya awali.
وَاضْمُمْ يَدَكَ إِلَىٰ جَنَاحِكَ تَخْرُجْ بَيْضَاءَ مِنْ غَيْرِ سُوءٍ آيَةً أُخْرَىٰ ﴿٢٢﴾
22. Na ambatisha mkono wako katika ubavu wako, utatoka ukiwa mweupe bila ya madhara yoyote. Ni Aayah (Ishara, Dalili) nyengineo.
لِنُرِيَكَ مِنْ آيَاتِنَا الْكُبْرَى ﴿٢٣﴾
23. Ili Tukuonyeshe baadhi ya Aayaat (Ishara, Dalili) Zetu kubwa kabisa.
اذْهَبْ إِلَىٰ فِرْعَوْنَ إِنَّهُ طَغَىٰ ﴿٢٤﴾
24. Nenda kwa Firawni, hakika yeye amepindukia mipaka ya kuasi.
قَالَ رَبِّ اشْرَحْ لِي صَدْرِي ﴿٢٥﴾
25. (Muwsaa) akasema: Rabb wangu, Nikunjulie kifua changu.
وَيَسِّرْ لِي أَمْرِي ﴿٢٦﴾
26. Na Niwepesishie shughuli yangu.
وَاحْلُلْ عُقْدَةً مِّن لِّسَانِي ﴿٢٧﴾
27. Na Fungua fundo (la kigugumizi) katika ulimi wangu.
يَفْقَهُوا قَوْلِي ﴿٢٨﴾
28. Ili wafahamu kauli yangu.
وَاجْعَل لِّي وَزِيرًا مِّنْ أَهْلِي ﴿٢٩﴾
29. Na Nifanyie msaidizi kutoka ahli zangu.
هَارُونَ أَخِي ﴿٣٠﴾
30. Haaruwn, ndugu yangu.
اشْدُدْ بِهِ أَزْرِي ﴿٣١﴾
31. Nitie nguvu kwaye.
وَأَشْرِكْهُ فِي أَمْرِي ﴿٣٢﴾
32. Na Mshirikishe katika shughuli yangu.
كَيْ نُسَبِّحَكَ كَثِيرًا ﴿٣٣﴾
33. Ili tukusabihi kwa wingi.
وَنَذْكُرَكَ كَثِيرًا ﴿٣٤﴾
34. Na tukudhukuru kwa wingi.
إِنَّكَ كُنتَ بِنَا بَصِيرًا ﴿٣٥﴾
35. Hakika Wewe Ni Mwenye Kutuona sisi daima.
قَالَ قَدْ أُوتِيتَ سُؤْلَكَ يَا مُوسَىٰ ﴿٣٦﴾
36. (Allaah) Akasema: Umekwishapewa ombi lako ee Muwsaa.
وَلَقَدْ مَنَنَّا عَلَيْكَ مَرَّةً أُخْرَىٰ ﴿٣٧﴾
37. Na kwa yakini Tulikufanyia ihsaan mara nyingine.
إِذْ أَوْحَيْنَا إِلَىٰ أُمِّكَ مَا يُوحَىٰ ﴿٣٨﴾
38. Tulipomfunulia ilhamu mama yako yale yaliyofunuliwa.
أَنِ اقْذِفِيهِ فِي التَّابُوتِ فَاقْذِفِيهِ فِي الْيَمِّ فَلْيُلْقِهِ الْيَمُّ بِالسَّاحِلِ يَأْخُذْهُ عَدُوٌّ لِّي وَعَدُوٌّ لَّهُ ۚ وَأَلْقَيْتُ عَلَيْكَ مَحَبَّةً مِّنِّي وَلِتُصْنَعَ عَلَىٰ عَيْنِي ﴿٣٩﴾
39. Kwamba, mtie (Muwsaa) katika sanduku, kisha mtie katika mto (wa Nile). Kisha nao mto utamtupa ufukoni ili amchukue adui Yangu na adui wake (Firawni). Na Nikakutilia mahaba kutoka Kwangu, na ili ulelewe vyema Machoni Mwangu.[5]
إِذْ تَمْشِي أُخْتُكَ فَتَقُولُ هَلْ أَدُلُّكُمْ عَلَىٰ مَن يَكْفُلُهُ ۖ فَرَجَعْنَاكَ إِلَىٰ أُمِّكَ كَيْ تَقَرَّ عَيْنُهَا وَلَا تَحْزَنَ ۚ وَقَتَلْتَ نَفْسًا فَنَجَّيْنَاكَ مِنَ الْغَمِّ وَفَتَنَّاكَ فُتُونًا ۚ فَلَبِثْتَ سِنِينَ فِي أَهْلِ مَدْيَنَ ثُمَّ جِئْتَ عَلَىٰ قَدَرٍ يَا مُوسَىٰ ﴿٤٠﴾
40. Alipokwenda dada yako akasema: Je, nikuelekezeni kwa ambaye atamlea? Kisha Tukakurudisha kwa mama yako ili yaburudike macho yake, na wala asihuzunike. Kisha ukaua mtu Tukakuokoa na janga, na Tukakujaribu majaribio mazito. Ukaishi miaka kwa watu wa Madyan, kisha ukaja kama ilivyokadiriwa ee Muwsaa.
وَاصْطَنَعْتُكَ لِنَفْسِي ﴿٤١﴾
41. Na Nimekutayarisha na kukuchagua kwa ajili Yangu ee Muwsaa.
اذْهَبْ أَنتَ وَأَخُوكَ بِآيَاتِي وَلَا تَنِيَا فِي ذِكْرِي ﴿٤٢﴾
42. Nenda wewe na kaka yako pamoja na Aayaat (Ishara, Dalili) Zangu, na wala msinyong’onyee katika kunidhukuru.
اذْهَبَا إِلَىٰ فِرْعَوْنَ إِنَّهُ طَغَىٰ ﴿٤٣﴾
43. Nendeni wawili nyie kwa Firawni, hakika yeye amepindukia mipaka ya kuasi.
فَقُولَا لَهُ قَوْلًا لَّيِّنًا لَّعَلَّهُ يَتَذَكَّرُ أَوْ يَخْشَىٰ ﴿٤٤﴾
44. Mwambieni maneno laini, huenda akawaidhika au akakhofu.
قَالَا رَبَّنَا إِنَّنَا نَخَافُ أَن يَفْرُطَ عَلَيْنَا أَوْ أَن يَطْغَىٰ ﴿٤٥﴾
45. Wakasema: Rabb wetu! Hakika sisi tunakhofu asije kuharakiza ubaya juu yetu au akapinduka mipaka kuasi.
قَالَ لَا تَخَافَا ۖ إِنَّنِي مَعَكُمَا أَسْمَعُ وَأَرَىٰ ﴿٤٦﴾
46. (Allaah) Akasema: Msikhofu. Hakika Mimi Niko pamoja nanyi, Nasikia na Naona.[6]
فَأْتِيَاهُ فَقُولَا إِنَّا رَسُولَا رَبِّكَ فَأَرْسِلْ مَعَنَا بَنِي إِسْرَائِيلَ وَلَا تُعَذِّبْهُمْ ۖ قَدْ جِئْنَاكَ بِآيَةٍ مِّن رَّبِّكَ ۖ وَالسَّلَامُ عَلَىٰ مَنِ اتَّبَعَ الْهُدَىٰ ﴿٤٧﴾
47. Basi mwendeeni, na mwambieni: Hakika sisi ni Rusuli wa Rabb wako, basi waachie wana wa Israaiyl watoke pamoja nasi, na wala usiwatese. Kwa yakini tumekujia na Aayah (Ishara, Dalili, Muujiza) kutoka kwa Rabb wako. Na amani iwe juu ya yule atakayefuata mwongozo.[7]
إِنَّا قَدْ أُوحِيَ إِلَيْنَا أَنَّ الْعَذَابَ عَلَىٰ مَن كَذَّبَ وَتَوَلَّىٰ ﴿٤٨﴾
48. Hakika tumefunuliwa Wahy ya kwamba adhabu itakuwa kwa yule atakayekadhibisha na akakengeuka.
قَالَ فَمَن رَّبُّكُمَا يَا مُوسَىٰ ﴿٤٩﴾
49. (Firawni) akasema: Basi ni nani Rabb wenu ee Muwsaa?
قَالَ رَبُّنَا الَّذِي أَعْطَىٰ كُلَّ شَيْءٍ خَلْقَهُ ثُمَّ هَدَىٰ ﴿٥٠﴾
50. (Muwsaa) akasema: Rabb wetu ni Yule Aliyekipa kila kitu umbo lake, kisha Akakiongoza.
قَالَ فَمَا بَالُ الْقُرُونِ الْأُولَىٰ ﴿٥١﴾
51. (Firawni) akasema: Basi nini hali ya karne za awali?
قَالَ عِلْمُهَا عِندَ رَبِّي فِي كِتَابٍ ۖ لَّا يَضِلُّ رَبِّي وَلَا يَنسَى ﴿٥٢﴾
52. (Muwsaa) akasema: Ujuzi wake uko kwa Rabb wangu katika Kitabu. Rabb wangu Hakosei na wala Hasahau.
الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ مَهْدًا وَسَلَكَ لَكُمْ فِيهَا سُبُلًا وَأَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَخْرَجْنَا بِهِ أَزْوَاجًا مِّن نَّبَاتٍ شَتَّىٰ ﴿٥٣﴾
53. Ambaye Amekufanyieni ardhi kuwa tandiko, na Akakupitishieni humo njia, na Akateremsha kutoka mbinguni maji. Na kwayo Tukatoa aina za mimea mbali mbali.
كُلُوا وَارْعَوْا أَنْعَامَكُمْ ۗ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّأُولِي النُّهَىٰ ﴿٥٤﴾
54. Kuleni na lisheni wanyama wenu. Hakika katika hayo bila shaka kuna Aayaat (Ishara, Dalili, Mazingatio) kwa wenye umaizi.
مِنْهَا خَلَقْنَاكُمْ وَفِيهَا نُعِيدُكُمْ وَمِنْهَا نُخْرِجُكُمْ تَارَةً أُخْرَىٰ ﴿٥٥﴾
55. Kutokana nayo (ardhi) Tumekuumbeni, na humo Tutakurudisheni, na kutoka humo Tutakutoeni mara nyingine.[8]
وَلَقَدْ أَرَيْنَاهُ آيَاتِنَا كُلَّهَا فَكَذَّبَ وَأَبَىٰ ﴿٥٦﴾
56. Na kwa yakini Tulimuonyesha (Firawni) Aayaat (Ishara, Dalili) Zetu zote, lakini alikadhibisha na akakataa kabisa.
قَالَ أَجِئْتَنَا لِتُخْرِجَنَا مِنْ أَرْضِنَا بِسِحْرِكَ يَا مُوسَىٰ ﴿٥٧﴾
57. (Firawni) akasema: Je, umetujia ili ututoe katika ardhi yetu kwa sihiri yako ewe Muwsaa?
فَلَنَأْتِيَنَّكَ بِسِحْرٍ مِّثْلِهِ فَاجْعَلْ بَيْنَنَا وَبَيْنَكَ مَوْعِدًا لَّا نُخْلِفُهُ نَحْنُ وَلَا أَنتَ مَكَانًا سُوًى ﴿٥٨﴾
58. Basi bila shaka tutakuletea sihiri mfano wake. Hivyo panga baina yetu na baina yako miadi, tusiiendee kinyume sisi na wala wewe, mahali patakapokuwa sawa.
قَالَ مَوْعِدُكُمْ يَوْمُ الزِّينَةِ وَأَن يُحْشَرَ النَّاسُ ضُحًى ﴿٥٩﴾
59. Akasema: Miadi yenu ni siku ya mapambo (sikukuu), na watu wakusanywe wakati wa dhuha (jua linapopanda).
فَتَوَلَّىٰ فِرْعَوْنُ فَجَمَعَ كَيْدَهُ ثُمَّ أَتَىٰ ﴿٦٠﴾
60. Basi Firawni akageuka, akakusanya hila zake, kisha akaja.
قَالَ لَهُم مُّوسَىٰ وَيْلَكُمْ لَا تَفْتَرُوا عَلَى اللَّـهِ كَذِبًا فَيُسْحِتَكُم بِعَذَابٍ ۖ وَقَدْ خَابَ مَنِ افْتَرَىٰ ﴿٦١﴾
61. (Muwsaa) akawaambia: Ole wenu! Msimtungie Allaah uongo, Akakufutilieni mbali kwa adhabu. Na kwa yakini ameambulia patupu anayetunga uongo.
فَتَنَازَعُوا أَمْرَهُم بَيْنَهُمْ وَأَسَرُّوا النَّجْوَىٰ ﴿٦٢﴾
62. Wakajadiliana shauri lao baina yao na wakanong’ona kwa siri.
قَالُوا إِنْ هَـٰذَانِ لَسَاحِرَانِ يُرِيدَانِ أَن يُخْرِجَاكُم مِّنْ أَرْضِكُم بِسِحْرِهِمَا وَيَذْهَبَا بِطَرِيقَتِكُمُ الْمُثْلَىٰ ﴿٦٣﴾
63. Wakasema: Hakika hawa wawili ni wachawi wanataka kukutoeni katika ardhi yenu kwa sihiri yao na waondoshe mila zenu zilizo kamilifu kabisa.
فَأَجْمِعُوا كَيْدَكُمْ ثُمَّ ائْتُوا صَفًّا ۚ وَقَدْ أَفْلَحَ الْيَوْمَ مَنِ اسْتَعْلَىٰ ﴿٦٤﴾
64. Basi jumuisheni kwa pamoja hila zenu, kisha fikeni kwa kujipanga safu. Na kwa yakini atafaulu leo atakayeshinda.
قَالُوا يَا مُوسَىٰ إِمَّا أَن تُلْقِيَ وَإِمَّا أَن نَّكُونَ أَوَّلَ مَنْ أَلْقَىٰ ﴿٦٥﴾
65. Wakasema: Ee Muwsaa, ima utupe wewe au tuwe sisi wa kwanza kutupa.
قَالَ بَلْ أَلْقُوا ۖ فَإِذَا حِبَالُهُمْ وَعِصِيُّهُمْ يُخَيَّلُ إِلَيْهِ مِن سِحْرِهِمْ أَنَّهَا تَسْعَىٰ ﴿٦٦﴾
66. (Muwsaa) akasema: Bali tupeni nyinyi. Tahamaki kamba zao na fimbo zao zikaonekana kwake kutokana na sihiri yao kwamba zinakwenda mbio.
فَأَوْجَسَ فِي نَفْسِهِ خِيفَةً مُّوسَىٰ ﴿٦٧﴾
67. Basi Muwsaa akahisi khofu katika nafsi yake.
قُلْنَا لَا تَخَفْ إِنَّكَ أَنتَ الْأَعْلَىٰ ﴿٦٨﴾
68. Tukasema: Usikhofu. Hakika wewe ndiye utakayeshinda.
وَأَلْقِ مَا فِي يَمِينِكَ تَلْقَفْ مَا صَنَعُوا ۖ إِنَّمَا صَنَعُوا كَيْدُ سَاحِرٍ ۖ وَلَا يُفْلِحُ السَّاحِرُ حَيْثُ أَتَىٰ ﴿٦٩﴾
69. Na tupa kilicho katika mkono wako wa kulia, kitameza vile walivyoviunda. Hakika walivyoviunda ni hila za mchawi, na wala mchawi hafaulu popote ajapo.
فَأُلْقِيَ السَّحَرَةُ سُجَّدًا قَالُوا آمَنَّا بِرَبِّ هَارُونَ وَمُوسَىٰ ﴿٧٠﴾
70. Basi wachawi wakajikuta wameanguka wakisujudu. Wakasema Tumemwamini Rabb wa Haaruwn na Muwsaa.
قَالَ آمَنتُمْ لَهُ قَبْلَ أَنْ آذَنَ لَكُمْ ۖ إِنَّهُ لَكَبِيرُكُمُ الَّذِي عَلَّمَكُمُ السِّحْرَ ۖ فَلَأُقَطِّعَنَّ أَيْدِيَكُمْ وَأَرْجُلَكُم مِّنْ خِلَافٍ وَلَأُصَلِّبَنَّكُمْ فِي جُذُوعِ النَّخْلِ وَلَتَعْلَمُنَّ أَيُّنَا أَشَدُّ عَذَابًا وَأَبْقَىٰ ﴿٧١﴾
71. (Firawni) akasema: Mmemwamini kabla sijakupeni idhini? Hakika yeye ndiye mkubwa wenu ambaye amekufunzeni sihiri. Basi bila shaka nitakukatenikateni mikono yenu na miguu yenu kwa kutofautisha, kisha nitakusulubuni katika mashina ya mitende. Na bila shaka mtajua yupi kati yetu ni mkali zaidi wa kuadhibu na wa kudumisha zaidi.
قَالُوا لَن نُّؤْثِرَكَ عَلَىٰ مَا جَاءَنَا مِنَ الْبَيِّنَاتِ وَالَّذِي فَطَرَنَا ۖ فَاقْضِ مَا أَنتَ قَاضٍ ۖ إِنَّمَا تَقْضِي هَـٰذِهِ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا ﴿٧٢﴾
72. (Wachawi) wakasema: Hatutokukhiyari kuliko ambayo yametujia ya dalili za waziwazi na Yule Aliyetuumba. Basi hukumu unavyotaka kuhukumu, kwani hakika wewe unahukumu (katika) uhai huu wa duniani tu.
إِنَّا آمَنَّا بِرَبِّنَا لِيَغْفِرَ لَنَا خَطَايَانَا وَمَا أَكْرَهْتَنَا عَلَيْهِ مِنَ السِّحْرِ ۗ وَاللَّـهُ خَيْرٌ وَأَبْقَىٰ ﴿٧٣﴾
73. Hakika sisi tumemwamini Rabb wetu ili Atughufurie madhambi yetu, na yale uliyotushurutisha katika mambo ya sihiri. Na Allaah Ni Mbora Zaidi na Mwenye Kudumu zaidi.
إِنَّهُ مَن يَأْتِ رَبَّهُ مُجْرِمًا فَإِنَّ لَهُ جَهَنَّمَ لَا يَمُوتُ فِيهَا وَلَا يَحْيَىٰ ﴿٧٤﴾
74. Hakika atakayemjia Rabb wake akiwa mhalifu, basi hakika atapata Jahannam. Hafi humo (akapumzika) na wala haishi (maisha ya raha).
وَمَن يَأْتِهِ مُؤْمِنًا قَدْ عَمِلَ الصَّالِحَاتِ فَأُولَـٰئِكَ لَهُمُ الدَّرَجَاتُ الْعُلَىٰ ﴿٧٥﴾
75. Na atakayemjia akiwa Muumini ametenda mema, basi hao watapata vyeo vya juu kabisa.
جَنَّاتُ عَدْنٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا ۚ وَذَٰلِكَ جَزَاءُ مَن تَزَكَّىٰ ﴿٧٦﴾
76. Jannaat za kudumu milele zipitazo chini yake mito, watadumu humo. Na hiyo ndio jazaa ya mwenye kujitakasa.
وَلَقَدْ أَوْحَيْنَا إِلَىٰ مُوسَىٰ أَنْ أَسْرِ بِعِبَادِي فَاضْرِبْ لَهُمْ طَرِيقًا فِي الْبَحْرِ يَبَسًا لَّا تَخَافُ دَرَكًا وَلَا تَخْشَىٰ ﴿٧٧﴾
77. Na kwa yakini Tulimfunulia Wahy Muwsaa kwamba: Safiri usiku pamoja na waja Wangu, wapigie njia kavu baharini, usikhofu kukamatwa na wala usikhofu (kuzama).
فَأَتْبَعَهُمْ فِرْعَوْنُ بِجُنُودِهِ فَغَشِيَهُم مِّنَ الْيَمِّ مَا غَشِيَهُمْ ﴿٧٨﴾
78. Basi Firawni akawafuata pamoja na jeshi lake. Yakawafunika humo baharini yaliyowafunika.
وَأَضَلَّ فِرْعَوْنُ قَوْمَهُ وَمَا هَدَىٰ ﴿٧٩﴾
79. Na Firawni akawapoteza watu wake, na wala hakuwaongoza.
يَا بَنِي إِسْرَائِيلَ قَدْ أَنجَيْنَاكُم مِّنْ عَدُوِّكُمْ وَوَاعَدْنَاكُمْ جَانِبَ الطُّورِ الْأَيْمَنَ وَنَزَّلْنَا عَلَيْكُمُ الْمَنَّ وَالسَّلْوَىٰ ﴿٨٠﴾
80. Enyi wana wa Israaiyl! Kwa yakini Tulikuokoeni kutokana na adui wenu, na Tukakuahidini upande wa kulia wa mlima, na Tukakuteremshieni al-manna na as-salwaa.[9]
كُلُوا مِن طَيِّبَاتِ مَا رَزَقْنَاكُمْ وَلَا تَطْغَوْا فِيهِ فَيَحِلَّ عَلَيْكُمْ غَضَبِي ۖ وَمَن يَحْلِلْ عَلَيْهِ غَضَبِي فَقَدْ هَوَىٰ ﴿٨١﴾
81. Kuleni katika vizuri Tulivyokuruzukuni, na wala msivuke mipaka katika hayo, ikakushukieni Ghadhabu Yangu. Na itakayemshukia Ghadhabu Yangu, basi kwa yakini ameangamia.
وَإِنِّي لَغَفَّارٌ لِّمَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ صَالِحًا ثُمَّ اهْتَدَىٰ ﴿٨٢﴾
82. Na hakika Mimi bila shaka Ni Mwingi mno wa Kughufuria kwa anayetubia na akaamini na akatenda mema, tena akathibiti katika njia ya sawa.
وَمَا أَعْجَلَكَ عَن قَوْمِكَ يَا مُوسَىٰ ﴿٨٣﴾
83. Na nini kilichokuharakisha ukaacha watu wako ee Muwsaa?
قَالَ هُمْ أُولَاءِ عَلَىٰ أَثَرِي وَعَجِلْتُ إِلَيْكَ رَبِّ لِتَرْضَىٰ ﴿٨٤﴾
84. (Muwsaa) akasema: Hao wako nyuma yangu, na nimeharakiza kukujia Rabb wangu ili Uridhike.
قَالَ فَإِنَّا قَدْ فَتَنَّا قَوْمَكَ مِن بَعْدِكَ وَأَضَلَّهُمُ السَّامِرِيُّ ﴿٨٥﴾
85. (Allaah) Akasema: Basi hakika Tumewatia mtihanini watu wako baada yako, na Saamiriyyu amewapoteza.[10]
فَرَجَعَ مُوسَىٰ إِلَىٰ قَوْمِهِ غَضْبَانَ أَسِفًا ۚ قَالَ يَا قَوْمِ أَلَمْ يَعِدْكُمْ رَبُّكُمْ وَعْدًا حَسَنًا ۚ أَفَطَالَ عَلَيْكُمُ الْعَهْدُ أَمْ أَرَدتُّمْ أَن يَحِلَّ عَلَيْكُمْ غَضَبٌ مِّن رَّبِّكُمْ فَأَخْلَفْتُم مَّوْعِدِي ﴿٨٦﴾
86. Basi Muwsaa akarejea kwa watu wake akiwa ameghadhibika na kusikitika. Akasema: Enyi watu wangu! Je, Rabb wenu Hakukuahidini ahadi nzuri? Je, imerefuka kwenu ahadi, au mmetaka ikushukieni ghadhabu kutoka kwa Rabb wenu, na kwa hiyo mkakhalifu miadi yangu?
قَالُوا مَا أَخْلَفْنَا مَوْعِدَكَ بِمَلْكِنَا وَلَـٰكِنَّا حُمِّلْنَا أَوْزَارًا مِّن زِينَةِ الْقَوْمِ فَقَذَفْنَاهَا فَكَذَٰلِكَ أَلْقَى السَّامِرِيُّ ﴿٨٧﴾
87. Wakasema: Hatukukhalifu miadi yako kwa khiyari yetu, lakini tulibebeshwa mizigo ya mapambo ya watu, basi tukaitupa na hivyo ndivyo Saamiriyyu alivyotupa.
فَأَخْرَجَ لَهُمْ عِجْلًا جَسَدًا لَّهُ خُوَارٌ فَقَالُوا هَـٰذَا إِلَـٰهُكُمْ وَإِلَـٰهُ مُوسَىٰ فَنَسِيَ ﴿٨٨﴾
88. Akawaundia ndama kiwiliwili chenye sauti. Wakasema: Huyu ndiye mwabudiwa wenu na mwabudiwa wa Muwsaa lakini amesahau (mwabudiwa wake).
أَفَلَا يَرَوْنَ أَلَّا يَرْجِعُ إِلَيْهِمْ قَوْلًا وَلَا يَمْلِكُ لَهُمْ ضَرًّا وَلَا نَفْعًا ﴿٨٩﴾
89. Je, hawaoni kwamba (huyo ndama) hawarejeshei neno, na wala hawezi kuwadhuru wala kuwanufaisha?
وَلَقَدْ قَالَ لَهُمْ هَارُونُ مِن قَبْلُ يَا قَوْمِ إِنَّمَا فُتِنتُم بِهِ ۖ وَإِنَّ رَبَّكُمُ الرَّحْمَـٰنُ فَاتَّبِعُونِي وَأَطِيعُوا أَمْرِي ﴿٩٠﴾
90. Na Haaruwn alikwishawaambia kabla: Enyi watu! Hakika mmetiwa mtihanini naye (ndama), na hakika Rabb wenu ni Ar-Rahmaan (Mwingi wa Rehma), basi nifuateni na tiini amri yangu.
قَالُوا لَن نَّبْرَحَ عَلَيْهِ عَاكِفِينَ حَتَّىٰ يَرْجِعَ إِلَيْنَا مُوسَىٰ ﴿٩١﴾
91. Wakasema: Hatutoacha kumwabudu mpaka Muwsaa arudi kwetu.
قَالَ يَا هَارُونُ مَا مَنَعَكَ إِذْ رَأَيْتَهُمْ ضَلُّوا ﴿٩٢﴾
92. (Muwsaa aliporejea) alisema: Ee Haaruwn! Nini kimekuzuia ulipowaona wanapotoka?
أَلَّا تَتَّبِعَنِ ۖ أَفَعَصَيْتَ أَمْرِي ﴿٩٣﴾
93. Kwamba unifuate. Je, umeasi amri yangu?
قَالَ يَا ابْنَ أُمَّ لَا تَأْخُذْ بِلِحْيَتِي وَلَا بِرَأْسِي ۖ إِنِّي خَشِيتُ أَن تَقُولَ فَرَّقْتَ بَيْنَ بَنِي إِسْرَائِيلَ وَلَمْ تَرْقُبْ قَوْلِي ﴿٩٤﴾
94. (Haaruwn) akasema: Ee mwana wa mama yangu! Usinishike ndevu zangu, wala kichwa changu. Hakika mimi niliogopa usije kusema: Umefarikisha baina ya wana wa Israaiyl na wala hukuchunga kauli yangu.
قَالَ فَمَا خَطْبُكَ يَا سَامِرِيُّ ﴿٩٥﴾
95. (Muwsaa) akasema: Una jambo gani ee Saamiriyy?
قَالَ بَصُرْتُ بِمَا لَمْ يَبْصُرُوا بِهِ فَقَبَضْتُ قَبْضَةً مِّنْ أَثَرِ الرَّسُولِ فَنَبَذْتُهَا وَكَذَٰلِكَ سَوَّلَتْ لِي نَفْسِي ﴿٩٦﴾
96. (Saamirriy) akasema: Niliona yale wasiyoyaona na nikateka teko (la udongo) katika kwato za (farasi wa) Jibriyl kisha nikautupa. Na hivyo ndivyo ilivyonishawishi nafsi yangu.
قَالَ فَاذْهَبْ فَإِنَّ لَكَ فِي الْحَيَاةِ أَن تَقُولَ لَا مِسَاسَ ۖ وَإِنَّ لَكَ مَوْعِدًا لَّن تُخْلَفَهُ ۖ وَانظُرْ إِلَىٰ إِلَـٰهِكَ الَّذِي ظَلْتَ عَلَيْهِ عَاكِفًا ۖ لَّنُحَرِّقَنَّهُ ثُمَّ لَنَنسِفَنَّهُ فِي الْيَمِّ نَسْفًا ﴿٩٧﴾
97. (Muwsaa) akasema: Nenda zako! Kwani hakika utakuwa katika uhai wako ukisema: Usiniguse![11] Na hakika una miadi hutovunjiwa. Na mtazame mwabudiwa wako ambaye umeendelea kukaa kumwabudu. Bila shaka tutamuunguza, kisha tutampeperusha baharini chembechembe.
إِنَّمَا إِلَـٰهُكُمُ اللَّـهُ الَّذِي لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۚ وَسِعَ كُلَّ شَيْءٍ عِلْمًا ﴿٩٨﴾
98. Hakika Mwabudiwa wenu wa haki Ni Allaah Ambaye hapana ilaah ila Yeye. Amekienea kila kitu kwa Ilimu Yake.
كَذَٰلِكَ نَقُصُّ عَلَيْكَ مِنْ أَنبَاءِ مَا قَدْ سَبَقَ ۚ وَقَدْ آتَيْنَاكَ مِن لَّدُنَّا ذِكْرًا ﴿٩٩﴾
99. Hivyo ndivyo Tunavyokusimulia miongoni mwa khabari zilizotangulia (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم). Na kwa yakini Tumekupa kutoka Kwetu Ukumbusho (Qur-aan).
مَّنْ أَعْرَضَ عَنْهُ فَإِنَّهُ يَحْمِلُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وِزْرًا ﴿١٠٠﴾
100. Atakayejitenga nayo, basi hakika yeye atabeba Siku ya Qiyaamah mzigo (wa dhambi).
خَالِدِينَ فِيهِ ۖ وَسَاءَ لَهُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ حِمْلًا ﴿١٠١﴾
101. Wadumu ndani yake (adhabu). Na mzigo mbaya ulioje kwao kuubeba Siku ya Qiyaamah.
يَوْمَ يُنفَخُ فِي الصُّورِ ۚ وَنَحْشُرُ الْمُجْرِمِينَ يَوْمَئِذٍ زُرْقًا ﴿١٠٢﴾
102. Siku litakapopulizwa baragumu. Na Tutawakusanya wahalifu Siku hiyo macho yao yakiwa rangi ya buluu (kwa kiwewe).
يَتَخَافَتُونَ بَيْنَهُمْ إِن لَّبِثْتُمْ إِلَّا عَشْرًا ﴿١٠٣﴾
103. Wakinong'onezana baina yao: Hamkukaa (duniani) isipokuwa (siku) kumi tu.
نَّحْنُ أَعْلَمُ بِمَا يَقُولُونَ إِذْ يَقُولُ أَمْثَلُهُمْ طَرِيقَةً إِن لَّبِثْتُمْ إِلَّا يَوْمًا ﴿١٠٤﴾
104. Sisi Tunajua zaidi yale wanayoyasema. Atakaposema mbora wao katika mwendo: Hamkukaa isipokuwa siku moja tu.
وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الْجِبَالِ فَقُلْ يَنسِفُهَا رَبِّي نَسْفًا ﴿١٠٥﴾
105. Na wanakuuliza (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kuhusu milima. Sema: Rabb wangu Ataing’olea mbali ibaki chembechembe.
فَيَذَرُهَا قَاعًا صَفْصَفًا ﴿١٠٦﴾
106. Kisha Ataiacha ardhi kuwa tambarare, uwanda ulio sawasawa.
لَّا تَرَىٰ فِيهَا عِوَجًا وَلَا أَمْتًا ﴿١٠٧﴾
107. Hutoona humo mdidimio wala mwinuko.
يَوْمَئِذٍ يَتَّبِعُونَ الدَّاعِيَ لَا عِوَجَ لَهُ ۖ وَخَشَعَتِ الْأَصْوَاتُ لِلرَّحْمَـٰنِ فَلَا تَسْمَعُ إِلَّا هَمْسًا ﴿١٠٨﴾
108. Siku hiyo watamfuata mwitaji hakuna kumkengeuka. Na sauti zitafifia kwa Ar-Rahmaan, basi hutosikia isipokuwa mchakato wa nyayo.
يَوْمَئِذٍ لَّا تَنفَعُ الشَّفَاعَةُ إِلَّا مَنْ أَذِنَ لَهُ الرَّحْمَـٰنُ وَرَضِيَ لَهُ قَوْلًا ﴿١٠٩﴾
109. Siku hiyo haitofaa shafaa’ah (uombezi) isipokuwa ya yule atakayepewa idhini na Ar-Rahmaan na Akamridhia kusema.[12]
يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ وَلَا يُحِيطُونَ بِهِ عِلْمًا ﴿١١٠﴾
110. Anajua yale yaliyoko mbele yao, na yale yaliyoko nyuma yao, na wala hawawezi kufikia kuelewa chochote cha Ujuzi Wake.
وَعَنَتِ الْوُجُوهُ لِلْحَيِّ الْقَيُّومِ ۖ وَقَدْ خَابَ مَنْ حَمَلَ ظُلْمًا ﴿١١١﴾
111. Nyuso zitanyenyekea kwa Al-Hayyu (Aliye Hai daima), Al-Qayyuwm (Msimamizi wa kila kitu).[13] Na kwa yakini ameharibikiwa abebaye dhulma.
وَمَن يَعْمَلْ مِنَ الصَّالِحَاتِ وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَلَا يَخَافُ ظُلْمًا وَلَا هَضْمًا ﴿١١٢﴾
112. Na yeyote atakayetenda mema naye ni Muumini, basi hatokhofu dhulma wala kupunjwa.
وَكَذَٰلِكَ أَنزَلْنَاهُ قُرْآنًا عَرَبِيًّا وَصَرَّفْنَا فِيهِ مِنَ الْوَعِيدِ لَعَلَّهُمْ يَتَّقُونَ أَوْ يُحْدِثُ لَهُمْ ذِكْرًا ﴿١١٣﴾
113. Na hivyo ndivyo Tumeiteremsha Qur-aan kwa Kiarabu, na Tukaisarifu waziwazi humo vitisho kadhaa, huenda wakapata kuwa na taqwa au ikawapa makumbusho.
فَتَعَالَى اللَّـهُ الْمَلِكُ الْحَقُّ ۗ وَلَا تَعْجَلْ بِالْقُرْآنِ مِن قَبْلِ أَن يُقْضَىٰ إِلَيْكَ وَحْيُهُ ۖ وَقُل رَّبِّ زِدْنِي عِلْمًا ﴿١١٤﴾
114. Basi Ametukuka Allaah kwa ‘Uluwa, Mfalme wa haki. Na wala usiiharakize Qur-aan (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kabla haikumalizwa kufunuliwa Wahy kwako. Na sema: Rabb wangu! Nizidishie Ilimu.
وَلَقَدْ عَهِدْنَا إِلَىٰ آدَمَ مِن قَبْلُ فَنَسِيَ وَلَمْ نَجِدْ لَهُ عَزْمًا ﴿١١٥﴾
115. Na kwa yakini Tulimpa Aadam ahadi kabla, lakini akasahau, na wala Hatukuona kwake azimio.
وَإِذْ قُلْنَا لِلْمَلَائِكَةِ اسْجُدُوا لِآدَمَ فَسَجَدُوا إِلَّا إِبْلِيسَ أَبَىٰ ﴿١١٦﴾
116. Na pindi Tulipowaambia Malaika: Msujudieni Aadam. Wakasujudu isipokuwa Ibliys, alikataa kabisa.
فَقُلْنَا يَا آدَمُ إِنَّ هَـٰذَا عَدُوٌّ لَّكَ وَلِزَوْجِكَ فَلَا يُخْرِجَنَّكُمَا مِنَ الْجَنَّةِ فَتَشْقَىٰ ﴿١١٧﴾
117. Tukasema: Ee Aadam! Hakika huyu (Ibliys) ni adui wako na wa mkeo, basi angalieni asikutoeni katika Jannah ukapata mashaka.
إِنَّ لَكَ أَلَّا تَجُوعَ فِيهَا وَلَا تَعْرَىٰ ﴿١١٨﴾
118. Hakika wewe humo hutopata njaa, na wala hutokuwa uchi.
وَأَنَّكَ لَا تَظْمَأُ فِيهَا وَلَا تَضْحَىٰ ﴿١١٩﴾
119. Na hakika wewe hutopata kiu humo, na wala hutopigwa na joto la jua
فَوَسْوَسَ إِلَيْهِ الشَّيْطَانُ قَالَ يَا آدَمُ هَلْ أَدُلُّكَ عَلَىٰ شَجَرَةِ الْخُلْدِ وَمُلْكٍ لَّا يَبْلَىٰ ﴿١٢٠﴾
120. Lakini shaytwaan alimtia wasiwasi, akasema: Ee Aadam! Je, nikuelekeze mti wa kudumu na ufalme usiochakaa?
فَأَكَلَا مِنْهَا فَبَدَتْ لَهُمَا سَوْآتُهُمَا وَطَفِقَا يَخْصِفَانِ عَلَيْهِمَا مِن وَرَقِ الْجَنَّةِ ۚ وَعَصَىٰ آدَمُ رَبَّهُ فَغَوَىٰ ﴿١٢١﴾
121. Basi waliula. Uchi wao ukawadhihirikia na wakaanza kujibandika majani ya Jannah. Na Aadam akamuasi Rabb wake, akapotoka.
ثُمَّ اجْتَبَاهُ رَبُّهُ فَتَابَ عَلَيْهِ وَهَدَىٰ ﴿١٢٢﴾
122. Kisha Rabb wake Akamteua, Akapokea tawbah yake na Akamwongoza.
قَالَ اهْبِطَا مِنْهَا جَمِيعًا ۖ بَعْضُكُمْ لِبَعْضٍ عَدُوٌّ ۖ فَإِمَّا يَأْتِيَنَّكُم مِّنِّي هُدًى فَمَنِ اتَّبَعَ هُدَايَ فَلَا يَضِلُّ وَلَا يَشْقَىٰ ﴿١٢٣﴾
123. (Allaah) Akasema: Teremkeni toka humo nyote, hali ya kuwa maadui nyinyi kwa nyinyi. Kisha utakapokufikieni kutoka Kwangu Mwongozo, basi atakayefuata Mwongozo Wangu, hatopotea na wala hatopata mashaka.
وَمَنْ أَعْرَضَ عَن ذِكْرِي فَإِنَّ لَهُ مَعِيشَةً ضَنكًا وَنَحْشُرُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ أَعْمَىٰ ﴿١٢٤﴾
124. Na atakayejitenga na Ukumbusho Wangu basi hakika atapata maisha ya dhiki, na Tutamfufua Siku ya Qiyaamah akiwa kipofu.[14]
قَالَ رَبِّ لِمَ حَشَرْتَنِي أَعْمَىٰ وَقَدْ كُنتُ بَصِيرًا ﴿١٢٥﴾
125. Atasema: Rabb wangu! Kwa nini Umenifufua kipofu, na hali nilikuwa naona?
قَالَ كَذَٰلِكَ أَتَتْكَ آيَاتُنَا فَنَسِيتَهَا ۖ وَكَذَٰلِكَ الْيَوْمَ تُنسَىٰ ﴿١٢٦﴾
126. (Allaah) Atasema: Hivyo ndivyo, zilikufikia Aayaat Zetu ukazisahau, na kadhalika leo unasahauliwa.
وَكَذَٰلِكَ نَجْزِي مَنْ أَسْرَفَ وَلَمْ يُؤْمِن بِآيَاتِ رَبِّهِ ۚ وَلَعَذَابُ الْآخِرَةِ أَشَدُّ وَأَبْقَىٰ ﴿١٢٧﴾
127. Na hivyo ndivyo Tunavyomlipa yule aliyevuka mipaka na hakuamini Aayaat za Rabb wake. Na bila shaka adhabu ya Aakhirah ni kali zaidi na ni ya kudumu zaidi.
أَفَلَمْ يَهْدِ لَهُمْ كَمْ أَهْلَكْنَا قَبْلَهُم مِّنَ الْقُرُونِ يَمْشُونَ فِي مَسَاكِنِهِمْ ۗ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّأُولِي النُّهَىٰ ﴿١٢٨﴾
128. Je, haijawadhihirikia tu kuwa ni kaumu ngapi Tumeziangamiza kabla yao, huku wakiwa wanatembea (kwa amani na raha) katika maskani zao? Hakika katika hayo bila shaka kuna Aayaat (Mazingatio, Mawaidha) kwa wenye kumaizi.
وَلَوْلَا كَلِمَةٌ سَبَقَتْ مِن رَّبِّكَ لَكَانَ لِزَامًا وَأَجَلٌ مُّسَمًّى ﴿١٢٩﴾
129. Na ingekuwa si neno lililotangulia kutoka kwa Rabb wako, na muda uliokadiriwa, bila shaka ingelazimika (adhabu hapa duniani).
فَاصْبِرْ عَلَىٰ مَا يَقُولُونَ وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ قَبْلَ طُلُوعِ الشَّمْسِ وَقَبْلَ غُرُوبِهَا ۖ وَمِنْ آنَاءِ اللَّيْلِ فَسَبِّحْ وَأَطْرَافَ النَّهَارِ لَعَلَّكَ تَرْضَىٰ ﴿١٣٠﴾
130. Basi subiri juu ya yale wanayoyasema. Na sabihi ukimhimidi Rabb wako kabla ya kuchomoza jua, na kabla ya kuchwa kwake. Na katika nyakati za usiku pia sabbih na katikati ya mchana, huenda ukapata ya kukuridhisha.
وَلَا تَمُدَّنَّ عَيْنَيْكَ إِلَىٰ مَا مَتَّعْنَا بِهِ أَزْوَاجًا مِّنْهُمْ زَهْرَةَ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا لِنَفْتِنَهُمْ فِيهِ ۚ وَرِزْقُ رَبِّكَ خَيْرٌ وَأَبْقَىٰ ﴿١٣١﴾
131. Na wala usikodoe kabisa macho yako kwa yale ya starehe Tuliyowaneemesha baadhi ya makundi (ya kikafiri) miongoni mwao. Hayo ni mapambo ya uhai wa dunia tu, ili Tuwajaribu kwayo. Na riziki ya Rabb wako ni bora zaidi na ni yenye kudumu zaidi.
وَأْمُرْ أَهْلَكَ بِالصَّلَاةِ وَاصْطَبِرْ عَلَيْهَا ۖ لَا نَسْأَلُكَ رِزْقًا ۖ نَّحْنُ نَرْزُقُكَ ۗ وَالْعَاقِبَةُ لِلتَّقْوَىٰ ﴿١٣٢﴾
132. Na amrisha ahli zako Swalaah, na dumisha uvumilivu juu ya mazito yake. Hatukukalifishi riziki bali Sisi Ndio Tunaokuruzuku. Na hatima njema ni kwa wenye taqwa.[15]
وَقَالُوا لَوْلَا يَأْتِينَا بِآيَةٍ مِّن رَّبِّهِ ۚ أَوَلَمْ تَأْتِهِم بَيِّنَةُ مَا فِي الصُّحُفِ الْأُولَىٰ ﴿١٣٣﴾
133. Na (makafiri) wakasema: Kwa nini hatuletei Aayah (Ishara, Dalili, Muujiza) kutoka kwa Rabb wake? Je, kwani hazikuwafikia hoja bayana zilizomo katika Sahifa za awali?[16]
وَلَوْ أَنَّا أَهْلَكْنَاهُم بِعَذَابٍ مِّن قَبْلِهِ لَقَالُوا رَبَّنَا لَوْلَا أَرْسَلْتَ إِلَيْنَا رَسُولًا فَنَتَّبِعَ آيَاتِكَ مِن قَبْلِ أَن نَّذِلَّ وَنَخْزَىٰ ﴿١٣٤﴾
134. Na lau Tungeliwaangamiza kwa adhabu kabla yake, wangelisema: Rabb wetu! Kwa nini Usituletee Rasuli tukafuata Aayaat Zako kabla hatujadhalilika na hatujahizika?
قُلْ كُلٌّ مُّتَرَبِّصٌ فَتَرَبَّصُوا ۖ فَسَتَعْلَمُونَ مَنْ أَصْحَابُ الصِّرَاطِ السَّوِيِّ وَمَنِ اهْتَدَىٰ ﴿١٣٥﴾
135. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Kila mmoja ni mwenye kungojea na kutazamia, basi ngojeeni na tazamieni. Karibuni mtajua ni nani mwenye njia iliyo sawa na ni nani aliyeongoka.
[1] الحروف المقطعة (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah):
Hizi ni herufi zinazojulikana kama الحروف المقطعة (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Tanbihi ya Al-Baqarah (2:1).
[2] Istawaa اسْتَوَى
Yuko juu kwa namna inayolingana na Uadhama na Ujalali Wake Yeye Mwenyewe Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Al-A'raaf (7:54) kwenye maelezo bayana ya maana yake, yenye kutofautiana na maana ya katika Suwrah Al-Baqarah (2:29) na Suwrat Fusswilat (41:11).
Na msimamo wa Salaf katika Tafsiyr ya Aayah yenye kitenzi hiki, ni kama huu uliopokelewa kuwa, Ja‘afar bin ‘Abdillaah na wengine miongoni mwao walisema: “Tulikuwa kwa Imaam Maalik bin Anas, akatokea mtu akamuuliza: Ee Abaa ‘Abdillaah! Allaah (سُبْحَانَهُ وَتَعَالَى) Anasema:
الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ ﴿٥﴾
“Ar-Rahmaan (Mwingi wa Rehma) Yuko juu ya ‘Arsh.” [Twaahaa (20:5)].
Je, ni vipi Istawaa? Basi Imaam Maalik hakuwahi kughadhibika kutokana na kitu chochote kile kama alivyoghadhibika kutokana na swali la mtu huyo. Kisha (Imaam Maalik) akatazama chini na huku akikwaruza kwaruza kwa kijiti kilichokuwa kwenye mkono wake mpaka akarowa jasho, halafu akanyanyua kichwa chake na kukirembea kile kijiti kisha akasema: ‘Vipi’ ni ghayr-ma’quwl (hakutambuliki), na Al-Istiwaa ghayr-maj-huwl (si jambo lisilojulikana), na kuamini hilo ni waajib (lazima), na kuuliza (au kuhoji hilo) ni bid’ah (uzushi), na nina khofu kuwa wewe ni mzushi!” Akaamrisha mtu huyo atolewe, basi akatolewa.”
[Al-Hilyah (6/325-326)]. Na pia imesimuliwa na Abu ‘Uthmaan As-Swaabuwniy katika ‘Aqiydatus Salaf Asw-haab Al-Hadiyth Uk. (17-18), kutoka kwa Ja‘afar bin ‘Abdillaah, kutoka kwa Maalik, na Ibn ‘Abdil-Barr katika At-Tamhiyd (7/151), kutoka kwa ‘Abdullaah bin Naafi’, kutoka kwa Maalik na Al-Bayhaqiyy katika Al-Asmaa wasw-Swifaat Uk. (408), kutoka kwa ‘Abdullaah bin Wahb, kutoka kwa Maalik. Ibn Hajar amesema katika Al-Fat-h (13/406-407) kuwa mlolongo wake ni mzuri, na imesahihishwa na Adh-Dhahabiy katika Al-‘Uluww Uk. (103). Imaam Muhammad Naaswirud-Diyn Al-Albaaniy amesema Hadiyth hii ni Swahiyh katika Mukhtaswar Al-‘Uluww cha Imaam Adh-Dhahabiy, na pia ameihakiki katika Uk. (131).
[3] ‘Arsh Ya Ar-Rahmaan Na Tofauti Yake Na ’Arsh Ya Wanaadam: Rejea Al-Haaqqah (69:17).
[4] Majina Mazuri Kabisa Ya Allaah (سبحانه وتعالى): Rejea Faharasa ya Majina Mazuri Kabisa Ya Allaah Na Sifa Zake.
[5] Kuthibitisha Sifa Ya Allaah (سبحانه وتعالى): Rejea Huwd (11:37) na Suwrah hii Aayah (46).
[6] Kuthibitisha Sifa Za Allaah (سبحانه وتعالى) Ni ‘Aqiydah Ya Ahlus-Sunnah Wal-Jamaa’ah:
Sifa Ya Allaah (سبحانه وتعالى) ya Kuona na Kusikia ni Sifa inayopaswa kuthibitishwa kama Alivyoitaja Mwenyewe. Na hii ni ‘Aqiydah ya Ahlus-Sunnah Wal-Jamaa’ah. Rejea Huwd (11:37) kwenye maelezo bayana. Na katika Suwrah na Aayah nyingi, Allaah (سبحانه وتعالى) Anataja kuwa Yeye Ni Mwenye Kusikia na Kuona. Rejea Ghaafir (40:20), An-Nisaa (4:58), (4:134), na Al-Mujaadalah (58:1). Na dalili mojawapo katika Sunnah ni:
عَنْ أَبِي مُوسَى الأَشْعَرِيِّ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ) قَالَ: كُنَّا مَعَ رَسُولِ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) فَكُنَّا إِذَا أَشْرَفْنَا عَلَى وَادٍ هَلَّلْنَا وَكَبَّرْنَا. ارْتَفَعَتْ أَصْوَاتُنَا فَقَالَ النَّبِيُّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم)َ: ((يَا أَيُّهَا النَّاسُ ارْبَعُوا عَلَى أَنْفُسِكُمْ فَإِنَّكُمْ لاَ تَدْعُونَ أَصَمَّ ولاَ غَائِبًا إِنَّهُ مَعَكُمْ إِنَّهُ سَمِيعٌ قَرِيبٌ تَبَارَكَ اسْمُهُ وَتَعَالَى جَدُّهُ))
Amesimulia Abu Muwsaa Al-Ash’ariyy (رضي الله عنه): Tulikuwa pamoja na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) na tukawa kila tukipanda bonde, tunafanya tahliyl (Laa Ilaaha Illa-Allaah), na tunaleta takbiyr (Allaahu Akbar). Zikapanda sauti zetu, na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Enyi watu, zihurumieni nafsi zenu, kwani hamumwombi kiziwi wala asiyekuwepo, hakika Yeye Yupo nanyi (kwa Ujuzi Wake), hakika Yeye Ni Mwenye Kusikia yote, Yupo Karibu, Limebarikika Jina Lake na Umetukuka Ujalali Wake.” [Al-Bukhaariy]
[7] Amani Ya Dunia Na Ya Aakhirah Kwa Atakayefuata Mwongozo:
Yaani: Atakayefuata Njia Iliyonyooka, na akafuata Sharia iliyo wazi, basi atapata na amani ya dunia na ya Aakhirah. [Tafsiyr As-Sa’diy]
[8] Ardhi: Tumeumbwa Kutoka Humo, Na Humo Tutarudishwa, Na Kutoka Humo Tutafufuliwa:
Alipotaja manufaa makubwa ya ardhi, na kujibishana kwake vyema na mvua Anayoiteremsha Allaah (سبحانه وتعالى) juu yake, na kwamba ardhi hii kwa Idhini ya Rabb wake, inatoa mimea ya namna mbalimbali, Allaah Akasema kwamba Ametuumba kutokana nayo, na ndani yake humo Ataturudisha tutakapofariki na kuzikwa humo, na kutoka humo Atatutoa tena mara nyengine (kufufuliwa). Kadhalika, Yeye Ametuumba tukapatikana kutokana na ardhi baada ya kuwa hatupo, na hili tumelijua fika na tumelithibitisha. Hivyo basi, Ataturejesha kwa kutufufua kutoka humo baada ya sisi kufa ili Atulipe matendo yetu tuliyoyafanya juu ya mgongo wake. Na hizi ni dalili mbili za kiakili zilizo wazi juu ya kurejeshwa tena; kutoa mimea kutoka katika ardhi baada ya kufa kwake, na kuwatoa wenye kuhesabiwa (matendo) kutoka humo kama walivyokuwa mwanzo. [Tafsiyr As-Sa’diy]
[9] Al-Manna Na As-Salwaa: Rejea Al-Baqarah (2:57).
[10] Saamiriyyu Aliyewapotosha Watu Kumwabudu Ndama:
Aayah hii kuanzia namba (88) hadi (97), zinataja kuhusu mtu katika kaumu ya Nabiy Muwsaa (عليه السّلام), ambaye alikuwa ni mkaribu wake, aliyeitwa Saamiriyyu. Alikuwa ni mtu mwenye akili na ujuzi maalum. Lakini alikuwa mnafiki na alikuwa mjanja mno! Alijua udhaifu wa watu. Basi pindi Nabiy Muwsaa (عليه السّلام) alipokwenda katika miyqaat (mahali na muda maalumu pa miadi) ya kuzungumza na Allaah (سبحانه وتعالى); rejea Al-A’raaf (7:142-143), alitumia ujanja wake kuwapumbaza watu na kwa lengo la kuwapotosha.
Alikusanya dhahabu walizokuwa nazo watu wa Firawni. Akayayusha dhahabu na kuimimina katika chombo chenye ukina fulani kinachotumika kufinyanga na kutoa shepu au umbo fulani baada ya myayuko kupoa na kuwa mgumu. Na dhahabu ilipopoa, alipasua chombo hicho akatoka ndama wa dhahabu aliyevutia watu machoni. Akapuliza ndani ya uwazi wa ndama ukatoa sauti kama ya ndama. Alimuunda ndama huyo kwa siri, kisha akamtoa kwa ghafla mbele ya watu. Kisha akaeneza uvumi ionekane kana kwamba watu walikuwa wakifanya ibaada hiyo ya kuabudu ndama na kwamba ni ibaada ya kawaida iliyokubalika. Watu walitumbukia katika njia zake za ujanja, wakadanganyika, wakamwabudu ndama na hivyo kuingia katika shirki kubwa. Walisahau kabisa kwamba Nabiy Muwsaa (عليه السّلام) aliwajulisha kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Ndiye Pekee Apasaye kuabudiwa kwa haki. Rejea Aayah namba (97) kwenye maelezo kuhusu adhabu Aliyopewa na Allaah (سبحانه وتعالى) kwa kitendo chake hiki kiovu kabisa.
[11] Adhabu Ya Saamiriyyu Duniani: Hatoweza Kugusa Watu Na Watu Hawataweza Kumgusa:
Saamiriyyu: Rejea Aayah namba (85), ni mtu katika kaumu ya Nabiy Muwsaa (عليه السّلام) ambaye ndiye aliyewaamrisha watu wamwabudu ndama. Basi adhabu yake ikawa ni hiyo ya yeye kutokuweza kugusa au kuguswa. Imaam As-Sa’diy (رحمه الله) amesema: Yaani: Utaadhibiwa maishani, na hakuna wa kukukaribia, na hakuna wa kukugusa, mpaka anayetaka kukukaribia, utamwambia: “Usiniguse, na usinikaribie!” Hiyo ni adhabu kwa ajili ya hilo, kwa vile aligusa kitu ambacho hakupaswa mtu kukigusa (kwato za (farasi wa Jibriyl) na kufanya kile ambacho hakuna mtu mwingine alifanya. [Tafsiyr As-Sa’diy]
[12] Hakuna Atakayemiliki Ash-Shafaa’ah (Uombezi) Isipokuwa Kwa Idhini Ya Allaah:
Rejea Al-Baqarah (2:255), An-Najm (53:26). Rejea pia Al-Israa (17:79) ambako kumetajwa kuwa Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) ni Nabii Pekee atakayeruhusiwa ash-shafaa’ah atakapokuwa katika Maqaaman Mahmuwdan (Cheo Cha Kuhimidiwa).
[13] Jina Tukufu Kabisa La Allaah (Al-Hayyu Al-Qayyuwm) Limo Katika Aayah Hii:
Rejea Al-Baqarah (2:255), Aal-‘Imraan (3:2).
[14] Kujitenga Na Ukumbusho Ni Kupata Maisha Ya Dhiki:
Aayah hii na Aayah zinazofuata (124-127), zinahusiana na hayo ya mtu anayejitenga au anayepuuza Ukumbusho wa Allaah (سبحانه وتعالى) kwamba atakuwa na maisha ya dhiki: Imaam As-Sa’diy (رحمه الله) amefasiri Aayah hii:
Yaani: (Kupuuza au kujitenga nacho) Kitabu ambacho kinataja kila yanayoamrishwa na kuyaacha kwa kuyapuuza. Au kufanya lilokubwa zaidi, nalo ni kukanusha na kukufuru. Basi atapata maisha ya dhiki. Yaani malipo yake, ni kuyafanya maisha yake, yawe ya dhiki na mashaka. Basi hana anachokipata isipokuwa adhabu tu. Na pia maisha ya dhiki, yamefasiriwa kuwa ni adhabu ya kaburi, kwamba kaburi litakuwa la kumdhikisha na hivo kumbana kabisa na ataadhibika humo. Hayo ni malipo ya kupuuza au kujitenga na Ukumbusho wa Rabb wake. Na hii ni mojawapo ya Aayah zinazodulisha adhabu ya kaburi. Na ya pili ni Kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):
وَلَوْ تَرَىٰ إِذِ الظَّالِمُونَ فِي غَمَرَاتِ الْمَوْتِ وَالْمَلَائِكَةُ بَاسِطُو أَيْدِيهِمْ أَخْرِجُوا أَنفُسَكُمُ ۖ الْيَوْمَ تُجْزَوْنَ عَذَابَ الْهُونِ بِمَا كُنتُمْ تَقُولُونَ عَلَى اللَّـهِ غَيْرَ الْحَقِّ وَكُنتُمْ عَنْ آيَاتِهِ تَسْتَكْبِرُونَ ﴿٩٣﴾
“Na lau ungeliona madhalimu pale wakiwa katika mateso makali ya mauti (ungeona jambo la kutisha mno), na Malaika wamenyosha mikono yao (wakiwaambia): Toeni nafsi zenu! Leo mnalipwa adhabu ya kudhalilisha kwa yale mliyokuwa mkiyasema juu ya Allaah pasi na haki, na mlikuwa mkitakabari msizifuate Aayaat Zake.” [Al-An’aam (6:93)]
Na ya tatu ni Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):
وَلَنُذِيقَنَّهُم مِّنَ الْعَذَابِ الْأَدْنَىٰ دُونَ الْعَذَابِ الْأَكْبَرِ لَعَلَّهُمْ يَرْجِعُونَ ﴿٢١﴾
“Na bila shaka Tutawaonjesha adhabu ndogo kabla ya adhabu kubwa huenda wakarejea (kutubia).” [As-Sadjah (32:21)]
Na ya nne ni Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى) kuhusu watu wa Firawni:
النَّارُ يُعْرَضُونَ عَلَيْهَا غُدُوًّا وَعَشِيًّا ۖ وَيَوْمَ تَقُومُ السَّاعَةُ أَدْخِلُوا آلَ فِرْعَوْنَ أَشَدَّ الْعَذَابِ﴿٤٦﴾
“Wanadhihirishiwa moto asubuhi na jioni, na Siku itakayosimama Saa (itasemwa): Waingizeni watu wa Firawni katika adhabu kali kabisa.” [Ghaafir (40:46)]
Waliosema kuwa ni adhabu ya kaburi ni Salaf. Na Wafasiri wengineo wanaona kuwa maisha ya dhiki ni ya ujumla; maisha ya duniani yanayomsibu anayepuuza au anayejitenga na Ukumbusho wa Rabb wake kama ghamu (na huzuni), dhiki, na maumivu, ambayo ni adhabu za kutangulia. Na katika maisha ya Barzakh, na katika maisha ya Aakhira kwa ujumla, ni maisha ya dhiki, na wala si vinginevyo. [Tafsiyr As-Sa’diy]
[15] Kuamrisha Ahli Kuswali:
عن أبي هريرة رضي الله عنه عن النبي صلى اللّه عليه وسلم أنه قال: ((مُرُوا أَوْلادَكُمْ بِالصَّلاةِ وَهُمْ أَبْنَاءُ سَبْعِ سِنِينَ، وَاضْرِبُوهُمْ عَلَيْهَا وَهُمْ أَبْنَاءُ عَشْرٍ، وَفَرِّقُوا بَيْنَهُمْ فِي الْمَضَاجِعِ)) البخاري
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Amrisheni watoto wenu kuswali wakiwa na umri wa miaka saba, na wapigeni (pigo khafifu wakiwa hawataki kuswali) wakiwa na umri wa miaka kumi, na watenganisheni vitanda.”(kuwatenganisha wasichana na wavulana vyumbani) [Al-Bukhaariy]
وَعَنِ ابْنِ عُمَرَ أَنَّ أَبَاهُ عُمَرَ بْنَ الْخَطَّابِ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ كَانَ يُصَلِّي مِنَ اللَّيْلِ مَا شَاءَ اللَّهُ حَتَّى إِذَا كَانَ مِنْ آخِرِ اللَّيْلِ أَيْقَظَ أَهْلَهُ لِلصَّلَاةِ يَقُولُ لَهُمْ: الصَّلَاةُ ثُمَّ يَتْلُو هَذِهِ الْآيَةَ: (وَأْمُرْ أَهْلَكَ بِالصَّلَاةِ وَاصْطَبِرْ عَلَيْهَا لَا نَسْأَلُكَ رِزْقًا نَحن نرزقك وَالْعَاقبَة للتقوى)
Amesimulia Ibn ‘Umar kwamba baba yake ‘Umar bin Al-Khattwaab (رضي الله عنه) alikuwa akiswali usiku kiasi Anavyomwezesha Allaah, mpaka inapofika mwisho wa usiku, huamsha ahli wake kwa ajili ya Swalaah huku akiwaambia: Swalaah! Kisha husoma Aayah hii:
وَأْمُرْ أَهْلَكَ بِالصَّلَاةِ وَاصْطَبِرْ عَلَيْهَا ۖ لَا نَسْأَلُكَ رِزْقًا ۖ نَّحْنُ نَرْزُقُكَ ۗ وَالْعَاقِبَةُ لِلتَّقْوَىٰ ﴿١٣٢﴾
“Na amrisha ahli zako Swalaah, na dumisha uvumilivu juu ya mazito yake. Hatukukalifishi riziki bali Sisi Ndio Tunaokuruzuku. Na hatima njema ni kwa wenye taqwa.” [Twaahaa (20:132) – Imepokelewa na Imaam Maalik na ameisahihisha Al-Albaaniy]
Rejea pia At-Tahriym (66:6) kwenye faida nyenginezo.
[16] Suhuf (Maandiko Matukufu) Na Tofauti Baina Yake Na Vitabu Vinginevyo Vya Mbinguni: Rejea Al-A’laa (87:18-19).