Maulidi: Hoja Dhidi Ya Uzushi Wa Maulidi Na Watetezi Wake

 

Hoja Dhidi Ya Uzushi Wa Maulidi Na Watetezi Wake

 

Alhidaaya.com

 

 

 

️Abu Bakr (Radhwiya Allaahu 'anhu) alitawala kwa muda wa miaka miwili. Naye ni Mkweli (Asw-Swidiyq) wa Ummah na ni Swahibu wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika pango, na hakufanya sherehe za Mawlid!!

 

 

️'Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu) alitawala kwa muda wa miaka kumi. Naye ni Mtenganishi baina ya Haki na baatwil (Al-Faaruwq) wa Ummah na aliyekuwa mwenye msukumo wa Ummah, na hakufanya sherehe za Mawlid!

 

 

️'Uthmaan (Radhwiya Allaahu 'anhu) alitawala kwa muda wa miaka kumi na tatu. Naye ni mume wa Mabint wawili (wa Nabiy Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), na ndiye aliyefanya hijrah mbili, na ndiye aliyekuwa mwenye hayaa zaidi katika Ummah huu, na hakufanya sherehe za Mawlid!

 

 

️'Aliy (Radhwiya Allaahu 'anhu) alitawala kwa muda wa miaka minne. Naye ni binamu wa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), na ni mume wa (Faatwimah bint ya Nabiy) bibi wa wa wanawake wa Peponi, na hakufanya sherehe za Mawlid!

 

 

️Al-Hasan (Radhwiya Allaahu 'anhu) alitawala kwa muda wa miezi sita. Naye ni mjukuu wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na ni bwana wa vijana wa Peponi, na hakufanya sherehe za Mawlid!

 

 

️ Mu'aawiyyah (Radhwiya Allaahu 'anhu) naye alitawala na hakufanya sherehe ya Mawlid. Naye alikuwa mbora katika Wafalme wa Kiislamu.

 

 

️ Ikaja Dola ya Al-Umawiyyah ikatawala na ndani yake alikuwepo Kiongozi mwadilifu 'Umar bin 'Abdil-'Aziyz (Rahimahu Allaah). Na ukaja utawala wa Dola ya Al-'Abbaasiyyah na ndani yake alikuwa Kiongozi bora Haaruwn Ar-Rashiyd (Rahimahu Allaah) na wote hao hawakufanya sherehe ya Mawlid!

 

 

️ Na Wanachuoni Ma-Imaam wanne wakubwa, Abu Haniyfah, Maalik, Ash-Shaafi'iy, Ahmad bin Hanbal (Rahimahum Allaah), wote hao hawakufanya sherehe ya Mawlid!!

 

 

️ 'Ulamaa wakubwa wa Haki wa Uislamu, na Wapenzi wakweli wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), wote hawakusherehekea Mawlid katika kipindi chote cha zile Karne bora zilizosifiwa, pamoja na kuwa walikuwa na ufahamu wa kina wa yale Aliyoyateremsha Allaah, na pamoja na ukubwa wa elimu yao ya shariy'ah katika Kitabu cha Allaah, na kwanini wasiwe hivyo ilhali wao ni wabebaji wa Qur-aan na wapokezi wa Athaar? Lakini pamoja na utukufu wao wote, hawakufanya sherehe ya Mawlid!!

 

 

️ Nasi twasema: "Kama hiyo sherehe ya Mawlid ni jambo zuri, basi wangetutangulia wote hao watukufu na watu bora katika Ummah huu tuliowataja huko juu.!!

 

 

️ Na tunasema kama alivyosema Imaam Maalik (Rahimahu Allaah):

"Kile ambacho hakikuwa ni Dini wakati ule (wa Mtume swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), basi hakiwezi kuwa Dini leo."

 

 

️ Na kinachofahamika kikamilifu, ni kwamba, hakuondoka Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuelekea katika maisha ya Aakhirah, isipokuwa Allaah Alimkamilishia Dini yake na Akazitimizia neema juu yake!

 

 

️ Na alituonya katika Sunnah zake, tusizue mambo katika Dini, na kufanya mambo ambayo hakuyafanya yeye wala Maswahaba zake!

 

 

️ Na tambua, Allaah Akurehemu, kuwa hizo Karne bora zilizotangulia zote hazikuwa zinajua kitu kiitwacho Sherehe za Mawlid!! Bali hilo ni jambo la kuzushwa ambalo lilizushwa na Al-Faatwimiyyuwn (Mashia) wakiongozwa na mtu aliyejiita Mu'izzud-Diyn, naye hakuwa Mtia nguvu na utukufu Dini kama alivyojiita, bali alikuwa Mdhoofishaji na Mdhalilishaji wa Dini!!

 

 

️ Kwenye utawala wa Mshia huyo, kulikuwa na ukafiri wa wazi, na ufasiq usiojificha, ambapo alihalalisha pombe, na akahalalisha ufuska, na akatangaza kujiweka mbali na wema waliotangulia kwa kuwatukana na kuwakufurisha Maswahaba juu ya Minbari. Mtu huyo mwovu ndiye aliyezua na kuanzisha Mawlid na akayafanya hayo Mawlid kuwa sita: Mawlid ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), Mawlid ya Faatwimah, Mawlid ya 'Aliy, Mawlid ya Al-Hasan na Mawlid ya Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhum), na Mawlid ya kwake mwenyewe!!

 

 

️ Kisha wakafuatia wajinga miongoni mwa Waislamu na kuwaiga hao Mashia (Al-Faatwimiyyuwn) katika uzushi huo. Na tambua wazi kuwa hakuna katika hao wanaosherehekea Mawlid, dalili zozote za kujuzisha jambo hilo, bali hutoa maandiko ambayo hayana mahusiano wala mafungamano yoyote, bali ni katika kutapatapa ili kuhalalisha wasionekane wanafanya kibubusa! Hoja zao na dalili zao wamezifahamu kinyumenyume na kupindua maandiko na kutumia hoja zisizothibiti na dhaifu. Hata hivyo, Wanachuoni wengi wamebainisha uzushi huo kwa kutoa Fataawa nyingi za kubatilisha uzushi huo.

 

 

️ Nasi tukiwauliza hao wenye kusherehekea, maswali matatu tu ambayo hawawezi kupata majibu yake:

 

 

1- Je, kufanya hizo sherehe za Mawlid ni Utiifu au Maasi?

 

Bila shaka watasema ni Utiifu, kwani wakisema kuwa ni Maasi, basi mjadala utakuwa umeshakwisha.

 

 

2- Ikiwa watasema ni Utiifu na kuna malipo juu yake, je, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliujua Utiifu huo au haukumpitikia?

 

Wakidai kuwa, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakuu jua na alipitikiwa na Utiifu huo (wa kusherehekea Mawlid na thawabu zinazodaiwa kupatikana ndani yake), basi ole wao, watakuwa wamemtuhumu Mwalimu Mkuu kuwa alikuwa mjinga na hajui!! Na huo ni Uzandiki mkubwa wa wazi!!

 

Na wakidai kuwa, alikuwa akijua huo Utiifu, basi hapo tutahamia kwenye swali la tatu, nalo ni:

 

 

3- Ikiwa watadai Mawlid ni Utiifu (katika kumtii Allaah na kuna malipo kwa hilo), na ikiwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alijua hilo, basi swali linakuja... je, yeye alilifikisha jambo hilo kwa Ummah wake?

 

Wakisema kuwa hajalifikisha kwa Ummah wake, basi huu utakuwa ni upeo wa uovu wa madai yao na ni kumtuhumu Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa kaficha jambo katika Ujumbe aliokabidhiwa atufikishie!! Ilhali katika Qur-aan, Allaah Anasema:

 

يَا أَيُّهَا الرَّسُولُ بَلِّغْ مَا أُنزِلَ إِلَيْكَ مِن رَّبِّكَ ۖ وَإِن لَّمْ تَفْعَلْ فَمَا بَلَّغْتَ رِسَالَتَهُ ۚ وَاللَّـهُ يَعْصِمُكَ مِنَ النَّاسِ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الْكَافِرِينَ﴿٦٧﴾

"Ee Rasuli! Balighisha yale yaliyoteremshwa kwako kutoka kwa Rabb (Mola) wako. Na usipofanya, basi utakuwa hukubalighisha ujumbe Wake." (al-Maaidah: 67)

 

Na wakisema alifikisha kwa Ummah wake hiyo khabari ya kusherehekea Mawlid, tutawambia, leteni dalili, na yako wapi matendo ya wema waliotangulia kuhusu hilo?

 

Na je, jambo hilo liliwafichikia Maswahaba, Matabiy'iyn na waliowafuata hao na wema wote waliotangulia wa Karne zilizo bora hadi ije kuwadhihirikia waliokuja baadae sana hao Mashia wa ki-Faatwimiyyiyn walionajisika?!

 

Na ikiwa ndio hivyo, basi sisi tunathibitisha kabisa kuwa hili ni jambo la bid'ah lilizozushwa na ndani yake kuna Maovu makubwa kwa madogo, na yote haya ni kwa madai kuwa watu wanasherehekea Mawlid!

 

 

Na Allaah Ndiye Mwenye Kutakwa Msaada!

 

 

 

Share