Maulidi: Hoja Za Wanaosherehekea Maulidi Na Majibu Yake

 

Alhidaaya.com

 

 

Zifuatazo ni hoja za watetezi wa mawlid na majibu yake.

 

1-Hoja Ya Kwanza Ya Watetezi Wa Mawlid: 

Aayah katika Suwrah Yuwnus:

قُلْ بِفَضْلِ اللّهِ وَبِرَحْمَتِهِ فَبِذَلِكَ فَلْيَفْرَحُواْ هُوَ خَيْرٌ مِّمَّا يَجْمَعُونَ

Sema: Kwa fadhila za Allaah na kwa rahmah Yake basi kwa hayo wafurahi. Hayo ni khayr kuliko wanayoyakusanya. [Yuwnus: 58] 

 

Jibu La Hoja Ya Kwanza La Watetezi Wa Mawlid:

Baadhi ya watetezi wa mawlid wanatoa hoja ya Aayah hii kuwa kauli ya  Allaah  (Subhaanahu wa Ta'aalaa) wafurahi, basi ni kufurahia mazazi ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) . Lakini tukitazama tafsiri ya Aayah hiyo kwa wafasiri wote wakubwa kama Ibnu Jariyr, Ibnu Kathiyr, Qurtubiy, Al-Baghaawiy, Ibnul-Arabiy na wengineo, hatukuti maana hiyo kabisa. Maana iliyotajwa na wafasiri ni wafurahi kwa yale yaliyowajia kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ya Uongofu na Dini ya haki. Na pia imefasiriwa kuwa, wafurahi kwa Qur-aan na Uislam, na imethibitisha haya  Aayah ya kabla yake inayosema:

 

يَا أَيُّهَا النَّاسُ قَدْ جَاءتْكُم مَّوْعِظَةٌ مِّن رَّبِّكُمْ وَشِفَاء لِّمَا فِي الصُّدُورِ وَهُدًى وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ

Enyi watu! Kwa yakini yamekujieni mawaidha kutoka kwa Rabb wenu, na shifaa ya yale yaliyomo vifuani, na mwongozo na rahmah kwa Waumini.[Yuwnus: 57]

 

Nayo ni Qur-aan. Na kama pia Aayah ya 170 ya Suwrah Aal 'Imraan isemayo, ((Na ni wenye kufurahia fadhila Zake)). Vilevile imefasiriwa kuwa fadhila Zake ni Uislaam, na Rahma Zake ni Qur-aan.

 

Amesema Ibnu Kathiyr katika tafsiyr yake kuhusu: ((uongofu na Rahma kwa Waumini)), ni kupata uongofu na Rahma kwa waumini waliosadiki na kukinaika. Kama zinavyoonyesha kauli Zake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) nyingine:

وَنُنَزِّلُ مِنَ الْقُرْآنِ مَا هُوَ شِفَاءٌ وَرَحْمَةٌ لِلْمُؤْمِنِينَ وَلا يَزِيدُ الظَّالِمِينَ إِلَّا خَسَاراً﴿٨٢﴾ 

Na Tunateremsha katika Qur-aan ambayo ni shifaa na rahmah kwa Waumini; na wala haiwazidishii madhalimu isipokuwa khasara.[Al-Israa: 82]

 

Na kauli Yake Allaah :Subhaanahu wa Ta'aalaa

قُلْ هُوَ لِلَّذِينَ آمَنُوا هُدىً وَشِفَاء

Sema: Hiyo ni kwa walioamini ni mwongozo na shifaa. [Fuswilat: 44]

 

Ama kuhusu Rahma kwa watu;  haiwi kwa mazazi ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) bali ni kwa kupewa kwake Utume na kutumwa kufikisha ujumbe kwa watu. Na dalili ni kutoka katika Qur-aan na Sunnah.

 

Dalili kutoka katika Qur-aan ni kwamba yeye ni Rahma kwa viumbe wote kutokana na kutumwa kwake na wala haikutaja kuzaliwa kwake. Anasema Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa: 

وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا رَحْمَةً لِلْعَالَمِينَ﴿١٠٧﴾

Na Hatukukutuma (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) isipokuwa ni rahmah kwa walimwengu. [Al-Anibyaa:107]

 

Na katika Sunnah ni Hadiyth:

عن أبي هريرة رضي الله عنه   قال: قيل : يا رسول الله ! ادع على المشركين . قال صلى الله عليه وسلم  (( إني لم أبعث لعانا  وإنما بعثت رحمة)) مسلم  

Kutoka kwa Abu Hurayrah Radhwiya Allaahu 'anhu ambaye amesema: Aliambiwa Nabiy(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) "Waombee (walaaniwe) Washirikina". Akasema Nabiy Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam ((Mimi sikupewa utume (sikutumwa kuja kuwa) ni mlaaniji (mwenye kuwaombea laana watu) bali nimepewa utume kuwa ni Rahma)) [Muslim]

 

2-Hoja Ya Pili Ya Watetezi Wa Mawlid: 

Aayah katika Suwrah Al-Ahzaab kwamba mawlid yanahusiana na kumswalia:

 

إِنَّ اللَّهَ وَمَلائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى النَّبِيِّ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ وَسَلِّمُوا تَسْلِيماً﴿٥٦﴾

Hakika Allaah na Malaika Wake wanamswalia Nabiy. Enyi walioamini mswalieni na msalimieni kwa mamkizi ya amani na kwa tasliymaa. [Al-Ahzaab: 56]

 

Jibu La Hoja Ya Pili La Watetezi Wa Mawlid:

Imaam Al-Bukhaariy anatuelezea tafsiri ya Aayah hiyo ni kuwa Swahaba Radhwiya Allaahu 'anhu walimuuliza Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa wamefahamu namna ya kumtakia amani juu yake, lakini hawafahamu jinsi ya kuswalia. Nabiy( Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia waseme, 'Allahumma Swalli 'alaa Muhammad wa 'ala aali Muhammad...' hadi mwisho kama ilivyo kwenye tashahhud ya Swalaah.

 

Na maana au tafsiri ya Aayah hiyo imeelezwa na wafasiri wa Qur-aan ambao wamenukuu Hadiyth yenye kufafanua hivyo.

  

Pia kumswali Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) si kwa mara moja kwa mwaka bali inatupasa tumsawalie kwa wingi kila mara kama ilivyothibiti fadhila zake katika Hadiyth ifuatayo:

 

عنْ عبد اللَّه بن عمرو بن العاص ، رضي اللَّه عنْهُمَا أنَّهُ سمِع رسُول اللَّه صَلّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّم يقُولُ : ((من صلَّى عليَّ صلاَةً ، صلَّى اللَّه علَيّهِ بِهَا عشْراً))   رواهُ مسلم

Imetoka kwa 'Abdullah ibn 'Amru ibn Al-'Aasw Radhwiya Allaahu 'anhumaa kwamba kamsikia Nabiy Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam anasema, ((Atakayeniswalia (kuniombea Rahma na amani) mara moja, Allaah Atamteremshia Rahma mara kumi)) [Muslim]

 

Pia Nabiy Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam ametufundishia nyakati kadhaa za kumswalia kama vile siku ya Ijumaa, baada ya adhaan, anapotajwa n.k wala hakuna dalili kwamba tumswalie siku ya kuzaliwa kwake

 

 3-Hoja Ya Tatu ya Watetezi Wa Mawlid:

Kufurahikia kuzaliwa kwa Nabiy Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam  ni jambo lililoamrishwa katika Qur-aan wakitaja Aayah mbili zifuatazo zinazohusiana na Nabiy Yahya 'Alayhis-sallam na Nabiy 'Iysa  : 'Alayhis-sallam.

 

وَسَلَامٌ عَلَيْهِ يَوْمَ وُلِدَ وَيَوْمَ يَمُوتُ وَيَوْمَ يُبْعَثُ حَيًّا﴿١٥﴾

Na amani iwe juu yake siku aliyozaliwa, na siku atakayokufa na siku atakayofufuliwa kuwa hai. [Maryam: 15] Akimaanishwa Yahya 'Alayhis-sallam. 

 

((وَالسَّلَامُ عَلَيَّ يَوْمَ وُلِدتُّ وَيَوْمَ أَمُوتُ وَيَوْمَ أُبْعَثُ حَيًّا﴿٣٣﴾

Na amani iwe juu yangu siku niliyozaliwa, na siku nitakayokufa na siku nitakayofufuliwa kuwa hai. [Maryam: 33] Akimaanishwa 'Iysa 'Alayhis-sallam.  

 

Jibu la hoja ya tatu la watetezi wa mawlid:

Aayah inasema ((amani...)). Je, ina maana kwamba, neno 'amani' ni sawa na kufurahikia? Vile vile Aayah hizo hazikutaja kuhusu mazazi  pekee bali zimetaja; kuzaliwa, kufa na kufufuliwa. Sasa vipi ichukuliwe kuzaliwa pekee bila ya kufariki au kufufliwa? Wanavyuoni wamekubaliana kwamba tarehe hiyo ya 12 Rabiy'ul Awwal inayodaiwa kuwa kazaliwa, ndio tarehe ya kufariki kwake. Lakini hakuna uhakika wa tarehe ya kuzaliwa kwake kwa sababu watu walikuwa wakihesabu tukio kutokana na matukio fulani, na kuzaliwa kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kulijulikana kuwa kazaliwa ‘aamul-fiyl (mwaka wa tukio la tembo) haikutajwa tarehe yake.      

 

4-Hoja Ya Nne Ya Wa Watetezi Wa Mawlid:

Kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akifunga siku ya Jumatatu ambayo ilikuwa siku ya kuzaliwa kwake kama ilivyotajwa katika Hadiyth ifuatayo, na hivyo basi aliiadhimisha siku ya kuzaliwa kwake:

 

عن أبي قتادة رضي الله عنه : أن النبي صلى الله عليه وسلم سئل عن صوم يوم الاثنين فقال: ((ذلك يوم ولدت فيه وأنزل علي فيه))  رواه الإمام مسلم

Imetoka kwa Abu Qataadah Radhwiya Allaahu 'anhu kwamba aliulizwa Nabiy Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam kuhusu kufunga Jumatatu akasema: ((Hiyo ni siku niliyozaliwa na siku ulioteremshwa kwangu [Utume])) [Imaam Muslim]

 

Jibu la hoja ya nne la watetezi wa mawlid:

Kuiadhimisha siku kuzaliwa kwake Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  ilikuwa kwa niyyah ya kumshukuru Allaah ndipo akawa anafanya ibada hiyo ya kufunga na wala hakusherehekea hata siku moja mawlid.  

 

Pia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakufunga siku maalum katika mwezi huu wa Rabiy'ul Awwal. Hakufunga tarehe 12 wala siku yoyote ile isipokuwa siku za Sunnah zinazojulikana Jumatatu na Alkhamiys pamoja na masiku meupe ambayo alifunga kila mwezi.     

 

5-Hoja Ya Tano Ya Watetezi Wa Mawlid:

Kwamba Swahaba walimpokea Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alipoingia Madiynah kwa qaswiydah na wengine walikuwa wakimsomea mashairi na qaswiydah za kumsifu na yeye alikuwa akikubali kusomewa hayo mashairi.

 

Jibu la hoja ya tano la watetezi wa mawlid:

Wanavyoni wametaja kwamba hakuna dalili ya kusomewa qaswiydah ya kupokelewa alipoingia Madiynah ambayo inataja: “Twala'al-badru 'alaynaa, min thaniyaatil wadaa'”.  Historia za kuaminika hazikutaja kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipita njia hiyo ya Thaniyaat al wadaa' wakati wa kuelekea Madiynah.

Pia haikuthibitika kwamba Swahaba walikuwa wakimsomea mashairi na qaswyidah siku ya kuzaliwa kwake, bali ilikuwa zaidi kunapotokea ushindi wa vita dhidi ya maadui.

 

6-Hoja Ya Sita Ya Watetezi Wa Mawlid:

Kwamba kusherehekea Mawlid ni kumpenda, kumuadhimisha, kumtukuza na ni kumbukumbu ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa walimwengu na kwamba inatupasa tufanye hivyo ili vizazi vyetu pia vipate kumtambua Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)

 

Jibu la hoja ya sita la watetezi wa mawlid:

Kumkumbuka na kumuadhimisha Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  kunatupasa kila siku katika maisha yetu kwa kumpenda na kufuata Sunnah zake, wala si kwa mara moja tu kwa mwaka.

 

Pia kumbukumbu ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alyahi wa aalihi wa sallam)  kwa walimwengu na vizazi vyetu zimeshabainishiwa na Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa katika Qur-aan na Sunnah nazo kwa kila siku; Anasema Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa 

وَرَفَعْنَا لَكَ ذِكْرَكَ﴿٤﴾

Na Tukakutukuzia kutajwa kwako? [Ash-Sharh:4]

 

Na kutukuzwa huko ni katika Swalah zetu tunapomswalia katika tashahhud, katika kutimiza Hajj na Swawm,  katika adhaan na iqaamah za Swalah, kwenye khutba, kumswalia anapotajwa jina lake, katika du’aa, tunaposoma au kusikia Hadiyth zake, katika kufuata Sunnah zake, katika vikao vya darsa na kadhalika, kwa hiyo ni kumbukumbu ya kila siku, kila wakati katika maisha yetu na sio siku moja tu kwa mwaka. 

 

7-Hoja Ya Saba Ya Watetezi Wa Mawlid:

Kwamba kuna bid'atun-hasanah (bid'ah nzuri).

Jibu la hoja ya saba la watetezi wa mawlid:

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alipotaja kuhusu bid'ah amesema:

 

((....وإِيَّاكُمْ ومُحْدثَاتِ الأُمُورِ فَإِنَّ كُلَّ بِدْعَةٍ ضلالَةٌ ))  رواه أبو داود ، والترمذِي وقال حديث حسن صحيح

((…na tahadharini na mambo ya uzushi kwani kila bid'ah ni upotofu)) [Abu Daawuud, At-Trimidhiy kasema Hadiyth hasan sahiyh]

 

Imetajwa:  'Kullu bid'atin dhwalaalah' (KILA bid'ah ni upotofu). Na ikiwa kauli hii wanaipinga kuwa si KILA bid'ah, basi wanasemaje kuhusu kauli za Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa Anaposema:

كُلُّ نَفْسٍ ذَآئِقَةُ الْمَوْتِ

Kila nafsi itaonja mauti. [Aal-'Imraan: 185]

 

 وَكُلَّ إِنسَانٍ أَلْزَمْنَاهُ طَآئِرَهُ فِي عُنُقِهِ وَنُخْرِجُ لَهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ كِتَابًا يَلْقَاهُ مَنشُورًا﴿١٣﴾ 

Na kila bin Aadam Tumemuambatanishia majaaliwa ya ‘amali zake shingoni mwake. Na Tutamtolea Siku ya Qiyaamah kitabu akutane nacho kimekunjuliwa. [Al-Israa:13]

 

Na,

 

كُلُّ نَفْسٍ بِمَا كَسَبَتْ رَهِينَةٌ﴿٣٨﴾

Kila nafsi iko katika rehani kwa yale iliyoyachuma. [Al-Mudathhir:38]

 

Na

كُلُّ شَيْءٍ فَعَلُوهُ فِي الزُّبُرِ ﴿٥٢﴾وَكُلُّ صَغِيرٍ وَكَبِيرٍ مُّسْتَطَرٌ ﴿٥٣﴾

Na kila kitu wakifanyacho kimo katika madaftari yanayorekodi. Na kila kidogo na kikubwa kimeandikwa.  [Al-Qamar:52-53]

 

Je, tutakanusha kwamba sio kila nafsi itaonja mauti? Au si kila mtu amefungiwa amali zake shingoni? Au si kila nafsi iko rahanini? Au si kila jambo tunalolifanya dogo na kubwa liko vitabuni? Bila shaka kauli ya Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa Inathibitisha kuwa kila binaadamu atakufa na kila mmoja ana hesabu yake atakayoikuta siku ya Qiyaamah. Kwa hiyo kauli ya 'kullu bid'atin dhwalaalah' (kila bid'ah ni upotofu) pia ina maana hiyo hiyo bila yakuwekwa “isipokuwa” (mawlid ni bid’ah hasanah).  

 

8-Hoja Ya Nane Ya Watetezi Wa Mawlid:  

Kwamba kuna baadhi ya mambo yamefanyika baada ya kufa kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na mengineyo yanaendelea kutendeka kwa hiyo ni bid'ah. Miongoni mwao ni; kukusanywa Qur-aan na kuwekwa katika Mswahafu na Abu Bakar Radhwiya Allaahu 'anhu kisha baadaye kuwekwa harakaat (vokali) katika Mswahafu. Pia 'Umar ibnul Khatwaab Radhwiya Allaahu 'anhu kuihamishwa Maqaam Ibrahiym kuwa mbali kidogo na Al-Ka’bah.  Pia kuongezwa adhaan ya pili na ya tatu siku ya Ijumaa na 'Uthmaan bin 'Affaan Radhwiya Allaahu 'anhu. Pia Swahaba hawakutumia kipaza sauti katika adhaan, au hawakufanya twawaaf juu katika ghorofa za Masjid Al-Haram, au hawakupanda magari bali walipanda ngamia, au hapakuweko na zana za utamaduni za kujifunza Dini kama radio, televisheni, mitandao, CD's na kadhalika. Kwa hiyo kutumia vitu hivyo pia ni bid'ah. 

 

Jibu La Hoja Ya Nane La Watetezi Wa Mawlid:

Kufuata waliyoyatenda Makhalifa hao watukufu, basi ni jambo aloamrisha Nabiy Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam ambaye amesema:

 ((... أُوصِيكُمْ بِتَقْوى اللَّه، وَالسَّمْعِ وَالطَّاعَةِ وإِنْ تَأَمَّر عَلَيْكُمْ عَبْدٌ حبشيٌ، وَأَنَّهُ مَنْ يَعِشْ مِنْكُمْ فَسَيرى اخْتِلافاً كثِيرا . فَعَلَيْكُمْ بسُنَّتي وَسُنَّةِ الْخُلُفَاءِ الرَّاشِدِينَ الْمَهْدِيِّينَ ، عضُّوا عَلَيْهَا بالنَّواجِذِ، وإِيَّاكُمْ ومُحْدثَاتِ الأُمُورِ فَإِنَّ كُلَّ بِدْعَةٍ ضلالَةٌ)  رواه أبو داود ، والترمذِي وقال حديث حسن صحيح

((Nakuusieni kumcha Allaah, usikivu na twaa hata ikiwa kiongozi wenu (Au atakayekuamrisheni) ni Mtumwa wa Kihabashi. Mtakaoishi miongoni mwenu mtaona ikhtilafu nyingi. Kwa hiyo shikamaneni na Sunnah zangu na Sunnah za Makhalifa waliongoka baada yangu. Ziumeni kwa magego (zikamateni kwa nguvu wala msiziache). Na tahadharini na mambo ya uzushi kwani kila bid'ah ni upotofu) [Abu Daawuud, At-Trimidhiy kasema Hadiyth hasan sahiyh] 

 

Na kukusanywa Qur-aan katika Mswahafu ilikuwa kwa sababu hapo awali Qur-aan ilihifadhiwa katika vifua vya Swahaba. Ikatokea haja ya kuikusanya Qur-aan katika Mswahafu kwa vile Swahaba wengi waliohifadhi Qur-aan waliuliwa katika vita vya Yamaamah, Swahaba wakaingiwa na hofu kwamba Qur-aan itakujwa kupotea na haitawafikia vizazi vya mbele. Ndipo ilipokusanywa baada ya ushauri mzito baina ya Makhalifa na Maswahaba. Kisha baada ya hapo ikaja kuwekewa harakaat kwa sababu kulihofiwa kwamba Qur-aan itakuja kusomwa kimakosa kwa vile lugha ya Kiarabu ilianza kupotea ufasaha wake, na si wepesi kuisoma lugha ya kiarabu bila ya harakaat kwa wasio na ujuzi wa hali ya juu wa lugha ya Kiarabu.  Likawa ni jambo lisilokuwa na budi kutendwa kwa sababu Qur-aan ni Mwongozo kwa walimwengu.

 

Kuhusu kufanya twawaaf ghorofani pia ni jambo lisilokuwa na budi ili ‘ibaadah hiyo ya muhimu kabisa itimizwe. Haiingii akilini kwamba watu wote waweze kufanya twawaaf ardhini kwa sababu ya msongamano wa Waislamu hapo.

 

Ama kuhusu vipaza sauti, njia za usafirishaji, vifaa vya utamaduni vya kujifunzia na kadhalika, vyote hivyo ni nyenzo tu za kuwepesisha kutekeleza ibada zetu. Kuchanganya nyenzo na ibada ni jambo lilisilokuwa la mantiki. Na Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa Mjuzi wa ghaibu, Amejua kuwa hali za Waislamu zitafikia kuhitajika hayo. Mfano kuhusu usafiri wa watu baina ya nchi kufika Makkah kutimiza Hajj, iwezekanaje usafiri kwa ngamia?  

 

Kwa hiyo panapotokea jambo linalohitajika kuwepesisha ibada zetu, Wanavyuoni hufutu jambo ambalo halina budi kutendwa kwa ajili ya manufaa ya Ummah. Na Allaah Anajua zaidi.

 اللَّهُمَّ  اَرِنا الْحَقَّ حَقاً وَارْزُقْنا اتِباعَه وَارِنا الباطِلَ باطلاً وَارْزُقْنا اجْتِنابه

Allaahumma Arinal-Haqqa Haqqaw-War-Zuqnat-tibaa'ah, Wa Arinal-Baatwila Baatwilaw-War-Zuqnaj-tinaabah.

 

Ee Allaah, Tuonyeshe haki kuwa ni haki Na Uturuzuku kuifuata. Na Tuonyeshe batili kuwa ni batili na Uturuzuku kuiepuka.

 

 

Share