Sha'baan: Fadhila Zake Na Uzushi Wa Niswfu Sha'abaan

 

 

Sha'baan - Fadhila Zake Na Uzushi Wa Niswfu Sha'baan

 

Abuu 'Abdillaah

 

Alhidaaya.com

 

 

 

BismiLLaah Wal-HamduliLLaah Waswalaatu Wassalaamu ‘alaa RasuuliLLaah, wa ba'ad

 

 

Mwezi wa Sha’baan ni mwezi wa nane katika kalenda ya Kiislam. Na ni mwezi ambao upo katikati ya miezi miwili mitukufu; Rajab na Ramadhwaan. Mambo ya kuzingatia katika mwezi huu ni kuweza kupambanua yaliyo sahihi na yaliyozushwa, kwani ingawa kuna fadhila zake mwezi huu lakini pia mengi yaliyoenea na yanayofanywa na watu, ni ya Upotofu.

 

 

Ni mwezi ambao Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akifunga sana Swawm za Sunnah kama ilivyothibiti katika Hadiyth ifuatayo kutoka kwa Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa):

 

 " كان رسول الله صلى الله عليه وآله وسلم  يصوم حتى نقول لا يفطر، ويفطر حتى نقول لا يصوم، وما رأيت رسول الله استكمل صيام شهر إلا رمضان وما رأيته أكثر صياماً منه في شعبان"    رواه البخاري ومسلم

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akifunga hadi tukadhani kuwa hatofungua kamwe, na alikuwa akiacha kufunga hadi tukadhani hatofunga tena. Sijamuona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akifunga mwezi mzima kama alivyokuwa akifunga Ramadhwaan, na sijamuona akifunga mara nyingi kama alivyofunga katika Sha’baan.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Swawm Na Fadhila Za Mwezi Wa Sha’baan

 

Juu ya kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akifunga mara nyingi zaidi katika mwezi wa Sha’baan kuliko miezi mingine ukiondosha Ramadhwaan, kama ambao unafungwa wote, hakuwahi hata mara moja kuufunga mwezi mzima wa Sha’baan. Na ni jambo ambalo lenye kuchukiza kufanya hivyo kama wanavyotueleza ‘Ulamaa kama kina Ibnul Mubaarak na wengi wengine, pia Swahaba Mtukufu Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) anasema ni makruwh (inachukiza) kufunga mwezi mzima wa Sha’baan kwani Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakufanya hivyo.

 

Imepokewa kuwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allahau ‘anhumaa) amesema: ‘‘Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwahi kufunga mwezi wowote kikamilifu isipokuwa Ramadhwaan. [Al-Bukhaariy]

 

 

Kukithirisha kwake Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ‘ibaadah katika mwezi huu wa Sha’baan, ni kutokana na maelezo yake mwenyewe alipoulizwa na Usaamah bin Zayd (Radhwiya Allaahu ‘anhu) sababu ya kufunga sana katika mwezi huu alijibu:

 

 ((ذاك شهر تغفل الناس فيه عنه، بين رجب ورمضان، وهو شهر ترفع فيه الأعمال إلى رب العالمين، وأحب أن يرفع عملي وأنا صائم))

“[Sha’baan] Huo ni mwezi ambao watu hawautilii sana maanani, ulio kati (ya miezi miwili mitakatifu) Rajab na Ramadhwaan, na ni mwezi ambao matendo yanapandishwa kwa Rabb wa ulimwengu. Nami napenda matendo yangu yapandishwe na hali nikiwa nimefunga” [An Nasaaiy, at-Targhiyb wat-Tarhiyb, uk. 425].

 

 

Hadiyth hii na Hadiyth nyengine za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) zinahimiza kufanya ‘amali njema pale watu wanapoghafilika na kumdhukuru Allaah kwa ‘ibaadah, kama kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika sehemu za masoko, maduka na biashara zingine, ambapo watu wameshughulishwa na biashara zao na pia katika nyakati za matatizo.  

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Ibaadah wakati wa matatizo (fitnah) ni kama uhamiaji (hijrah) kwangu.” [Muslim] 

 

 

Faida na ubora wa kumwabudu Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) wakati watu wameghafilika kutokana na kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) zimekuja kwa sababu ‘Ibaadah katika nyakati kama hizo ni ngumu zaidi kuliko kumwabudu Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) wakati kila mtu amefungamana na ‘Ibaadah.                    

 

Swawm katika mwezi wa Sha’baan ni mazoezi kabla ya Ramadhwaan. Hata hivyo, kufunga mwezi mzima wa Sha’baan ni makruwh (hakupendezi) na ni kinyume na Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

  

Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) amesema: “Msiutangulie Ramadhwaan kwa (Swawm) siku moja au mbili, ila kwa wale tu wenye mazoea ya Swawm kila mara, na kwa hali hiyo hao wanaweza kufunga (siku hizo)” [Al-Bukhaariy]

 

 

Pia imekatazwa Swawm katika mwisho wa Sha’baan kwa nia ya kutozikosa siku za mwanzo wa Ramadhwaan, isipokuwa kwa wale wenye tabia na mpangilio wa Swiyaam na ikawa siku za mwisho za Sha’baan zimetokezea sambamba na siku ambazo mtu yule kawaida huwa anafunga, kama vile za Jumatatu na Alkhamiys au imemkuta akiwa anaendelea kulipa Swawm ya deni.

 

Imeripotiwa katika Swahiyh Al-Bukhaariy kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Swawm katika mwisho wa Sha'baan kumekatazwa ili kuweka tofauti kati ya Swawm za Sunnah na Swawm za faradhi.”

 

Vile vile ni kinga ya kuwakinga watu na kuanguka katika mtego wa shaytwaan, ambaye amewashawishi Ahlul-Kitaab (Waliopewa Vitabu) kuongeza Swawm zaidi ya zile Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alizowafaradhishia. Kwa sababu hiyo hiyo, imekatazwa pia Swawm siku ya ‘Yawmu Shakk”. Siku ya shaka ni ile siku ambayo watu hawana uhakika juu ya kuanza kwa Ramadhwaan, kwa sababu ya hali ya mawingu kutokuwa safi na mwezi kutoonekana au sababu nyinginezo.

 

Na Imaam Ibn Rajab (Rahimahu Allaah) amesema: ''Swawm katika Sha’baan ni bora kuliko Swawm katika masiku matakatifu (ambayo ni Dhul Qa'dah, Dhul-Hijjah, Muharram na Rajab zilizotajwa katika Suwrah At-Tawbah Aayah ya 36), na Swawm zilizo bora ni zile (zitambulikazo) ambazo ziko karibu na Ramadhwaan, kabla au baada. Hadhi na daraja ya Swawm hizi ni kama ya zile za Swalaah za Sunnah za Rawaatib, ambazo huswaliwa kabla na baada ya Swalaah za fardhi na ambazo huwa ni vijazilio vya upungufu wa zile Swalaah za fardhi. Na hali kama hiyo ndiyo ile ile ya Swawm zitambulikazo ambazo huwa kabla na baada ya Ramadhwaan, Kama ambavyo Swalaah za Sunnah za Rawaatib zilivyo bora kuliko Swalaah zingine za kujitolea (za Sunnah), na hivyo ndivyo Swawm zitambulikazo (zilizo katika miezi) ya kabla na baada ya Ramadhwaan zilivyo bora kuliko Swawm nyinginezo.'' [Taz. Latwaaif Al-Ma'aarif fiyma li Mawaasim al'aam minal Wadhwaaif, cha Ibn Rajab al Hanbaliy].

 

 

Niswfu Sha’baan: Kuna Ukweli Wowote? 

 

Pamoja na ubora huo na daraja hiyo ya mwezi wa Sha’baan, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakuihusisha siku maalum katika mwezi wa Sha’baan kwa Swawm.  Alikuwa akifunga kwa wingi iwezekanavyo lakini hakutueleza na wala hakuichagua siku ya tarehe 15 ya Sha’baan kufunga kutokana na sifa zake alizozitaja hapo nyuma, ila tu ametaja fadhila za usiku huu kutokana na Hadiyth ifuatayo ambayo hata hivyo haikutaja kuwa kuna ‘ibaadah maalum inapaswa ifanyike siku hii au usiku wake.

 

 عن أبي موسى الأشعري رضي الله عنه عن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال: ((إن الله ليطلع في ليلة النصف من شعبان فيغفر لجميع خلقه إلا لمشرك أو مشاحن))   رواه ابن ماجة وحسنه الألباني في السلسلة الصحيحة  

Imetoka kwa Abuu Muwsaa Al-Ash'ariyy (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Allaah Hutokea Katika usiku wa 15 wa Sha’baan, na Huwaghufuria wote isipokuwa washirikina na wale wenye uadui kwa wengine.”  [Ibn Maajah na imesemwa kuwa ni Hadiyth Hasan na Shaykh Al-Albaaniy].

 

Jambo la kushangaza ni kwamba wengi katika Waislam kwa uchache wa elimu na pia kwa kufuata mafundisho yasiyo sahihi ambayo amesingiziwa nayo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), wameitenga siku hiyo ya Niswfu Sha’baan kwa Swawm na kusimama kisimamo cha usiku na kusoma nyiradi mbalimbali ambazo wamezitunga na pia kusherehekea kwa namna mbalimbali. Sehemu nyingi ulimwenguni hufanya sherehe na Swawm pamoja na kuswali sana usiku kwa kuiadhimisha siku hiyo ambayo huamini ni ya aina yake.

 

 

Kuna waliyoipa jina la Shab-i-Baraah au Laylatul Baraah (usiku wa kuachiwa huru [na moto], au wa kusamehewa) kama huko bara Hindi, Pakistan na Bangladesh. Na kwengine hujulikana zaidi kwa Niswfu Sha’baan n.k. ambapo katika siku hiyo wanaamini kuwa ni siku ya kusamehewa kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anawaachia huru waja Wake walio motoni kutokana na mojawapo ya Hadiyth zisizo sahihi zilizohusishwa na mwezi huu wa Sha’baan kama hii

 

“Allaah Anawaachia huru waja wake walio motoni kulingana na idadi ya nywele zilizo katika ngozi za mbuzi/kondoo wa Banu Kalb.”

 

Vilevile kuna itikadi potofu kabisa katika siku hii, ambapo kuna baadhi ya watu wanaamini kuwa kushuka kwa Malaika na Ar-Ruwh (Jibriyl) usiku huo kama ilivyo katika Suwratul-Qadr Aayah ya 4, wao wameelewa maana yake ni kuwa Ruwh iliyokusudiwa katika Suwrah hiyo ni roho za wale waliokufa! Na kwamba 'roho' hizo zashushwa na kurejea duniani na kukutana na wake wa wenye hizo roho na jamaa zao wengine. Na kwa sababu hiyo, wale wajane hupika vyakula bora vilivyokuwa vikipendwa na hao waume zao waliokufa kisha huviandaa na kusubiri ziara zao kutoka huko walipo.

 

Baadhi ya watu pia huzuru makaburi katika siku hiyo na kuwaombea maghfirah wale wote waliokufa mwezi wa Sha’baan uliopita na huo walio nao.

 

Katika Suwrah hiyo ya Al-Qadr ambayo watu hao wameifasiri na kuielewa kinyume, Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

تَنَزَّلُ الْمَلَائِكَةُ وَالرُّوحُ فِيهَا بِإِذْنِ رَبِّهِم مِّن كُلِّ أَمْرٍ ﴿٤﴾

Wanateremka humo Malaika na Ar-Ruwh (Jibriyl) kwa idhini ya Rabb wao kwa kila jambo.  [Al-Qadr: 4]

 

 

Kwanza, Aayah hii huelezea Usiku wa Qadr ambao ni usiku wa mwezi wa Ramadhwaan na sio wa siku au tarehe 15 ya Sha’baan.

 

Pili, maana ya neno Ruwh katika Aayah hiyo ni Malaika Jibriyl ('Alayhis-Salaam), yaani watashuka Malaika pamoja na Jibriyl (pamoja na kwamba naye ni Malaika ila kutajwa kwake pekee bila kuingizwa katika kundi zima la Malaika hao, ni hadhi yake kuu) na sivyo kama wanavyodhani watu kuwa hiyo Ruwh ni roho za waliokufa (Taz. Tafsiyr ya Ibn Kathiyr).

 

Vilevile itikadi ya kwamba roho za waliokufa zitarejea tena ulimwenguni si sahihi kutokana na mafundisho Swahiyh ya Qur-aan na Sunnah.

 

Pia wengine wameuhusisha huo usiku wa katikati ya mwezi wa Sha’baan na maneno “Laylatin Mubaarakatin” (Usiku uliobarikiwa) yaliyo katika Aayah ya 3 katika Suwrah Ad-Dukhaan:

 

إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةٍ مُّبَارَكَةٍ ۚ إِنَّا كُنَّا مُنذِرِينَ﴿٣﴾

Hakika Sisi Tumeiteremsha (Qur-aan) katika usiku uliobarikiwa, hakika Sisi daima ni Wenye kuonya. [Ad-Dukhaan: 4]

 

 

Wakifasiri huo usiku uliobarikiwa kuwa ni wa 15 Sha’baan. Lakini hiyo ni tafsiyr potofu kabisa kwani inajulikana wazi bila shaka kuwa “Laylatin Mubaarakatin” iliyokusudiwa hapo kwenye Suwrah hiyo ni usiku uliopo katika mwezi wa Ramadhwaan. Na kama ilivyo wazi ni kwamba Qur-aan imeteremshwa katika mwezi wa Ramadhwaan na si katika mwezi wa Sha’baan na wala si katika tarehe 15 ya Sha’baan. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anathibitisha hilo katika Suwratul Baqarah:

 

شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ ۚ  

  Mwezi wa Ramadhwaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan ili iwe mwongozo kwa watu na hoja bayana za mwongozo na Furqaan (upambanuo).  [Al-Baqarah: 195]

 

 

Basi hayo wayasemayo baadhi ya watu kuwa usiku huo ni usiku wa kuamkia mwezi 15 Sha’baan ambao pia wanauita 'Qismatur Rizq' (Mgao wa riziki) si maneno ya kweli, bali ni uzushi na upotofu uliozoeleka na ambao umeenezwa katika Dini hii tukufu na kuichafua na kuivuruga hadi imekuwa sasa ni vigumu sana kupambanua la batili na la haki katika Dini hii iliyokamilika na isiyo na haja ya nyongeza za waongezao.

 

 

Pia du’aa zisomwazo ndani ya usiku huo zina kila aina ya uzushi kama walivyobainisha ‘Ulamaa wa kutegemewa. Na hayo ya kujikusanya usiku huo na kusoma du’aa hizo na nyiradi mbalimbali ni jambo ambalo halimo katika mafunzo ya Kitabu chetu kitukufu na wala katika Sunnah.

 

 

‘Ulamaa mabingwa wa fani ya Hadiyth wamebainisha kuwa hakuna hata Hadiyth moja iliyo Swahiyh katika Hadiyth zilizozagaa ambazo zinazungumzia fadhila na utukufu wa mwezi wa Sha’baan au tarehe 15 ya Sha’baan isipokuwa hiyo iliyotajwa juu ya kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Hutokea usiku huo na kuwaghufuria waja Wake isipokuwa waliomshirikisha na wenye uadui baina yao. Na zaidi ni kwamba Hadiyth zote ima dhaifu au mawdhwu'u (za uongo/ kutungwa). ‘Ulamaa mbali mbali kama Imaam Ash-Shawkaaniy, Ibnul Jawziy, Ibnu Hibbaan, Al Qurtwubiy (Rahimahumu Allaah) wamekemea mno na kuzikana Hadiyth au mapokezi hayo yasiyo sahihi kuhusiana na Sha’baan au siku hiyo ya Niswfu Sha’baan. [Rejea vitabu vyao kama Al Fawaaidul Majmuw'ah, Mawdhwu'aatul Kubraa na Tafsiyr al-Qurtwubiy).

 

 

Baadhi Ya Hadiyth Za Kutungwa:

 

 

Katika baadhi ya Hadiyth za kutungwa ni kama zile zisemazo:

 

“Katika siku hii (ya 15 Sha’baan) Allaah Huwaachia huru watu kutoka katika Moto wa Jahannam idadi inayolingana na nywele zilizomo katika kondoo wa kabila la Banu Kalb.” [Na Hadiyth hii Imaam At-Tirmidhiy anasema ni mbovu na dhaifu]

 

Na nyingine inasema:

 

“Yeyote atakayeswali rakaa kumi na nne za Swalaah katika usiku wa tarehe 15 ya Sha’baan atapata ujira ulio sawa na kufunga Swawm na Hija ya miaka ishirini.”

 

na pia isemayo:

 

“Kuwa ubora wa siku hii ni kwa sababu jaala ya mwana Aadam ndiyo huwa katika siku hii, pia mipango ya mazazi na vifo hupangwa.”

 

 

Na Riwaayah dhaifu nyinginezo ni kama zifautazo:

 

·     “Ee Allaah Tubarikie katika (mwezi wa) Rajab na Sha’baan na tufikishie Ramadhwaan.”

 

·     “Ubora wa mwezi wa Sha’baan (kulinganisha na miezi mingine) ni sawa na ubora wangu kuliko Manabii wengine.”

 

·     “Ukifika usiku wa Sha’baan basi mswali usiku wake na mfunge mchana wake.”

 

·    “Masiku matano huwa du'aa hazirejeshwi; Usiku wa mwanzo wa Rajab, na Usiku wa Niswfu Sha’baan, na Usiku wa Ijumaa, na Usiku wa ('Iyd) Al-Fitwr, na Usiku wa ('Iyd) ya Kuchinja.”

 

·     “Amenijia Jibriyl ('Alayhis Salaam) na akaniambia kuwa huu Usiku wa Niswfu Sha’baan Allaah Huwatoa kwenye Moto watu kwa idadi ya kila unyoya wa mbuzi/kondoo wa Banu Kalb.”

 

·     “Ee 'Aliy, atakayeswali katika Usiku wa katikati ya Sha’baan Swalaah ya Rakaa mia kwa kusoma Qul Huwa-Allaahu Ahad mara elfu moja, Allaah Atamkidhia mahitaji yake yote ya Usiku huo.”

 

·     “Atakayesoma katika Usiku wa Niswfu Sha’baan Qul Huwa-Allaahu Ahad mara elfu moja Allaah Atamtumia Malaika elfu moja watakaomjia kumpa bishara njema.”

 

·     “Atakayeswali katika Usiku wa Niswfu Sha’baan Rakaa mia tatu akasoma katika kila rakaa Qul-Huwa-Allahu Ahad mara thelathini, basi atakuwa miongoni mwa kundi litakalopewa shafaa’ah (Uombezi) ikiwa ni katika watu waliostahiki Moto.”

 

·     “Sha’baan ni mwezi wangu.”

 

·     “Atakayehuisha Usiku wa 'Iyd na Usiku wa Niswfu Sha’baan hautokufa moyo wake siku zitakapokufa nyoyo.”

 

·     “Atakayehuisha Masiku matano, atapata Jannah; Usiku wa Tarwiyah (katika Hajj), na Usiku wa 'Arafah, na Usiku wa Yawmun-Nahr (siku ya kuchinja), na Usiku wa 'Iyd Al-Fitwr, na Usiku wa Niswfu Sha’baan.”

 

 

Hadiyth zote hizo hapo juu hazina uthibitisho wowote wa usahihi wake katika Shariy’ah.  Kwa hiyo hakuna Hadiyth hata moja sahihi yenye kuthibitisha kuitenga au kuihusisha siku ya tarehe 15 ya Sha’baan kufanya ‘ibaadah maalum kama kufunga au kuswali Swalaah za usiku (Qiyaamul Layl). Na kufanya hivyo ni uzushi na upotofu ambao unapingana na mafundisho ya kipenzi chetu Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Ama kwa yule aliyezoea kuswali Swalaah za Usiku kila mara basi haikatazwi kwake kuswali vilevile usiku huo, kisichofaa ni mtu ambaye hana ada ya kuswali Swalaah za usiku lakini usiku huo akawa haukosi kwa kuamini kuwa una fadhila kubwa.  

 

 

Pia tunapata mafundisho kuwa kutenga siku maalum kwa ‘ibaadah maalum ni jambo linalokwenda kinyume na Shariy’ah isipokuwa lile lililotajwa au kufundishwa na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kama kufunga siku ya 'Ashuraa na siku ya ‘Arafah kwa asiye katika Hijjah ambazo ametubainishia sababu zake. Lau kama hili la kufunga Niswfu Sha’baan lingekuwa lina umuhimu na faida kwetu basi Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) angetueleza na angelifanya yeye mwenyewe katika uhai wake. Na kama kuna siku bora katika wiki basi ni Ijumaa na ambayo imependekezwa kwetu kufanya matendo mazuri na pamoja na ubora wake huu Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakutuamrisha Swawm siku hiyo wala kuusimamisha usiku wake kwa Swalaah. Na kama ingekuwa inaruhusiwa kama wafanyavyo hao wenye kutenga siku maalum kwa ‘ibaadah na kuacha masiku yote yaliyobaki ya mwaka mzima, basi ingekuwa ni awlaa kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kutusisitiza tulifanye hilo katika siku ya Ijumaa kutokana na ubora wake. Lakini Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakufanya hivyo.

 

 

Bali yeye mwenyewe Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Msitenge Usiku (wa kuamkia) Ijumaa kuutenga na usiku mwengine (wowote) kwa kuswali, na msitenge siku ya Ijumaa miongoni mwa masiku kwa kufunga, ila yule aliyezoea kufunga na funga yake ikaangukia siku hii [Ijumaa].” [Muslim]

 

 

Na hili latuthibitishia wazi kuwa ‘ibaadah na matendo yote mazuri hayafanywi katika siku fulani au usiku maalum tu na kuachwa nyingine, maana kufanya hivyo hakutatimiza wajibu wa mja wa kumuabudu Rabb wake. Mja hupaswa kumwabudu Rabb wake siku zote za umri wa maisha yake yote hadi atakapoiaga dunia, kwani ‘ibaadah ni kusudio la msingi la kuumbwa kwake. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَاعْبُدْ رَبَّكَ حَتَّىٰ يَأْتِيَكَ الْيَقِينُ﴿٩٩﴾

  Na mwabudu Rabb wako mpaka ikufikie yakini (mauti).  [Al-Hijr: 99]

 

 

Na ndivyo ilivyokuwa ada Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kumwabudu Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) muda wote wa mwaka mzima, masiku yote, usiku na mchana alitumia katika kumtumikia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). 

 

 

Ukumbusho Katika Sha’baan

 

Iwapo bado unahitajika kulipa Swawm za faradhi za Ramadhwaan iliyopita, fanya haraka kulipa kabla ya Ramadhwaan nyingine haijafika. Hairuhusiwi kuchelewesha Swawm zilizokosekana mpaka kufikia Ramadhwaan inayofuata, isipokuwa katika hali ya ulazima (mfano udhuru unaokubalika ambao umeendelea baina ya Ramadhwaan mbili).

 

Mama wa Waumini 'Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) amesema: “Ilikuwa nnazo siku za kulipa za Ramadhwaan na sikuweza kuzilipa isipokuwa (katika mwezi wa) Sha’baan.”  [Al-Bukhaariy]

 

 

Yeyote aliyekuwa na uwezo wa kulipa Swawm zilizompita kabla ya Ramadhwaan (ya pili) na asifanye hivyo, basi atalazimika kuzilipa baada ya Ramadhwaan (ya pili), na zaidi analazimika kutubia na kumlisha maskini mmoja kwa kila siku iliyompita.    Huu ni msimamo wa Maimaam: Maalik, Ash-Shafi’iy na Ahmad. Na unaoonekana kuwa Swahiyh zaidi.

 

 

Wa Allaahu A’lam

 

 

 

Share