Kumposa Mwanamke Katika Eda

SWALI:

Asalaam alaykum. Mimi ninaswali, je! Naweza kumposa mwanamke aliyekuwa ndani ya eda, haku nikisubiri  amalize nimuoe? Ahsante 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Shukrani sana kwa swali lako kuhusu mas-ala ya posa wakati wa Eda. Zipo aina tofauti za Eda, na kila hali ina sharti zake katika suala hili. Miongoni mwazo ni:

1.    Eda kwa Aliyefiliwa: Haifai kwa mwanamme kumposa mwanamke katika eda hilo wazi wazi kama kusema: Nataka kukuoa. Uharamu wake wameafikiana Mafaqihi. Hata hivyo, inafaa kuonyesha hamu yake katika hilo bila kuwa wazi. Hii ni kujali hisia za mwanamke katika wakati wa majonzi ya kuondokewa na mumewe. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema: “Wala si vibaya kwenu katika kupeleka posa kwa ishara tu kwa wanawake waliomo edani au mkadhamiria katika nyoyo zenu. Allaah Anajua kwamba nyinyi mtawakumbuka. Lakini msiwaahidi kwa siri, ila mnene maneno mema. Wala msiazimie kufunga ndoa mpaka eda ifike mwisho wake. Na jueni kwamba Allaah Anajua yaliyomo katika nafsi zenu. Basi tahadharini naye. Na jueni kwamba Allaah ni Mwenye kusamehe na Mpole” (2: 235).

Katika ishara ya kuwa una hamu naye ni kusema: Mimi nataka kuoa au Nataraji wepesi wa kupata mke mwema.

2.    Eda ya Talaka Rejea: Katika hali hii haifai kumposa mwanamke kwa wazi au hata kwa ishara. Hii ni kuwa bado yeye ni mke wa mtu na wanaweza kurudiana. Hakika kukaa eda kwake ni kutoa nafasi ya kusameheana na kuweza kurudiana na mumewe kabla ya eda kumalizika. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema: “Na mtakapowapa wanawake talaka nao wakamaliza eda yao, basi msiwazuie kuolewa na waume zao endapo baina yao wamepatana kwa wema” (2: 232).

 

3.    Eda baada ya Talaka Tatu: haifai kumposa mwanamke huyo kwa kuafikiana kwa wanazuoni, lakini wakatofautiana katika kutoa ishara kwa hilo. Kauli ya jamhuri ni kuwa inajuzu kutoa ishara na hiyo ni kwa ujumla wa kauli ya Aliyetukuka: “Wala si vibaya kwenu katika kupeleka posa kwa ishara tu kwa wanawake waliomo edani” (2: 235). Pia Hadiyth ya Faatwimah bint Qays (Radhiya Allaahu ‘anha) ambaye aliambiwa na Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipoachwa talaka tatu na mumewe: “Kaa eda katika nyumba ya Ibn Umm Maktuum kwani yeye ni kipofu hivyo kuweza kuvua nguo zako. Utakapomaliza eda utanijulisha”. Katika lafdhi nyingine: “Usinipitilize kwa nafsi yako” (Muslim). Hii inajuzisha ishara ya posa katika eda aina hii.

Na Allah Anajua zaidi

 

Share