Imaam Ibn Baaz: Nasaha Kwa Du'aat Wa Kisalafi

 

Nasaha Kwa Du'aat Wa Kisalafi

 

Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah)

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah) amesema:

 

"Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kahimiza uadilifu na yaliyo mema na fadhila; na kaharamisha dhulma, unyanyasaji, na kushambuliana.

 

Kamtuma Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na ujumbe ule ule aliowapa Mitume waliotangulia wa kuita watu kwenye Tawhiyd (Kumpwekesha Allaah) na kuwanasihi watu kutumia muda wao kufanya ‘Ibaadah kwa ajili ya Allaah peke Yake. Na akamwagiza Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kusimamisha uadilifu na haki na kukataza aina yoyote ile ya ‘Ibaadah kwa asiyekuwa Allaah, na akakataza mgawanyiko na kudhulumu haki za watu.

 

Imekuwa ni jambo lenye kuenea siku hizi katika hao wanaojiita Wanachuoni na Du’aat (Walinganiaji) kuwasema vibaya Du'aat wengine pamoja na wale wanaotafuta elimu, ima ni kwa siri au kwa Dhahiri hadharani.

 

Wanafikia hadi kuwarekodi wenzao kwenye kanda na kisha kutawanya kwa watu, au (kuwasema) kwenye mihaadharah yao waifanyao Misikitini. Hili ni jambo linalopingana na maamrisho ya Allaah na Rasuli Wake kwa njia nyingi zikiwemo:

 

 

Kwanza, Kufanya hivyo ni kumfanyia ukhalifu na kwenda kinyume na haki za Waislamu, Wanachuoni na Du'aat (wanaolingania katika Sunnah) ambao wamefanya jitihada kubwa kuwafundisha watu kufuata itikadi iliyo Sahihi, na kujibidiisha katika kufanya Da’wah na kuandika vitabu venye manufaa, na kwa hili wanakuwa na sifa za Waislamu wabora.

 

 

Pili, hili linapelekea kuvunja umoja wa Waislamu na kueneza mpasuko baina yao, japokuwa wao wanahitaji kuungana na kuwa mbali na migawanyiko na uvumi, haswa pale Du`aat wanaosengenywa ni katika Ahlus-Sunnah Wal Jamaa’ah ambao wanajulikana kwa kupiga vita Bid'ah (Uzushi katika Dini) na ushirikina na kuwafichua wale ambao wanawaita watu katika hayo.

 

Na hanufaiki yeyote yule kwa mambo haya (ya kusengenyana, kutuhumiana, kushambuliana na kudhulumiana) isipokuwa maadui zetu kama vile Makafiri, Wanafiki, na watu wa bid’ah.

 

 

Tatu, hili linawasaidia zaidi watu wasio waadilifu, Masekula, Wamagharibi na wasioamini Mungu, hao wanajulikana kwa kusambaza uvumi mbalimbali kuwachafua Du'aat ili watu wawachukie ili kufikia malengo yao.

 

Udugu wa Waislamu unatakiwa uzuie Waislamu katika kuwasaidia maadui wa Uislamu katika kuwadhuru Waislamu wenzao, wakiwa ni wanafunzi watafutaji elimu, Walinganiaji na wengineo.

 

 

Nne, hili linawapotosha watu wa kawaida na Wanachuoni; kueneza uvumi wa uongo, kunapelekea katika kusengenya, umbea; kufungua milango ya shari kwa wale wenye mioyo dhaifu. Wanaoeneza uvumi wa uongo, wanaamsha fitnah na kuwadhuru Waumini kwa dhulma.

 

 

Tano, Pia madai yao mengi katika hizo Radd zinazotolewa huwa ni ya uongo; ni ya kudhania tu na Shaytwaan huyafurahia.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'alaa) Anasema:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اجْتَنِبُوا كَثِيرًا مِّنَ الظَّنِّ إِنَّ بَعْضَ الظَّنِّ إِثْمٌ ۖ وَلَا تَجَسَّسُوا وَلَا يَغْتَب بَّعْضُكُم بَعْضًا ۚ أَيُحِبُّ أَحَدُكُمْ أَن يَأْكُلَ لَحْمَ أَخِيهِ مَيْتًا فَكَرِهْتُمُوهُ ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ تَوَّابٌ رَّحِيمٌ﴿١٢﴾

 

“Enyi walioamini! Jiepusheni sana na dhana (mbaya), kwani hakika baadhi ya dhana ni dhambi. Na wala msifanyiane ujasusi, na wala wasisengenyane baadhi yenu wengineo...” [Al-Hujuraat 49:12]

 

Mu-umin anatakiwa aweke dhana njema katika maneno ya Mu-umin mwenzake.

 

Baadhi ya Salaf (Wema waliotangulia) wamesema:

 

"Usitie fikra mbaya katika maneno ya ndugu yako, huenda yakatafsirika vizuri zaidi."

 

 

Sita, Ikiwa Wanachuoni na watafutaji elimu, watafanya Ijtihaad, hakuna madhara maadam watakuwa na sifa na uwezo huo (za kufanya Ijtihaad).

 

Kama wapo watakaowapinga kwa Ijtihaad hiyo, basi wanatakiwa wapinge katika njia nzuri ya kufikia katika Haki katika njia iliyo karibu bila ya kufungua milango kwa Shaytwaan kuwadhuru Waumini. Na kama hili haliwezekani (la kufanya kwa siri) basi na ikiamuliwa wafanye hadharani basi ifanyike kwa upole bila ya mashambulizi ambako kunaweza kupelekea kwao kukataa Haki, bila ya kuwashambulia na kuhukumu niyyah zao.

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisema,

"Nawajua watu fulani wanasema hili na lile."

 

 

Nawanasihi hao waliowasengenya Du`aat, wafanye Tawbah kwa Allaah kwa walichokiandika ama walichokisema, kilichopelekea kupotosha vijana, na kuwatia vinyongo na chuki, na kuwapotezea malengo yao katika kutafuta elimu na kuifanyia kazi Da`wah, na kuwashughulisha na uvumi na kuwatafutia watu makosa yao kwa makusudi.

 

Kadhaalika, nawanasihi walipe waliyoyafanya, ima kimaandishi au kwa njia zingine, ili kujisafisha wao kwa matendo hayo na kuondosha athari ya waliyoyasema huko nyuma.

 

Vilevile wafanye matendo yenye manufaa ambayo yatawakurubisha karibu na Allaah na kuwanufaisha watu; na hadhari kupupia kuwahukumu (Waislamu kwa kuwaita wao) ni Makafiri, Mafasiki na Wazushi bila ushahidi wowote.

 

 

Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

“Anayemuita nduguye Kafiri, basi litamstahikia hilo mmoja kati yao.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Inatakikana kwa watafutaji elimu wa Haki na wanaojifunza, kurejea kwa Wanachuoni wakubwa endapo watakutana na mambo yenye utata, na hivyo itawafanya wawekewe wazi na kuondoshewa mashaka na utata walionao, hayo ni kulingana na Anavyosema Allaah katika Suwrat An-Nisaa:

 

وَإِذَا جَاءَهُمْ أَمْرٌ مِّنَ الْأَمْنِ أَوِ الْخَوْفِ أَذَاعُوا بِهِ ۖ وَلَوْ رَدُّوهُ إِلَى الرَّسُولِ وَإِلَىٰ أُولِي الْأَمْرِ مِنْهُمْ لَعَلِمَهُ الَّذِينَ يَسْتَنبِطُونَهُ مِنْهُمْ ۗ وَلَوْلَا فَضْلُ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَتُهُ لَاتَّبَعْتُمُ الشَّيْطَانَ إِلَّا قَلِيلًا ﴿٨٣﴾

 

“Na linapowafikia jambo lolote la amani au la khofu hulitangaza. Na lau wangelirudisha kwa Rasuli na kwa wenye madaraka kati yao, wale (Wanavyuoni) wanaotafiti miongoni mwao wangelilijua. Na lau si fadhila ya Allaah juu yenu na Rahmah Yake kwa yakini mngelimfuata shaytwaan (nyote) ila wachache tu.” [An-Nisaa 04:83]

 

 

Allaah ndiye Msimamizi wa kuwapangia Waislamu mambo yao, kuwaegemeza mioyo yao kwenye Taqwaa, kuwaongoza Wanachuoni wote wa Kiislamu na wote wanaolingania katika Haki na yale yenye kumridhisha Allaah na yenye kuwanufaisha watu; Akiwakusanya wao katika uongofu; Akiwahifadhi wao na njia ya upotofu na kutofahamiana; na kuwafanya wao kuungana katika Haki na si kwenye Baatwil. Yeye Ndiye Mweza Pekee wa kufanya hayo.

 

 

Swalah na Salaam za Allaah ziwe juu ya Rasuli Muhammad, familia yake, Maswahaba zake, na wale wote wenye kufuata uongofu wake hadi Siku ya Hesabu.”

 

 

[Fataawa Imaam Ibn Baaz, mj. 7]

 

 

Share