Kula Chakula Cha Halali

 

 

SWALI:

 

Leo ningependa kuja na suali hili: Katika Sura ya 5 (Al Maida) aya nambari 5 inasema: '' Leo mmehalalishiwa kila vilivyo vizuri. Na chakula cha walio pewa Kitabu ni halali kwenu, na chakula chenu ni halali kwao. Na pia wanawake wema miongoni mwa Waumini, na wanawake wema miongoni mwa walio pewa Kitabu kabla yenu, mtakapo wapa mahari yao, mkafunga nao ndoa, bila ya kufanya uhasharati wala kuwaweka kinyumba. Na anaye kataa kuamini bila shaka amali yake imepotea, naye katika Akhera atakuwa miongoni mwa wenye khasara. ''

Jee Sheikh kwa watu wanaoishi nchi za Ulaya panapo vyakula vyao hawa watu wa kitabu kama Mc donars na nyengine inaruhusiwa kuingia na kula bila katika vyakula vyao kama nyama ya ng'ombe ambayo hatujui kama imechinjiwa jina la Allah? Nashukuru na nategemea kupata majibu kutoka kwenu. Ahsanteni sana

 

 


 

JIBU: 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Uislamu umehalalisha kila lililo zuri na ALLAAH سبحانه وتعالى    hakubali ila zuri katika kila jambo. Jambo ambalo limehalalishwa na Allaah سبحانه وتعالى au Mtume Wake  صلى الله عليه وآله وسلمbasi linakuwa na maslahi kwetu na lililoharamishwa linakuwa ni lenye madhara. Mwanadamu anapofanya ovu anasema kuwa tumeamrishwa hilo na Allaah سبحانه وتعالى, lakini Allaah سبحانه وتعالى    yuko mbali na jambo hilo. Allaah سبحانه وتعالى    Anasema:

}}وَإِذَا فَعَلُواْ فَاحِشَةً قَالُواْ وَجَدْنَا عَلَيْهَا آبَاءنَا وَاللّهُ أَمَرَنَا بِهَا قُلْ إِنَّ اللّهَ لاَ يَأْمُرُ بِالْفَحْشَاء    أَتَقُولُونَ عَلَى اللّهِ مَا لاَ تَعْلَمُون{{

{{“Na wanapofanya mambo machafu husema: Tumewakuta nayo babu zetu, na Allaah ametuamrisha hayo. Sema: Hakika Allah haamrishi mambo machafu. Mnamzulia Allah msiyoyajua}} Al-A'araaf:  28

  

Na Allaah سبحانه وتعالى  anatueleza kwamba hakuharamisha isipokuwa yaliyo machafu na sio yale mazuri. Anasema:

}}قُلْ مَنْ حَرَّمَ زِينَةَ اللّهِ الَّتِيَ أَخْرَجَ لِعِبَادِهِ وَالْطَّيِّبَاتِ مِنَ الرِّزْقِ قُلْ هِي لِلَّذِينَ آمَنُواْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا خَالِصَةً يَوْمَ الْقِيَامَةِ كَذَلِكَ نُفَصِّلُ الآيَاتِ لِقَوْمٍ يَعْلَمُونَ{{

 }}  قُلْ إِنَّمَا حَرَّمَ رَبِّيَ الْفَوَاحِشَ مَا ظَهَرَ مِنْهَا وَمَا بَطَنَ وَالإِثْمَ وَالْبَغْيَ بِغَيْرِ الْحَقِّ وَأَن تُشْرِكُواْ بِاللّهِ مَا لَمْ يُنَزِّلْ بِهِ سُلْطَانًا وَأَن تَقُولُواْ عَلَى اللّهِ مَا لاَ تَعْلَمُونَ{{

{{Sema: Ni nani aliyeharimisha pambo la Allah alilowatolea waja wake, na vilivyo vizuri katika riziki. Sema hivyo ni kwa walioamini katika uhai wa duniani, na Siku ya Kiyama vitakuwa vyao wao tu. Namna hivi tunazieleza Ishara kwa watu wanao jua}}.

 {{Sema: Mola  wangu ameharamisha mambo machafu ya dhahiri na ya siri, na uasi bila ya haki, na kumshirikisha Allah na asichokiletea uthibitisho, na kumzulia Allah msiyoyajua}} Al-A'araaf    32 – 33 .

 

 Na katika Hadiyth ni ile iliyopokea kwa Abu Hurayrah رضي الله عنه   kwamba Mtume wa Allaah صلى الله عليه وآله وسلم amesema:

((Hakika Allaah سبحانه وتعالى  ni Mzuri na Hakubali ila zuri. Na hakika Allaah سبحانه وتعالى   amewaamrisha Waislamu yale aliyowaamrisha Mitume. Akasema Allaah سبحانه وتعالى  ‘Enyi Mitume! Kuleni vizuri na fanyeni mema’ (23: 51). Na akasema tena Allah Aliyetukuka: ‘Enyi mlioamini! Kuleni vizuri Tulivyowaruzuku (2: 172)))   [Muslim].

 

Kwa aya na Hadithi zinatutaka sisi tule vilivyo vizuri na hiyo ni kwa maslahi yetu wenyewe. Na miongoni mwa vilivyo vizuri vya Ahlul Kitaab (waliopewa Kitabu). Allah anasema:

}}الْيَوْمَ أُحِلَّ لَكُمُ الطَّيِّبَاتُ وَطَعَامُ الَّذِينَ أُوتُواْ الْكِتَابَ حِلٌّ لَّكُمْ وَطَعَامُكُمْ حِلُّ لَّهُمْ {{

{{Leo mhelalalishiwa kila vilivyo vizuri. Na chakula cha waliopewa Kitabu ni halali kwenu, na chakula chenu ni halali kwao}}  Al- Maaidah :5  

  

Inatakiwa tuelewe kuwa aya zinazoteremshwa na Allaah سبحانه وتعالى    ni kwa ajili ya kutekelezwa na Waislamu wa zama zote na kila sehemu katika hii dunia. Hebu tuangalie Mufasirina wa Qur’ani wanatueleza vipi katika suala hili.

Chakula cha kuchinja hakiwi halali kwa Waislamu ila kichinjwe na Muislamu au myahudi au Mnasara (Mkristo), kwa sharti ile ya kuchinja – sio kuwanyonga. Ama wasiokuwa hawa hakiwi halali wanachokichinja. Ama chakula kisichokuwa cha kuchinja ni halali kwa Muislamu kukila hata kikitengenezwa na makafiri, kwa madhehebu ya Kisuni maadamu:

             -         Hujaona kuwa kimeingia najisi

              -       Si katika vile vyakula vilivyokatazwa na Uislamu

 

Wafasiri wanachambua:

“Vyakula vya Ahlul Kitaab” inajumlisha wanyama wanaochinjwa na wao. Na chakula cha waliopewa Kitabu ni halali kwenuina maana ya kuwa hakuna vikwazo kwetu au kwao kula chakula pamoja. Waislamu wanaruhusiwa kula chakula pamoja na Ahlul Kitaab na wao pia kula na Waislamu. Lakini kukaririwa kwa sentensi “vilivyo vizuri na safi” ni muhimu sana. Hii inamaanisha kuwa Waislamu hawafai kula vyakula vyao, ikiwa Ahlul Kitaab  hawatachunga kanuni muhimu kwa muono wa Uislamu au wakachanganya vitu katika vyakula na vinywaji ambavyo si halali. Kwa mfano, ikiwa hawatataja jina la Allaah سبحانه وتعالى juu ya mnyama wanaomchinja, nyama hiyo itakuwa haramu kwa waislamu. Hivyo hivyo, ikiwa pombe au nyama ya nguruwe au kitu chochote haramu kitaandaliwa, Waislamu hawataruhusiwa kukaa meza moja na wao. Kanuni hiyo hiyo ndiyo inayotumika kwa vyakula na vinywaji vya wasiokuwa Waislamu isipokuwa Waislamu hawafai kula nyama ya wanyama waliochinjwa na wasiokuwa Waislamu (wasiokuwa Ahlul Kitaab). "

 

"Maana ya ayah ii kwa ufupi ni kuwa kuanzia siku hii ya leo vyote vilivyo vizuri na safi vinaruhusiwa kwenu, Waislamu. Kwa vile Allaah سبحانه وتعالىhakukataza, vyakula vya Mayahudi na Manasara inaruhusiwa kwa msingi wa ile ruhusa ya asli ya kukubaliwa. Kwa hivyo mnaweza kula nyama ya wanyama waliochinjwa au kuwindwa, nao wanaweza kula mliochinja au kuwinda. Japokuwa Uislamu unachukua msimamo mkali kwa washirikina, unakua laini kwa wale waliopewa Kitabu kwani wao wako karibu na Waislamu katika itikadi zao kuhusu wahyi, utume na misingi mingine ya Dini. Uislamu unaturuhusu kula nao, kuoa wanawake wao na kwa jumla kuwa na mahusiano ya kijamii na wao. Matumizi ya kauli, “Vyakula vya Ahlul Kitaab ni halali kwenu” kwa ujumla wake inajumlisha nyama, mazao na vyakula vyengine. Vyote hivi ni halali kwetu sisi isipokuwa vile vilivyo haramu kwa mfano nyama ya nguruwe, mzoga, damu inayo tiririka, kwani hizi ni haramu bila kujali ikiwa vinatoka kwa Mnaswara, Myahudi au Muislamu. Ikiwa mtu hatomsikia Mnasara au Myahudi akitaja jina lisilokuwa la Allaah سبحانه وتعالى  kama kutaja jina la Yesu au mtawa Fulani wakati wa kuchinja mnyama, nyama anayopatiwa ni halali. Lakini ikiwa atataja jina lisilokuwa la Allaah سبحانه وتعالى  basi itakuwa haramu, kulingana na baadhi ya mafakihi ambao wanaosema kuwa hiyo inaingia katika fungu la vile vinavyotolewa kwa asiyekuwa Allaah سبحانه وتعالى ilhali wengine wanasema kuwa vyakula vya waliopewa Vitabu vinaruhusiwa kwetu na Allaah سبحانه وتعالى  ambaye ni mjuzi kwa wanayosema wakati wa kuchinja."

 

Allah ametaja alivyoviharamisha kwa Waumini katika vilivyo vichafu na kuhalalisha vizuri. Kisha akataja hukmu ya waliochinjwa na Ahlul Kitaab akasema: “Na chakula cha waliopewa Kitabu ni halali kwenu”. Amesema Ibn ‘Abbaas, Abu Umamah, Mujaahid, Sa‘iyd bin Jubayr, ‘Ikrimah, ‘Atwaa’, al-Hasan, Makhuul, Ibraahim an-Nakha‘i, Muqaatil bin Hayyaan: Yaani waliochinja, na hili jambo wamekubaliana wanazuoni kuwa wanyama wanaochinja ni halali kwa waislamu kwani wao wanaitakidi kuwa ni haramu kuchinja kwa asiyekuwa Allaah سبحانه وتعالى na hawataji katika kuchinja isipokuwa jina la Allaah سبحانه وتعالى japokuwa wao wanazo itikadi nyingine ambazo haziendi sambamba na utukufu wa Allaah سبحانه وتعالى. Wanavyuoni wa Kihanafi, Shafi‘i na Hanbali wanaruhusu kuliwa kwa sehemu za mnyama aliyechinjwa na Myahudi japokuwa kwao ni haramu kama mafuta na wametoa dalili ya Hadithi ya ‘Abdullah bin Mughaffal رضي الله عنه   wakati alipochukua kiriba cha mafuta kilichotupwa na Myahudi katika Vita vya Khaybar (Sahiih). Na dalili nyingine ni ile Hadithi inayotueleza baada ya vita vya Khaybar mwanamke wa Kiyahudi kwa jina Zaynab alimchomea Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  paja la kondoo na kulitia sumu naye akala na katika kula Sahaba mmoja, Bishr bin al-Bara’ bin Ma‘rur رضي الله عنه   aliaga dunia kwa sumu hiyo baada ya kula (Ibn Kathiir, Tafsiirul Qur’aanil Adhiim, Mjalada wa pili).

 

Kwa muhtasari kutoka kwa yale tuliyoyanukuu tunaona ya kwamba:

1.   Wanyama wote wa halali wanaochinjwa na Ahlul-Kitaab wamehalalishwa kwa Waislamu isipokuwa inapojulikana kwa uwazi kuwa wamechinjwa kwa njia ambayo haikubaliki katika Uislamu.  Lakini katika hilo haifai kuchunguza na kudadisi dadisi kuona wanavyofanya. 

2.     Vyakula vyingine ambavyo si vya wanyama Waislamu wanaruhusiwa kula bila tatizo lolote ila ima kinapochang'anywa na vyakula vilivyo haramu.

Katika hali ambayo ipo katika Ulaya au Marekani, Muislamu anaweza kula vyakula vyao ikiwa havijapikwa pamoja na vyakula ambavyo ni haramu bila ya tatizo lolote.

 

Hapa napenda kutoa tanbihi kwa muulizaji na Waislamu wengine hasa ndugu yetu muulizaji alipouliza kuhusu migahawa (Restaurants) ya Mc Donald’s. Kwanza  hakika asili ya vitu vyao (hiyo migahawa na si vyote viuzwavyo humo) ni halali lakini lakini inategemea na vinavyotengenezwa ndani yake na namna ya upikaji, maana  baada ya kufanya utafiti tumegundua haya yafuatayo:

·  Kuna mwenzetu alikuwa akifanya kazi huko anasema kuwa hakuna kizuizi katika kuandaa nguruwe na vyakula vingine huko jikoni; mtu anaweza kukatakata nguruwe au kushika na hapo hapo akashika kuku au nyama nyingine, na vyombo vinatumika hivyo hivyo n.k.)

 

·   Huwa wanachoma nyama zao katika chuma (grill) ile ile wanayochomea nyama ya nguruwe. (Hili tumelifanyia utafiti kwa kupiga simu mgahawa mojawapo wa Mc Donald na kupata jibu hilo kuwa kweli huwa wanafanya hivyo). 

 

Kwa hivyo, inampasa Muislamu ahakikishe na jambo hilo kwa kufanya utafiti, kabla ya kula chakula chao.

 

Jambo la pili ambalo pia muhimu ni kwamba ipo Fatwa ambayo imetolewa na wanavyuoni kadhaa ya kwamba migahawa na bidhaa nyingine ambazo zinatengenezwa na kampuni za Kiyahudi zinataka zisusiwe kwani asili mia kubwa ya faida zao inapelekwa kwenda kuisaidia serikali ya Kiyahudi  ili kuwaua ndugu zetu wa Palestina. Na miongoni mwa migahawa ya Kiyahudi ni Mc Donald’s ambayo Waislamu wanatakiwa wasusie na hata migahawa ya Kimarekani ambazo pia inasaidia Maisraeli kwa kiasi kikubwa kama Pizza Hut, Pizza Inn, Domino’s Pizza, Kentucky’s Popeye, Burger King, Mc Burger, Wendy’s. Na hili si jambo gumu kwani kuna migahawa mingi na 'take aways' nyingi za Waislam zinazouza HALAAL.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share