Imaam Kasahau Kurukuu, Je, Swalaah Yake Ni Sahihi?

 SWALI:

Kwa mfano imam amesahau kwenda rukuu akapitiliza hadi sujudu...kisha ankumbuka kua hajaenda rukuu...

 

Mwisho wa swala pia asitoe sajda tu sahwi...je inaswii swala yake


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Rukuu ni nguzo ya Swalaah, na kuisahau hadi Swalaah kumalizika, kunaifanya Swalaah kubatilika. Na nguzo yoyote nyingine itakayoachwa kwenye Swalaah, inaifanya Swalaah kubatilika hadi itakaporejewa kisha na kisha kusujudiwa Sijdah mbili za kusahau.

 

Kuhusu qadhiyyah ya huyo Imaam, ilipaswa Maamuma wamkumbushe kama alisahau kurukuu, na si kumwachia hadi akaondoka.

 

Kwa hali hiyo, Swalaah ile ilikuwa ni baatwil (imebatilika).

 

Alipaswa ima arejee rakaa nzima baada ya kukumbuka au kukumbushwa, au arejee nguzo ile na vyote vinavyofuatia baada ya nguzo ile. Hizo ni rai mbili za Wanachuoni. Wako wanaoona ni kuwa anayeiacha nguzo akakumbuka baada ya Swalaah, basi arejee rakaa nzima.

 

Na wako Wanachuoni wanaoona kuwa arejee ile nguzo na vile vinavyofuatia baada ya ile nguzo. Kama alisahau kurukuu, basi arejee kurukuu atakapokumbushwa au kukumbuka, na kisha anyanyuke I'tidaal na kisha kusujudu sijdah mbili na kisha salaam. Na baada ya hapo asujudu tena sijdah mbili za kusahau na kisha kutoa salaam tena.

 

Kadhaalika Wanachuoni wanasema kuwa nguzo haiwezi kulipwa kwa sijdah za kusahau, bali nguzo ni jambo la lazima kwenye Swalaah na hivyo lazima irudiwe.

 

Anasema Mwanachuoni mkubwa Faqiyh, Imaam Ibn 'Uthaymiyn (Rahimahu Allaah):

"Nguzo au sehemu za lazima (za Swalaah) ni Lazima na ni muhimu zaidi kuliko zile 'Waajibaat' za Swalaah. Lakini kuna ikhtilaaf kuhusu nguzo za Swalaah na Waajibaat za Swalaah; nguzo za Swalaah haziwezi kulipwa kwa kusujudiwa sajdah mbili za kusahau, lakini Waajibaat zinaweza kulipwa au kutoshelezwa kwa kusujudu sijdah mbili za kusahau."

[Ash-Sharh Al-Mumti', mj. 3, uk. 315]

 

Na akasema tena (Allaah Amrehemu):

"Ushahidi kuwa nguzo haziwezi kulipwa kwa kusujudiwa sijdah mbili za kusahau, ni kuwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitoa salaam baada ya kuswali rakaa mbili za Adhuhuri au Alasiri (alisahau akaziswali pungufu badala ya nne akaswali mbili), akamaliza na kisha kukamilisha (zile alizokuwa kazisahau baada ya kukumbushwa) na kisha akasujudu sijdah mbili za kusahau. Hii inajulisha kuwa nguzo za Swalaah haziwezi kulipwa kwa kusujudu sijdah mbili za kusahau; bali zinapaswa kutekelezwa (kurudiwa zinaposahaulika)."

[Ash-Sharh Al-Mumti', mj. 3, uk. 323]

 

Hapa chini kwenye viungo vifuatavyo kuna faida za ziada vilevile:

 

Nguzo Za Swalah, Vitendo Vya Waajib Na Sunnah Katika Swalah

http://alhidaaya.com/sw/node/2553

 

Swalaatul-Masbuwq - Anapokosa Rak’ah Katika Swalaah Ya Jamaa’ah Afanyeje? Anatakiwa Asome Suwratul Faatihah Na Suwrah Ndogo Katika Raka’ah Alizozikosa?

http://alhidaaya.com/sw/node/6661

 

Na Allaah ni Mjuzi zaidi

Share