Ka'ab bin Maalik (رضي الله عنه)

Ka'ab bin Maalik (Radhwiya Allaahu 'anhu)

 

Muhammad Faraj Saalim As-Sa'ay

 

 Na Wale Watatu Waliongoshwa..

 

Hiki ni kisa cha kusisimua juu ya Maswahaba watatu (Radhwiya Allaahu ‘anhum), waliofanya makosa, na walipomuendea Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) kumuomba msamaha, aliwataka wasubiri mpaka Allaah (Subhaanahu wa Taala) Atakapoteremsha hukmu juu yao, wakati wenzao waliofanya kosa lile lile walipomuendea Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) hakuwataka wasubiri, bali aliwakubalia udhuru wao, akawaombea maghfira, kisha akamauchia Allaah juu ya ukweli wa udhuru wao.

Hili ni fundisho kubwa kwetu Waislamu la kujifunza subira katika kutafuta radhi za Allaah, pamoja na kujifunza namna gani Maswahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) walikuwa watiifu kwa kiongozi wao na kipenzi chao Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam).

 

Maswahaba watatu hawa (Radhwiya Allaahu ‘anhum) walisubiri mpaka ardhi yote wakaiona dhiki, juu ya ukubwa wake, na mpaka wakatambua kuwa hapana pa kukimbilia isipokuwa kwake Subhaanahu wa Taala.

 

Hiki ni kisa cha vita vya Taabuuk, ambapo kwa mara ya mwanzo jeshi la Waislam lilijitayarisha kupambana na jeshi kubwa la Warumi katika mwaka wa 9 Hijri wakati wa joto kali sana, katika vita vilivyojulikana kama ni  Vita vya Dhiki.

 

Watu wapatao themanini katika watu wa Madina hawakufuatana na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) kwenda Taabuuk kushiriki katika vita hivyo, watu ambao wengi kati yao walikuwa ni wanafiki ambao aya za Qur-aan zilikwisha teremka juu yao kuwajulisha watu juu ya unafiki wao.

Walikuwepo pia wasioshiriki kwa sababu ya maradhi au udhaifu wa siha zao au kwa sababu ya kutokuwa na uwezo wa kumiliki wanyama wa kuwapanda kuwapeleka vitani. Na wengine hawakushiriki kwa sababu ya uvivu tu.

 

Ka’ab bin Maalik (Radhwiya Allaahu ‘anhu), mmoja katika Maswahaba waliojulikana kwa ucha Mungu ambaye pia alikuwa mmoja katika washairi maarufu sana wa Kiislam hakushiriki katika vita hivyo.

Ka’ab alishiriki pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) katika vita vyote dhidi ya washirikina isipokuwa vita vya Badr, na hii ilikuwa kwa sababu Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) alipotoka na kundi dogo la Waislam wapatao mia tatu na kidogo katika vita hivyo vya Badr hakuwa na nia ya kupigana vita vikubwa, bali alikuwa na nia ya kuuteka msafara mdogo wa Abu Sufiyaan uliokuwa ukitokea nchi ya Shaam.

 

Katika vita vya Uhud, Ka’ab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alibadilishana nguo na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam). Yeye alivaa nguo za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) zenye rangi ya manjano  na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) alivaa nguo za Ka’ab (Radhwiya Allaahu ‘anhu).

Katika vita hivyo Ka’ab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipata majeraha kumi na moja.

 

Hebu tumuache Ka’ab mwenyewe (Radhwiya Allaahu ‘anhu) atuhadithie kisa chake cha kutokushiriki katika vita hivyo vya Taabuuk.

Anasema Ka’ab (Radhwiya Allaahu ‘anhu):

Sikupata kuwa katika hali nzuri kwa hali na mali kama nilivyokuwa wakati watu wakijitayarisha na vita hivyo. Wallahi sikupata kukusanya wanyama wawili wa kunipeleka vitani isipokuwa katika vita hivyo. Na ilikuwa kawaida ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) anapotaka kupigana vita vyovyote hutoa ishara kama kwamba anataka kupigana vita vingine, (Isipokuwa katika vita hivi hakufanya hivyo kwa sababu ya umbali wa Safari na ukali wa joto), mpaka ulipowadia wakati wa vita hivyo vilivyokuwa katika joto kali sana, safari ndefu, pamoja na maadui wengi sana.

 

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) alikuwa katika hali ya kujitayarisha, na Waislam pia wakawa katika hali hiyo, na watu walikuwa wengi sana.

Nikasema:

'Kesho mimi nitajitayarisha nijiunge nao.'

Nikawa nakwenda nikirudi bila ya kufanya chochote, huku nikijisemesha nafsini mwangu:

'Wakati wowote ninapotaka nitaweza kujitayarisha nijiunge nao'.

Nikaendelea na hali hiyo mpaka mambo yalipoanza kupamba moto, na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) alipoamua kuondoka asubuhi ya siku ya pili yake pamoja na Waislam, na mimi bado sikuwa nimejitayarisha kwa chochote.

Nikasema:

'Nitajitayarisha siku ifuatayo baada ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) kuondoka, au hata baada ya siku mbili kisha nitakutana nao njiani kabla ya wao kuwasili Taabuuk.'

Nikatoka asubuhi ya siku ya pili ili nianze kujitayarisha na kununua mahitajio yangu ya vitani, hatimae nikarudi nyumbani bila kufanya chochote.

Nikawa katika hali hiyo mpaka zikatufikia habari kuwa Waislam wamekwishawasili Taabuuk na kwamba vita vishaanza, ndipo iliponipitikia niondoke ili niwawahi. Yareti ningefanya hivyo. Lakini sikujaaliwa.

Nikawa kila ninapotoka nje ya nyumba yangu na kuonana na watu, ninahuzunika sana na kuona uchungu kwa sababu sikuwa nikimuona mtu yeyote aliye kufu yangu. Sikuwa nikiwaona isipokuwa wale watu waliokuwa wakijulikana kuwa ni wanafiki, au wale waliokuwa na udhuru wa kutokwenda vitani kwa sababu ya umasikini, udhaifu wa hali zao au maradhi.

 

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) hakuuuliza juu yangu mpaka walipowasili Taabuuk, akasema huku akiwa amekaa pamoja na watu:

"Amefanya nini Ka’ab?"

Mmoja katika watu wa Bani Salama akasema:

"Limemzuia tandiko lake na kuwatazama awapendao."

Mu’adh bin Jabal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akasema:

"Maneno mabaya yaliyoje uliyosema; Wallahi ewe Mtume wa Allaah sisi tunavyomjua ni mtu anayependa kheri tu".

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu alayhi wa Sallam) akanyamza.

 

Ka’ab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) anaendelea kuelezea:

"Niliposikia kuwa misafara inaanza kurudi nikaanza kujisemesha huku nikifikiri uongo upi niuseme hata Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) (anisadiki na) asighadhibike nami? Nikawaendea jamaa zangu wale wenye hekima kutaka ushauri wao.

Wakati Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) alipowasili Madina, mimi nilikuwa nishafikia uamuzi kuwa sina budi kumwambia ukweli, na kwamba nikisema uongo sitoweza kuokoka nao. Nikaamua kuwa lazima niseme kweli tu.

Asubuhi iliyofuata Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) aliwasili, na ilikuwa kawaida yake anapowasili kwanza huenda msikitini kuswali rakaa mbili, kisha hukaa hapo muda kidogo kwa ajili ya kusikiliza matatizo ya watu.

Wale waliobaki Madina wasiende vitani wakaanza kumuendea huku wakimtolea (kila aina ya) udhuru, na walikuwa kiasi cha watu themanini na kidogo hivi.

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) aliwakubalia wote udhuru wao na kuwaombea maghfira na kumuachia Mola wao ukweli wa udhuru walioutoa. Nilipomsogelea mimi na kumsalimia alitabasamu huku akionyesha dalili ya kughadhibika nami, kisha akaniambia:

"Njoo."

Nikamuendea mpaka nikakaa mbele yake.

Akaniuliza:

"Nini kilichokufanya ubaki nyuma, si ulikuwa ushajitolea kupigana?"

Nikamwambia:

"Ndiyo, Wallahi ningeulizwa suali hili na mwengine asiyekuwa wewe katika watu wa dunia ningeweza kusalimika kwa kutoa udhuru wowote ule. Lakini nilijishauri sana nikaona kuwa ikiwa nitakutolea udhuru wowote wa uongo leo ukaridhika nami, Allaah Atakujulisha na utakuja kunichukia. Na iwapo nitakuambia ukweli, ukaujua ukweli juu yangu, mimi nategemea msamaha wa Allaah. Wallahi sikuwa na udhuru wowote, Wallahi sikupata kuwa na nguvu na uwezo wa kifedha kuliko siku niliyokuacha na kubaki nyuma.'

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) akaniambia:

"Ama huyu amesema kweli. Inuka na ungoje mpaka Allaah Atakapotoa uamuzi wake juu yako."

Nikainuka na kuondoka hapo, na watu wa kabila la Bani Salamah wakainuka kunifuata, wakaniambia:

"Wallahi sisi tunavyokujuwa ni kuwa hujapata kufanya kosa kabla ya hili, kwa nini umeshindwa kutoa udhuru (wowote) kama walivyofanya wengine? Ingelitosha kufuta dhambi yako kwa maghfira atakayokuombea Mtume kwa Allaah.

Wakawa wanaendelea kunilaumu mpaka nikafikiria nirudi tena kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) na kutoa udhuru wowote na kujidanganya nafsi yangu.

Kisha nikawaambia:

"Yuko mwengine aliyekuwa kama mimi?"

Wakasema:

"Wawili, wamesema kama ulivyosema na wakaambiwa kama ulivyoambiwa".

Nikauliza:

"Nani hao?"

Wakaniambia;

"Miraarah bin Rabi’al Umariy na Hilaal bin Umayyah Al Waqi’iy."

Hawa ni watu wawili wacha Mungu waliopigana vita vya Badr na walijulikana kuwa ni wenye mfano mwema.

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu alayhi wa Sallam) akaamrisha sote watatu tusisemeshwe na mtu.

 

Tukawa tunawaepuka watu na wao wanatuepuka. Haukupita muda watu wakaanza kutubadilikia hata nikaichukia ardhi ikawa kama nisiyoijua. Tukaendelea katika hali hiyo muda wa siku hamsini. Wenzangu walijikalia majumbani mwao wakilizana, lakini mimi nilikuwa kijana zaidi kupita wao na mwenye ustahamilivu zaidi. Nikawa natoka na kuswali msikitini pamoja na Waislam, huku nikitembea sokoni, lakini hakuna mtu anayenisemesha. Nilikuwa nikimkabili Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) na kumsalimia akiwa amekaa mahali pake baada ya Swalah, kisha hujiuliza nafsini mwangu:

'Mdomo wake ulitikisika kuijibu salamu au haukutikisika?'

Mara nyingi huswali karibu yake, na baada ya Swalah, humtizama kwa kuibiaibia huku nikijishughulisha na dua baada ya Swalah, na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) alikuwa mara nyingine akiniangalia, lakini ninapomuangalia mimi, yeye huugeuza uso wake.

 

Dhiki ya kupigwa pande ilipozidi nikaamua siku moja kwenda nyumbani kwa Abu Qataadah ambaye ni mtoto wa ami yangu, na nilikuwa nikimpenda sana. Nikaparamia ukuta, nikaingia uani na kugonga mlango wa nyumba yake, nikaingia ndani na kumsalimia. Wallahi hakuijibu salamu yangu.

Nikamuambia:

"Aba Qataada! Unavyonijua mimi je, simpendi Allaah na Mtume wake?"

Akanyamaza asinijibu kitu. Nikamuuliza tena suala hilo hilo, akanijibu:

'Allaah na Mtume wake ndio wanaojua.'

Machozi yakanitoka. Nikaondoka na kuruka ukuta nikatoka nje.

 

Siku moja nilipokuwa nikitembea sokoni nikamsikia mmoja katika watu wa Shaam aliyekuja kufanya biashara ya vyakula akisema:

'Nani atakayenipeleka kwa Ka’ab bin Maalik?'

Watu wakamuelekeza kwangu. Akanijia na kunipa barua iliyotoka kwa mfalme Ghassan iliyoandikwa yafuatayo:

'Nimepata habari kuwa sahibu yako amekupiga pande, na Mola wako amekufanya usiwe na raha, kwa hivyo njoo kwetu tutakuliwaza.'

Nikasema moyoni mwangu:

'Huu pia ni mtihani mwengine.’

 

Nikaitumbukiza barua ile ndani ya tanuri la moto na kuiunguza, na ilipofika siku ya arubaini katika zile siku hamsini, mjumbe kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) alinijia na kuniambia:

"Kwa hakika Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) anakuamrisha usimkaribie mkeo."

Nikamuuliza:

'Nimtaliki au nifanyeje?'

Akaniambia:

'Bali uwe mbali naye na usimkaribie.'

Na wenzangu wale wawili wakapewa amri kama niliyopewa mimi.

Nikamuambia mke wangu:

'Nenda kwa wazee wako na ubaki kwao mpaka Allaah Atakapotoa amri yake.'

 

Mke wa Hilaal bin Umayyah alikwenda kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) na kumuambia:

'Ewe Mtume wa Allaah, kwa hakika mume wangu Hilaal ni mtu mzima asiyeweza kujitumikia mwenyewe na hana mfanyakazi wa kumsaidia, utachukizwa iwapo nitabaki kwake na kumhudumia?'

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) akamuambia:

'Hapana (sitochukizwa), lakini asikukaribie'.

Akasema:

'Wallahi yeye hana haja ya kufanya jambo lolote. Tokea yalipotokea yaliyotokea, mpaka leo hana isipokuwa kulia tu.'

 

Baadhi ya watu wangu wakaniambia:

'Na wewe ungelimuomba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) amruhusu mkeo akutumikie kama alivyomruhusu mke wa Hilaal bin Umayyah.'

Nikawaambia:

'Wallahi mimi sitomuomba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam). Sijui atanijibu nini nitakapomuomba, kwa sababu mimi ni kijana bado.'

Nikaendelea katika hali hiyo kwa muda wa siku kumi nyingine, mpaka zikakamilika siku hamsini tokea Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) alipowataka watu wasitusemeshe.

 

Baada ya kuswali Swalah ya alfajiri ya siku ya hamsini, nikapanda juu ya dari la mojawapo ya nyumba zetu na kukaa. Na wakati nilipokuwa katika hali ile Aliyoisema Allaah kuwa:

'Hata ardhi ikawa dhiki kwao, pamoja na wasaa wake' [At-Tawbah: 118]  

 

 

Nikasikia sauti kali ikitokea juu ya jabali ikisema:

'Ewe Ka’ab pokea habari njema.'

Pale pale nilipo nikaporomoka na kusujudu, nikajua kuwa faraja imekwishawasili.

Baada ya Swalah ya alfajiri Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) aliwatangazia watu juu ya kusamehewa kwetu na Allaah, na watu wakatoka na kuanza kutupa habari njema hizo. Wengine wakaja kwangu na wengine wakaenda kwa sahibu zangu.

Walikuja wakiwa wamepanda wanyama wao na wengine kwa miguu kwa ajili ya kutupongeza. Na aliponijia yule niliyeisikia sauti yake akinipa habari njema pale mwanzo, nilimvisha guo langu kama ni zawadi yake. Wallahi sikuwa nikimiliki isipokuwa nguo hiyo tu, na mimi nikaazima nguo nyingine za kuvaa, kisha nikaelekea msikitini kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam), huku watu wakinijia makundi kwa makundi wakinipongeza na kuniambia:

'Tunakupongeza kwa toba iliyokuja kutoka kwa Allah.'

'Nilipoingia msikitini, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) alikuwa amekaa akiwa amezungukwa na watu, na Twalhah bin ‘Ubaydullah alikuwa wa mwanzo kunijia mbio na kunipa mkono na kunipongeza. Hakusimama na kunipongeza katika Muhaajirin mahali pale isipokuwa Twalhah, sitomsahau kwa tendo lake hilo.

 

Nilipomsalimia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) huku uso wake ukiwa unang'ara kwa furaha, na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) anapofurahi, uso wake huwa unang'ara mfano wa kipande cha mwezi, akaniambia:

'Pokea habari njema za kufikiwa na siku bora kupita siku zote tokea ulipozaliwa.'

Nikamuuliza:

'Msamaha huu umetoka kwako ewe Mtume wa Allaah, au kutoka kwa Allaah?'

Akanijibu:

'Bali kutoka kwa Allaah.'

Nikiwa bado nimekaa mbele yake nikamuambia:

'Ewe Mtume wa Allaah, kwa ajili ya kutubiwa kwangu huku, nataka kutoa mali yangu yote sadaka kwa ajili ya Allaah.'

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu alayhi wa Sallam) akaniambia:

'Zuia mali yako, kwani hiyo ni kheri yako.'

Nikamuambia:

'Mimi nitazuia sehemu yangu ya Khaybar'.

 

Nikawa kila siku naiambia nafsi yangu:

'Mweyezi Mungu Ameniokoa kwa ajili ya kusema kweli. Kwa ajili hiyo katika maisha yangu sitotamka isipokuwa kweli tu. Kwani Wallahi simjui Muislam yeyote aliyepata mtihani mkubwa kutoka kwa Allah kwa ajili ya kusema kweli tokea siku niliyozungumza na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) mpaka leo hii, kuliko mtihani nilioupata mimi. Na mimi namuomba Allaah Anihifadhi katika siku zangu zilizobaki."

(Mwisho wa maneno ya Ka’ab bin Maalik (Radhwiya Allaahu ‘anhu).

 

Kisa hiki ni sababu ya kuteremshwa kwa aya zifuatazo zilizomo katika Suratut-Tawbah:

 

"Allaah Amekwishapokea toba ya Nabii na Wahajiri na Ansari

waliomfuata katika saa ya dhiki, pale baada ya kukaribia nyoyo za baadhi

yao kugeuka. Basi akapokea toba yao, kwani hakika Yeye kwao wao ni Mpole na ni Mwenye kuwarehemu.

Na pia wale watatu walioachwa nyuma hata dunia wakaiona dhiki juu ya

ukunjufu wake, na nafsi zao zikabanika, na wakayakinika kuwa hapana pa

kumkimbia Allaah isipokuwa Kwake Yeye. Kisha Akawaelekea kwa rehema yake ili nao waendelee kutubu. Hakika Allaah Ndiye Mwenye kupokea toba na Mwenye kurehemu”.

Enyi mlio amini! Mcheni Allaah, na kuweni pamoja na wakweli.

Haiwafalii watu wa Madina na Mabedui walio jirani zao kubakia nyuma

wasitoke na Mtume, wala kujipendelea nafsi zao kuliko yeye. Hayo ni kwa kuwa hakiwapati kiu, wala machofu, wala njaa, kwa ajili ya Njia ya Allaah, wala hawendi mahali panapowaghadhibisha makafiri, wala hakiwapati chochote kutokana na maadui, ila huandikiwa kuwa ni kitendo chema. Hakika Allaah Haupotezi ujira wa wanaofanya mema.

Wala hawatoi cha kutoa kidogo wala kikubwa, wala hawalivuki bonde, ila

huandikiwa, ili Allaah Awalipe bora ya waliyokuwa wakiya- tenda.”

At-Tawbah -117- 121

 

Na haya ndiyo wanayostahiki Muhaajiriyn (Watu wa Makkah) na Ma-Answaar (Watu wa Madina), pamoja na makabila yanayokaa nje ya Madina, kwa sababu wao ndio walioubeba Uislam juu ya vichwa vyao na wakapambana na kila aina ya dhiki, tabu na mateso.

Watu hawa walikuwa wakati wote wakisubiri ishara tu kutoka kwa kiongozi wao Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu alayhi wa Sallam) akiwataka kwenda kupigana Jihadi, na bila ya kurudi nyuma walikuwa wakiuitikia mwito wake.

Walistahiki maghfira na ujira mwema kutoka kwa Mola wao kutokana na kila bonde walilopitia na kila usiku waliokesha na kila njaa waliyostahamili huku wakiwaghadhibisha makafiri kwa kushikamana kwao na kwa ushujaa wao. Walistahiki maghfira kutokana na kila jeraha walilopata katika kupigana Jihadi, na kutokana na kila kidogo au kikubwa walichotoa kwa ajili ya Mola wao.

 

Ama kuhusu wale wanafiki waliobaki nyuma bila udhuru wowote kisha wakaenda kutoa  udhuru wa uongo kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) Allaah Alisema juu yao:

 

"Watakutoleeni udhuru mtapowarudia. Sema: Msitoe udhuru; hatukuaminini.

Allaah Amekwishatueleza khabari zenu. Na Allaah na Mtume wake wataviona vitendo vyenu. Kisha mtarudishwa kwa Mjuzi wa ya siri na ya dhaahiri; naye Atakuambieni mliyokuwa mkiyatenda.

Watakuapieni kwa Allaah mtakaporudi kwao ili muwaachilie mbali.

Basi waachilieni mbali. Hakika hao ni najsi, na makaazi yao ni Jahannamu, kuwa ni malipo kwa waliyo kuwa wakiyachuma.

Wanakuapieni ili muwe radhi nao. Basi hata mkiwa radhi nao nyiye,

Allaah Hawi radhi na watu wapotofu."

At Tawbah - .94-96

 

Share