Mwanamke Kutoboa Pua Na Kuvaa Kipini

 

Mwanamke Kutoboa Pua Na Kuvaa Kipini

 

Alhidaaya.com 

 

 

SWALI:

 

Je inafaa mwanamke kutoboa pua?

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Suala hili la kujitoboa mwanamke lina hali kadhaa ambazo zimekubalika na zilizokataliwa.

 

 

Wanachuoni wanaona kutoboa masikio kwa kuvaa hereni ni jambo lenye kukubalika lakini kwa sharti pambo hilo lihifadhike kama yanavyohifadhika mapambo ya mwanamke yeyote yule wa Kiislamu. Na hayapaswi kuonekana na ambaye si Mahram wake.

 

 

Kadhaalika, suala la kutoboa masikio lilifanywa na wanawake Swahaba. Kwa hiyo ni jambo lenye kukubalika na lina asli.

 

 

Hata hivyo, kutoboa masikio na kuvaliwa mapambo yake ya hereni kunapaswa kusionekanwe na wasiomuhusu mwanamke huyo.

 

 

Ama kuhusu kutoboa pua kama lilivyo swali la muulizaji, Wanachuoni wa Kamati Ya Kudumu Ya Utafiti Wa Kielimu Na Utoaji Fatwa, wanaona vilevile kutoboa pua kwa malengo ya mapambo ya mwanamke, kunaruhusika na hakuhesabiwi kuwa ni kubadilisha maumbile ya Allaah au kujidhuru.

 

[Fataawa Al-Lajnah Ad-Daaimah Lil Buhuwth Al-‘Ilmiyyah Wal Iftaa (24/36)]

 

 

Lakini, izingatiwe sana kuwa, msimamo Wanachuoni wa Kamati Ya Kudumu Ya Utafiti Wa Kielimu Na Utoaji Fatwa (Al-Lajnatu Ad-Daaimah) ni kuwa mwanamke anapaswa kuvaa Niqaab na hapaswi kuacha uso wake wazi, na kwa hali hiyo, Fatwa hiyo, inahusu mwanamke anayevaa Niqaab na si wanaoacha nyuso zao wazi na kuonesha hayo mapambo yao ya puani kama wanavyofanya wanawake wengi wa nchi za Asia kama India, Pakistan, Bangladesh, Sri Lanka, Maldives, Nepal, Afghanistan n.k. ambao wao ada zao wanawake wanatoboa pua zao na kuvaa vipini kama mapambo; lakini wengi wao hawafuniki nyuso zao.

 

 

Ama kutoboa kitovu, au kwenye sehemu za siri au kwenye ulimi n.k. kama wanavyofanya wanawake wengi wa bara la Ulaya na Marekani zote za kaskazini na kusini na maeneo mengine mbalimbali, Wanachuoni wamelipinga hilo na kulikemea kwani ni ada chafu za kikafiri na pia ni katika kujidhuru na tafiti nyingi zimethibitisha madhara ya kiafya yanayopatikana katika matendo hayo.

 

 

Kadhaalika, ada hizo zimeanzishwa na wanawake waovu wasio na maadili na wenye kuhamasisha uzinifu na uchafu. Na haifai kabisa kuiga watu waovu na wachafu katika matendo yao.

 

 

Kwa hali hiyo, kutoboa pua na kuvaa vipini puani, pamoja na kuwa kuna Wanachuoni wameliruhusu na wengine wameona ni kujiadhibu na kujibadilisha kama alivyoona Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) lakini akasema kama wengine wanaona linafaa na kuna miji inafanya hivyo kama ada zao, basi hakuna ubaya.

 

 

Hata hivyo, jambo lenye kupaswa kuepukwa na wale wanawake wasiojifunika nyuso zao kwani haifai kuonesha mapambo ya mwanamke kwa wanaume wasiomhusu kishariy’ah. Na ilivyo wazi ni kuwa wanawake wengi wanaotoboa pua na kuvaa vipini huwa hawavai Niqaab; na hivyo kuweka mapambo yao wazi wazi kuonekana na wanaume wasiowahusu na kupelekea kusababisha fitnah nyingi na madhambi.

 

 

Na Allaah ni Mjuzi zaidi.

Share