Mwanamke Kuswali Taraawiyh Msikitini

 

Mwanamke Kuswali Taraawiyh Msikitini

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Kuna mwanamke anaitamani jamaa ya swala ya Tarawehe katika Ramadhani, anauliza, anaweza kuomba ruhusa kwa mumewe ili aweze kuhudhuria tarawehe msikitini katika jamaa?

 

Na ikitokea hakupewa ruhusa na mumewe, anaweza kuiswali tarawehe mwenyewe nyumbani kwake?

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Asli ya Swalaah ya mwanamke ni nyumbani kwake.

 

 

Lakini hakuna makatazo ya kuswali Msikitini ikiwa atajistiri vizuri kishariy'ah na kujiepusha na marembo na manukato na mengine yasiyofaa kishariy'ah.

 

 

Wanachuoni kama Imaam Ibn Baaz na Ibn 'Uthaymiyn (Rahimahuma Allaah) wote wawili wanasema kuwa mwanamke ikiwa ataona kuna maslaha makubwa ya kuswali Taraawiyh Msikitini -baada ya kupata idhini ya mumewe- au ikiwa atakwenda na mumewe, basi hakuna ubaya kwake (mwanamke) kuswali Taraawiyh Msikitini.

 

 

Kadhaalika ni sawa kwa mwanamke kuswali Msikitini ikiwa anaona ataswali kwa utulivu zaidi akiwa Msikitini na ikiwa anaona atapata Swaalah ndefu zaidi na kunufaika na kisomo cha Imaam Msikitini. Au ikiwa atahisi uvivu akiwa nyumbani, kwa hali hiyo, inaruhusiwa na hakuna tatizo kwake kwenda Msikitini kuswali Taraawiyh.

 

 

Na ikiwa ataswali nyumbani kwake, hilo ni bora zaidi. Na anaweza kukusanya wanawake wenzake hapo nyumbani akaswali nao na mmoja akaswalisha.

 

 

Vilevile Imaam hao wawili wanaona hakuna ubaya ikiwa mwanamke hana kiasi kikubwa cha Qur-aan alichohifadhi, basi anaweza kusoma kutumia Msahafu. Lakini ni bora kusoma kwa hifdh kuliko kushika Msahafu kwani kuna kupoteza Sunnah ya kufunga mikono kwenye Swaalah.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi.

Share